Ibadhi.com

KWANZA-KUMTAKASA ALLAH MTUKUFU NA KILA UPUNGUFU

MASUALA YA KIITIKADI

Kwa kuwa itikadi ni katika yaliyo muhimu zaidi ya mwanzo kwa muislam, basi inapambanuka itikadi ya AHLULHAQ WAL ISTIQAAMA kuwa kwake mbali na kila itikadi mbovu zilopinda, na hiyo ni kwa sababu ya kuchukua kwao katika Qur an na Sunnah ambayo haizungukwi na shaka hata kidogo.

KWANZA-KUMTAKASA ALLAH MTUKUFU NA KILA UPUNGUFU

Maibadhi wanamtaksa Allah mtukufu utakaso wa moja kwa moja wala hawamshabihishi na viumbe, yeye Allah mtukufu amejisifu yeye mwenyewe kwa kusema.

كَمِثْلِهِ شَيْءٌ ۖ وَهُوَ السَّمِيعُ الْبَصِيرُ :١١

"Hapana kitu kama mfano wake. Naye ni Mwenye kusikia Mwenye kuona" Shuura:11
 
Na kwa msingi huu, wao – maibadhi – huzirejesha aya mutashaabiha ((zenye tafsiri zaidi ya moja katika quran)) kuzipeleka katika aya zenye tafsiri moja isyo na shaka, kwa kutekeleza amri ya Allah mtukufu  na kufuata uongofu wake:
 
هُوَ الَّذِي أَنْزَلَ عَلَيْكَ الْكِتَابَ مِنْهُ آيَاتٌ مُحْكَمَاتٌ هُنَّ أُمُّ الْكِتَابِ وَأُخَرُ مُتَشَابِهَاتٌ: آل عمران: ٧
 
“Yeye ndiye aliye kuteremshia Kitabu hichi. Ndani yake zimo Aya muhkam,( zenye maana wazi.) Hizo ndizo msingi wa Kitabu hichi. Na ziko nyengine za mifano(mutashaabiha, zenye maana zaidi ya moja). Ama wale ambao nyoyoni mwao umo upotovu wanafuata zile za mifano kwa kutafuta fitna, na kutafuta maana yake; na wala hapana ajuaye maana yake ila Mwenyezi Mungu. Na wale wenye msingi madhubuti katika ilimu husema: Sisi tumeziamini, zote zimetoka kwa Mola wetu Mlezi. Lakini hawakumbuki hayo isipo kuwa wenye akili.” IMRAN : 7
 
Na Muhkam ni aya zilizoko wazi maana yake, kwa mfano:
 
لَمْ يَلِدْ وَلَمْ يُولَدْ:الإخلاص: ٣  

“Hakuzaa wala hakuzaliwa” ikhlas 3

Mfano wa pili:

وَأَحَلَّ اللَّهُ الْبَيْعَ وَحَرَّمَ الرِّبَا  (البقرة: 275)

 “Na Allah mtukufu amehalalisha biashara na ameharamisha riba” Baqarah:275
 
Maana ipo wazi wala haihitaji tafsiri ya ziada, amma Mutashaabih ni ile inayokubali maana zaidi ya moja, inahitaji ufafanuzi na tafsiri ya ziada, kwa mfano :
 
 
 وَقَالَتْ الْيَهُودُ يَدُ اللَّهِ مَغْلُولَةٌ غُلَّتْ أَيْدِيهِمْ وَلُعِنُوا بِمَا قَالُوا بَلْ يَدَاهُ مَبْسُوطَتَانِ يُنفِقُ كَيْفَ يَشَاءُ وَلَيَزِيدَنَّ كَثِيرًا مِنْهُمْ مَا أُنزِلَ إِلَيْكَ مِنْ رَبِّكَ طُغْيَانًا وَكُفْرًا وَأَلْقَيْنَا بَيْنَهُمْ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاءَ إِلَى يَوْمِ الْقِيَامَةِ كُلَّمَا أَوْقَدُوا نَارًا لِلْحَرْبِ أَطْفَأَهَا اللَّهُ وَيَسْعَوْنَ فِي الأَرْضِ فَسَادًا وَاللَّهُ لاَ يُحِبُّ الْمُفْسِدِينَ (المائدة: 64).
 
 

“Bali neema zake zimekunjuliwa -mikono yake miwili  iwazi-” Maidah :64 na maana ya mikono hapa ni neema zake za dhahiri na za siri, au neema zake na uwezo wake na tafsiri hii inakuweka mbali na kumfananisha Allah mtukufu na kumuwekea Mwili.

Na ajihadhari Muislam mwenye akili na kauli ya wenye kumwekea Allah mtukufu Mwili, wasemao : “Sisi tunamsifu Allah kwa yale aliyojisifu mwenyewe” ikawa hawatafsiri yale maneno, wala hawachukui lugha ya mifano katika masuala ya sifa za Allah mtukufu.

Kwa hivyo itikadi yao hiyo imewapeleka kusema kuwa Allah mtukufu ana viungo vya uhakika, mfano wakasema Allah mtukufu ana mikono miwili ya uhakika ispokuwa haifanani na yetu – Ametukuka Allah na ametakasika na itikadi hii ya makosa -, na ili ikubainikie kuwa tamko lao hilo ni kosa, wala haiwafiqiani na Haki, zingatia Kauli yake Allah mtukufu:

تَجْرِي بِأَعْيُنِنَا جَزَاءً لِمَنْ كَانَ كُفِرَ (القمر: 14)

“Inakwenda kwa ulinzi wetu –macho yetu-” maana yake inapita kwa uangalizi na huruma ya Allah mtukufu, kwani haiwi kiakili kuwa Meli inapita ndani ya jicho, kwani Allah mtukufu hana macho, Allah mtukufu ametakasika na huu wasifu wa kumpa Allah mtukufu mwili, yeye hakuna kitu kilicho mfano wake, huku tukijua kuwa aya nyingi za Qur an zimeteremka kwa namna ya mfano yaani Mutashaabiha siyo Muhkama, na kwa aili hiyo inakuwa na maana ya zaidi ya moja, hivyo inahitaji ufafanuzi na tafsiri.

Mfano:

الرَّحْمَنُ عَلَى الْعَرْشِ اسْتَوَى (طه: 5)

“Arrahmani, Mwingi wa Rehema, aliye tawala juu ya Kiti cha Enzi” Taha:5

Kustawi katika aya hii ina maana  ya kutawala, kushinda na nguvu,  na maana yake ni kuwa Arshi na viumbe vingine vyote baada ya kuumbwa vilimnyenyekea Allah mtukufu kwa utiifu, na dalili ya hayo inadhihirika katika aya inayofuata baada yake

لَهُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ وَمَا بَيْنَهُمَا وَمَا تَحْتَ الثَّرَى (طه: 6)

 “Ni vyake vyote vilivyomo mbinguni na vilivyomo katika ardhi, na vilivyomo baina yao, na vilivyomo chini ya ardhi” Taha : 6

Kwa hivyo neno “kustawi” sio kwa maana ya kukaa – ametakasika Allah na kugawika au kuwa na sehemu -, na bora ya tafsiri ya Qur-an ni Qur an kujitafsiri yenyewe, na Allah mtukufu amejisema mwenyewe kupitia ulimi wa Sayyidna Huud – A.S. –

 إِنِّي تَوَكَّلْتُ عَلَى اللَّهِ رَبِّي وَرَبِّكُمْ مَا مِنْ دَابَّةٍ إِلاَّ هُوَ آخِذٌ بِنَاصِيَتِهَا إِنَّ رَبِّي عَلَى صِرَاطٍ مُسْتَقِيمٍ (هود: 56)
 
“Hakika Mola wangu Mlezi yuko juu ya Njia Iliyo Nyooka.” Hud:56
 
Herufi “alaa” katika aya mbili zilopita haimaanishi kuwa juu kikawaida kwa Allah mtukufu, -bali kimaana- kwani  yeye Allah mtukufu alikuwepo  bila ya kuwa na sehemu na wakati, naye ni mkwasi asiyehitajia viumbe vyake.
 
Kwa hivyo haijuzu kumsifu Allah mtukufu kuwa yupo katika sehemu kama mbingu, Arshi. Siraat, kwa kutegemea baadhi ya hadithi Ahadi (zilizopokewa na watu wachache) au Hadithi za uongo, Amesema Allah mtukufu:
 
وَهُوَ الَّذِي فِي السَّمَاءِ إِلَهٌ وَفِي الأَرْضِ إِلَهٌ وَهُوَ الْحَكِيمُ الْعَلِيمُ (الزخرف: 84)

 “Na Yeye ndiye Mwenyezi Mungu mbinguni, na ndiyeMwenyezi Mungu katika ardhi, Naye ndiye Mwenye hikima, Mwenye ujuzi” Zukhruf: 84


Na amesema:

أَلَمْ تَرَى أَنَّ اللَّهَ يَعْلَمُ مَا فِي السَّمَاوَاتِ وَمَا فِي الأَرْضِ مَا يَكُونُ مِنْ نَجْوَى ثَلاَثَةٍ إِلاَّ هُوَ رَابِعُهُمْ وَلاَ خَمْسَةٍ إِلاَّ هُوَ سَادِسُهُمْ وَلاَ أَدْنَى مِنْ ذَلِكَ وَلاَ أَكْثَرَ إِلاَّ هُوَ مَعَهُمْ أَيْنَ مَا كَانُوا ثُمَّ يُنَبِّئُهُمْ بِمَا عَمِلُوا يَوْمَ الْقِيَامَةِ إِنَّ اللَّهَ بِكُلِّ شَيْءٍ عَلِيمٌ (المجادلة: 7)

 

“Hauwi mnong'ono wa watu watatu ila Yeye huwa ni wanne wao, wala –mnong’ono- wa –watu- watano ila Yeye huwa ni wa sita wao. Wala –mnong’ono wa watu- wachache kuliko hao, wala walio wengi zaidi, ila Yeye yupo pamoja nao popote pale walipo” Mujaadila:7
 
Basi uwepo wake Allah mtukufu ni uwepo wa ilmu na kukizunguka kila kitu, yaani yeye si mwili wala maana isiyokuwa na mwili, lakini yeye ni mmoja amekamilika kwa dhati yake. Na kwa dalili zilizopita na nyinginezo, zenye kumtakasa Allah mtukufu na kufanana na viumbe  AHLUL HAQQ WAL ISTIQAAMA wanaitakidi KUTOWEZEKANA KUONEKANA ALLAH MTUKUFU, kwa kuwa amejisifu katika kitabu chake kwa kusema: 
 
لاَ تُدْرِكُهُ الأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الأَبْصَارَ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِير (الأنعام: 103)
 
 
“Vyenye kuona havimfikilii bali Yeye anavifikilia vyenye kuona. Naye ni Mjuzi, Mwenye khabari” An’aam 103

Na ni katika yenye kujulikanwa kuwa sifa za Allah mtukufu hazibadiliki wala hazigeuki, kama ambavyo yeye ni mpweke, mwenye kuhitajiwa katika dunia, naye ndio hivyo hivyo akhera, na kama ambavyo haonekanwi katika dunia basi hatoonekana Akhera.

Amma wale ambao wanasema Allah mtukufu ataonekana, hakika fikra zao dhaifu za kibinadamu  zitawapeleka katika kumfananisha muumba na viumbe, hupelekea hilo kuondosha Haiba na utukufu katika moyo, “Qur an tukufu imezingatia ombi la mayahudi la kutaka kumuona Allah mtukufu ni jambo baya na maasiya miongoni mwa maasi”  na kwa ajili hiyo Aliwaadhibu kwa RADI, lau ingelikuwa kumuona Allah mtukufu ni neema ya peponi, isingewashukia RADI, wala hatujawahi kusikia kuna mtu aliomba neema halafu  Allah mtukufu akamuadhibu kwa RADI, amesema Allah mtukufu:
 
يَسْأَلُكَ أَهْلُ الْكِتَابِ أَنْ تُنَزِّلَ عَلَيْهِمْ كِتَابًا مِنْ السَّمَاءِ فَقَدْ سَأَلُوا مُوسَى أَكْبَرَ مِنْ ذَلِكَ فَقَالُوا أَرِنَا اللَّهَ جَهْرَةً فَأَخَذَتْهُمْ الصَّاعِقَةُ بِظُلْمِهِمْ ثُمَّ اتَّخَذُوا الْعِجْلَ مِنْ بَعْدِ مَا جَاءَتْهُمْ الْبَيِّنَاتُ فَعَفَوْنَا عَنْ ذَلِكَ وَآتَيْنَا مُوسَى سُلْطَانًا مُبِينًا (النساء: 153) 
 
“Walisema: Tuonyeshe Allah mtukufu wazi wazi. Wakapigwa na radi kwa hiyo dhulma yao.” Nisaa:153 na zingatia neon lake “KWA HIYO DHULMA YAO” linatuambia neno hilo kuwa kuomba kumuona Allah mtukufu inazingatiwa ni DHULMA.

Na kwa hivyo ikawa jawabu ya Allah mtukufu kwa Musa –Alayhi salaam-
 
وَلَمَّا جَاءَ مُوسَى لِمِيقَاتِنَا وَكَلَّمَهُ رَبُّهُ قَالَ رَبِّ أَرِنِي أَنظُرْ إِلَيْكَ قَالَ لَنْ تَرَانِي وَلَكِنْ انظُرْ إِلَى الْجَبَلِ فَإِنْ اسْتَقَرَّ مَكَانَهُ فَسَوْفَ تَرَانِي فَلَمَّا تَجَلَّى رَبُّهُ لِلْجَبَلِ جَعَلَهُ دَكًّا وَخَرَّ مُوسَى صَعِقًا فَلَمَّا أَفَاقَ قَالَ سُبْحَانَكَ تُبْتُ إِلَيْكَ وَأَنَا أَوَّلُ الْمُؤْمِنِينَ (الأعراف: 143)
 
 “Allah mtukufu akasema: Hutoniona” Aaraf:143

Mfano wa chalenji ya Allah mtukufu kwa washirikina kwa qauli yake:
  
يَاأَيُّهَا النَّاسُ ضُرِبَ مَثَلٌ فَاسْتَمِعُوا لَهُ إِنَّ الَّذِينَ تَدْعُونَ مِنْ دُونِ اللَّهِ لَنْ يَخْلُقُوا ذُبَابًا وَلَوْ اجْتَمَعُوا لَهُ وَإِنْ يَسْلُبْهُمُ الذُّبَابُ شَيْئًا لاَ يَسْتَنقِذُوهُ مِنْهُ ضَعُفَ الطَّالِبُ وَالْمَطْلُوبُ (الحج: 73)
 
 “Hakika wale mnao waomba badala ya Allah mtukufu, hawatoumba hata nzi ijapo kuwa watakusanyika kwa hilo” Hajj:73

Na herufi ya “Lan” katika aya mbili ni katika herufi za kukataa za milele duniani na akhera na inafidisha kukatisha tamaa, maana yake ni kuwa hakika kumuona Allah mtukufu haiwezekani kutokea duniani na akhera, kama isivyowezekana kutokea kwa   washirikina kuumba nzi, duniani na akhera.

Amma aya mbili za suurat Alqiyama:
إِلَى رَبِّهَا نَاظِرَةٌ (القيامة: 23)
 
 “Zipo nyuso siku hiyo zitao ng'ara, Zikingojea rehma za Mola wao Mlezi.” Qiyama 22 -23. Zinatafsiriwa na aya mbili za wazi zinazofuatia baada yake:
 
وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ بَاسِرَةٌ (القيامة: 24)
تَظُنُّ أَنْ يُفْعَلَ بِهَا فَاقِرَةٌ (القيامة: 25)
“Na zipo nyuso siku hiyo zitakuwa zimekunjama, Zinajua ya kuwa zitafikiwa na adhabu ivunjayo uti wa mgongo.” Qiyama 24 – 25

Kundi la mwanzo, nyuso zao zinang’aa, zenye furaha, zikingojea rehma za Allah mtukufu. Na kundi la pili nyuso zo zimekunjamana, zenye khofu, zinangojea adhabu na ghadhabu za Allah mtukufu.
 
Na hizi aya nne zilizopita zinafasiriwa na aya zilizopo katika Suurat abasa
 
وُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ مُسْفِرَةٌ (عبس: 38)
ضَاحِكَةٌ مُسْتَبْشِرَةٌ (عبس: 39)
وَوُجُوهٌ يَوْمَئِذٍ عَلَيْهَا غَبَرَةٌ (عبس: 40)
تَرْهَقُهَا قَتَرَةٌ (عبس: 41)
 

“Siku hiyo ziko nyuso zitakazo nawiri, Zitacheka, zitachangamka. Na nyuso siku hiyo zitakuwa na mavumbi, kiza totoro kitawafunika” Abasa 38 – 41

Kisha aya hizi zinaongelea kuhusu nyuso zenye kung’aa, zilochangamka, zenye furaha, amma kuona ni jambo lenye kushikamana na macho sio uso. Ewe ndugu yangu  -mwenye kumpwekesha Allah mtukufu-, Jua kuwa kuomba kumuona Allah mtukufu ni katika itikadi za kiyahudi, usijifananishe nao katika itikadi yao mbovu, ukapotea. Muabudu mola wako ukimtakasa na kumfananisha na viumbe wake. Na hadithi zilopokewa katika maudhui  hii ya kutaka kumuona Allah mtukufu ni Hadithi pweke –zilopokewa na wachache-(Aahaadi) au za kutungwa , na vitabu vingi vimetungwa kuzikosoa hadithi hadithi hizo, wamevitunga wanachuoni wasiokuwa Maibadhi, na hadithi hizi Aahadiyyah haziwi ni hoja katika mambo ya kiitikadi kama inavyojulikanwa hilo kwa wanachuoni.
 
 

 

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment