Ibadhi.com

TOFAUTI BAINA YA MADHEHEBU KATIKA NAMNA YA SALA

TOFAUTI BAINA YA MADHEHEBU KATIKA NAMNA YA SALA

Tunamwambia mwenye kushangaa tofauti ndogo iliyopo baina ya madhehebu ya Ibadhi na madhehebu zingine kuhusu namna ya kusali: Ibadhi ni wenye pupa ya kujifananisha na Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-. katika sala yake, vile alivyosema: "Salini kama mlivoniona mimi nikisali" sala ya kiibadhi ndio ile ile sala ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-, hakika wamesilmu watu wa Oman mwaka wa sita Hijriya kupitia kwa sahaba Amru bin Al-as, zama za uhai wa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na kwa mujibu wa mafundisho ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-, alibakia Amru bin Al-as katika nchi ya Oman ili aeneze dini ya kiislam na asimamie utekelezwaji wake, na wala hakuondoka ispokuwa baada ya kufa wa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na hapana shaka yoyote kuwa aliwafundisha sala kama alivyoiona sala hiyo kwa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-,

Baada ya kufa kwa Mtume s.a.w. alirudi Amru akiwa na Waoman katika mji wa Madina, wakakutana na Khalifa Abubakr – Allah mtukufu amridhie- akawasifu sana, na bila shaka aliiona sala yao na wao waliiona sala yake na sala ya masahaba – Alla awaridhie -– na katika yenye kutilia mkazo kuwa sala ya waoman ni kama sala ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-, ni kuwa sahaba mtukufu Maazin biin Ghaadhubah Muomani alimzuru Mtume wa rehma na uongofu mjini Madina, kisha akarejea Oman akiwa kaombewa dua za kheri na Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- akiwa na namna ya sala aloiona kutoka kwa mwalimu wa viumbe, Muhammad –Sallallahu alayhi wasallam- na kama alivoiona namna hiyo ya sala kutoka kwa masahaba watukufu.

Kwa ajili hiyo Ibadhi katika namna ya kusali wanachukua hadithi zilokuwa sahihi na dalili zenye nguvu, zilothibiti, wala hawazigeukii hadithi dhaifu au zenye khilaf ndani yake, kama ambavyo wanachuoni kutoka madhehebu zote za kiislam wanakubaliana usahihi wa sala ya kiibadhi, bila ya kunyanyua mikono wala kuifunga wala kutikisa kidole, wala kusema aamin, na wenye kusema kuwa inapendelewa hayo mambo hawajakubaliana katika namna ya kuyafanya, wala katika idadi ya vitendo hivyo.

Na tukizifikiri hadithi zenye nguvu zilopokewa kutoka kwa Nabii wa rehma nayo ni hadithi ya mwenye kukosea katika sala yake, mtu huyu alikuwa hasali vizuri, Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- akamuamrisha arudie sala yake mara tatu akisema " Sali tena, hakika wewe hujasali" akasema Yule mtu " Namuapia Allah mtukufu ambaye amekutuma kwa haki, siwezi kusali vizuri zaidi ya hivi, nifundishe" kapokea Muslim na Abu daawud Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- alimbainishia yaliyo ya wajibu katika sala na hakuna ndani yake kunyanyua mikono wala kuifunga, na kwa ajili hiyo wamesema wapambanuaji wa hadithi: " Hakika yaliyotajwa katika hadithi hiii ni ya WAJIB katika sala , na ambavyo havikutajwa SIO WAJIB" na haya ndiyo aliyosema Mwanachuoni mkubwa Alsan’ani mwenye kitabu "Subulussalaami" amesema: "Jua, hakika hadithi hii ni tukufu, wanachuoni wamerudia sana katika kuitolea dalili kuwa vilivyotajwa ni wajib katika sala na vile ambavyo havikutajwa sio wajibu"

Na kwa msingi huu katika sala, Maibadhi wamefanyia kazi yale walokubaliana waislamu na kuacha waliyotofautiana, Amesema Imaam Nawawi naye ni katika Madhehbu ya Shafi katika ufafanuzi wake wa Sahiih Muslim "Wamekubaliana – wanachuoni – kuwa hakuna wajibu wowote wa kunyanyua mikono", na anaona Imam Malik – Imam wa madhehebu ya Malikiyya – kuwa kunyanyua mikono katika sala ni makruhu katika hali zote katika riwaya ilopokewa. Ameyataja hayo Imaam Qurtubi, Mfasiri mashuhuri katika kuifasiri Suurat Alkawthar, kufunga mkono ni makruhu katika rai mashuhuri ilopokewa kutoka kwa Malik, nayo ndiyo aloiandika katika kitabu chake cha Mudawwana, Amehadithia kutoka kwake Imam Malik, pia Al’eini katika Sharhul hidaaya, na ameihadithia pia kutoka kwa Ibn Zubeir, Hassan, Ibn Sirin, na imehadithiwa kutoka kwa Awzai kauli ya kukhiyarisha, madhehebu ya Imaam Maliki na Jumhuur ya wanachuoni wa madhehebu ya Maaliki ni kuachia mikono kama alivyohadithia Imaam Nawawi katika sharhi ya sahihi Muslim"

Na imekuja katika tafsir ya Alqurtubi Mjeled wa 10 uk 197 na katika kitabu cha ((Mukhtaswar Maa laysa fil mukhtaswar)) kutoka kwa Malik kuwa alikuwa hanyanyui mikono yake miwili popote katika sala, na amesema Ibn Qasim "Sikumuona Malik akinyanyua mikono yake popote wakati wa kuhirimia, na amesema: Ninachopendelea zaidi ni kuacha kunyanyua mikono wakati wa ihram"

Ijulikanwe kuwa Imam Malik alikuwa akichota fiqh yake kutoka kwa watu mji wa Madina wenye nuru, na katika hili kuna ishara kuwa watu wa Madina walikuwa hawafungi mikono yao katika sala kujifananisha na sala ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na kwa kuwa Imaam Jabir bin Zaid – Imaam wa madhehebu alichukua namna ya kusali kutoka kwa Mama wa waumini Sayyida Aisha – mke wa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na ameipokea kutoka kwa Mtoto wa Ammi wa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na kutoka kwa wakubwa wa masahaba – Allah awe radhi nao – hakika yeye hakuwaona wala hakupokea kutoka kwao mambo ya kunyanyua mikono na kuifunga, bali amepokea Imaam Rabii bin Habiib kuwa Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- amesema "Nawaona watu watakuja baada yangu, watanyanyua mikono yao katika sala kama mikia ya farasi washupavu", na katika hadithi ya Muslim kutoka kwa Jabir bin Samura amesema: alitutokea Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- akasema " Kuna nini, nakuoneni mmenyanyua mikono yenu katika sala kama mikia ya farasi washupavu, TULIZANENI katika sala"

Said Al Habsy

Website: https://www.ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment