Ibadhi.com

29. NAOMBA KUELEWESHWA KUHUSU IBADHI.

Assalaam 'alaykum.

Naomba kueleweshwa kuhusu misingi ya dhehebu hili la ibaadhi, ambalo inasemekana ni dhehebu kongwe kuliko hili la Sunni.

Naomba kuelewesha misingi yake, maana huwa naona katika baadhi ya miji hasa kule bara, misikiti ya ibaadh inaitwa misikiti ya waarabu.

Nakuomba ndugu yangu Mohmd Sali, au mwingine yoyote anayeweza kunielewesha basi anipe elimu hiyo, tafadhali.

JAWABU:

Waalaykum salam wa rahmatullahi wa barakatuh.

Ni kweli madhehebu hii ya Ibadhi ni kongwe zaidi kuliko madhehebu za Kisunni, hili halina shaka ndani yake, kielimu Madhehebu ya Ibadhi inajishika na Imam wake Jabir bin Zaid Al-Uzdi Al-Omani aliyezaliwa Firq Oman mwaka wa 18 Hijiria naye alichukua elimu yake kwa Masahaba wa Mtume S.A.W moja kwa moja, na hakuna tafauti kuhusu uadilifu wa Imamu huyu na kuwa yeye ni mmoja wa Matabiina wakubwa waliobobea kielimu hadi kufikia Sahaba Ibnu Abbaas R.A kusema: "Ajabu kwa watu wa Iraqi, vipi wanatuhitajia sisi hali yuko kwao Jabir bin Zaid?!! Lau wangalimkusudia watu wa Mashariki na Magharibi basi ingaliwatosheleza Elimu yake."

Kwa upande mwengine tunakutia unasibisho wa Madhehebu hii uko kwa Imam Abdullah bin Ibadhi Al-Tamimi R.A, naye kwa makubaliano aliishi -akiwa ni mwanaharakati wa upinzani dhidi ya Dola ya Bani Umayyah- katika zama za Masahaba R.A.

Pia Madhehebu ya Ibadhi haijawahipo kukosekana katika tarehe nzima ya Waislamu juu ya kushambuliwa na kufanyiwa uadui wa kivita na upotoshaji wa uhakika wake, nao uadui uliosababisha kumaliza uwepo wao katika baadhi ya miji kama vile Yemen na Hijaz, Maibadhi wengi waliuliwa kidhulma, pia kuchomwa moto vitabu vingi, na fatwa za kukandamiza Ibadhi mpaka leo hii bado hazijakatika, lakini juu ya yote hayo Ibadhi ilibakia kuwa ni mti uliokita vizuri kidalili na hoja bila kujiingiza katika dhulma za wengine, na kunufaika kwa matunda yake kila mtaka haki kwa dalili katika safu za Waislamu katika kila zama.

Ama misingi ya Madhehebu hii ni:-

 1. Kujifunga vizuri na Kitabu cha Allah mtukufu, na Sunna ya Mtume Muhammad S.A.W, na Malazimisho ya Kiakili.
 2. Kujiweka katika nafasi yenye usalama zaidi katika yale waliyotafautina Waislamu.
 3. Na kulazimika na uadilifu wa Kiislamu bila kujali upendeleo wa aina yoyote.

Ama kuhusu Misikiti ya Ibadhi kuitwa Misikiti ya Waarabu, na pengine kuitwa Ibadhi kuwa Madhehebu ya Waarabu, hilo halihusiani na Mafundisho ya Ibadhi, bali hayo ni kwa sababu ya wenyeji wa miji ya Uswahilini walipoona kuwa Misikiti hiyo inashughulikiwa na Waarabu wa Oman, pia hawajazoea kumuona Muibadhi asiyekua Muomani basi wao wenyewe wakajiwekea kizingiti hicho cha Uarabu ili kutokubali haki kwa dalili; kwani mwenyeji wa asili ya kiafrika akisikia kuwa Msikiti wa Waarabu na Madhehebu ya Waarabu huwa tayari ameshajiwekea kizuizi cha kinafsi baina yake na Ibadhi ikilichosimama juu ya misingi ya ubaguzi.

Na sisi tunawahakikishia watu wote, kuwa Ibadhi ni Madhehebu pekee katika Uislamu isiyobeba mafundisho ya kibaguzi, watu wote mbele ya Dini ni sawa, na kila mtu anayo haki ya kuwa Muibadhi bila kujali rangi yake wala kabila lake wala utaifa wake wala cheo chake wala mali yake, wako Maibadhi wengi sana ambao sio Waarabu wa Omani kama vile Maibadhi wa Algeria na Senagal na Mali na Libya na Tunisia, bali hata Afrika Mashariki wapo wenyeji wa asili ya Afrika walio Maibadhi.

Na ili tulijue hili kwa wazi kama tutatizama suala la kupatikana kiongozi wa kuongoza Taifa la Kiislamu, tunakutia katika Madhehebu za Kisunni kunazingatiwa shuruti ya Uquraishi ambayo ni shatri ya Ukabila kuwa ni Shuruti ya msingi, pia tukenda kwa Shia tunakutia kunazingatiwa shuruti ya Uahli Baiti ambayo ni Sharti ya Ukabila na ukoo hasa kuwa ni shuruti ya msingi, ama ukija katika Ibadhi hakuna sharti hiyo aslan, Muislamu yoyote mwenye elimu na uchamungu na uwezo wa kuongoza akiridhiwa na Waislamu kuwa kiongozi wao basi atakuwa ni Khalifa Amiri wa Waumini hata kama atakua ni Muhabeshi mweusi iliyobonyea pua yake basi utiifu wake kwa Waumini utalazimika.

Ama zaidi yaliyoitafautisha Ibadhi na Madhehebu nyengine za Uislamu baada ya hilo la Uongozi ni:

 1. Kumuitakidi Allah mtukufu kuwa ni mkwasi aliyetangulia kila kisichokua yeye, basi ametakasika na sifa za viungo na harakati, pia ametakasika na uwezekano wa kuonekana kwa macho duniani na akhera, pia ametakasika na uwezekano wa kusifika kwa sifa zisizokua dhati yake au zenye kuhitajia viumbe vyake, basi kusifika kwake ni kidhati na si kwa kutegemea sifa.
 2. Ulazima wa kuitakidi kuwa kila kisichokua Allah mtukufu ni kiumbe, basi Quraani ni kiumbe bila shaka yoyote, na maneno ya Allah yote ni viumbe miongoni mwa viumbe vyake, kwani maneno hayo ni athari ya sifa ya Usemaji wa kidhati wa Allah mtukufu.
 3. Ulazima wa kuitakidi kuwa Imani kisheria haikubaliani na dhambi kubwa yoyote, basi yoyote atakayeasi kwa dhambi kubwa atakua yuko nje ya duara la imani na kuwa ndani ya duara la ukafiri mpaka atubie kwa Allah mtukufu, ni sawa dhambi kubwa hiyo ni ya kishirkina au si ya kishirikina, basi hakuna ulazima wa kuwa Kafiri ni Mshirkina, ingawa kuna ulazima wa kuwa Mshirkina ni kafiri, basi kila Mshirikina ni Kafiri lakini si kila Kafiri ni Mshirkina, kutokana na hapo wanavyuoni wetu wakasema kuwa ukafiri uko aina mbili:-
  1. Ukafiri wa kishirkina kwa waliomo katika madhambi ya kishirkina.
  2. Na ukafiri wa kinafiki pia umeeitwa ukafiri wa neema kwa aliyemo katika dhambi kubwa isiyokua ya kishirkina, na huyu anazingatiwa kuwa ni Muislamu ana haki zote za Waislamu isipokua Walaa-yah tu, basi kwa yule mwenye kujua dhambi yake atamuweka katika Baraa-a mpaka atubie kwa Allah mtukufu.
 4. Tunaitakidi kuwa Muumini siku ya kiama hapatwi na khofu wala huzuni, na makosa yake aliyotubia kwayo yote yatasitiriwa kwa uombezi wa Mtume S.A.W na wenye kuombea (Shafaa), basi hatuna itikadi ya Muumini yoyote kuingia katika Moto wala kupata khofu wala fazaa siku ya Kiama.
 5. Kunaitakidi kuwa mwenye kukubaliwa mema yake zimekua nzito mizani zake, na ambaye tayakataliwa mema yake ndiye ziliyefifia mizani zake, na Allah anawakubalia Wachamungu nao ndio aliowaandalia Pepo, wala hawakubalii Mafasiki waliojitosa katika kumuasi Allah mtukufu na wakafa wakiwa ni wakaidi wa kutubia, hakika hao hawaridhii Allah mtukufu, nao ndio Madhalimu waliotakabari, na hao ndio Makafiri ambao Allah kawaandalia moto.
 6. Tunaitakidi kuwa Pepo ina milango yake ambayo Waumini Wachamungu wataingia kupitia milango hiyo, pia Moto una milango yake ambayo Waovu Mafasiki wataingizwa kupitia milango hiyo, wala hatuamini kuwepo Daraja liitwalo Swiraati juu ya Jahannamu ambayo waovu watingia motoni kwa kuanguka kutokea mwenye Daraja hilo, tunasema kuwa Itikadi hiyo ya Sirati juu ya Jahannamu ni batili; kwani iko kinyume na Quraani tukufu.
 7. Tunaamini kuwa atakaeingia Peponi atabakia humo milele akineemeka bila kutoka wala kufa wala kumalizika, na atakaeingia Motoni atabakia humo milele akiadhibika bila kutoka wala kufa wala kumalizika, basi hatuna sisi itikadi ya kutolewa motoni, wala itikadi ya kusamehewa bila ya kutubia, na tunasema kuwa Itikadi ya kutoka motoni na kusamehewa bila kutubia ni itikadi batili iliyojengeka juu ya uzushi wa matarajiohewa.
 8. Tunaamini ulazima wa kumpenda kila Muumini Mchamungu kwa ajili ya Allah mtukufu nao ndio Walaa-yah. Pia tunaamini ulazima wa kumchukia kila Kafiri Fasiki uliebainika ufasiki wake kwa jili ya Allah mtukufu nayo ndiyo Baraa-a, na ulazima wa kutomuweka katika mapenzi wala katika chuki kwa yule ambaye imetatiza hali yake au kutobainika uchamungu wake au ufasiki wake nao ndio Wuquufu.
 9. Hatuoni usahihi wa ndoa ya Muislamu kwa aliyezini naye hata kama watatubia, basi Muibadhi ikiwa ni mwanamke au mwanaume anajua vyema kuwa kuzini ni kujifungia mlango wa ndoa milele baina yake na yule aliyezini naye.
 10. Hatuoni usahihi wa kunyanyua au kunfunga mikono katika sala, wala kuitikia amina, wala kuleta dua ya kunuti, wala kusoma kisomo zaidi Alhamdu katika rakaa zote za Adhuhuri na Alaasiri.

Haya ndiyo muhimu iliyopambika kwayo Madhehebu ya Ibadhi kwa mafundisho yake.

Na mwisho tunasema kuwa jina la Ibadhi tumeitwa na wengine, na sisi baada ya muda tumekubali jina hilo kuwa ni anuani (Title) kwa kuona dharura ya kudhibiti tafauti zilizotokea baina ya Waislamu na kuhusisha athari za tafauti hizo kwa wahusika wake ili kila chuo kibebe mzigo wake na kihusishwe na mambo yake, basi tusibebeshwe ya wengine katika yenye tafauti ndani yake.

Ibadhi hatuoni uhalali wa kumfanyia ubabe wa kumkandamiza Muislamu yoyote aliyetafautina na sisi kimadhehebu kwa sababu ya tafauti ya kimadhehebu, basi hatuna sisi Fatawa chinjachinja dhidi ya Waislamu wa Madhehebu nyengine zilizo tafauti na Ibadhi, bali tunaona wajibu wa kushirikiana na wengine katika yale yenye makubalino na kuheshimiana katika yenye fatauti.

Lau kuwa Ibadhi ina mafundisho ya kuwafanyia ubabe waislamu wa Madhehebu nyengine za Waislamu, basi Afrika Mashariki kungelimwagika damu nyingi sana ya wasiokuwa Maibadhi kuanzia Karne ya 17 A.D mpaka ya 20 A.D; kwani jeshi la Imamu Muadilifu wa Oman Seif bin Sultan Al-Yaarubi R.A liliingia Afrika Mashariki kwa kuitika wito wa Waislamu wa miji ya Afrika Mashariki wa kumtaka msaada wa kukombolewa kutokana na uvamizi na ulowezi na unyanyasaji wa Wareno, basi Imam Seif Al-Yaarubi R.A aliitika wito huo na kutuma jeshi la kupambana na Wareno na wakomboa Wasilamu kutokana na mavamizi ya Wakiristo hao wa Kireno, Basi Imam Seif Al-Yaarubi R.A kwa kushirikiana na Waislamu wenyeji wa miji ya Afrika Mashariki aliweza kuwashinda vita wavamizi hao mpaka kuwazingira katika Ngome yao ya Mombasa (Fort Jesus) kwa muda wa Miaka miwili na miezi tisa mpaka wakasalimu amri na kuwatokomeza kabisa katika mwaka 1698 A.D, basi lau kuwa Ibadhi inahimiza kuwafanyia ubabe na kukandamiza Waislamu kwa misingi ya tafauti za kimadhehebu kwa hakika asingalibakia muislamu yoyote Afrika Mashariki akiwa salama isipokua Muibadhi tu; kwani Serikali ya Imam Seif bin Sultan Al-Yaarubi R.A ilikua ni Serikali iliyosimama kwa misingi ya Kiislamu nayo iliheshimu mafundisho yake kikamilifu kupitia Madhehebu ya Ibadhi na Maulamaa wa Dini ambao mapitisho ya kisiasa yalikua mikononi mwao, nayo ilikua ni Dola yenye nguvu sana, na kuanzia hapo miji yote ya Afrika Mashariki iliendelea kuwa chini ya himaya ya Serikali ya Oman na Watawala wake waliofuata mpaka kumalizika kwa Ufalme wa Kibusaidi katika visiwa vya Zanzibar mwaka 1964 A.D.

Wabillahi taufiqi.

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment