Ibadhi.com

13. UFAFANUZI KUHUSU IBADHI. 4

MSALAFI:

? يحرفون بعض أمور الآخرة وينفون حقيقتها كالميزان والصراط .

Wanafanya Tafsiri mbadala (metaphorical Interpretation) katika mambo yatakayotokea Qiyaama mathalan Mizani na Siraat ((Njia ya kwenda Peponi))

[Ahlu sunnah hatufanyi Taawili wala tafsiri mbadala bali tunaamini na kuchukua kama ambavyo tumefundishwa na Mtume wetu عليه السلام

JAWABU:

Tunamuambia huyu Msalafi kuwa Itikadi sahihi haijipinzi wala haipingani na Quraani tukufu, na sisi mpaka hivi sasa hatujaona katika Quraani tukufu pahala ilipotajwa hiyo Siraati iliyotundikwa juu ya Jahannamu iliyo kali kuliko upanga na nyembamba kama unywele na kunyakuliwa watu chini yake ambayo Masalafi wanaiitakidi, Quraani iko wazi kabisa kuwa wataokaostahiki kuadhibiwa motoni watapelekwa kwenye Moto wa Jahannamu, na kuwa Moto una milango yake inayofunguliwa na kufungwa, na bila shaka milango ndiyo sehemu iliyotayarishwa kwa kuingia katika nyumba husika; kwa hiyo Jahannamu ina milango yake na Allah ametueleza mpaka idadi ya hiyo milango kuwa ni 7, wala haijatueleza kuwepo Siraati juu yake, na bila shaka wenye kuitakidi Siraati wametegemea mapokezi wanayoitakidi kuwa ni Sahihi, ama sisi hatuoni usahihi wa mapokezi hayo kwa sababu ya kupingana kwake na Quraani tukufu.

Ama kuhusu Aya ya Suuratu Maryam:

((وَإِن مِّنكُمْ إِلَّا وَارِدُهَا ۚ كَانَ عَلَىٰ رَبِّكَ حَتْمًا مَّقْضِيًّا * ثُمَّ نُنَجِّي الَّذِينَ اتَّقَوا وَّنَذَرُ الظَّالِمِينَ فِيهَا جِثِيًّا))

((Na hakuna yoyote kati yenu ila atauingia limekua hilo ni jambo lililokwishapitishwa, kisha tutawaokoa waliomchamungu na tutawaacha madhalimu humo wakiyayatika)) [Maryam 71-72]

Tutasema kuwa wakhutubiwa katika suala la kuuingia moto katika Aya hii ni wale waliozungumzwa kabla yake nao ni wenye kukanusha ufufuo wa siku ya Kiama wamekhutubiwa kwa njia ya kuelekewa (Iltifaatu), kwa hiyo hao ndio wenye kuambiwa kuwa hakuna yoyote kati yenu nyinyi wenye kukanusha ufufuo ila atauingia tu huo moto wa Jahnnamu, ama Wachamungu wao Allah mtukufu ameshatueleza kuwa siku hiyo watakua katika Amani kamilifu na wataepushwa na Jahannamu bali hata vishindo vyake hawatavisikia na huko ndiko kuokolewa kwao, amesema Allah katika Sura hiyo hiyo:

((يَوْمَ نَحْشُرُ الْمُتَّقِينَ إِلَى الرَّحْمَٰنِ وَفْدًا * وَنَسُوقُ الْمُجْرِمِينَ إِلَىٰ جَهَنَّمَ وِرْدًا))

((Siku tutakapo wakusanya Wachamungu wakiwa wageni wakirimiwa kwa Mwingi wa rehema. * Na tutakapo wakokota waovu kuiendea Jahannamu kwa kuiingia)) [Maryam 85-86]

Kwa maana hiyo Wuruudi (Kuiingia) ni kwa Waovu tu si kwa Wachamungu.

Na amesema Allah mtukufu:

((إِنَّ الَّذِينَ سَبَقَتْ لَهُم مِّنَّا الْحُسْنَىٰ أُولَٰئِكَ عَنْهَا مُبْعَدُونَ * لَا يَسْمَعُونَ حَسِيسَهَا ۖ وَهُمْ فِي مَا اشْتَهَتْ أَنفُسُهُمْ خَالِدُونَ * لَا يَحْزُنُهُمُ الْفَزَعُ الْأَكْبَرُ وَتَتَلَقَّاهُمُ الْمَلَائِكَةُ هَٰذَا يَوْمُكُمُ الَّذِي كُنتُمْ تُوعَدُونَ))

((Hakika wale waliotanguliwa na kupata wema kutoka kwetu hao wataekwa mbali na moto * hawatasikia ndirimo zake nao katika yanayotamaniwa na nafsi zao watabakia * hautawahuzunisha mshitiko mkuu na watakutana na Malaika: Hii ndio siku yenu ambayo mulioahidiwa)). [Al-Anbiyaa 103-105]

Ama kuhusu Suala la Mizani sisi Itikadi yetu ni uzani wa zile mizani zilizotajwa katika Quraani tukufu, wala hatuna Itikadi na Mizani ya vitangara viwili vya kushindanisha mema kwa maovu, na tunasema wazi wazi kuwa Mizani hiyo ya vitangara viwili haipo Akhera wala haina utajo katika Quraani tukufu.

Kwa hakika Quraani imetuambia kuwa:

((وَالْوَزْنُ يَوْمَئِذٍ الْحَقُّ ۚ فَمَن ثَقُلَتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَٰئِكَ هُمُ الْمُفْلِحُونَ * وَمَنْ خَفَّتْ مَوَازِينُهُ فَأُولَٰئِكَ الَّذِينَ خَسِرُوا أَنفُسَهُم بِمَا كَانُوا بِآيَاتِنَا يَظْلِمُونَ ))

((Uzani siku hiyo ni haki, basi yule ambaye mizani zake -ni nyingi- zitakua nzito hao ndiwo waliofanikiwa na yule ambaye mzani zake -ni nyingi- zitakua nyepesi hao ndiwo ambao wamezikhasiri nafsi zao kwa walivokua wakidhulumu kwa Aya zetu)) [A-Aaraaf 8-9]

Na Allah mtukufu amesema:

((فَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ خَيْرًا يَرَهُ * وَمَن يَعْمَلْ مِثْقَالَ ذَرَّةٍ شَرًّا يَرَهُ ))

(Atakayetenda uzito wa tembe ya vumbi ya jema lolote ataiona * na atakayetenda uzito wa tembe ya vumbi ya shari yoyote ataiona) [Al-zilzalah 7-8]

Mchamungu ataona mizani za mema yake yaliyokubaliwa zimekua nzito na kuwa maovu yake yamesitiriwa na kuepushwa nayo atazidi furaha kwa hayo, ama fasiki muovu kafiri -ni sawa ukiwa ukafiri wake ni wa kishirikina (Mshirikina) au wa kineema (Mnafiki muislamu asi mkaidi wa kutubia)- yeye huyo ataona mema yake yamekataliwa kwa sababu ya ufasiki wake kwani Allah amawakubalia Wachamungu ambao ndio aliowatayarishia Pepo, basi huyo mizani za mema yake zimefifia kwani amezongwa na maovu yake na jahannamu ndio mafiko yake adumu humo milele.

Sasa ikiwa wewe umeamua kijidanganya kwa riwaya za kutengezewa kwa ajili ya matarajio hewa na ukaridhika kujinasibisha na Usalafi ukaacha uongofu wa Quraani ulio wazi na usio na shaka yoyote, ukakubali kubebeshwa fikra inayopingana na Quraani tukufu kwa kupitia nyimbo ya Fahamu ya Salafu Saalih, na ukaogopa kuitwa Muatwila na Mkhawariji shauri yako, jiulize tu hivi kweli atakua Saalih iwapo atapingana na Quraani tukufu?!!!

Hivi hamujui kuwa amesifiwa katika Uislamu yule aliyesifiwa kwa sababu ya kujishika vizuri na mafundisho ya Allah mtukufu, na amelaumiwa katika Uislamu yule aliyelaumiwa kwa sababu ya kutoheshimu mafundisho ya Allah mtukufu?

Hivi muna shaka na Kitabu cha Allah mtukufu?

Sh. Hafidh Al-Sawafi

Website: ibadhi.com Email Anwani ya barua pepe hii inalindwa kutokana na spambots. JavaScript lazima iwe itawezeshwa kwa kuweza kuona.
Add comment