Ibadhi.com

PILI:KUBAKIA MOTONI MILELE-1.UKAFIRI WA NEEMA

KUBAKIA MOTONI MILELE KWA WAKAIDI WALIOBAKIA KATIKA MADHAMBI MAKUBWA -BILA KUTUBIA MPAKA AKAFARIKI-


Na katika mas’ala haya kuna masuala mengi yanaingia ndani yake:

1. UKAFIRI WA NEEMA

Wanaitakidi AHLUL HAQI  WAL  ISTIQAAMA kuwa mwenye kudumu katika madhambi makubwa  bila ya kutubia hata akafariki anahesabiwa kuwa ni Kafiri (Ukafiri wa Neema), kwa kuwa yeye amepinga Neema ya Allah mtukufu na wala hakuitumia katika kumtii yeye, Amesema Allah mtukufu:

قَالَ الَّذِي عِنْدَهُ عِلْمٌ مِنْ الْكِتَابِ أَنَا آتِيكَ بِهِ قَبْلَ أَنْ يَرْتَدَّ إِلَيْكَ طَرْفُكَ فَلَمَّا رَآهُ مُسْتَقِرًّا عِنْدَهُ قَالَ هَذَا مِنْ فَضْلِ رَبِّي لِيَبْلُوَنِي أَأَشْكُرُ أَمْ أَكْفُرُ وَمَنْ شَكَرَ فَإِنَّمَا يَشْكُرُ لِنَفْسِهِ وَمَنْ كَفَرَ فَإِنَّ رَبِّي غَنِيٌّ كَرِيمٌ (النمل: 40)

“Ili anijaribu nitashukuru au nitakufuru” Naml:40

إِنَّا هَدَيْنَاهُ السَّبِيلَ إِمَّا شَاكِرًا وَإِمَّا كَفُورًا (الإنسان: 3)

 
“Hakika Sisi tumembainishia Njia. Ama ni mwenye kushukuru, au mwenye kukufuru” Insaan:3

Na katika sunnah Amesema Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- “Ahadi iliyopo baina yetu na wao ni Sala. Atakayeiwacha atakuwa amekufuru”(27)
Na kwa hayo mwenye kufanya madhambi makubwa, anazingatiwa kuwa ni Kafiri Ukafiri wa neema isipokuwa yeye atafanyiwa kama wanavyofanyiwa waislamu wengine pamoja na kumnasihi na kumlingania atubie, Akipuuza basi hatopendwa kwa ajili ya Allah mtukufu bali atachukiwa kwa ajili ya Allah mtukufu kwa kule kukosa uchamungu na wema, -hii ni hukmu yake duniani- Amma hukmu yake ya Akhera itakuwa ni Moto milele – Allah mtukufu atukinge nao – kama hakutubia kabla ya kufa, Amesema mola wetu baada ya kutaja Shirki, Uuuaji, na zinaa
 
وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ يَلْقَ أَثَامًا (الفرقان: 68)
يُضَاعَفْ لَهُ الْعَذَابُ يَوْمَ الْقِيَامَةِ وَيَخْلُدْ فِيهِ مُهَانًا (الفرقان: 69)
إِلاَّ مَنْ تَابَ وَآمَنَ وَعَمِلَ عَمَلاً صَالِحًا فَأُوْلَئِكَ يُبَدِّلُ اللَّهُ سَيِّئَاتِهِمْ حَسَنَاتٍ وَكَانَ اللَّهُ غَفُورًا رَحِيمًا (الفرقان: 70)
 
“Na atakaye fanya hayo atapata makosa,  Atazidishiwa adhabu Siku ya Kiyama, na atadumu humo akiwa ni mwenye kudharauliwa, Isipo kuwa atakaye tubu…” Furqan 68 – 70

Kundi kubwa la wanachuoni wa kisunni kama Baihaqi, Ibn al –araby, na Ibn Hajar, wamekubaliana na Ibadhi katika kuthibitisha ukafiri wa Neema au Ufasiqi, na hayo ndiyo yanayodhihiri katika kitendo cha Maimam Bukhari, Muslim, na Ibn Hibban, katika Sahiha zao”  Ijulikanwe wao Kufru ya neema huiiita “UKAFIRI CHINI YA UKAFIRI”
 
 
____________________________________________________________________________________________________________________
 
27- Ameipokea Imaam Rabii katika Musnad yake kutoka kwa Abu ubaidah kutoka kwa Jabir bin Zaid kutoka kwa Ibn Abbas, no 303. Kama alivyoipokea Imaam Muslim, Abu Daawud, Tirmidhi kutoka kwa Jabir bin Zaid – R.A. – kwa lafdh “ BAINA YA MTU NA SHIRKI NI KUACHA SALA” na hii ni riwaya ya Muslim. Na katika riwaya ya Tirmidhi “BAINA YA UKAFIRI NA IMANI NI KUACHA SALA” na katika riwaya yake nyingine “BAINA YA MJA NA USHIRIKINA AU UKAFIRI NI KUACHA SALA” na katika nyingine “BAINA YA MJA NA UKAFIRI NI KUACHA SALA” na katika riwaya nyingine aloipokea Nasaaiy na Tirmidhi kutoka kwa Buraidah –R.A.- amesema Mtume S.A.W. “AHADI ILIYOPO BAINA YETU NA WAO NI SALA, ATAKAYEIWACHA AMEKUFURU”,
Na katika riwaya ya Muslim, mlango wa Iman, mlango wa kubainisha usahihi wa kutumia jina la Ukafiri kwa mwenye kuacha sala, na Abu Daawud katika SUNNAH mlango wa Raddul irjaa, na Tirmidhi katika Iman mlango wa yale yaliyokuja katika kuacha sala, na Upokezi wa Alnnasaai katika sala, mlango wa hukmu ya kuuacha sala, na ameipokea pia Ahmad katika Musnad, na Ibnu Maajah, Annasaai, Ibnu Maajah, Haakim, na ameisahihisha na Adhahabiy ameawafikiana naye, nayo ni Hadithi sahihi.
 
___________________________________________________________________________________________________________________
 
 
 
 
 
Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment