Ibadhi.com

TATU: KUUMBWA KWA QUR-AN ILIYOTEREMSHWA

KUUMBWA KWA QUR-AN ILIYOTEREMSHWA

Masuala haya ni ya kisiasa zaidi kuliko kuwa ya kiitikadi, yalianza mwishoni mwa dola ya Amawiyya, aliyadhihirisha Alja’ad bin Dirham  na akayafanya kuwa ni fitna baina ya waislamu, baadhi ya waliopindukia mipaka wakayafanya ni katika mambo ya msingi bali wakawakufurisha wasemao kuwa Quran ni kiumbe pamoja na nguvu ya dalili zao, na hapana shaka kuwa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na masahaba walikuwa wanaitakidi kuwa Allah mtukufu ni Muumbaji wa kila kitu na kila asiyekuwa Allah mtukufu ni kiumbe.
Ibadhi Wanaitakidi kuwa Quran ni maneno ya Allah mtukufu, kwake yeye imeanza, lakini siyo ya tangu kama utangu wa Allah mtukufu, Allah mtukufu aliyaumba kisha akayateremsha katika usiku wa cheo kuja katika mbingu ya dunia, kisha akayateremsha kwa Mtume Muhammad –Sallallahu alayhi wasallam- kwa kuachanishwa kwa mujibu wa matukio kwa muda wa miaka ishirini na tatu, na kama ambavyo Allah mtukufu alivyoumba mvua na chuma kisha akavishusha ndivyo hivyo hivyo alivyoumba Qur-an (( maneno yake)) kisha akayashusha.

KUGAWANYIKA KWA MANENO YA ALLAH MTUKUFU

Maneno ya Allah mtukufu yamegawanyika sehemu mbili:
1. Maneno ya dhati na inakusudiwa kukataa ububu ((sifa ya kutokusema)) kwa Allah mtukufu, au inasemwa  sifa ya kimaana kwa ajili ya kukataa kinyume chake ((kutokusema))
2. Maneno ya Lafdhi  nayo ni maelezo kwa herufi na maneno yaliyoteremshwa (( sifa ya kivitendo, mpya, iliyoumbwa)), kwa hivyo elimu ya Allah mtukufu kuhusu Quran ni ya tangu, yaani ni muhali kwa Allah mtukufu kuwa mjinga wa hayo, mambo yote na vitu vyote ni vyenye kujulikanwa na Allah mtukufu tangu zamani ((ya tangu)), lakini kitu chenye kujulikanwa kwa Allah mtukufu kinaweza kuwa cha tangu (( hakikutanguliwa na kutokuwepo)) kama kujua kwa Allah mtukufu kuwa yeye ni msikivu tangu kale, naye bila shaka ni msikivu tangu kale. Au chenye kujulikanwa na Allah mtukufu kinaweza kuwa kilichotokezea (( kiumbe kilichotanguliwa na kutokuwepo )), kama kujua kwa Allah mtukufu kwa ilmu yake ya tangu kuumba watu, lakini huko kuumba watu ni kitu kilichotokezea, vile vile kujua kwa Allah mtukufu kwa tangu, kuumba Qur an, lakini kuumbwa kwa Qur an ni jambo lilotokezea baadaye”
Na dalili ya kuumbwa kwa Quran ni kuwa Allah mtukufu amekisifu kitabu chake kimetokezeshwa katika suurat Al anbiyaa:
 
مَا يَأْتِيهِمْ مِنْ ذِكْرٍ مِنْ رَبِّهِمْ مُحْدَثٍ إِلاَّ اسْتَمَعُوهُ وَهُمْ يَلْعَبُونَ (الأنبياء: 2)
Hayawafikilii Dhikri mpya kutoka kwa Mola wao Mlezi"  Anbiya : 2 Na katika suurat Alshuaraa:
 
وَمَا يَأْتِيهِمْ مِنْ ذِكْرٍ مِنْ الرَّحْمَنِ مُحْدَثٍ إِلاَّ كَانُوا عَنْهُ مُعْرِضِينَ (الشعراء: 5)
“Wala hauwafikii Ukumbusho (muhdath -iliotokezeshwa) mpya kutoka kwa Arrahman” Ashuaraa:5

Na “Muhdath”  ni jina la chenye kufanywa, na maana ya haya ni kuwa Allah mtukufu ameitokezesha baada ya kuwa haikuwepo. Na hii ni kinyume cha utangu moja kwa moja.
Na dalili nyingine ya kuumbwa Qur an ni :
إِنَّا جَعَلْنَاهُ قُرْآنًا عَرَبِيًّا لَعَلَّكُمْ تَعْقِلُونَ (الزخرف: 3)

“Hakika Sisi tumeijaalia Qur'ani kwa Kiarabu” Zukhruf:3
 
وَكَذَلِكَ أَوْحَيْنَا إِلَيْكَ رُوحًا مِنْ أَمْرِنَا مَا كُنْتَ تَدْرِي مَا الْكِتَابُ وَلاَ الإِيمَانُ وَلَكِنْ جَعَلْنَاهُ نُورًا نَهْدِي بِهِ مَنْ نَشَاءُ مِنْ عِبَادِنَا وَإِنَّكَ لَتَهْدِي إِلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ (الشورى: 52)
“-Qur-an- Tumeijaalia kuwa ni Nuru” Ashhura:52
 
Na neno kujaalia hapa ni kwa maana ya  kukifanya kama alivyosema Allah mtukufu katika kuumba usiku na mchana:
 
وَجَعَلْنَا اللَّيْلَ لِبَاسًا (النبأ: 10)
وَجَعَلْنَا النَّهَارَ مَعَاشًا (النبأ: 11)
Na tumeujaalia usiku ni nguo*Na tumeujaalia mchana ni wa kuchumia maisha"  Annaba:10 -12, Na zipo dalili zingine,  zirejee katika vitabu vingine.

Basi hii Quran ambayo ni maelezo kuhusu herufi na maneno inazingatiwa kuwa ni kiumbe kilichotokezeshwa, kwa kukosekana uhusiano wa maneno ya kinafsi na maneno ya kilafdhi.
Katika wanachuoni wa ahlusunnah walioweka wazi kuwa Quran ni kiumbe Al imam Fakhru Razzi, na Taahir bin Aashur, nayo ndiyo inavyoelekea kuwa ni maneno ya Albukhari pale alipoulizwa na mtu kuhusu kuitamka qur an akasema “ Vitendo vyetu vimeumbwa, na lafdhi zetu ni katika vitendo vyetu”

Navyo ndivyo inavyofahamika katika mkusanyiko wa maneno ya Ibn Taimiyyah, rejea kitabu ((Muqtadhaa Madh –hab ibn Tayimiyya Anna l qur aan makhluuq)), cha mtunzi wake Ahmad Mahmoud Mansour
Na wametofautina wenye kusema utangu wa Qur –an kwa zaidi ya qauli 50, Amesema Ibn Taimiya “Na wamefariqiana wafuasi wa Ahmad bin Hambal karibia ya qauli khamsini 50”  na baada ya ikhtilafu hii, hivi ni katika akili muislam kubaki anatukuza qauli za watu ambao hawasifiki na kukingwa na kukosea ? watu wote kunachukuliwa kutoka kwao na kunarejeshwa ispokuwa kwa Muhammad s.a.w. tu (( kwake inachukuliwa tu hairejeshwi))
 
Anasema mwanachuoni Abu Is haaq “ Huenda hukmu ya usawa zaidi katika mas ala hii ni kusema kuwa Khilaf iliyopo ni ya kilafdhi, kwa sababu wenye kusema imeumbwa wanamaanisha quran isomwayo iandikwayo, na wasiokuwa wao wanamaanisha maana zake, wallahu aalam”

 

 

 

 

 

 

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment