Home MAJIBU YA TUHUMA JUU YA IBADHI

MAJIBU YA TUHUMA JUU YA IBADHI

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

1. TUHUMA YA KUKUFURISHA MASAHABA (R.A)
Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja Aali zake na Masahaba wake waongofu na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya Kiama.

TUHUMA.
Miongoni mwa tuhuma batili zilizotufikia, ni tuhuma ya kukufurisha Masahaba wa Mtume (s.a.w) -Allah awaridhie-, basi wamesema: “Ibadhi wanakufurisha Masahaba wa Mtume (S.A.W)”.

Na hao wenye kutuhumu humalizia katika tuhuma zao kutaja Masahaba hawa:-

Othman bin Affaan.
Twalha bin Ubaidllahi.
Zubeir bin Al-Awaam.
Aliy bin Abi Twalib.
Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Amru bin Al-Aaswi.
Abdullahi bin Qais (Abu Mussa Al-Ash-ari).
Hassan bin Aliy.
Hussein bin Aliy.
Allah awaridhie Masahaba wote wa Mtume wetu (s.a.w).

JAWABU.
Kwanza: Inapaswa tufahamu kuwa Ibadhi inatafautisha baina ya:

Mafundisho.
Misimamo binafsi.
Basi tunapaswa tuzingatie vizuri sana, na tujue kuwa ni jambo la kawaida kumkuta mwanachuoni fulani amekamatana na msimamo wake katika suala fulani, na pengine akapata wa kumuunga mkono katika msimamo wake huo, ni sawa msimamo huo umejengwa juu ya Mafundisho ya Madhehebu au juu ya rai yake binafsi.

Kutokana na hapo, ni kosa kuifanya misimamo ya wanachuoni kuwa ndiyo mafundisho ya Madhehebu, hata kama misimamo hiyo imejengwa juu ya mafundisho ya Madhehebu, kwa sababu msimamo unabakia katika uhakika wake wa kukamatana na muhusika wake mahususi tu, na kuwa hiyo ni rai yeke binafsi, basi utamuhusu yeye na yule mwenye kukubaliana naye peke yao tu.

Pili: Baada ya kufahamu hilo la kwanza tuzingatie haya yafuatayo:-

Miongoni mwa mafundisho ya Ibadhi ni ulazima wa Al-Walaayah na Al-Baraa-a, na lililo muhimu hapa ni hili la Al-Baraa-a, nayo ni kujitenga na kumchukia kila aliyemo katika dhambi kubwa yoyote ile bila kuvunja haki wala kufanya uadui dhidi ya mali yake wala nafsi yake. Basi inalazimika kuitakidi ukafiri wa yule aliyemo katika dhambi yoyote kubwa, na hapa inapasa tuzinduke kuwa ukafiri katika mafundisho ya Ibadhi haumaanishi ushirikina kama ilivyo katika Madhehebu vyengine za kiislamu, bali humaanisha ufasiki na udhalimu na uovu tu, kwa hiyo kila mshirikina ni kafiri lakini sio kila kafiri ni mshirikina; basi muasi mshirikina na muasi asiyekuwa mshirikina wote ni makafiri kama ilivyokuwa wote ni mafasiki na waovu na madhalimu, na kila Kafiri haki yake ni Baraa-a, na kila aliyemo katika Baraa-a huyo ni Kafiri.
Kuitakidi kuwa fulani yuko katika Baraa-a hakumaanishi hukumu kuwa ni mja wa Motoni kiuhakika; kwa sababu Baraa-a hii ni hukumu ya kalifisho la kidhahiri, na hukumu hiyo hailazimishi uhakika halisi kuwa uko hivyo; kwani uwezakano wa kutubia aliyeingizwa katika Baraa-a bila kujulikana toba yake upo, kama ilivyokua uwezekano wa kukosea aliyefanya Baraa-a upo; kwa hiyo Baraa-a ya dhahiri ni kalifisho la kisheria linamuhusu muhusika wake tu, nayo haitoi elimu ya Ghaibu.
Katika Ibadhi hakuna fundisho la kumshurutisha muibadhi yoyote kukufurisha au kutukana sahaba yoyote, si katika hao waliopo katika orodha wala mwengine yoyote, kwa maana hiyo, tuhuma ya kuwa Ibadhi inakufurisha sahaba ni tuhuma hewa na batili, nayo ni tuhuma isiyojengeka juu ya misingi ya uadilfu wa kielimu.
Sisi hatukatai kuwepo baadhi ya Wanavyuoni wetu waliopita, na pengine hata baadhi ya wanaelimu waliopo, kuwa wao ni wenye kuitakidi Baraa-a kwa hao waliotajwa hapo juu katika Masahaba au baadhi yao, au wengine wasiokuwa hao; kwani hilo ni katika yenye uwezekano kiasili, lakini likipatikana hilo linabakia kuwa ni misimamo binafsi ya wahusika wake tu kwa mujibu wa yaliyosihi kwao usahihi ambao unahakikisha kuwepo kwa sifa ya ufasiki kwa yule waliyemfanyia Baraa-a ya kidhahiri, basi hayo yatabakia kuwa ni katika misimamo binafsi ya wahusika wake, na sio mafundisho katika mafundisho ya Kiibadhi; kwa hiyo kuyachukua hayo na kuyasalitisha kwa Ibadhi wote ni jaribio la kidhalimu la kuwapachikia wengine yasiyokua yao wala kuridhia kwao.
SABABU ZILIZOPELEKEA BAADHI YA WANAVYUONI WETU KUITAKIDI BARAA-A KWA MASAHABA HAO WALIOTAJWA HAPO JUU
KWANZA:
Tufahamu kuwa Uislamu ni dini iliyojengeka juu ya misingi ya uadilifu:

Allah mtukufu anatuambia katika Qur-ani tukufu:

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ كُونُواْ قَوَّامِينَ بِالْقِسْطِ شُهَدَاء لِلّهِ وَلَوْ عَلَى أَنفُسِكُمْ أَوِ الْوَالِدَيْنِ وَالأَقْرَبِينَ إِن يَكُنْ غَنِيًّا أَوْ فَقَيرًا فَاللّهُ أَوْلَى بِهِمَا فَلاَ تَتَّبِعُواْ الْهَوَى أَن تَعْدِلُواْ وَإِن تَلْوُواْ أَوْ تُعْرِضُواْ فَإِنَّ اللّهَ كَانَ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرًا

((Enyi mulioamini: Kuweni wasimamizi kwa uadilifu mashahidi kwa ajili ya Allah hata kama ni dhidi ya nafsi zenu au wazazi wawili au jamaa wa karibu, ikiwa ni tajiri au fakiri basi Allah ana haki zaidi kuliko hao, musifuate mapendwa moyo kwa kutofanya uadilifu, na kama mutapindisha au mutakwepa basi hakika Allah kwa munayoyafanya ni mwenye kuyajua vizuri sana))

[Anisaa 4/135]

Mtume wetu (S.A.W) anatuambia:

إِنَّمَا أَهْلَكَ الَّذِينَ قَبْلَكُمْ أَنَّهُمْ كَانُوا إِذَا سَرَقَ فِيهِمْ الشَّرِيفُ تَرَكُوهُ وَإِذَا سَرَقَ فِيهِمْ الضَّعِيفُ أَقَامُوا عَلَيْهِ الْحَدَّ وَايْمُ اللَّهِ لَوْ أَنَّ فَاطِمَةَ بِنْتَ مُحَمَّدٍ سَرَقَتْ لَقَطَعْتُ يَدَهَا

((Hakika yaliwaangamiza waliopita kabla yenu, walikuwa anapoiba mwenye cheo wao (Sharifu) humuacha, na anapoiba dhaifu wao (mnyonge) humsimamishia adabu ya sheria, naapa Wallahi lau Fatima binti Muhammad (Mtoto wake wa kike) ataiba basi nitaukata mkono wake)).

[Bukhari 3288, 4304 Muslim 1688]

Khalifa wa kwanza Abu Bakar A-Sidiiq (r.a) alipopewa ahadi ya uongozi alisimama, na katika aliyowaambia watu:

أَطِيعُوني ما أَطَعْتُ اللَّهَ ورسولَه فإِذا عَصَيْت اللَّهَ ورسولَه فلا طاعةَ لي عليكم

((Nitiini nikiendelea kumtii Allah na Mtume wake, basi nikija nikimuasi Allah na Mtume wake hakutakuwa na utiifu kwenu wa kunitii mimi)).

Na wala hakusema ((Munitii mimi kwa sababu ya usahaba wangu na kuchaguliwa kwangu, na hamuna haki ya kuniasi hata nikimuasi Allah na Mtume wake)).

Kwa hiyo, ni dhahiri kuwa uadilifu ndiyo njia ya Uislamu, na upendeleo umepigwa vita ndani ya Uislamu; kwa maana hiyo Usahaba sio muhuri wala ngao ya kuondoshewa hukumu za kisheria iwapo kosa litatokezea kwa mmoja wao yoyote yule, kwa hakika Masahaba wamestahiki sifa njema na cheo kikubwa kwa sababu ya kushika kwao vizuri mafundisho ya dini na kuyanusuru (Uchamungu) na sio kwa kuwafumbia macho iwapo litadhihiri kosa kwao.

PILI:

Sote tunafahamu kuwa hakuna Aya hata moja katika Qur-ani tukufu iliyomtaja kiuanisho yoyote katika Masahaba hao waliotajwa hapo juu, achilia bali kuwepo Aya iliyombashiria Pepo kiuanisho yoyote katika Masahaba hao au mwengine yoyote.

Na Mtume wetu Muhammad (s.a.w) ametuaeleza haya:

((إِنِّي فَرَطُكُمْ عَلَى الْحَوْضِ مَنْ مَرَّ عَلَيَّ شَرِبَ وَمَنْ شَرِبَ لَمْ يَظْمَأْ أَبَدًا لَيَرِدَنَّ عَلَيَّ أَقْوَامٌ أَعْرِفُهُمْ وَيَعْرِفُونِي ثُمَّ يُحَالُ بَيْنِي وَبَيْنَهُمْ. قَالَ أَبُو حَازِمٍ فَسَمِعَنِي النُّعْمَانُ بْنُ أَبِي عَيَّاشٍ فَقَالَ هَكَذَا سَمِعْتَ مِنْ سَهْلٍ فَقُلْتُ نَعَمْ فَقَالَ أَشْهَدُ عَلَى أَبِي سَعِيدٍ الْخُدْرِيِّ لَسَمِعْتُهُ وَهُوَ يَزِيدُ فِيهَا فَأَقُولُ إِنَّهُمْ مِنِّي فَيُقَالُ إِنَّكَ لَا تَدْرِي مَا أَحْدَثُوا بَعْدَكَ فَأَقُولُ سُحْقًا سُحْقًا لِمَنْ غَيَّرَ بَعْدِي))

((Hakika mimi nitakutana nanyi katika hodhi, na yule atakayenipitia hapo atakunywa, na yule atakayekunywa hatopata kiu milele, na kwa hakika watanijia watu nawajuwa na wao wananijuwa kisha kutazuiwa baina yangu na baina yao)) Akasema Abu Hazim: Basi akanisikia Nuuman bin Abi Ayaash naye akasema: Namna hivi ulisikia kutoka kwa Sahl? Nikasema: Ndio. Akasema: “Nashuhudia kwa Abu Said Al-Khudri hakika nimemsikia naye anaongeza ndani yake: ((Basi nitasema: ((Hakika hao ni katika mimi (Masahaba wangu Masahaba wangu))). Hapo patasemwa: Hakika wewe hujui waliyozusha baada yako. Basi nitasema: Awe mbali, awe mbali, yule aliyebadilisha baada yangu))

[Bukhari 3349, 6583, 6584 Muslim 2290, 2297]

Riwaya hiyo iko wazi kuhusu hali ya baadhi ya Masahaba wa Mtume (s.a.w) vipi watakavofukuzwa siku ya Kiama katika Hodhi lake S.A.W., na kuwa miongoni mwa sifa zao:

Ni wenye kutokana na Mtume wetu Muhammad S.A.W yaani jamaa zake hasa, na ujamaa huo unawezekana ni wa Kikabila au Ukoo.
Na kosa lao ni kuwa wao walibadilisha baada ya Mtume S.A.W.
Kwa maana hiyo kusifiwa Masahaba kwa wema ni kwa sababu ya Uchamungu wao na uadilifu wao na kushika kwao dini vizuri, basi sababu ikiondoka bila shaka sifa ya wema nayo itaondoka; kwa sababu sifa hiyo ni tawi ambalo shina lake ni Uchamungu na Uadilifu ambao ndiyo sifa ya kuwemo mja katika utiifu wa Allah mtukufu na Mtume wake (s.a.w).

MATOKEO MUHIMU YA KITAREHE
Tukijerea katika tarehe ya matokeo ya waislamu baada ya kufa Mtume (s.a.w) tutakutia matokeo yaliyotokea katika zama za Masahaba (r.a), nayo ni kama ifuatavyo:

Yalifanyika mapinduzi dhidi ya Uongozi wa Othman bin Affaan kwa kuzingirwa Ikulu kwa muda wa siku 40, na kupelekea hilo kuuliwa Kiongozi huyo wa Dola katika mwaka wa 35 Hijiria, na hayo yalipatikana baada ya Othman kutawalia uongozi kwa muda wa miaka 12.
Kuchaguliwa Aliy bin Abi Twalib baada ya kuuliwa Othman, na miongoni mwa waliompa ahadi ya Uongozi na utiifu (Baia) ni:
Zubeir bin Awaam.
Twalha bin Ubaidillahi.
Walioshiriki katika mapinduzi ya kumuondoa madarakani Othman bin Affaan.
Baada ya uteuzi wa Imam Aliy bin Abi Twalib kulitokea mmeguko uliofanywa na Masahaba: 1. Zubeir bin Awaam. 2. Twalha bin Ubaidillahi. 3. Bibi Aisha Mke wa Mtume (s.a.w). Mashaba hao watatu walikwenda Iraqi wakiwa pamoja na waliowakubaliana nao, na kutokea huko walianzisha uasi dhidi ya Imam Aliy bin Abi Twalib kwa madai ya kudai kisasi cha mauaji ya Othman bin Affan.
Katika mwaka wa 36 Hijiria, vilipiganwa vita maarufu kwa jina la Vita vya Ngamia, ni vita alivyopigana Imam Aliy kwa kuuzima uasi wa Zubeir bin Awaam na Twalha bin Ubaidillah na Bibi Aisha R.A na walio pamoja nao katika uasi walioufanya idhidi ya Dola ya Kiislamu, vita hivo viliitwa vita vya Ngamia (Jamal) kutokana na Ngamia aliyekuwa ni kipando cha Bibi Aisha (r.a), na vita hivo vilipelekea kuuliwa Zubeir bin Awaam na Twalha bin Ubaidillahi na kuchukuliwa Bibi Aisha Mke wa Mtume (s.a.w) akiwa mateka katika jeshi la Imam Aliy bin Abi Twalib.
Katika mwaka wa 37 Imam Aliy alijikuta mbele ya Uasi mwengine uliotokea Shaam, uasi huu mara hii ulikua chini ya Uongozi wa Masahaba wawili 1. Muawiyah bin Abi Sufiayan na 2. Amru bin Aasi.
Katika mwaka 37 Hijiria vilipiganwa vita maarufu kwa jina la Vita vya Siffain, ni vita vya pili alivyopigana Imam Aliy kwa kuuzima uasi dhidi ya Dola ya Kiislamu uliofanywa na Masahaba 1. Muawiyah bin Abi Sufiyan na 2. Amru bin Al-Aasi na walio pamoja nao, vita hivi vilipelekea kuuliwa waislamu wengi ambao ni Masahaba na Matabiina tu kwa wakati ule, miongoni mwa waliouliwa ni Sahaba maarufu Ammaar bin Yaasir (r.a) akiwa katika safu za Imam Aliy akilipiga vita kundi la waasi lililomuua, na Mtume (s.a.w) alimwambia Ammaar: ((Litakuua kundi la waasi)) [Bukhari 447, 2812 Muslim 2916] na Hadithi hii ni Mutawaatir.
Katika vita vya Siffain, Muawiyah baada ya kuona anashindwa vita akaleta ujanja wa kisiasa wa kutaka sulhu baina yake na Aliy bin Abi Twalib.
Wito wa Muawiyah wa kutaka sulhu ulipelekea kugawika safu za jeshi la Imam Aliy katika migawiko miwili:
Waliopinga wito wa Muawiyah wa kutaka Suluhu, walifanya hivo kwa kuona kwao kuwa hukumu ya Allah tayari ipo katika Kitabu chake ya kulipiga vita kundi la waasi mpaka kuzima uasi wao, kwa hiyo si katika mambo ya kusuluhishwa bali ni katika mambo ya kupitishwa hukumu ya Allah mtukufu moja kwa moja, hawa walijulikana kuwa ni Wasomi (Al-Qurraau).
Waliokubali wito wa Muawiyah, nao walikuwa wengi ukilinganisha na wale waliopinga.
Imam Aliy alikubali masimamo wa wengi waliokubali wito wa Muawiyah, hapo wale waliopinga wito huo wa Sulhu walijitoa katika safu za Imam Aliy kwa kukataa kwao kushiriki na kusaidia katika waliloliona ni asi na uvunjaji wa Hukumu ya Allah kwa rai za watu, na hilo lilipelekea kupatikana kundi la tatu nalo ndilo kundi la Watu wa Naharawani (Al-Qurraau).
Wito wa Muawiyah wa kufanya sulhu ulikubalika rasmi na Imam Aliy, na kila upande ulichagua mwakilishi wake, nao ndiwo hao mahakimu wawili Masahaba:
Abu Mussa Al-Ashari ni hakimu wa upande wa Aliy.
Amru bin Al-Aasi ni hakimu kupande wa Muawiyah.
Matokeo ya Sulhu iliyofanywa na Mahakimu hao wawili (Abu Mussa Al-Ashari na Amru bin Al-Aasi) ni kumuizua Imam Aliy katika Uongozi, na hapo ndipo Al-Quraau (Watu wa Naharawani) walipomchagua Kiongozi naye ni Imam Abdullahi bin Wahab Al-Rasibi (r.a) kwa njia ya Shuura na kumpa Baia ya kisheria.
Imam Aliy alipinga matokeo ya Sulhu iliyofanywa na Mahakimu wawili (Abu Mussa Al-Ashari na Amru bin Al-Aasi) na kubatilisha wito wa Muawiyah, lakini akajikuta yuko mbele ya Kiongozi mpya aliyechaguliwa kwa njia sahihi naye ni Imam Abdullahi bin Wahbi Al-Rasibi (r.a).
Imam Aliy alimpeleka Ibn Abbaas (r.a) ili kuzungumza na Imam Abdullahi Al-Rasibi na walio pamoja naye kihoja na dalili, lakini Ibn Abbaas (r.a) alirudi akiwa ameshindwa kihoja, naye alichukua msimamo wa kujitoa katika jeshi la Imam Aliy na kusema neno lake mashuhuri ((Ikiwa sikuwa katika safu yao hao, basi sitokuwa dhidi yao)) akiwakusudia Wananaharawani.
Katika mwaka wa 38 Hijiria Imam Aliy aliamua kuwapiga vita Ahalu Naharawani nao walipigana nae. Ingawa Imam Aliy alishinda katika vita hivyo alivyowapiga Wananaharawani na kupelekea kuuliwa wengi wao akiwemo Imam Abdullahi bin Wahab Al-Rasibi (r.a), lakini vita hivo vilidhoofisha nguvu ya Imam Aliy kiasi cha kukosa uwezekano wa kumuelekea tena Muawiyah kijeshi, na hilo lilipelekea kujiimarisha Muawiyah na kujishughulisha katika kuichukuwa miji kimabavu na kuhodhi madaraka.
Mwaka wa 40 Hijiria, Abdurahman bin Muljim Al-Muradi alimuua Imam Aliy kwa kumnyemelea wakati wa Sala ya Alfajiri na , na baada yake Wafuasi wake wakampa ahadi ya uongozi (Baia) mwanawe Hassan.
Hassan na Hussein wana wa Imam Aliy katika mwaka huo huo walifanya sulhu na Muawiyah, na kuuachia uongozi katika mikono ya Muawiyah na kuanza rasmi Dola ya Bani Umayyah, nao uliitwa mwaka wa Jamaa.
Sasa katika matokeo haya muhimu ya kitarehe, tunaporejea na kuyaangalia kuiadilifu tunapata kuwa kulipatikana Watu wa Naharawani, nao ni wale waliojitenga kwa kujitoa kwao katika safu za Imam Aliy wakati alipoamua kukubali wito wa Muawiyah wa kuingia katika Sulhu, kiistilahi sulhu hii inajulikana kwa jina la (TAHKIIM) na Watu wa Naharawani walijulikana kuwa ni (MUHAKKIMAH), waliitwa hivyo kwa sababu wao walitoa hukumu moja kwa moja kwa neno lao ((LAA HUKMA ILLAA LILLAHI)), maana yake ((HAKUNA HUKUMU ISIPOKUWA YA ALLAH TU)), neno lao hilo lilikuwa ni ishara ya wazi ya msimamo wao wa kujishika na Qur-ani tukufu na kujifunga na hukumu ya Allah mtukufu aliyokwisha ihukumu kwa waasi, nayo ni hukumu ya kulipiga vita kundi la waasi mpaka kuzima uasi wao na kuirejea katika amri ya Allah nayo ni Amri ya kumtii Kiongozi muadifu ambaye kwa wakati huo alikua ni Imam Aliy bin Abi Twalib.

Huenda mtu akasema:

Kama hiyo ndiyo hukumu, basi kwa nini wao walitoka nje ya utiifu wa Imam Aliy na kupinga yale aliyoamua ya kukubali sulhu? Kwa nini walijitoa katika safu yake na kujitenga? Jee! hilo si kosa?

Jawabu: Kwa hakika sote tunafahamu kuwa mafundisho ya Uislamu yanasema ((hakuna kumtii kiumbe kwa kumuasi Muumba)), na hapa tunakumbusha neno la Khalifa wa kwanza Abu Bakar (r.a):

((Nitiini nikiendelea kumtii Allah kwenu, basi nikija nikimuasi (Allah) hakutakuwa na utiifu kwenu wa kunitii)).

Vile vile Kiongozi katika Uislamu anapochukuwa Ahadi ya uongozi hulazimika na sharti ya kumtii Allah na Mtume wake (S.A.W), na kwa maana hiyo akitoka nje ya utiifu wa Allah na Mtume wake S.A.W huwa amevunja sharti ya utiifu kwa Waislamu, na Allah mtukufu amewakataza Waumini kwenye kitabu chake kwa muwambia:

((Na wala musisaidiane katika dhambi na uadui))

[Maaidah 2]

Kwa hiyo kujitoa kwao katika safu za Imam Aliy ni haki bila ya shaka yoyote kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu; kwani wao walijiepusha kusaidia na kushiriki katika kufanyika kosa la wazi waliloliona, nalo ni kosa la kuvunja hukumu ya Allah mtukufu ya kulipiga vita kundi la Muasi kwa kufuata rai ya Muasi Muawiyah ya kufanya naye Suluhu.

Tukilifahamu hili, tutajuwa kuwa Watu wa Naharawani walikuwa ni wasomi wenye uoni wa mbali sana, nao walikuwa katika msimamo sahihi kabisa kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu.

Kwa hiyo ni jambo la kawaida tukakutia katika safu za Ibadhi kuwapo baadhi ya wanaelimu waliodhihirisha Baraa-a kwa Masahaba hao tuliowataja, kwani wao walifanya hivyo kwa kuzingatia kuthibiti upande wao uhakika wa makosa waliyojitosa ndani yake kwa mujibu wa sheria bila ya kuthibiti kutubia kwao kutokana na makosa hayo ambayo ni:

Kuwatia makosani waliofanya mapinduzi ya kumuondoa Othman bin Affaan madarkani na kumuua.
Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Amru bin Al-Aaswi.
Kuanzisha siasa batili ya kudai kisasi cha damu ya Othman bin Affan.
Twalha bin Ubaidllahi.
Zubeir bin Al-Awaam.
Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Amru bin Al-Aaswi.
Kutoka katika utiifu wa kiongozi wa Umma Imam Aliy bin Abi Twalib na kumpiga vita bila ya haki ya kufanya hivo, bali kwa msingi batili wa kudai kisasi cha damu ya Othman bin Affaan.
Twalha bin Ubaidllahi.
Zubeir bin Al-Awaam.
Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Amru bin Al-Aaswi.
Kukubali wito batili wa kundi la waasi, nao ni wito wenye madhumuni ya kuvunja hukumu ya Allah mtukufu iliyo wazi katika Kitabu chake.
Aliy bin Abi Twalib.
Abdullahi bin Qais (Abu Mussa Al-Ash-ari).
Amru bin Al_aasi
Hassan bin Aliy.
Hussein bin Aliy.
Kuingia katika utekelezaji wa wito batili wa waasi wenye madhumuni ya kuvunja hukumu ya Allah mtukufu.
Amru bin Al-Aaswi.
Aliy bin Abi Twalib.
Abdullahi bin Qais (Abu Mussa Al-Ash-ari).
Kuwatia makosani waliokataa kushiriki katika kosa la kukubali wito wa waasi ambao madhumuni yake ni kuvunja hukumu ya Allah mtukufu.
Aliy bin Abi Twalib.
Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Amru bin Al-Aaswi.
Abdullahi bin Qais (Abu Mussa Al-Ash-ari).
Kuwapiga vita waliokataa kushiriki katika kosa la kukubali wito wa waasi wito wenye madhumuni ya kuvunja hukumu ya Allah mtukufu.
Aliy bin Abi Twalib.
Hassan bin Aliy.
Hussein bin Aliy.
Kumkubalia muasi katika lengo lake na kuusalimisha Uongozi katika mikono ya Muasi.
Hassan bin Aliy.
Hussein bin Aliy.
Hizi ndizo sababu kuu zilizopelekea baadhi ya wanavyuoni wetu kuwaingiza Masahaba hao katika hukumu ya Baraa-a; kwa yale yaliyosihi kwao.

Sisi upande wetu, kwa wakati wetu huu wa leo, tunasema neno la Sheikh wetu wa zama hizi, naye ni Sheikh Ahmed bin Ahmed Al-Khalili -Allah mtukufu amuhifadhi na atunufaishe kwa elimu yake- amesema alipoulizwa kuhusu Masahaba (r.a):

((Sisi hatujalazimishwa kufuatilia yale yaliyokwishapita, na kwa hakika kinachotulazimu sisi ni kusawazisha na kuboresha ya wakati wetu, na tuanze na nafsi zetu, na gurudumu ya siku halirudi nyuma, basi haiwezekani kuyadiriki yaliyokwishapita wala kuyatengeneza yaliyokwisha haribika, basi tuna nini sisi hata tushughulike na yaliyokwishapita na kuacha kushughulikia majukumu yetu ya wakati tuliomo ndani yake.

Na lililokwishapita kabla yako hata kama ni kwa saa * liachie kulishughulikia, kwani hilo sio utiifu.)). Na Allah ndiye anayejua zaidi. [ Fatwa Aqidah 2/305].

Na kwa hakika waliyoyasema baadhi ya wanavyuoni wetu katika hukumu za Baraa-a kuhusu Masahaba hao au baadhi yao, sisi tunayaangalia kuwa ni anuani ya uadilifu usiokuwa na upendeleo katika Madhehebu ya Ibadhi, na hilo linahakikisha kuwa Ibadhi imesimama katika mafundisho sahihi ya Uislamu, basi hayo ni alama ya wazi kuwa Madhehebu ya Ibadhi haina maathiriko ya kupendelea, si kiukoo, wala kicheo, wala kwa chochote kile, na katika Ibadhi hawezi kiongozi kuchezea uadilifu aslan.

Basi asitujie mtu na kutuambia Mwanachuoni wenu fulani amemkufurisha Sahaba Fulani; kwani sisi tutamuambia ikiwa amemkufurisha bila ya haki ya kumkufurisha iliyothibiti kwake atakua amekosea, ama ikiwa amemkufurisha kwa haki ya kumkufurisha iliyothibiti kwake basi huo ni uadilifu wa Kiislamu hakuna doa ndani yake, isipokua kwa wale wenye maradhi ya upendeleo katika nafsi zao.

Wabillahi taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

2. NYUSO SIKU HIYO ZITAN`GARA
TUHUMA BATILI:
Tumepokea tuhuma batili dhidi ya Ibadhi katika mlango wa Tafsiri, tuhuma inasema kuwa Ibadhi wanapinga Aya ya Qur-ani tukufu iliyoko katika Suuratu Al-qiyaamah 22-23.

((وجوه يومئذ ناضرة * إلى ربها ناظرة))

((Nyuso siku hiyo ni zenye kun`gara * Kwa Mola wake tu ni zenye kusubiria))

Walenga wa tuhuma hiyo wamefikia upeo wa kusema eti Ibadhi “Kuhusu Aya inayosema Allah ataonekana basi ‘kuona’ katika hiyo Ayah imepewa tafsiri ya kusubiri rukhsa kutoka kwa Mola kuingia Peponi”

JAWABU:
Ndugu zangu.

Kwa hakika sisi tunashangaa sana, vipi inafikia watu kumzulia Allah uongo mweusi hivi hivi -tena bila hata ya kuona haya- kwa kumsemea lisilokuwemo katika Kitabu chake na kulifanya ni sehemu ya Aya iliyomo katika Kitabu chake, wamefanya hivyo si kwa lolote bali ni kwa ajili ya kuinusuru Itikadi yao batili, na kuipotosha Itikadi ya wengine.

Wapi Allah mtukufu amesema kwenye Kitabu chake ((Allah ataonekana))?!!

Neno “kuona” ambalo wanatuhumiwa Ibadhi kulipa Tafsiri ya “kusubiria ruhusa kutoka kwa Allah mtukufu ya kuingia Peponi”, neno hilo liko wapi katika Qur-ani tukufu na katika Aya gani?!!

Ikiwa ni neno ((Naadhirah)) lililokuja katika Aya tukufu ya Suuratu Al-qiyaamah; kwa hakika neno hilo ni ((Naadhirah)) na sio ((Raaiyah)), basi vipi mapendwa moyo yao hawa yamefikia upeo wa kumzulia Allah uongo?!!

Kwa sababu ((Raaiyah)) ndilo neno lenye maana ya kuona na sio ((Naadhirah)).

Ndugu zangu.

Neno ((Naadhirah)) limekuja katika Qur-ani tukufu kwa maana ya kusubiria, ametuambia Allah mtukufu katika Suuratu Anamli Aya ya 35 kuhusiana na Malkia wa Mamlaka ya Sabaa:

وإني مرسلة إليهم بهدية فناظرة بما يرجع المرسلون

((Na hakika mimi nimewatumia zawadi, basi ni mwenye kusubiria kwa watakayorudi nayo wajumbe))

Kama tunavyoona kuwa katika Aya tukufu limekuja neno ((Naadhirah)) ni lile ile lililoko katika Suuartu Al-Qiyaamah, nalo halikubeba maana ya kuona, bali limebeba maana ya kusubiria.

Tukirejea tena katika bustani ya Qur-ani tukufu tunalikutia neno hili hili likiwa limeambatanishwa na herufi ya ((Ilaa)) ambayo wao hudai madai hewa eti neno hili likiambatanishwa na herufi ya ((Ilaa)) huwa halina maana nyengine isipokuwa ya kuona, lakini madai yao hayo yanakadhibishwa na Qur-ani tukufu, na ulimi wa kiarabu pia; kwa sababu neno hilo limekuja kwa njia ya kitendo kama ilivyo katika Suuratu Al-Aaraf 198.

((وتراهم ينظرون إليك وهم لا يبصرون))

((Na unawaona wanakuangalia na hali wao hawaoni))

Aya iko wazi kuwa ((yandhuruuna ilaika)) katika Aya hii tukufu maana yake ni kuangalia na sio kuona, bali zaidi ya hapo ni kuwa Aya inatuambia kuwa kuangalia kunaweza kupatikana bila ya kuona, kwani wao ni wenye kuangalia lakini hawaoni; kwa maana hiyo kuangalia hakulazimishi kuona hata kama chenye kuangaliwa ni chenye uwezekano wa kuonekana.

Tukirudia tena katika Aya ya Suuratu Al-Qiyaamah, ikiwa tutalichukua neno ((Naadhirah)) kwa maana ya kuangalia, ambayo pia inakubalika katika maana ya neno ((Naadhirah)) tunaipata maana yake ni kama ifuatavyo.

((وجوه يومئذ ناضرة * إلى ربها ناظرة))

((Nyuso siku hiyo ni zenye kun`gara * Kwa Mola wake tu ni zenye kuangalia))

Tunapata kuwa neno hili ((Naadhirah)) kumbe linachukua hapa moja katika maana mbili:

1. Kusubiria.

2. Kuangalia.

Sasa tuje katika maana ya pili ya kuangalia ambayo tayari tumeshaeleza kwa ushahidi ulio wazi na utokao katika Qur-ani tukufu kuwa kuangalia hakulazimishi kuona, tunapata tena kuwa muangalio huo haulazimiki kuwa ni muangalio wa kuona; kwa maana hiyo pia huwezi kuivisha maana ya muangalio wa kuona kwa kujihukumia tu.

Na sote tunafahamu kuwa maneno huchukuliwa kwa maana kusudiwa kwa wenye akili.

Kwa mfano:

Raisi amewaahidi wana kijiji kuwajengea shule, na shule bado haijajengwa na muda wa kutimiziwa ahadi ya waliyoahidiwa unakaribia, Mkuu wa Mkoa au Wilaya akamuandikia Raisi ((Muheshimiwa Raisi hakika wana kijiji chetu wanakuangalia wewe tu)).

Bila shaka wenye akili zao timamu wanafahamu kuwa muangalio uliotajwa katika maneno hayo si muangalio wa kuona, bali ni muangalio wa kutarajia na kusubiria utimizaji wa ahadi ya Muheshimiwa Rais.

Sasa ndugu zangu tukirudia katika Aya tukufu, tunafahamu sote kuwa ndani yake limetumika neno ((siku hiyo)) nayo bila ya shaka yoyote ni siku ya Kiama kabla ya wahusika wa nyuso hizo kuingia katika Pepo aliyoitayarisha Allah mtukufu kwa ajili yao; kwa maana hiyo basi (Nyuso za watu wema siku ya kiama ni zenye kun`gara nazo zi zenye kumuangalia Mola wake tu.))

Sasa ndugu zangu Aya si itakuwa wazi kabisa kuwa huo ni muangalio wa kusubiria kwa matarajio yasiyo kuwa na shaka kutimiziwa wao ahadi aliyowaahidi Allah mtukufu?!!

Kwa maana hiyo, huo sio muangalio wa kuona kwa macho hata kwa mujibu wa Itikadi ya Mawahabi inayosema kuwa Allah ni wenye uwezekano wa kuonekana kwa macho, basi Aya hiyo bado haiwezi kuwa ni andiko safi la kuthibitisha kuonekana Allah siku ya Kiama; kwa sababu maana ya kusubiria na kutarajia ina nguvu zaidi kuwa ndiyo maana lengwa ya Aya hiyo kwa mujibu wa maelezo yake.

Ndugu zangu.

Wenye akili wanapoambiwa maneno bila ya shaka yoyote huyaondoshea maana isiyowezekana na kuyachukua kwa maana inayokubaliana na wahusika wake, kwa mfano mwenye akili timamu ukimwambia “Bwana wee! Ametujia simba msikitini akatoa khotuba sio mchezo bwana” basi moja kwa moja anaondosha kusudio la simba mnyama wa porini, kwa sababu hilo haliwezekani kimazoea kwa mujibu wa akili, kwa maana hiyo maana ya mnyama pori anaifuta katika kamusi ya maana kusudiwa ya neno simba katika maneno yale, na kuchukua pahala pake maana iliyokusudiwa kwa mujibu wa muhusika na vielelezo vya maneno ikiwa ya Shujaa, au maana ya mwenye sauti nzito ya kushitua…

Na katika Qur-ani tukufu limekuja katika Suuratu Ala-Imraana Aya ya 77 neno (Nadhara) likiwa limeambatanishwa na herufi ya (Ilaa).

إِنَّ الَّذِينَ يَشْتَرُونَ بِعَهْدِ اللَّهِ وَأَيْمَانِهِمْ ثَمَنًا قَلِيلًا أُولَٰئِكَ لَا خَلَاقَ لَهُمْ فِي الْآخِرَةِ وَلَا يُكَلِّمُهُمُ اللَّهُ وَلَا يَنظُرُ إِلَيْهِمْ يَوْمَ الْقِيَامَةِ

((Hakika wale wanaonunua kwa Ahadi ya Allah na viapo vyao thamani ndogo, hao hawana sehemu katika Akhera, na hatowasemeza Allah na HATOWAANGILIA SIKU YA KIAMA….))

Sasa ndio tuseme kuwa Allah hatowaona hao siku ya kiama?!!

Haliwezekani hilo; kwa sababu maana hiyo haiwezekani katika haki ya Allah mtukufu.

Basi bila shaka maana kusudiwa ni kuwa hatowarehemu, na hapa tunapata kuwa kuangaliwa na Allah mtukufu siku ya kiama maana yake ni kurehemewa, basi bila ya shaka kuangaliwa Allah mtukufu na waja wake katika siku hiyo ni kutarajia na kusubiria mapeo ya Rehma zake Allah mtukufu.

Ndugu zangu.

Ibadhi itikadi yetu ni kuwa Allah ndiye aliyeumba kila kitu; kwa hiyo kuwepo kwake kumetangulia viumbe vyake vyote; kwani mtendaji hukitangulia kitendo chake, na tunaitakidi kuwa hakuna chenye kushirikina na Allah katika sifa yoyote ya Allah mtukufu, basi Allah ndiye wa mwanzo bila ya kuanza, sisi ni wenye kuitakidi kuwa sehemu zote ni viumbe vyake Allah mtukufu kama tunavyoitakidi kuwa kila kilichomo katika kiumbe nacho ni kiumbe bila ya shaka yoyote; kwa maana hiyo haiwezekani Allah mtukufu kusifika kwa sifa yoyote yenye lazimisho la mipaka ya kudhibitika kisehemu, kwa hiyo Allah mtukufu haiwezekani kuonekana na kilichopo katika sehemu kama ilivyokua haiwezekani kufanana na kilichopo katika sehemu.

Na Allah mtukufu amejisifu katika Kitabu chake kwa neno lake katika Suuratu Al-An-Aami Aya 102 mpaka 103.

ذَٰلِكُمُ اللَّهُ رَبُّكُمْ ۖ لَا إِلَٰهَ إِلَّا هُوَ ۖ خَالِقُ كُلِّ شَيْءٍ فَاعْبُدُوهُ ۚ وَهُوَ عَلَىٰ كُلِّ شَيْءٍ وَكِيلٌ * لَّا تُدْرِكُهُ الْأَبْصَارُ وَهُوَ يُدْرِكُ الْأَبْصَارَ ۖ وَهُوَ اللَّطِيفُ الْخَبِيرُ

((Huyo ndiye Allah Mola wenu. Hakuna mungu isipokuwa yeye tu. Muumbaji wa kila kitu basi muabuduni yeye tu. Na yeye juu ya kila kitu ni msimamizi. Havimdiriki vyenye kuona na yeye anavidiriki vyenye kuona na yeye ni Allattifu Alkhabiiru))

Na kudiriki maana yake ni kufikia na kupata, kwa maana hiyo kudiriki kwa nyenye kuona ni kule kuona kwake, na Aya hii haikubali maana nyengine isipokua hii, nayo ni maana inayokubaliana na utukufu wake Allah mtukufu na ukamilifu wake Allah mtukufu; kwa sababu Allah mtukufu ni Mkwasi asiyefikiwa na wasifu wa kuhitaji.

Allah mtukufu ametuambia katika Qur-ani yake katika suuratu Shuaraa aya ya 61 na 62:

فَلَمَّا تَرَاءَى الْجَمْعَانِ قَالَ أَصْحَابُ مُوسَىٰ إِنَّا لَمُدْرَكُونَقَالَ كَلَّا ۖ إِنَّ مَعِيَ رَبِّي سَيَهْدِينِ

((Basi yalipoonana makundi mawili wakasema watu wa Mussa: “Sisi ni wenye kudirikiwa” Akasema (Mussa): Hapana hakika Mola wangu yuko pamoja nami ataniongoza)).

Basi kama ilivyokuwa watu wa Mussa walivyokhofia kufikiwa na maadui zao ambako ndiko alikokanusha Mtume Mussa (a.s) ndivyo Allah alivyokanusha uwezekano wa kufikiwa na vyenye kuona ikiwa ni macho au moyo au fikra au chochote kile, na kiwe kitakachokuwa uoni wake huwezi kumfikia Allah mtukufu, basi Allah mtukufu si mwenye uwezekano wa kuonekana na kiumbe yoyote yule.

Wabillahi Taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

3. HADITHI ZA KUONEKANA ALLAH, AMETAKASIKA ALLAH NA KUONEKANA -1
بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliye mkwasi asiyefanana na chochote asiyedirikiwa kwa macho, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Ama baada ya hayo.

Imetufikia tuhuma inayosema kuwa Ibadhi wanapinga na kukataa sunna ya Mtume (s.a.w) katika aliyofundisha kama yalivyokuja katika Hadithi sahihi zilizopokewa na Bukhari na Muslim na wengineo ya kuwa Waumini watamuona Allah mtukufu siku ya Kiama.

JAWABU:
Kwa hakika Ibadhi wanapokataa Hadithi zenye mafundisho ya itikadi ya kuonekana Allah mtukufu siku ya kiama, huwa wanafanya hivo kwa misingi madhubuti iliyojengeka katika misingi ya kumtakasa Mtume (s.a.w) na mafundisho yasiyokuwa yake, kwa hiyo Ibadhi hawajapinga Sunna, wala hawajapinga na Hadithi sahihi, bali wanakataa Ibadhi ni uzushi na uongo alionasibishwa nao Mtume (s.a.w), na sote tunafahamu kuwa mapokezi ya Hadithi yanaweza yakawa sahihi au dhaifu; kwa maana hiyo kukataa mapokezi ya hadithi hakumaanishi kupinga Sunna, kwa sababu mapokezi ya hadithi hayawi sunna mpaka yathibiti, na Ibadhi wanaona kuwa hadithi hizo za kupandikiza itikadi ya kuonekana Allah mtukufu si sahihi kwa sababu zifuatazo:

Ibadhi wanamtakasa Mtume (s.a.w) na uwezekano wa kupingana na Qur-ani tukufu.
Ibadhi wanamtakasa Mtume (s.a.w) na uwezekano wa kupingana na malazimisho ya Kiakili.
Ibadhi wanamtakasa Mtume (s.a.w) na uwezekano wa kujipinza katika mafundisho yake, hasa hasa mafundisho ya kiitikadi.
Ama la kwanza linapatikana kwa kupingana mafundisho ya hadithi hizo na maandiko safi ya Qur-ani tukufu, nayo ni maandiko yafuatayo:

Neno lake Allah mtukufu: ((Vyenye kuona yeye [Allah mtukufu] havimdiriki..)) [Al-Anaam 103], na kudiriki vyenye kuona ni kuona kwake, wala hakuna kutafautiana katika lugha kuwa macho yakimuona tayari yatakua yamemdiriki kwani kuona kwake ndiko kudiriki kwake, basi Allah mtukufu alipojitakasa na uwezekano wa kudirikiwa na vyenye kuona ikiwa ni macho au vyengine vyovyote akawa Allah mtukufu amejisifu kwa kujitakasa na uwezekano wa kuonekana na kiumbe chake chochote kile.
Neno lake Allah mtukufu ((Hakuna chochote kilicho mfano wake [Allah mtukufu] naye ni Msikivu Muoni)) [Shuura 11], bila shaka kuonekana kitu chochote kunalazimisha kufanana na vyenye kuonekana, wala haisemwi kama ni hivyo basi na kutoonekana ni kufanana na visivoonekana, kwa sababu hakuna kisichoonekana na Allah mtukufu, kwa hiyo hukumu na kutoonekana baadhi ya viumbe ni hukumu inayohusiana na viumbe fulani tu, hukumu hiyo hailazimishi kuwa hicho kisichoonekana na viumbe fulani ndio hakionekani na viumbe vyengine waliobakia, bali itakua ni batili isiyokua na shaka kusema kuwa kitu hicho hakionekani na Allah mtukufu, kwa maana hiyo ni wazi kabisa kuwa kutoonekana Allah mtukufu na kiumbe chochote ni ukamilifu wake peke yake Allah mtukufu asiyefanana na chochote kile.
Neno lake Allah mtukufu ((Hutoniona..)) [Al-Aaraf 143]. Neno hili aliambiwa Mtume Mussa (a.s.w) na yeye ni miongoni mwa Mitume watano wa daraja ya juu kabisa, nalo ni neno lililoachiwa bila ya kufungwa na wakati mahususi, na Allah mtukufu hasifiki kwa sifa ya kubadilika; kwa maana hiyo ikathibiti kuwa hukumu ya neno hilo ni ya milele, na ikiwa Mtume Mussa (a.s.w) hatamuona Allah mtukufu basi hukumu hiyo kwa wengine walio katika daraja yake ni sawa, na kwa walio chini ya daraja yake ndio kabisa hawatomuona Allah mtukufu. Na ikiwa itasemwa kuwa Mtume Mussa (a.s.w) alitaka kumuona Allah mtukufu hapa duniani na hilo ndilo alilokataliwa; kwa sababu haliwezekani hapa duniani. Tutasema: Kwa hiyo Mtume Mussa (a.s.w) alikuwa hajuwi kuwa hilo haliwezekani hapa Duniani naye akaliomba, au atakuwa ameomba kitu kisichowezekana naye anajua kuwa hakiwezekani?!! Na yote mawili haifai kuyasema katika haki ya Mtume Mussa A.S.W; kwa maana hiyo ikathibiti kuwa Mtume Mussa (a.s.w) amelitaka hilo ili iwe njia ya kuwakatisha tamaa wenye kulitaka hilo; kwa hiyo dalili imetimia na hoja imesimama kuwa hilo si lenye kuwezekana kwa Allah mtukufu, kwa hiyo hakuna njia ya kuwezekana kwa wengine walio katika darja yake au walio chini ya daraja yake.
Ama la pili la kiakili liko wazi kabisa; kwa sababu akili inapitisha lazimisho la kuwa Allah mtukufu ndiye aliyeumba viumbe vyote, kwa hiyo uwepo kwake umetangulia viumbe vyake, basi uwepo wa Allah mtukufu ni kabla ya uwepo wa kiumbe chochote, na bila ya shaka miongoni mwa viumbe vyake ni sehemu (space), na lazimisho la hili kuwa Allah mtukufu hasifiki kwa sifa za kulazimika na kuwepo sehemu ndio zipatikane, na ndio maana ya kuwa yeye hajafanana na chochote kile, kwa hakika akili inapitisha lazimisho la kuwa kila chenye kuonekana ni lazima kiwe katika sehemu ya kukidhibiti; kwa maana hiyo kisichowezekana kudhitiwa kwa mipaka ya sehemu hicho hakina uwezekano wa kuonekana, na Allah mtukufu hasifiki kwa uwezekano wa kudhitiwa kwa mipaka ya sehemu; kwani yeye alikuwepo kabla ya sehemu; kwa sababu sehemu ni kiumbe miongoni mwa viumbe vyake, kwa hiyo hakuna uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu kwa mujibu wa malazimisho ya Kiakili, amesema Sheikh Abu Hassan Al-Bisyani (r.a): ((Na kwa hakika yeye Allah mtukufu ni mwenye hekima, hamtumi kwa vitabu vya haki aliye muongo)) akimaanisha (r.a) kuwa: Haiwezekani Mtume yoyote katika Mitume ya Allah mtukufu akadhibishwe na malazimisho ya kiakili.

Ama la tatu, ni kwa sababu zimethibiti riwaya kutoka Mtume (s.a.w) zenye kubeba mafundisho ya kumtakasa Allah mtukufu na uwezekano wa kuonekana, nazo ni Riwaya sahihi kwa Makubaliano, na hapa tunakuletea riwaya mbili:

Amesema Mtume (s.a.w): ((Hakika Allah mtukufu kuzuizi chake ni nuru, lau kitamfunua kwa hakika utukufu wa dhati yake ungeliunguza vyote vitayofikiwa na uoni wake katika viumbe vyake)) [Muslim 179, Abu Daudi 493, Ibnu Maajah 195], Riwaya hii iko wazi kabisa kuwa hakuna uwezekano wa kuonekana Allah mtukufu, na kuwa hilo la kuonekana Allah mtukufu liko kinyume na utukufu wake Allah mtukufu.
Amesema Mtume (s.a.w): ((Na hakuna baina ya watu wa peponi na kumuona Mola wao isipokuwa rubega ya kiburi katika dhati yake ndani ya Pepo ya Adeni)) [Bukhari 4878, 4879, 7444 Muslim 180] Rubega ya kiburi ni kiwakilishi cha sifa ya kiburi, nayo ni sifa ya Dhati ya Allah mtukufu, na madhumuni ya Hadithi hii ameyabainisha Al-Haafidh Ibnu Hajar Al-Asqalani katika Sherhe yake Fat-hu Al-Baari ya hadithi no 7444 naye ni mwanachuoni wa Kisunni maarufu amesema: ((Na maana ya hadithi ya mlango huu ni kuwa: KWA MUJIBU WA UTUKUFU WA ALLAH NA KUJITOSHELEZA KWAKE ASIONEKANE NA YOYOTE)) [Ibnu Hajjar Al-Asqakani Fat-hu 13/433]. Kwa hakika Hadithi hii iko wazi kabisa kuwa Itikadi ya kuonekana Allah mtukufu inapingana na Utukufu na Kujitosheleza kwa Allah mtukufu.
Baada ya bayana hii, tukijaaliwa tutakuja kueleza yale yaliyomo katika hizo riwaya ambazo Ibadhi wanatuhumiwa eti kuzikataa ni kukataa na kukanusha sunna, na hiyo in shaa Allah itakuwa ni sehemu ya pili ya jawabu yetu hii panapo majaaliwa.

Usikose kujisomea Itikadi yetu ya kutoonekana Allah mtukufu kwa kubofya hapa>>

Asante sana

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

4.MIKONO KATIKA SALA
Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na Masahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Ama baad
Tumepokea tuhuma ya kuwa Ibadhi wanapinga Sunna ya Mtume (s.a.w) kwa kutonyanyua mikono yao katika sala na kutoifunga bila ya kuwa na dalili yoyote katika kuachia mikono yao katika sala.

JAWABU:
Kwanza ifahamike kuwa suala hili ni suala la matawi ya kifiqhi ambayo Waislamu wana wasaa wa kuvumiliana ndani yake, amesema Ibnu Baaz Mufti wa Saudia aliyepita:

…ومن أرسل فصلاته صحيحة لكنه ترك الأفضل ولا ينبغي في هذا التنازع بين الإخوان..اهـ [عبدالعزيز بن عبدالله بن عبدالرحمن بن باز / مجموع الفتاوى ومقالات متنوعة 11/146]

“Na mwenye kuachia mikono yake sala yake ni sahihi lakini atakua ameacha lililo bora zaidi, na haipasi kuvutana katika hili baina ya ndugu”.

Amesema Mufti wa Oman Samaahatu Sheikh Al-Khalili -Allah amuhifadhi-:

واعلم أن مسلك أصحابنا في الصلاة الاحتياط بعدم الأخذ إلا بالروايات التي لا يحوم حولها أي ريب في المسائل المختلف فيها، لأن الصلاة هي الركن الثاني من أركان الإسلام الذي يلي العقيدة مباشرة، والمحققون من العلماء على اختلاف مذاهبهم لا يقبلون الحديث الآحادي حجة في المسائل الاعتقادية لعدم إفادة القطع فكانت الصلاة المجاورة للعقيدة في الترتيب حرية بالحيطة، على أن من العلماء من قال في صلاة أصحابنا: إنها ثابتة بالإجماع؛ لأن ما يتركونه من الأعمال فيها مختلف فيه عند غيرهم، ومن قال به لا يرى تركه يؤدي إلى بطلان الصلاة. اهـ [الفتاوى 1/252-253]

((Na ujue kuwa njia ya As-Haabu wetu (Ibadhi) katika sala ni kuchukua tahadhari kwa kutochukua isipokua mapokezi yasiyofikiwa na wasi wasi wowote katika masuala yaliyoingiwa na tofauti; hayo ni kwa sababu sala ndio nguzo ya pili katika nguzo (tano) za Uislamu, nayo ndiyo nguzo inayofuatilia moja kwa moja baada ya Itikadi tu, na wanavyuoni wenye kuhakiki -juu ya kutofautiana madhehebu zao- hawakubali hadithi aahadii (iliyokuja kwa njia ya dhana) kuwa ni hoja katika masuala ya Itikadi; hayo ni kwa sababu ya kutopatisha kwake -hadithi hiyo- uhakika wa yakini, na kwa sababu sala iko jirani wa Itikadi kiutaratibu basi ikawa ina haki zaidi ya kuichukulia tahadhari, juu ya kuwepo miongoni mwa wanavyuoni waliosema kuhusu sala ya As-Haabu wetu (Ibadhi): Hakika ni sala sahihi kwa makubaliano ya wote; kwa sababu vitendo walivoviacha vimeingiwa na mizozo ndani yake kwa wengine, na mwenye kuvikubali haoni ubatilifu wa sala kwa kuachwa vitendo hivo.)) [Al-Allaamah Ahmed Al-Khalili Al-Afatawa 1/253].

Kutokana na uhakika huo tulio ueleza tutajua kuwa katika suala hili la kufunga mikono na kuinyanyua kuna uhakika huu ufuatao:

Ni suala lenye khitilafu nyingi ndani yake kwa wenye kulithibitisha, na khitilafu hiyo ni dalili ya udhaifu wake.
Makubaliano ya wenye kuthibitisha kufunga mikono, kuwa si katika vitendo vya lazima katika sala; kwa hiyo mwenye kuwacha kunyanyua na kufunga mikono sala yake itakuwa sahihi bila ya wasi wasi wowote, na bila shaka kujiondoa katika khitilafu ni bora kuliko kukita ndani yake.
Inabainika wazi kuwa Ibadhi wapo katika msimamo wenye usalama zaidi katika suala hili; kwani wameachana na ya yale yenye wasi wasi na yenye mizozo ndani yake.
Tujue kuwa hakuna kutafautiana katika safu za Ibadhi kuhusu suala hili, na kuwa haifai kunyanyua wala kufunga mikono katika sala.

Ya ajabu katika suala hili:

Ni kuwaona wenye kulithibitisha wanalishadidia sana bila ya hoja wala dalili ya kubatilika sala ya asiyelifanyia kazi.
Ni kuwaona wenye kulithibitisha wanatofautiana wao kwa wao katika suala hili na kila mmoja anaona dalili zake ndio sahihi na za wengine ni dhaifu:
Hanafi: Wanaona kufungwa mikono chini ya kitovu, nao wana hoja zao pia wanadhoofisha hoja za wengine.
Maliki: Wanaona kunyanyua mikono wakati wa kuhirimia tu, kisha kuirejesha katika hali yake kama ilivyokuwa kabla, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
Shaafii: Wanaona kufunga mikono juu ya tumbo karibu ya kifua, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
Hambali: Wanaona kufunga mikono iwe juu ya kifua karibu na shingo, nao wana hoja zao na kudhoofisha hoja za wengine.
Mtume (S.A.W) amesema:

((صلوا كما رأيتموني أصلي))

 

((Salini kama munavoniona nasali)).

Inafahamika na wote kuwa kunyanyua na kufunga mikono ni vitendo vya dhahiri; basi vipi kuwe na kutafautiana ndani yake kama kweli vimethibiti?!

Kwa hakika yote hayo yanaonesha udhaifu wa tuhuma hii wanayotuhumiwa kwayo Ibadhi, na kubainika kuwa hiyo ni tuhuma hewa; hasa hasa tukizingatia kuwa kila watetezi wa madhehebu -mbali na kufanya jaribio la kuthibitisha usahihi wa msimamo wao- pia wanadhoofisha hoja za wengine kidalili, na wote wanakusanyika katika chuo kimoja cha Ahalu Sunna wal-Jamaa.

Tukirudia katika Hadithi zilizopokewa katika suala hili tunazikutia si sahihi kiuhakiki; kwani hadithi yenye nguvu zaidi katika hizo ni hadithi aliyoipokea Bukhari naye hakupokea katika sahihi yake isipokua hadithi hiyo tu katika suala zima la kufunga mikono, nayo haina bayana ya kuwa inatoka kwa Mtume (s.a.w), imekuja ndani yake:

“كان الناس يؤمرون أن يضع الرجل اليد اليمنى على ذراعه اليسرى في الصلاة)) قال أبو حازم: لا أعلمه إلا يَنْمِي ذلك إلى النبي صلى الله عليه وسلم قال إسماعيل: يُنمَى ذلك ولم يقل يَنمِي. [البخاري: 740]

((Walikuwa watu wakiamrishwa, mtu aweke mkono wake wa kulia juu ya dhiraa yake ya kushoto katika sala)). Amesema Abu Haazim: Silijui hilo isipokua analiegemeza kwa Nabii S.A.W. Amesema Ismail: Linaegemezwa hilo wala hakusema analiegemeza. [Bukhari 740]

Suali hapa. Nani aliyekua akiamrisha na wakati gani?!!!

Hadithi hii:

Imepita kwa Malik bin Anas, naye ni Imamu wa Madhehebu ya Maliki, Imam Malik hakuifanyia kazi Hadithi hii. Hivi wao wanaweza kumtuhumu Imam Malik kutofanyia kazi Sunna ya Mtume (s.a.w)?!!.
Riwaya hii ina utata ndani yake; kwani Bukhari ameipokea kupitia Mashekhe wake wawili nao ni Abdullahi bin Maslamah na Ismail bin Abi Uwais ambao wote wawili wameipokea kutoka kwa Imam Malik na yeye ameipokea kutoka kwa Abu Haazim. Masheikh hawa wa Bukhari wametofautina:
Abdullahi bin Maslamah anasema kuwa Abu Haazim alisema: “Silijui hilo isipokuwa analiegemeza kwa Nabii (s.a.w).
Ismail bin Abi Uwais anasema: “Hapana Abu Hazim hakusema hivyo, bali alisema: “Linaegemezwa hilo kwa Mtume (s.a.w)”.
Inaonesha kuwa Sheikh Abdullahi bin Maslamah alitaka kumsemea Abu Haazim kuwa kasema Sahaba Sahal bin Saad ambae riwaya imesimamia kwake ndiye aliye liegemeza hilo kwa Mtume (s.a.w) kuwa ndiye aliyekuwa akiamrisha watu, lakini Shekh Ismail bin Abi Uweis akalikataa hilo na kulidiriki kwa kusema kuwa Abu Haazim alisema kuwa hilo lilikuwa linaegemezwa kwa Mtume (s.a.w).

Kwa hiyo ni nani aliyekuwa akiliegemeza?!!

Riwaya ina utata, na riwaya yenye utata ni dhaifu.

UHAKIKA
Sisi sote tunajua vizuri, kuwa baada ya kuanguka Dola ya Khalifa wa nne Aliy bin Abi Twalib (k.a.w) mwaka 40 Hijiria ulifuatia utawala wa kibabe na mabavu wa Mfalme Muawiyah bin Abi Sufiayan Al-Umawi na Mafalme waliofuatia baada yake, utawala huo wa Bani Umayyah makao makuu yake yalikuwa Shaam katika mji wa Damascus – Syria, na tunafahamu vizuri kuwa Shaam ndio kitovu cha Ahalu Al-Kitaabi (Mayahudi na Manasara), na sote tunafahamu kuwa mapokezi ya Hadithi yalichezewa na kupelekea hilo kusemewa na kupenyezewa Mtume (s.a.w) yasiyokuwa yake, na kwa sababu hiyo ndio ikaanza elimu ya kuchunguza Hadithi za Mtume (s.a.w) na kuzihakiki; ili kuzijuwa ni zipi dhaifu na zipi sahihi, pia tunafahamu vizuri vipi Masahaba na Matabiina walivokuwa wakijitahidi katika kufanyia kazi Sunna ya Mtume wetu (s.a.w).

Sasa tuangalie haya yafuatayo:

Mosi:

Anatuambia Mwanachuoni wa Kisunni Ibnu Rushd Al-Hafiid katika Sharhu Bidaayatu Al-Mujtahid wa Nihaayatu Al-Muqtasid 1/323 haya yafuatayo:

 

المسألة الخامسة: اختلف العلماء في وضع اليدين إحداهما على ألخرى في الصلاة، فكره ذلك مالك في الفرض وأجازه في النفل، ورأى قوم أن هذا الفعل من سنن الصلاة وهم الجمهور.

والسبب في اختلافهم أنه قد جاءت آثار ثابتة نقلت فيها صفة صلاته عليه الصلاة والسلام ولم ينقل فيها أنه كان يضع يده اليمنى على اليسرى، وثبت أيضا أن الناس كانوا يؤمرون بذلك. اهـ

 

((Suala ya tano: Maulamaa wametofautiana katika kuweka mikono mmoja wao juu ya mwengine katika sala, basi akalichukia hilo Maliki katika faridha na akalikubali katika nafila, na watu wengine wakaona kuwa kitendo hicho ni katika sunna za sala, nao ni jamuhuri. Na sababu ya kutofautiana kwao, ni kuwa zimekuja athari zilizothibiti ambazo imenakiliwa ndani yake sifa ya sala yake (s.a.w), na haikunakiliwa humo kuwa yeye alikuwa akiweka mkono wake wa kulia juu ya wa kushoto. Na imethibiti pia kuwa watu walikuwa wakiamrishwa kwa hilo…..)) mwisho wa kunukuu.

Pili:

Anatuambia Mwanachuoni wa Kisunni Abu Bakar Muhamad bin Ibarahim bin Mundhir Niisabuuri (318 HJ) katika kitabu chake Al-Ishraafu ala madhaahibi Al-Ulamaa 2/12:

ورأت جماعة إرسال اليد، وممن روينا ذلك عنه: ابن الزبير، والحسن البصري، وإبراهيم النخعي. اهـ

((Na wameona jamaa kunyoosha mikono (katika sala), na miongoni mwa tuliopokea hayo kuwa kwao ni: Ibnu Zubair, na Hassan Al-Basari, na Ibrahim Anakhaii)) mwisho wa kunukuu.

Inafahamika vizuri kuwa Hassna Al-Basari na Ibrahim Anakhaii ni katika Matabiina wakuu, na Ibnu Zubair ni miongoni mwa Masahaba allah awaridhie, hivi tunaweza kuwatuhumu hawa kuwa walipingana na Sunna na Mtume (S.A.W).

Imekuja katika Twabaqaatu Al-Huffadhi cha Mwanachuoni wa Kisunni Dhahabii 3/213 kuwa Abdurazaq amesema:

((Sijamuona (mtu) aliyekuwa akisali vizuri kuliko Ibnu Juraij, amechukuwa (sala yake) kutoka kwa Ataa, na Ataa amechukua (sala yake) kutoka kwa Ibnu Zubar, na Ibnu Zubair amechukua (sala yake) kutoka kwa Abu Bakar Siddiiq, na Abu Bakar ameichukuwa (sala yake) kutoka kwa Nabii (s.a.w)…))

Na sisi tumeona kuwa Ibnu Zubair hakuwa akifunga mikono katika sala.

Sheikh Al-Imam Mohammad Aaabid -Mufti wa Madhehebu ya Maliki katika mji wa Makka katika zama zake- anatuambia katika kitabu chake Al-qaulu Al-faslu ukurasa wa 3:

(أقول) هذه الشبهة فاسدة من ثلاثة أوجه (الوجه الأول) القبض لم يرو من طريق صحيح ليس فيه مقال إلا من طريق سهل بن سعد المروي في الموطأ والبخاري ومسلم وليس في البخاري غيره، حدثنا عبدالله بن مسلمة عن مالك عن أبي حازم عن سهل بن سعد قال: “كان الناس يؤمرون أن يضع الرجل يده اليمنى على ذراعه اليسرى في الصلاة” قال أبو حازم: لا أعلمه إلا ينمي ذلك للنبي صلى الله عليه وسلم. وهو مع كونه لا غبار عليه في صحة إسناده لا أولا ولا آخرا إلا أن الداني قال في أطراف الموطأ هذا الحديث معلول لأنه ظن من أبي حازم لقوله لا أعلمه إلخ ورده ابن حجر بأن أنا حازم لو لم يقل لا أعلمه إلخ لكان في حكم المرفوع.. اهـ

((Nasema: tuhuma hii ni batili kwa njia tatu: Njia ya kwanza: Hakika (tendo la) kufunga mikono halijapokewa kwa njia sahihi hata moja iliyosalimika na maneno ya kusemwa ndani yake, isipokua njia ya Sahal bin Saad iliyopokewa katika Muwatwaa na Bukhari na Muslim)) -kisha akaileta husika Bukhari kisha akasema: ((Pamoja na kuwa usahihi wa sanadi yake hauna doa lolote sio mwanzo wala mwisho, lakini Adaanii katika Atraafi Muwatwaa amesema: “Hadithi hii ni maaluul; kwa sababu ni dhana kutokea kwa Abu Hazim kwa neno lake silijui hilo … na ameirejesha Ibnu Hajar kwa sababu lau kuwa Abu Haazim hakusema silijui hilo… ingelikua katika hukumu ya kurufaishwa”)).

Imekuja katika kitabu cha Tarikhi Abi Zur-aa Damashqii riwaya no. 1785:

وحدثني عبد الرحمن بن إبراهيم عن عبدالله بن يحيى المعافري عن حيوة عن بكر بن عمرو أنه لم ير أبا أمامة -يعني ابن سهل- واضعا إحدى يديه على الأخرى قط ولا أحدا من أهل المدينة حتى قدم الشام فرأى الأوزاعي وناسا يضعونه.

Amenihadithia Abdurahmani bin Ibarahim kutoka kwa Abdullahi bin Yahya Al-Maafiri kutoka kwa Haiwa kutoka kwa Bakar bin Amru kuwa yeye hakuwahi kumuona Abu Umaamah -yaani mwana wa Sahal- akiweka mokono wake mmoja juu ya mwengine hata mara moja, wala (hakuwahi kumuona) yoyote katika watu wa Madina, mpaka alipofika Shaam ndio akamuona Auzaaii na watu wanaiweka.

Amepokea Ibnu Abi Shaibah (mpokezi wa Kisunni) katika Musannaf 3/319 riwaya no. 3958 katika riwaya za Taabii maarufu Hassan Al-Basri -naye hakua akifunga mikono katika sala kama ilivotangulia- kuwa Mtume (s.a.w) amesema:

“كأني أنظر إلى أحبار بني إسرائيل واضعي أيمانهم على شمائلهم في الصلاة”

((Kama mimi naona wataalamu wa dini wa Bani Israili wakiwa wanaweka mikono yao ya kulia juu ya mikono yao ya kushoto katika sala)).

Hebu tuangalie kwa jicho la uadilifu ndugu zangu, hivi inawezekana katika wakati huo wa Masahaba na Matabiina -Allah awaridhie- kuwa kufunga mikono katika sala hakujulikani katika mji aliokufa ndani yake Mtume wetu (s.a.w) ikiwa kweli ni Sunna ya Mtume wetu (S.A.W)?!! Kisha tendo hilo linafanyiwa kazi Shaam (ambako ndio makazi hasa ya Ahalu Al-kitaabi). Kisha tendo hilo ikaingiwa na utata wa kila rangi katika kuthibiti kwake na namna ya utendaji wake. Hivi inawezekana tendo hilo liwe ni Sunna ya Mtume wetu Muhammad (S.A.W)?!!

Ndugu zangu, sio ajabu kwa Ibadhi kutofunga mikono katika sala; kwa sababu wao wakati huo ndio waliokuwa waislamu wa Oman ambao waliusihi uislamu tokea mwaka wa sita Hijiria kabla ya kufa Mtume wetu (s.a.w) kwa miaka minne, tena kwa hiyari zao, na hawakukubali kuathirika na fitna zilizotokea katika zama hizo, na kwa hiyo walikuwa mbali na athari zake, bali lililo ajabu ni kusemwa etu Ibadhi wanapingana na Sunna ya Mtume (s.a.w) hali ya kuwa uhakikisho unasema kuwa hilo si Sunna ya Mtume (s.a.w) bali ni penyezo la malengo ya kisiasa lenye makusudio ya kuwajuwa ni nani waliokuwa katika safu za Muawiya na wenzake, na nani wako katika asili ya wema waliotangulia (r.a)?.

Tukirudia tena, tunasema kiasili Muislamu anaposimama katika sala huwa hafungi mikono; kwa hiyo kutofunga mikono katika sala hakuhitaji dalili, isipokuwa dalili ya mkusanyo na ujumla, kama vile kuhakikisha unyenyekevu katika sala ambako kunalazimisha kutofanya harakati yoyote ndani yake, kwa hiyo mwenye kuja na tendo la ziada ndiye anayetakiwa athibitishe madai yake.

Na kwa kumalizia kidalili, tunasema kuwa Mtume (s.a.w) amekataza kunyanyua mikono katika Sala katazo la ujumla, kwa hiyo linakusanya kukatazwa kila harakati za kunyanyua mikono katika sala, ikiwa ni kiunyanyua, au kuifunga, au kutikisa kitu katika hiyo mikono kwa kukinyanyua kwa makusudi, ikiwa ni kidole au chenginecho.

Anatuambia Mtume wetu (s.a.w):

“ما لي أراكم رافعي أيديكم كأنها أذناب خيل شمس؟!! اسكنوا في الصلاة”

((Vipi mimi nakuoneni munanyanyua mikono yenu kama kwamba ni mikia ya farasi wakaidi?! Tulizaneni katika sala)) [Muslim 430 Ahmed 20875 Abu Daudi 823]

Kwa hiyo Ibadhi wapo katika kutekeleza fundisho la Mtume (s.a.w) la kutulizana katika Sala, si wakaidi mbele ya kemeo la Mtukufu wa Daraja (S.A.W) ni wenye kutulizana kama alivyotufundisha Mtume (s.a.w), sala yetu haina harakati yoyote ya kuvunja utulivu ndani yake.

Walhamdulillahi.

KWA KUSIKILIZA KWA SAUTI DARSA INAYOHUSIANA NA MADA HII – PLAY HAPO CHINI.

Asante sana.

Wabillahi taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

5. HAKIKA ALLAH HASAMEHE KUSHIRIKISHWA YEYE

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu asiyekuwa na mshirikna na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja na kila aliyeongoka kwa ungofu wake mpaka siku ya Malipo.

TUHUMA.

Imetufikia tuhuma batili inayosema kuwa Ibadhi inapingana na Qur-ani kwa kutokubali Itikadi ya kusamehewa waislamu wenye makosa ambao wamekufa bila ya kutubia; kwa sababu Allah mtukufu amesema kuwa yeye hasamehe dhambi ya kushirikishwa tu na anasamehe madhambi yote yaliyokuwa chini ya ushirikina kama ilivyo katika Qur-ani [Nisaa 48 na 116]; kwa hiyo muislamu hata akifanya madhambi ataendelea kuwa ni mja wa kusamehewa tu; kwa sababu dhambi zake sio za kishirkina, kwa hiyo ima atasamehewa bila ya kuadhibiwa au atasamehewa baada ya kuadhibiwa kwa muda katika moto.

JAWABU:

Kwa hakika Ibadhi ni madhehebu inayokamatana vizuri sana na Qur-ani tukufu, ni mwiko katika Ibadhi kupingana na Qur-ani tukufu, bali ni maarufu katika safu zao kuwa chochote kinachopingana na Qur-ani hicho kitakuwa ni batili na hakitapata nafasi katika safu zao, hili ni maarufu katika safu za Ibadhi.

Ama hukusu Aya tukufu, nazo ni Aya mbili ambazo zimo katika Suuratu Nisaa zinasema:

 1. ((Hakika Allah hasamehe kushirikishwa yeye, na anasamehe yaliyo chini ya hapo kwa anayemtaka, na mwenye kumshirikisha Allah kwa hakika amezua kosa kubwa sana)) [Nisaa 48]
 2. ((Hakika Allah hasamehe kushirikishwa yeye na anasamehe yaliyo chini ya hapo kwa anayemtaka, na mwenye kumshirikisha Allah kwa hakika amepotea upotevu wa mbali sana)) [Nisaa 116]

Hizo ndizo Aya zenyewe ambazo Ibadhi wanatuhumiwa kwenda nazo kinyume, na Aya hizo zote mbili zimeteremka kwa Washirikina kama yalivyo wazi hayo katika sehemu zake ndani ya Msahafu, ya mwanzo ni kwa Washirikina wa Ahalu A-Kitabi, na ya pili ni kwa Washirikina wa Kikuraishi wenye kuabudu Masanamu.

Kwa hali yoyote ile, mazingatio ni mafundisho yaliyomo katika Aya hizo na sio sababu ya kuteremka kwake; kwani walio sababu yake ni baadhi tu ya wakusidiwa.

Tunafahamu sote, kuwa Allah mtukufu anasamehe madhambi yote, anasamehe hata madhambi ya ushirikina kwa mwenye kurejea kwake basi Allah mtukufu anamsamehe, hili halina shaka nalo ni lenye makubaliano ya wote.

Kutokana na hapo, Aya hizi -maana yake katika sehemu yake ya mwanzo- zinatuambia kuwa Allah mtukufu hasamehe dhambi ya kushirikishwa yeye kwa mwenye kuendelea na ushirikina wake.

Na katika hili hakuna kutofautiana ndani yake.

Tukija katika sehemu ya pili ya Aya hizi, nayo ni ile inayosema: ((na anasamehe yaliyo chini ya hapo kwa anayemtaka)) tunapata kuwa wahusika wa madhambi yasiyokuwa ya kishirikina wako makundi mawili nayo ni:

 1. Aliotaka Allah mtukufu kuwasamehe.
 2. Asiotaka Allah mtukufu  kuwasamehe.

Kwa maana hiyo, Aya hizi hazikuiacha hukumu ya kusamehewa kuwaenea wote waliojitosa katika madhambi hayo, bali zimeifunga hukumu hiyo kwa wale ambao Allah mtukufu ametaka kuwasamehe tu; kwa hiyo kutoa hukumu ya kusamehewa waislamu wenye kujitosa katika madhambi makubwa bila kutubia, huko kutakuwa ni kwenda kinyume na mafundisho ya Aya hizi wazi wazi; kwa  kuwepo uwezekano wa kuwemo hao katika asiotaka Allah mtukufu kuwasamehe, basi vipi hawa watu wamefikia kuvunja uwezekano huu bila ya dalili katika Kitabu cha Allah?!! Kisha wanapindukia mipaka kwa kuituhumu Ibadhi eti inakwenda kinyume na Qur-ani tukufu, hali ya kuwa Ibadhi kwa kushikamana vizuri na kitabu cha Allah mtukufu imekwenda kinyume na matamano hewa yaliyowazonga hao.

Tunafahamu sote, kuwa Allah mtukufu kwa fadhila zake na rehma zake huwasamehe washirikina wenye kuingia katika uislamu; kwani ushirkina wao pamoja na madhambi yao mengine waliyoyafanya katika hali ya ushirkina wao yote hayo husamehewa kwao pale wanapoingia katika Uislamu, na kuanzia hapo -waislamu hao wapya- huanza sahifa zao mpya, na Allah mtukufu ametuambia kwenye kitabu chake ((Yule ambaye Allah ametaka kumuongoa hukifungua kifua chake kwa ajili ya Uislamu)) [Anaam 125].

Kutokana na hapo inadhihiri maana ya kwanza ya Aya hizi tukufu, kuwa Aya hizi zinawahusu Washirikina peke yao; kwani sehemu ya pili ya Aya hizo itakuwa maana yake ((na (Allah mtukufu) anasamehe yaliyo chini ya ushirkina katika madhambi kwa anayemtaka kumuongoa kwa Uislamu miongoni mwao hao  Washirikina)) kwani hakika kusilimu kwake ni kusamehewa ushirikina wake na yaliyo chini ya ushirkina katika madhambi yake.

Hiyo ni maana ya kwanza inayokubaliana na mafundisho ya Aya hizo tukufu, nayo ni maana mahususi kwa Washirkina tu; kwa hiyo -maana hiyo- haihusiani na Waislamu waasi wasiotubia.

Sasa tuje katika maana ya pili ya Aya hizi tukufu, nayo ni maana ya mkusanyo, kwa maana ((anasamehe madhambi yaliyo chini ya ushirkina kwa anayemtaka)).

Suala linakuja, ni nani hao wenye madhambi yaliyo chini ya ushirkina ambao Allah mtukufu ametaka kuwasamehe? Na nani ambao Allah mtukufu hakutaka kuwasamehe miongoni mwao?

Huenda mtu akasema: Sasa huko ni kumuingilia Allah katika maamuzi yake, si tuwache tu yeye mwenyewe ndiye ataamua.

Tunamjibu: Sisi hatuna mamlaka ya kuingilia matakwa ya Allah, lakini inatulazimu kusadikisha matakwa yake katika aliyohukumu, kwa hiyo sisi ni wenye kusadikisha aliyotaka na kuyaamua katika hukumu zake kwa mujibu wa alivyotueleza, na hili ni wajibu kwetu.

Tukifahamu hilo, tunasema kuwa Allah mtukufu kwa hekima yake ametueleza Itikadi potofu zilizowavaa waliopita kabla yetu hususan Ahalu Al-Kitabi (Mayahudi na Manasara), na kuzieleza Itikadi hizo potofu ni ishara wazi ya kutuhadharisha sisi yasije yakatupata maradhi ya upofu wa kiitikadi yaliyowapata wao hao, na hili lina dalili tosha ya kuwa haiwezekani kuthibitishwa katika Uislamu aibu za uma zilizopita ambazo zimefedheheshwa na Qur-ani tukufu.

Tukumbuke kuwa hawa wenye kuituhumu Ibadhi kwa tuhuma hii, wao wamefanya hivo kwa kutetea Itikadi zao ambazo hazina mashiko katika Kitabu cha Allah mtukufu, itikadi hizo zinasema kuwa Muislamu hata afanye madhambi namna gani -na asitubie- basi yeye atasamehewa tu, kwa hiyo ataingia Peponi bila ya kuadhibiwa, na kama ataadhibiwa basi adhabu yake ni ya muda tu si yenye kuendelea milele, kwa hiyo atatolewa Motoni na kuingia Peponi baada ya hapo.

Allah mtukufu ametuambia kwenye Kitabu chake kitukufu:

((Na walifuatia baada yao KIZAZI KIBAYA WALIORITHI KITABU, WAKASHIKA ANASA ZA HAYA MAISHA DUNI NA WAKASEMA: “TUTASAMEHEWA SISI!”. NA IKIWAJIA TENA ANASA KAMA HIYO WATAISHIKA PIA)). [Aaraaf 169]

Hapa tunaona wazi wazi asili ya Itikadi hiyo ya kusamehewa tu, na kuwa hiyo ni Itikadi batili iliyonasibishwa na Kizazi kibaya kilichorithi Kitabu cha Allah bila ya kuongozeka kwacho, basi vipi Itikadi hiyo hiyo ya Kizazi kibaya kwa mujibu wa Qur-ani iwe ndio Itikadi ya Qur-ani tukufu?!!!

Kisha Allah mtukufu akatueleza kwenye Kitabu chake kitukufu:

((Hayo ni kwa sababu wao wamesema: Hautatugusa moto isipokuwa siku chache. Na yakawadanganya katika dini yao hayo waliyokuwa wameyazua)) [Aala Imraan 24]

Hapa tunaona asili ya Itikadi hiyo ya kuadhibiwa kwa muda, na kuwa Itikadi hiyo ni batili iliyonasibishwa na uongo uliozuliwa na kuchomekwa katika dini ya wabatilifu, na kuwa uongo huo ni wenye kupelekea katika kudanganyika katika dini.

Na bila shaka, Mja akiitakidi kuwa yeye hata akifanya maasi namna gani -hata kama hatotubia- basi mafanikio ni yake tu 100%, mja huyo atakuwa ni mwepesi wa kuingia katika wimbi la kumuasi Allah mtukufu tena bila ya kujali.

Sasa tukirudia tena katika Qur-ani tukufu, tunakutia kuwa Allah mtukufu amehukumu kwa wenye kumuasi yeye na Mtume wake kuwa hao watapata adhabu ya Jahannamu humo watabakia mielele anatuambia Allah mtukufu:

((Isipokuwa ufikishaji kutoka kwa Allah na risala zake. Na yoyote mwenye kumuasi Allah na Mtume wake kwa hakika huyo atapata Moto wa Jahannamu watabakia humo milele)) [Jinni 23]

Tunafahamu sote kuwa Allah mtukufu -kwa fadhila zake- anakubali toba za wenye kutubia kwake; kwa maana hiyo, Aya hii iko wazi kuwa hukumu hiyo ndiyo aliyoitaka Allah mtukufu kwa yoyote mwenye kumasi yeye na Mtume wake kisha hakutubia kabla ya kufa kwake. 

Amesema Allah mtukufu:

((Na hakuna usamehevu kwa wale wanaofanya maovu mpaka yanapomfikia mmoja wao mauti husema: “Mimi natubia hivi sasa”. wala kwa wale wanaokufa hali ya kuwa wao ni Makafiri. Hao tumewaandalia adhabu yenye kuumiza sana)) [Nisaa 18]

Kwa maana hiyo, ni wazi kabisa kuwa Allah mtukufu ametaka kuwasamehe wale wote waliotubia kwake kabla ya kufikiwa na mauti, na kuwa yeye hakutaka kuwasamehe wale wote walio wakaidi wa kutubia kwake mpaka wakafikiwa na mauti, hili liko wazi kabisa.

Na Allah mtukufu anatumbia kwenye Kitabu chake:

((Ikiwa mutajiepusha na makubwa muliokatazwa tutakufichieni (tutakusameheni bila kufikwa na fedheha yoyote) makosa yenu na tutakuingizeni maingizo ya kukirimiwa)) [Nisaa 31].

Tunajuwa sote -bila shaka yoyote- kuwa Allah mtukufu amekataza kuasiwa yeye katika amri zake kama alivyokataza kutendwa makatazo yake.

Basi Aya hii iko wazi, kuwa wasiojiepusha na madhambi makubwa hao ni wenye kuchukuliwa na mawimbi ya madhambi yao yote, makubwa na madogo, na yatawazonga maovu yao siku ya Kiama, na wao hao hawatosamehewa wala kusitiriwa kwa maovu yao waliyoyafanyia ukaidi wa kutubia kwa Mola wao.

Allah mtukufu atuepushe kuwa miongoni mwao waovu hao na atupe taufiki yake katika mema na kutubia kwake kabla ya kufikiwa na mauti. (Ameen).

Wabillahi Taufiiq. 

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

6. TUHUMA YA KUKAFIRISHA MTUME (S.A.W)
بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliye mkwasi asiyefanana na chochote asiyedirikiwa kwa macho, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Ama baada ya hayo.

Tumepokea tuhuma batili iliyotolewa na mmoja wa maduaati wa kisalafi (wahabi), akiwatuhumu Maibadhi kwa kudai kuwa: “Ibadhi wanakufurisha hadi Mtume (s.a.w); kwa sababu imekuja katika kitabu chao kinachoitwa Qaamuus Shariia: ((Na hili -yaani la kuonekana Allah- kwetu sisi ni katika ukafiri mkubwa wa kumkufuru Allah mwingi wa rehema, na kwa Nabii ni katika uzushi mkubwa kabisa aliozuliwa, na lau kuwa atayasema hayo Nabii yoyote miongoni mwa Manabii basi tungelishuhudia ya kuwa yeye amemkufuru Allah mwingi wa fadhila, tena amekuwa mlaaniwa ni miongoni mwa ndugu wa Shetani)), na Sheikh huyo wa Kiibadhi alikua akizungumzia suala la kutoonekana Allah mtukufu na hali ya kuwa Mtume (s.a.w) amesema kuwa tutamuona Allah mtukufu; kwa hiyo Mtume (s.a.w) kwa mujibu wa Itikadi yake huyu Sheikh wa Kiibadhi atakuwa ni mwenye kulaaniwa tena ni katika ndugu wa Shetani” Astaghfirullah. Mwisho wa kunakili tuhuma ya huyu Msalafi, Allah amuongoe.

JAWABU:
Imekuja katika Kitabu Qaamus Shariia juzuu ya 5 ukurasa 399-405 cha Sheikh Jumayyil bin Khamis A-Saadi (r.a) chini ya Anuani hii:

فصل: ومن سيرة الشيخ العالم ناصر بن أبي نبهان الخروصي إلى من سأله مترجما عن لسان النصارى

((Kituo: Na katika sera ya Sheikh Mwanachuoni Naasir bin Abi Nabhani Al-Kharousi kwa aliyemuuliza kwa kutarujumiwa kutoka katika lugha ya Manasara.))

Sera ya Mwanachuoni, kusudio lake ni barua yenye kufafanua suala la kielimu lililoingiwa na utata ndani yake, sasa ndani ya sera hii ndiyo yaliyokuja hayo maneno aliyoyakata huyo Msalafi (Muwahabi) mwenye kutunga hiyo tuhuma batili dhidi ya Ibadhi.
Sheikh Naasir bin Abi Nabhan Al-Kharousi (r.a), ni mmoja wa wanaelimu wetu Wakubwa walioishi Zanzibar – Mtoni, naye alifariki mwaka 1263 Hijiria sawa na mwaka 1847 Miladi.
Anuani ya barua yake hiyo (Sera) inaonyesha wazi, kuwa hilo lilikuwa ni uchambuzi wa jawabu yake aliyomjibu mmoja wa Wakiristo (Manasara) kuhusiana na suali lake ambalo kiasili lilikuwa ni kwa lugha ya Kiengereza (Engilsh).
Sasa Mawahabi -kama kawaida yao- wanakusudia mtindo wa kuharibu maandiko na kuyapotosha kwa namna yoyote ile ilimradi wapate njia ya kunusuru batili yao au kumvunja aliyetafautiana nao, na hilo ndilo lililofanyika katika uundaji wa tuhuma hiyo batili. Na uhakiki wa haya tunayoyasema uko wazi kabisa ndani ya tuhuma hiyo batili anayaona kila mwenye kuzingatia.

Basi tunamuambia huyu Msalafi (Muwahabi): Kwani kuna ubaya gani katika hayo aliyoyasema Sheikh wetu Imam Naasir Al-Kharousi (r.a)? Hivi hujui kua:-

Maibadhi tunamtakasa Allah mtukufu na uwezekano wa kuonekana na kiumbe chake chochote kama tunavyomtakasa na uwezekano wa kuwa na mshirika au kufanana na kiumbe chake chochote, na kwa maana hiyo, kama ilivyokuwa ni haki kwetu kusema: “Lau kuwa Nabii atakuja na kutuambia kuwa yeye ni Mungu mweza (Mshirika) pamoja na Allah mtukufu itakuwa ni haki kwetu kushuhudia ukafiri wake Nabii huyo, na kulaaniwa kwake, na kuwa Nabii huyo atakuwa ni ndugu wa Sheitani” basi vile vile ni haki kulisema hilo hilo katika maudhui ya kuonekana Allah mtukufu kama alivyolisema Sheikh Naasir Al-Kharousi (r.a).
Lugha hiyo -kama inavyoonekana- ni lugha ya makadirio ya kutokea yalisokua na uwezekano wa kutokea kwake kwa mujibu wa Itikadi ya msemaji, nao ni mtindo maarufu wa kuhakikisha ubatilifu wa jambo kwa kuzingatia asili ya lile jambo lenyewe bila kuzingatia msemaji wake, imekuja katika Qur-ani tukufu ((Na yoyote miongoni mwao (Malaika) atakayesema: Hakika mimi ni mungu pasina yeye (Allah mtukufu), basi huyo tutamlipa Jahannamu, na namna hivo tunawalipa Madhalimu)) [Anbiyaa 29]. Kama ilvyokuwa kudai Uungu ni jambo batili hata kama atalisema Malaika miongoni mwa Mlaika -nao wametakasika na kulesema hilo- basi pia kudai itikadi ya kuonekana Allah mtukufu ni jambo batili hata kama atalisema Nabii miongoni mwa Manabii -nao wametakasika na kulisema hilo-. Hili ndilo alilolikusudia Sheikh wetu (r.a).
Huyo Muwahabi mbona anashindwa kutoa maelezo kamili ya Sheikh wetu Naasir bin Abi Nabhaan Al-Kharousi (r.a)? Amesema: ((Na miongoni mwa makubwa tusiyokubaliana na wao ndani yake, na ubainisho wa hayo umo katika vitabu vyao, ni kuwa, wao wameitakidi katika itikadi yao kuwa Nabii (s.a.w) aliiona Dhati ya Mola wake kwa muangalio wa jicho katika hii Dunia, na kuwa yeye alipandishwa kwake mpaka akawa karibu na yeye hasa (kimasafa), na kuwa hilo ni peo maalumu la kukirimiwa alilohusishwa nalo katika hii Dunia, ama siku ya Kiama, ni kuwa wao wote wataiangalia Dhati ya Allah mtukufu, vile vile na ndani ya Pepo, na kuwa yeye atawashukia wao au atawatokezea wao katika kila Ijumaa inayowazunguka ndani ya Pepo, basi wote waliomo katika Pepo watakwenda katika maono ya kumuona yeye, na mimi sijui hasa kuwa wao wamekusudia ni sehemu mahususi katika hiyo Pepo, au kila mmoja atamuona hali ya kuwa yupo katika sehemu yake mfano wa jua watu wanaliona katika ardhi nalo liko mbinguni?!!!!. Na hili -la kueleza kuonekana Allah kwa namna hiyo- kwetu sisi ni katika ukafiri mkubwa wa kumkufuru Allah mwingi wa rehema, na kwa Nabii ni katika uzushi mkubwa kabisa aliozuliwa, na lau kuwa atayasema hayo Nabii yoyote miongoni mwa Manabii, basi tungelishuhudia ya kuwa yeye amemkufuru Allah mwingi wa fadhila, tena amekuwa mlaaniwa ni miongoni mwa ndugu wa Shetani, lakini haiwezekani kabisa kabisa kuwa Manabii wa Allah wapotee, na amesema Allah mtukufu ((Allah anajua zaidi wapi auweke ujumbe wake)) [Anaam 142]. Na sisi tunashuhudia kuwa Allah ni kitu na haki, na kuwa dhati yake haionekani wala hawezi kuiona kiumbe yoyote; kwani yeye sio kitu cha kuonekana, na haiwezekani kufanyika kitu kimuone yeye kama ilivyokuwa haiwezekani kufanyika kitu kikawa mafano na yeye…)).
Madai ya kusema kuwa Mtume wetu (s.a.w) amesema kuwa Allah ataonekna siku ya kiama ni madai batili kwa mujibu wa Itikadi yetu sisi Maibadhi, na hayo yako wazi katika meneno ya Sheikh Naasir Al-Kharousi (r.a) aliposema: ((Na hili -la kueleza kuonekana Allah kwa namna hiyo- kwetu sisi ni katika ukafiri mkubwa wa kumkufuru Allah mwingi wa rehema, na kwa Nabii ni katika uzushi mkubwa kabisa aliozuliwa)) kisha akasema: ((lakini haiwezekani kabisa kabisa kuwa Manabii wa Allah wapotee)).
Tunamuambia huyu Muwahabi kuwa tuhuma yako hiyo ingalikuwa ni tuhuma sahihi lau kuwa Sheikh Naasir Al-Kharousi (r.a) anakubali kuwa Mtume (s.a.w) ameyasema hayo munayoitakidi nyinyi kuwa kayasema, lakini Sheikh (r.a) ni mwenye kumtakasa Mtume (s.a.w) na uongo huo iliomo katika riwaya hizo batili zenye kutoa taswira ya kuwa Allah ni kiwiwili kama mtu, tena anajigeuza na kujibadilsha badilisha kimaumbile kiasi cha kushindwa kujilikana na waumini wake atakapowajia na kumona hata watafikia kujikinga na Allah mtukufu kutokana na yeye mwenyewe kwa sababu ya ubaya wa sura yake atakayowajia kwayo siku ya kiama kama yalivyo hayo katika sahihi bukhari na sahihi muslim na vitabu vyengine vya Hadithi.

Kwa maelezo kuhusu riwaya hizo batili za uongo wa wazi rejea kiunganishi hapo chini.

.

Wabillahi Taufiq.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

7. TUHUMA YA KUADHIBIWA WATU MOTONI MILELE
﴿بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliye mwingi wa rehma na mkali wa kuadhibu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad alikuongozwa na mola wake wa Qur-ani tukufu iliyobarikiwa na kujaaliwa kuwa uongofu wa wachamungu mpaka kitasimama kiama, pia Allah mtukufu awape na rehma na amani hizo waja wake wema wote walioongoka kwa uongofu wa Mtume wake Muhammad mpaka siku ya malipo.

Amaa baada ya hayo:

Kwa hakika imetufikia tuhuma iliyokuja kwa njia ya ulizo inayosema: (mbona kiibadhi munafutu watu wataingia motoni milele, wakati kwa madhehebu menginge wale wenye chembe za imani in shaallah watatoka?)

JAWABU YA TUHUMA HII NI KAMA IFUATAVYO:

Kwanza: Tufahamu kuwa Ibadhi hatufutu kuingia watu motoni milele kama ilivyokuja katika suali, hio sio kweli.

Ibadhi itikadi yetu ni kubakia waovu -peke yao- katika moto milele; kwa maana hiyo, tunaitakidi kuwa moto ni nyumba ya kuadhibiwa waovu tu milele.

Pili: Tukiichunguza itikadi ya kuadhibiwa kwa muda huko akhera tunakutia kuwa:

Ni itikadi isiyo na utajo wa kuthibitishwa katika Qur-ani tukufu, kwa hiyo hakuna katika Qur-ani tukufu bishara yoyote ya kumalizika adhabu kwa yoyote yule atakayeadhibiwa motoni.
Ni itikadi potofu kwa mujibu wa Qur-ani tukufu; kwani imetajwa kuwa ni uzushi uliopenyezwa katika dini uliofanywa na waliopita kabla yetu (Ahalu Al-Kitaabi).
Ni Itikadi inayopelekea kutoheshimu Kitabu cha Allah mtukufu.
Ibadhi ni madhehebu inayojishika vizuri na Qur-ani tukufu, na katika misingi yake madhubuti ni kutozingatia pokezi lolote la hadithi iwapo litapingana na Qur-ani tukufu na kulihukumu pokezi hilo kuwa ni uzushi aliobandikwa nao Mtume (s.a.w); kwa hiyo riwaya zilizokuja kupitia wapokezi wa madhehebu mengine ambazo ndio tegemeo lao katika kuitakidi itikadi ya kuadhibiwa kwa muda motoni iwapo wataadhibiwa humo kama wanavyoitakidi, riwaya hizo ni batili kwetu sisi na uongo alozuliwa Mtume wetu Muhammad (s.a.w), na kuwa riwaya hizo asili yake ni upotevu wa Ahalu Al-Kitabi wenye lengo la kupandikiza katika umma huu na kuuambukiza maradhi yao ya kiitikadi, na Qur-ani tukufu inatuambia kuhusu Ahalu Al-Kitabi:

﴿وَدَّ كَثِيرٌ مِنْ أَهْلِ الْكِتَابِ لَوْ يَرُدُّونَكُمْ مِنْ بَعْدِ إِيمَانِكُمْ كُفَّارًا حَسَدًا مِنْ عِنْدِ أَنْفُسِهِمْ مِنْ بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُمُ الْحَقُّ فَاعْفُوا وَاصْفَحُوا حَتَّى يَأْتِيَ اللَّهُ بِأَمْرِهِ إِنَّ اللَّهَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾.

1. ((Wanatamani wengi katika Ahalu Al-Kitabi (Mayahudi na Manasara) lau watakurejesheni baada ya kuamini kwenu muwe makafiri, ni hasadi kutoka ndani ya nafsi zao baada ya kuwabainikia wao haki..)) [Baqarah 109].

﴿وَلَنْ تَرْضَى عَنْكَ الْيَهُودُ وَلَا النَّصَارَى حَتَّى تَتَّبِعَ مِلَّتَهُمْ قُلْ إِنَّ هُدَى اللَّهِ هُوَ الْهُدَى وَلَئِنِ اتَّبَعْتَ أَهْوَاءَهُمْ بَعْدَ الَّذِي جَاءَكَ مِنَ الْعِلْمِ مَا لَكَ مِنَ اللَّهِ مِنْ وَلِيٍّ وَلَا نَصِيرٍ﴾.

2. ((Na hawatoridhika na wewe Mayahudi na Manasara mpaka ufuate mila yao. Sema uongofu wa Allah ndio uongofu, na ikiwa utafuata mapendwamoyo yao baada ya yale yaliyokujia katika elimu hutapata wewe kutoka Allah kipenzi yoyote wala muokoaji wowote)) [Baqarah 120]

Aya hizi zinatupa ishara nzito za wazi na safi vipi juhudi za Mayahudi na Manasara dhidi ya Uislamu zilivyoanza mapema sana, kutokana na hapo tunapata kujua hekima ya kutajwa sana mambo yao ndani ya Qur-ani na kufedheheshwa mapotofu yao.

Allah mtukufu anatuambia kuhusu Itikadi ya kuadhibiwa kwa muda na kusamehewa bila ya kutubia kuwa ni itikadi potofu walizozizua Ahalu Al-Kitabi.

﴿فَخَلَفَ مِنْ بَعْدِهِمْ خَلْفٌ وَرِثُوا الْكِتَابَ يَأْخُذُونَ عَرَضَ هَذَا الْأَدْنَى وَيَقُولُونَ سَيُغْفَرُ لَنَا وَإِنْ يَأْتِهِمْ عَرَضٌ مِثْلُهُ يَأْخُذُوهُ أَلَمْ يُؤْخَذْ عَلَيْهِمْ مِيثَاقُ الْكِتَابِ أَنْ لَا يَقُولُوا عَلَى اللَّهِ إِلَّا الْحَقَّ وَدَرَسُوا مَا فِيهِ وَالدَّارُ الْآخِرَةُ خَيْرٌ لِلَّذِينَ يَتَّقُونَ أَفَلَا تَعْقِلُونَ﴾.

((Basi walifuatia baada yao waliofuatia, walirithi kitabu wakawa wanachukua pato hili la chini na wanasema tutasamehewa tu sisi, na likiwajia pato mfano wake watalichukua, hivi halikuchukuliwa kwao agano la kitabu ya kuwa wasije wakamsemea Allah isipokuwa haki tu na wakasoma yaliyomo ndani yake?!! Na nyumba ya Akhera ni bora ni kwa wenye kumchaAllah, hivi hamuzingatii?!!)) [Aaraf 169].
﴿وَمِنْهُمْ أُمِّيُّونَ لَا يَعْلَمُونَ الْكِتَابَ إِلَّا أَمَانِيَّ وَإِنْ هُمْ إِلَّا يَظُنُّونَ﴾﴿فَوَيْلٌ لِلَّذِينَ يَكْتُبُونَ الْكِتَابَ بِأَيْدِيهِمْ ثُمَّ يَقُولُونَ هَذَا مِنْ عِنْدِ اللَّهِ لِيَشْتَرُوا بِهِ ثَمَنًا قَلِيلًا فَوَيْلٌ لَهُمْ مِمَّا كَتَبَتْ أَيْدِيهِمْ وَوَيْلٌ لَهُمْ مِمَّا يَكْسِبُونَ﴾﴿وَقَالُوا لَنْ تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَعْدُودَةً قُلْ أَتَّخَذْتُمْ عِنْدَ اللَّهِ عَهْدًا فَلَنْ يُخْلِفَ اللَّهُ عَهْدَهُ أَمْ تَقُولُونَ عَلَى اللَّهِ مَا لَا تَعْلَمُونَ﴾﴿بَلَى مَنْ كَسَبَ سَيِّئَةً وَأَحَاطَتْ بِهِ خَطِيئَتُهُ فَأُولَئِكَ أَصْحَابُ النَّارِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾﴿وَالَّذِينَ آمَنُوا وَعَمِلُوا الصَّالِحَاتِ أُولَئِكَ أَصْحَابُ الْجَنَّةِ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ﴾.

2. ((Na miongoni mwao si wenye kusoma, hawajui Kitabu isipokuwa matarajiohewa, na hawakuwa wao isipokuwa ni kudhania tu * Basi ole wao wale wanaoandika Kitabu kwa mikono yao kisha wanasema: “haya yanatoka kwa Allah” ili wajinunulie kwayo thamani ndogo, basi ole wao kwa hayo iliyoyaandika mikono yao, na ole wao kwa hayo wanayoyachuma * na wamesema: Hautatugusa sisi moto isipokuwa siku chache (Adhabu ya muda). Sema: Hivi mumechukuwa ahadi kwa Allah basi hatokwenda kinyume na ahadi yake, au munamsemea Allah mambo musiyoyajua?!! * naam yoyote atakayechuma ubaya wowote na akazungukwa na kosa lake, basi hao ndio watu wa motoni humo wao watabakia * na wale walioamini na wakatenda mema hao ni watu wa peponi humo wao watabakia)) [Baqarah 78-82].

﴿أَلَمْ تَرَ إِلَى الَّذِينَ أُوتُوا نَصِيبًا مِنَ الْكِتَابِ يُدْعَوْنَ إِلَى كِتَابِ اللَّهِ لِيَحْكُمَ بَيْنَهُمْ ثُمَّ يَتَوَلَّى فَرِيقٌ مِنْهُمْ وَهُمْ مُعْرِضُونَ﴾﴿ذَلِكَ بِأَنَّهُمْ قَالُوا لَنْ تَمَسَّنَا النَّارُ إِلَّا أَيَّامًا مَعْدُودَاتٍ وَغَرَّهُمْ فِي دِينِهِمْ مَا كَانُوا يَفْتَرُونَ﴾.

3. ((Hivi hujawaona wale waliopewa sehemu ya Kitabu wanaitwa kwenye Kitabu cha Allah ili kihukumu baina yao kisha hukataa kundi miongoni mwao na wao ni wenye kukengeuka * hayo ni kwa sababu wao wamesema: Hauotatugusa sisi moto isipokuwa siku chake (adhabu ya muda), na yakawahadaa wao katika dini yao yale waliyokuwa wakiyazusha)) [Aala Imraan 23-24].

Aya hizo zinatupa uwazi wa upotefu wa itikadi iliyozungumzwa ndani yake kuwa ni itikadi potefu na mbovu, nazo ziko wazi kuwa wao waliitakidi kuwa hata wakimuasi Allah mtukufu basi watasamehewa tu madhambi yao hata kama hawakutubia, na ikiwa wataadhibiwa basi adhabu yao ni ya muda kwa siku chache tu, bila shaka haya ni maradhi mabaya sana, na sote tunajua hata kama wagonjwa ni tofauti lakini maradhi yao ni yale yale. Na haiwezekani kuwa Allah mtukufu abainishe itikadi potofu na aiseme kuwa ni uzushi katika dini kisha itikadi hiyo hiyo iwe ndiyo itikadi ya haki katika dini yake; kwani haiwezekani kuitia aibu haki na kuisema kuwa ni upotofu, huko kutakuwa ni kuwalengea watu aibu inayokubalika kwa mlengaji kuwa ni haki isiyo aibu.

Hakika sisi Ibadhi huwa tunawashangaa sana wale wanye kuitakidi kuwa kuna watu watakaoadhibiwa adhabu ya muda katika moto kisha watatolewa humo na kuingizwa katika pepo, tunawashangaa; kwani tunapowauliza: watu hao ni watu gani? Hapo hutujibu kuwa: watu hao ni waumini waliokufa hali ya kuwa wamejitosa katika madhambi makubwa yasiyokuwa ya kishirikina kisha hawakutubia kwayo.

Hivi hawa wenye kuyitakidi itikadi hiyo wamepata wapi kuwa muumini ataadhibiwa motoni?!!

Allah kwenye kitabu chake anatuambia wazi wazi kupitia waja wake wema:

﴿رَبَّنَا إِنَّكَ مَنْ تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنْصَارٍ﴾.

((Ewe Mola wetu, hakika yule utakayemtia motoni huyo kwa hakika umemdhalilisha, na hawana madhalimu (yoyote) wa kuwanusuru)) [Aala Imraan 192] wakati huo huo Allah mtukufu anatuambia kuwa siku ya kiama hatowadhalilisha waumini aslan:

﴿يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا تُوبُوا إِلَى اللَّهِ تَوْبَةً نَصُوحًا عَسَى رَبُّكُمْ أَنْ يُكَفِّرَ عَنْكُمْ سَيِّئَاتِكُمْ وَيُدْخِلَكُمْ جَنَّاتٍ تَجْرِي مِنْ تَحْتِهَا الْأَنْهَارُ يَوْمَ لَا يُخْزِي اللَّهُ النَّبِيَّ وَالَّذِينَ آمَنُوا مَعَهُ نُورُهُمْ يَسْعَى بَيْنَ أَيْدِيهِمْ وَبِأَيْمَانِهِمْ يَقُولُونَ رَبَّنَا أَتْمِمْ لَنَا نُورَنَا وَاغْفِرْ لَنَا إِنَّكَ عَلَى كُلِّ شَيْءٍ قَدِيرٌ﴾

((Enyi mulioamini tubieni kwa Allah toba ya kweli ili Mola wenu akufichinei makosa yenu na akuingizeni katika pepo inayopita chini yake mito katika siku ambayo Allah hatowadhalilisha Nabii na wale walioamini pamoja naye, nuru yao itatembea mbale yao na kuliani mwao watasema: Mola wetu tutimizie sisi nuru yetu na utusamehe sisi; hakika wewe juu ya kila kitu ni muweza)) [Tahriim 8].

Kwa hiyo Ibadhi hatuitakidi aslan kuwa kuna muumini atadhalilishwa kwa kuingizwa katika Moto siku ya kiama; kwa hiyo suala la kuwemo muumini yoyote katika udhalilifu wa kuadhibiwa katika moto ni suala batili kwa mujibu wa Itikadi yetu tuliyoichukua katika Qur-ani ambayo ni uongofu kwa wachamungu.

Basi sisi Ibadhi tunaitaikidi kuwa moto ni nyumba ya makafiri tu peke yao kama alivyotuambia Allah mtukufu kwenye kitabu chake:

﴿ النَّارُ وَعَدَهَا اللَّهُ الَّذِينَ كَفَرُوا ﴾

((Moto amewaandila Allah wale waliokufuru)) [Hajj 72] kwa hiyo haingii humo isipokuwa kafiri tu, ama muumini yeye hatoguswa na moto wa akhera aslan, wala hatofikwa na huzuni yoyote huko,

﴿وَيُنَجِّي اللَّهُ الَّذِينَ اتَّقَوْا بِمَفَازَتِهِمْ لَا يَمَسُّهُمُ السُّوءُ وَلَا هُمْ يَحْزَنُونَ﴾.

((Na atawaokoa Allah wale waliomcha kwa kufaulu kwao, hapana baya litakalowagusa wao, na wao hawatahuzunika)) [Zumar 61]

Kwa hiyo mwenye kusema kuwa waumini wataguswa na moto au watafikwa na huzuni siku ya kiama huyo amesema kinyume na Qur-ani, sisi Ibadhi hatuna haja na neno lake huyo, na tunamtakasa Mtume wa Allah (s.a.w) na uwezekano wa kusema kinyume na Qur-ani.

Tufahamu kuwa Ibadhi tunaitakidi kuwa sababu ya kuadhibiwa motoni ni ukafiri tu, na kila dhambi kubwa ni ukafiri; kwa hiyo:

Yoyote atakayekuwemo katika mwenendo wa Maluuni Ibilis wa kufanya kiburi mbele ya kutubia kwa dhambi yake yoyote, huyo atakuwa pamoja naye katika Jahannam milele.
Na yoyote atakayekuwemo katika mwenendo wa Baba yetu Mrehemewa Adam wa kurejea na kutubia kwa Allah mtukufu kwa dhambi aliyoteleza huyo atakuwa pamoja naye katika Pepo milele.
Na sisi Ibadhi hatuna itikadi ya kuwa ukafiri ni ushirikina tu kama wanavyoitakidi Khawariji na Masunni, bali Itikadi yetu ni kuwa ukafiri na ufasiki na udhalimu na uovu majina yote hayo yanamaanisha madhambi makubwa yote, kwa hiyo Ushirkina ni ukafiri kwa sababu ni dhambi kubwa, kwa maana hiyo:

Kila dhambi ya ushirikina ni ukafiri.
Si kila dhambi ya ukafiri ni ushirikina.
Na ifahamike kuwa Itikadi yetu katika hili ni kwa njia ya kusadikisha aliyotuambia Allah mtukufu; kwani hakuna mkweli zaidi kuliko yeye, basi aliyotuambia katika kitabu chake bila shaka ndiyo aliyoyataka kwa waja wake; kwa hiyo neno la kusema: “Allah akitaka kuwatoa katika moto atawatoa na kuwaingiza katoka Pepo”, ni sawa sawa na kusema: “Allah akitaka kuwatoa waja wema katika Pepo awatoa na kuwaingiza katika Moto”. Basi ifahamike kuwa sisi tunasadikisha aliyoyataka Allah mtukufu kwa waja wake kwa mujibu wa andiko lake.

Wabillahi taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

8. TUHUMA YA KUNASIBISHWA IBADHI NA DHUL-KHUWEISWIRA (DHU THUDAYYAH) - 1

بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliyetuamrisha kuhakikisha ukweli na remha na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja na Aali zake na Masahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Ama baada ya hayo:

Imetufikia tuhuma batili yenye kusema kuwa Muasisi wa mwanzo wa Uibadhi ni Dhu Al-Khuweswirah (l.a) katika vita vya Hunain kama ilivyokuja katika Sahihi kuwa Mtu huyo wakati Mtume (s.a.w) alipokuwa anagawa ngawira alimfuata Mtume (s.a.w) na kumwambia: ((Muhammad hufanyi uadilifu, fanya uadilifu)) Mtume (s.a.w) akamwambia: ((Hakika umengamia ikiwa mimi sifanyi uadilifu basi nani mwengine atafanya uadilifu?)) Masahaba wakataka kumpiga, Mtume (s.a.w) Akawambia: ((Muacheni kwani hakika asili kizazi cha mtu huyu watatoka Khawariji hao ni mbwa wa watu wa motoni)).

JAWABU:

Kwanza:

Sisi hatukatai kuja kwa mapokezi yanayozungumzia Makhawariji, na miongoni mwa mapokezi hayo ni yale aliyoyapokea Imam Rabii bin Habib (r.a) katika Musnad.

Abu Ubaydah, kutoka kwa Jaabir bin Zayd, kutoka kwa Abu Sa`id L-Khudriy (R.A.A.), kasema, “Nimemsikia Mjumbe wa Allah (S.A.W.) akisema, “

«يَخْرُجُ فِيكُمْ قَوْمٌ تَحْقِرُونَ صَلاَتَكُمْ مَعَ صَلاَتِهِمْ، وَصِيَامَكُمْ مَعَ صِيَامِهِمْ، وَأَعْمَالَكُمْ مَعَ أَعْمَالِهِمْ، يَقْرَؤُونَ الْقُرْآنَ وَلاَ يُجَاوِزُ حَنَاجِرَهُمْ، يَمْرُقُونَ مِنَ الدِّينِ كَمَا يَمْرُقُ السَّهْمُ مِنَ الرَّمِيَّةِ، تَنْظُرُ فِي النَّصْلِ فَلاَ تَرَى شَيْئًا؛ ثُمَّ تَنْظُرُ فِي الْقِدْحِ فَلاَ تَرَى شَيْئًا؛ ثُمَّ تَنْظُرُ فِي الرِّيشِ فَلاَ تَرَى شَيْئًا، وَتَتَمَارَى فِي الفُوقِ».

Maana yake, “Watatoka watu miongoni mwenu mtazidharau Sala zenu, juu ya Sala zao, na funga zenu, juu ya funga zao, na vitendo vyenu (vyema) juu ya matendo yao, wanasoma Qur`ani lakini haivuuki koo zao (haifiki Qur`ani katika mioyo yao). Wanatoka katika dini mfano wa mshale unavyochopoka kwenye kiwindwa, ukikiangalia chuma cha mshale huoni kitu, kisha ukiuangalia ufito wa mshale huoni kitu, tena ukiangalia manyoya yanayofungwa katika kichwa cha mshale huoni kitu, utabakia unatia shaka, huna uhakika endapo kichwa cha mshale kimekazika vyema, au namna gani, ili muradi huna uhakika”. [Rabii 36]

Kwa maana hiyo Makhawariji waliokusudiwa katika hadithi hii -bila shaka- ni watu waovu na wapotofu, hili halina shaka yoyote ile, na kwa upande wetu Ibadhi tunajitenga na Makhawariji wote wa aina hiyo.

Na sisi tunaporejea katika mapokezi yaliyokuja katika maudhui hii tunapata katika mjumuiko wa hadithi -zote takriban- zinazozungumzia Khawariji kuwa sifa zao ni:

 1. Watakuwa wingi wa Ibada kiasi cha kudharau mmoja wetu ibada zake mbele ya ibada zao.
 2. Watakuwa wasomaji wazuri sana wa Qur-ani tukufu.
 3. Watakuwa ni wenye kuua waislamu, na kuwaacha wasiokuwa waislamu.
 4. Ni mbwa wa watu wa motoni.
 5. Watakuwa ni vijana wadogo watakaopatikana mwisho wa wakati.

Na hapa tunazingatia kuwa sio aibu katika uislamu kuwa mwingi wa ibada wala kuwa msomaji mzuri wa Qur-ani; kwa sababu hayo ndiyo yanayotakiwa yapatikane kwa Waislamu, kwa maana hiyo aibu yao haipo hapo, lakini kuja kwake katika maelezo ya hadithi ni kwa hekima ya kutahadharishwa na udhahiri wao, basi tusije tukakhadaika kwa wingi wa Ibada zao na umahiri wao wa kusoma Qur-ani, na sisi leo kama tutatafuta vizuri ni nani walio wingi wa Ibada na umahiri wa kusoma Qur-ani kiasi cha kuweza kudharau mmoja wetu ibada zake na usomaji wake wa Qur-ani, basi tutawakuta kuwa hao ni wale wanaojinasibisha na Usalafi (Mawahabi).

Tukija kwa upande mwengine tukiangalia ni nani katika mafundisho yao wenye Itikadi za kuwaitakidi Waislamu wengine wasiokuwa wao kuwa ni Makafiri Washirikina walioritadi ambao ni halali kuuliwa na kupigwa vita na kuhodhiwa mali zao kwa njia ya ngawira, na kuwafanyia kila ubabe na fujo tatukutia si wengine isipokuwa ni hao hao wanaojinasibisha na Uaslafi (Mawahabi).

Mtume (s.a.w) aliwasifu katika riwaya nyengine kuwa Khawariji ni mbwa wa watu wa motoni, bila shaka tunafahamu sote kuwa mbwa kazi yake ni kumtumikia bwana wake, yuko tayari kufa kwa ajili ya bwana wake, twabaan sote tunafahamu kuwa watu wa motoni ni Washirkina (Mayahudi, Manasara…) na Mafasiki wote.

Sasa tukiangalia mafundisho ya makundi ya Waislamu ni yapi yaliyopata nafasi ya kutumiliwa na Watu wa motoni na kupelekea wanavyuoni wa mafundisho hayo kutoa fatwa za kuridhisha matakwa na watu wa motoni? Hatutapata wengine isipokuwa ni hao hao wanaojinasibisha na Usalafi (Mawahabi), kwani wao:

 1. Ndio wenye mafundisho ya chinjachinja dhidi ya wale wasiokubaliana na wao katika Itikadi yao ya kumsifu Allah mtukufu kwa sifa za viungo na umwili wa kuenewa na eneo.
 2. Mafundisho yao yanasema kuwaambia wafuasi wao kuwa Allah anasamehe madhambi yote yasiyokua ya kishirkina tu, kwa hiyo hata ukifanya madhambi yote (Uzinifu, wizi, uongo, ulawiti, kuvunja haki za wazee, kulewa, kuua, ujambazi, riba…) na usitubie, basi wewe utakuwa ni mja wa Peponi tu bila ya shaka yoyote, yaani ni mafundisho yanachochea ufasiki  na udhalimu katika jamii za Waislamu na kuutetea.

Mtume wetu Muhammad (s.a.w) amebainisha katika hadithi hizo asili ya aibu za Khawariji, nayo ndiyo iliyosababisha kwao kuingia katika sifa zao mbaya kama tulivozieleza, na asili hiyo si nyengine bali ni kuwa Qur-ani haivuuki koromeo zao, na hili liko wazi kuwa wao hawatakubaliana na Qur-aani tukufu wala hawatakuwa katika uongofu wake, na kama ukiwapa Aya basi wao wataipinga kwa neno la wanaowategemea tu wanakuambia (Fahamu Salafu Saliih) huku Itikadi zao zitapingana na Qur-ani wazi wazi, hivi Salafu Saalih walipingana na Qur-aani?!!.

Sasa tukiangalia katika makundi yote ya Waislamu wenye sifa hiyo tutakutia pia kuwa ni haohao wanaojinasibisha na Usalafi, kiasi cha kufikia kusema kwao kuwa huna ruhusa wewe ya kuifahamu Qur-ani isipokuwa kama walivyoeleza watangulizi wao kwa mujibu wa riwaya zao tu, wanasema kwa fahamu ya salafu saalih.

Pili: Neno baya siku zote hujulikana; kwa sababu hua halina mizizi madhubuti, hulegalega na kuwa rahisi kulin`goa na hapo kukosa neno hilo pa kukaa, ama neno zuri hilo huwa na mizizi madhubuti ya kulizuia bila kulegalega, na matunda yake hupatikana kila wakati kwa idhini ya Allah mtukufu.

Ama kuhusu hadithi iliyokuja kwa kumtaja Dhu Al-Khuwaisirah ambayo imepitia kwa njia ya Abu Said Al-Khudri (r.a) nayo ni hadithi inayopatikana katika vitabu vyenye kutegemewa katika uwanja wa hadithi, hususan Sahihi Bukhari na Sahihi Muslim, jawabu yetu ni kama ufuatavyo:

 1. Tunatakiwa tufahamu kuwa kuwemo hadithi katika vitabu haitoshelezi kuihukumu kuwa ni sunna ya Mtume S.A.W., kwa sababu ya kuwepo uwezekano wa kuwa hadithi hiyo ni dhaifu na kutothibiti.
 2. Tukichunguza ongezeko hili la kutwajwa Dhu Al-Khuwaisira katika hadithi za Khawariji tunalikutia kuwa ni ongezeko alilopwekeka nalo Ibnu Shihaabi Zuhuri kutoka kwa Abu Salamah kwa njia ya Abu Saidi Al-Khudri (r.a). 

Na ili tuifahamu zaidi nukta hii, ni kuwa Sahaba Abu Saidi Al-Khudri (r.a) alihadithia hadithi ya Khawariji, na miongoni mwa waliopokea kutoka kwake ni Abu Salamah ambaye miongoni mwa wapokezi walioipokea kutoka kwa Abu Salamah huyu ni Ibnu Shihaabi Zuhuri. 

Sasa uhakika ni kuwa ziada hiyo ya Dhu Al-Khuweisirah hawakuipokea wapokezi wengine walioipokea hadithi hiyo kutoka kwa Abu Salamah, na la ajabu ni kuwa wamegongana na Zuhuri katika mapokezi yao, nao ni:

 1. Mohamed bin Ibrahim Ataimi.
 2. Al-As-wad bin Al-Alaa.
 3. Mohamed bin Amru.

Riwaya ya Zuhuri kaipokea Bukhari kwa no. 6933 ambayo mwisho wake inasema: [Amesema Abu Said Al-Kudri (r.a): “Ninashuhudia nimesikia kutoka kwa Nabii (s.a.w), na ninashuhudia kuwa Ali aliwauwa na mimi niko pamoja naye, basi aliletwa huyo Mtu kwa mujibu wa sifa alizomsifu Nabii (s.a.w).”].

Wakati huo huo katika kitabu hicho hicho Sahihi Bukhari riwaya no 6931 anapokea [Mohamed bin Ibrahim Ataimi kutoka kwa Abu Salamah na kwa Ataa bin Yasaar kuwa wawili hao (Abu Salamah na Ataa bin Yasaar) walimwendea Abu Said Al-Khudri (r.a), na wakamuuliza kuhusu Waharuriyah na kumwambia: Jee! Umemsika Nabii (s.a.w) akisema kitu kuhusu wao? Akasema: Sijui ni nini Waharuriyah.]

Sasa la kushangaza hapa, ni kuwa: vipi Zuhuri katika riwaya yake anaeleza kutoka kwa Abu Salamah kutoka kwa Abu Said Al-Khuduri (r.a) huyu huyu akiwa anashuhudia kuwa Imam Ali aliwaua Khawawariji naye yuko pamoja naye na wakusudiwa ni hao hao Waharuriyah, kisha Mohamed bin Ibarahim Ataimi anasimulia kutoka kwa Abu Salama huyo huyo -tena sio peke yake na Ataa bin Yasaar- kuwa Abu Saidi Al-Khudri (r.a) huyo huyo hawajui hao hao alioshuhudia kuwa Imam Aliy kawaua na yeye yuko pamoja naye?!!!!! Hebu tuzinduke.

Kutokana na hapa tunaona wazi wazi kuwa ongezeko la Zuhuri ni mchezo uliopitishwa -katika riwaya hii- nao ni mchezo wenye lengo la kuwabandika Mashahidi wa Naharawani Allah awaridhie -ambao ndio Waharuriyah- sifa ya Ukhawariji, sifa ambayo haipo kwao kiuhakika.

Halafu la ajabu, ni kuwa Imam Ali mwenyewe anawaepushia Watu wa Naharawani sifa ya Ushirikina na sifa ya Unafiki, na kwa maana hiyo hawawi isipokuwa ni Waumini tu; kwani mja asiyekua mshirkina wala mnafiki huyo hatakua isipokua ni muumini tu.

Amepokea Al-Baihaqi katika Sunan Al-kubra riwaya no. 16722 kuwa kuna mtu alisema: Nani anayemkumbuka nyumbu siku walouliwa Washirkina? Anamaanisha Watu wa Naharawani. Akasema Ali bin Abi Twalib: ((Ushirikina wameukimbia hao)). Akasema: Basi ni Wanafiki?. Akasema: ((Wanafiki hawamtaji Allah isipokuwa kidogo)) Akasema: Basi walikuwa nani?!! Akasema: ((Ni watu walitufanyia uadui tukanusudriwa dhidi yao)).

Basi kutokana na hapa inadhihiri wazi wazi kuwa wapinzani wa Mashahidi wa Naharawani R.A walipoona kuwa hakuna hoja ya kielimu wala ya kimantiki ya kuweza kuwatia makosani wakaingia katika upangaji wa sababu ya kuwaingiza Mashahidi hao wa haki katika makosa kupitia riwaya za kupanga na kutunga, ndio wakaleta alama ya ajabu, nayo ni alama ya kuwemo katika safu zao mtu kibutumkono, eti ndio iwe alama ya upotevu wao!!!!

Na katika ajabu ni kukutia riwaya sahihi waliyoipokea Al-Haakim 2657, na Ahmed bin Hambal 656 na Al-Baihaqi 16741, 16742, ambayo ndani yake kuna maneno haya:

Bibi Aisha (r.a) anauliza: “Ni kitu gani kilichonifikia kutoka kwa watu wa dhimmah (Mayahudi na Manasara wanaoishi chini ya dola ya kiislamu) wanakizungumza wakisema: Dhu Thudayy Dhu Thudayy?

Abdullahi bin Shaddaad anajibu: “Nilimuona na nilisimama pamoja na Aliy (r.a) akiwa katika waliouliwa, basi Ali aliita watu na akasema: Jee! Munamjua huyu? Hapo wengi waliokuja wakasema: Kwa hakika nilimuona katika Msikiti wa Bani fulani anasali, na nimemuona katika Msikiti wa Bani fulani anasali, na hakuja mtu yoyote wa kuthibitisha kuhusu mtu huyo isipokua kwa neno hilo tu.

Bibi Aisha (r.a) anauliza: Ni lipi neno la Ali (r.a) wakati alipomsimamia (mtu huyo kibutumkono) kama wanavyodai watu wa Iraqi?

Abdullahi bin Shaddaad akajibu: Nilimsikia akisema: Amesema kweli Allah na Mtume wake.

Bibi Aisha (r.a): Jee! Ulisikia kwake akisema jengine lisilokuwa hilo?

Abdullahi bin Shaddaad: Ewe Mola wangu hapana (sikusikia).

Bibi Aisha (r.a): Ni kweli, amesema kweli Allah na Mtume wake, Allah amrehemu Ali (r.a), hakika yeye -ilikuwa katika maneno yake- haoni kitu kinachompendeza isipokuwa husema: Amesema kweli Allah na Mtume wake, basi wanakwenda Watu wa Iraqi wanamzulia uongo na wanamuongezea hadithi)). Mwisho wa kunukuu.

Haya yote yanatupa ukweli kuwa huyo Dhu Thudayyah hakuwa akijulikana aslan -hata na Bibi Aisha (r.a)- kwa sifa mbaya, wala kuwa yeye ni alama ya watu waovu, na kuwa huo ni uongo wa hadithi za kuongezea, na asili yake ni wanadhimma (Mayahudi na Manasara) wa Iraqi.

Juu ya kuwa suala la kuwepo mtu wa sifa mbaya katika safu za watu wema hakuathiri kitu chochote kwa walio wema, na katika hili kuna msingi muhimu ulio maarufu wa Qur-aani tukufu unaosema ((Na habebi mbebaji mzigo wa mwengine)) hivi kuliwadhuru nini watu wa Mtume Mussa A.S kuwa Qaaruni au Saamiriyu katika safu zake?!!

Tujihadhari ndugu zangu na tuhakikishe mambo tunaposikia, tusije tukabebeshwa mizigo ya watu wengine waliodhulumu kiujinga.

Wabillahi Taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

9. TUHUMA YA SALA YA IJUMAA
Assalaamu Alaikum
Ndugu zanguni nauliza, kuna shutuma tunapewa nayo inasema: MAIBADHI kuwa zamani tulikuwa hatuswali SWALATUL JUMAA; kwa hiyo wanatumia mfano huu ili kuwaonesha UMMA kuwa sisi ni madhaifu na hatufai kufuatwa.
Naomba mutueleweshe juu ya shutuma hii.

JAWABU
Hii shutuma ni batili nayo haina nafasi kwa wenye kufahamu; kwa sababu suala la sala ya Ijumaa ni suala lenye tofauti katika masharti ya kulazimika kwake, na katika hili kuna wasaa wala hakuna dhiki kwa wenye kufahamu.
Twabaan tunafahamu sote kuwa katika Uislamu kuna hukumu zenye kuambatana na sababu au shatri au kuzuizi, hili linafahamika kwa wenye kujishughulisha na elimu ya usulu fiqhi.
Na suala la Sala ya Ijumaa ndani ya Uislamu kwa madhehebu zake zote lina khilafu hukusiana na sharti zake, na khilafu pia hiyo ipo pia katika safu za Ibadhi, na miongoni mwa Sharti hizo ni kupatikana uongozi wa Kiislamu (Uimamu wa kuongoza Jamii) mwenye kuamrisha kusaliwa Ijumaa.

Na Sharti hii imezingatiwa kutokana na Haidthi ya Jabir bin Abdillahi (r.a) kuwa Mtume (s.a.w) alisema: ((Na mujuwe kuwa Allah amekufaradhishieni Ijumaa katika kisimamo changu hichi katika siku yangu hii katika mwezi wangu huu kuanzia mwaka wangu huu mpaka kitasimama Kiama, basi yoyote atakayeiwacha katika uhai wangu au baada yangu na yeye anaye kiongozi muadilifu au dhalimu kwa kuidharau (Ijumma) au kuipinga (Ijumaa) basi Allah asikusanye mambo yake, wala asibarikie katika jambo lake, tena ifahamike kuwa hana Sala huyo, wala hana Zaka huyo, wala hana Hijja huyo, wala hana Funga huyo, wala hana wema huyo, mpaka atubie, basi atayetubia Allah mtukufu atamsamehe huyo)) [Ibnu Maajah 1081, Baihaqi Sunan Kubraa 5570]

Sharti hii pia ina tofauti ndani yake, jee! ni sharti ya usahihi au ni sharti ya kulazimika?

Kwa wenye kuona kuwa ni Sharti ya Usahihi basi hawaoni usahihi wa sala ya Ijumaa bila ya kuwepo uongozi wa kiisalamu; kwa maana hiyo haitofaa kusimamishwa bila ya kutimia sharti hiyo, na ambao wataisali bila ya kuwepo sharti hiyo ni sawa na mwenye kusali bila ya Udhu.

Na wenye kuona kuwa ni Sharti ya kulazimika wanaona kuwa sio lazima tu kuisimamisha, na kama itasimamishwa basi ni sahihi, kwa hiyo Jamaa wakiamua kuisimamisha italazimika kwa kupatikana kunadiwa kwake kwa njia inayofaa.

Sasa sisi Ibadhi kwa upande wetu suala lenye khilafu kama hizi huwa tunajifunga na msimamo wa marejeo ya wakati, nayo ni yale anayoyaona Mwanachuoni Mujtahidi aliye marejeo ya zama husika, ameulizwa Samaahatu Sheikh Al-Khalili (h.a) kuhusu kufaa kusimamishwa Sala ya Ijumaa katika Dola iliyopo chini ya hukumu serikali isiyokuwa ya Kiislamu mfano wa Tanzania, naye akajibu:

“Inatosheleza kuwa katika ngazi za juu mwenye kukubali shahada mbili (Muislamu) hata kama hazifanyii kazi (Asi) katika kukubalika kusali sala ya Ijumaa, na ukutosheleze kuwa Wema waliopita waliisali chini ya kivuli cha Dola ya Bani Umayyah nao (Bani Umayyah) ndiwo waliobadilisha hukumu za Allah, na kuwaingiza waja wema wa Allah katika madhila na kuwadhulumu, na inawezekana kuitwa Kiongozi hata Kafiri wa Kimila (Mshirikina), kwa hakika amesema Allah mtukufu kuhusiana na Firauni na wasaidizi wake ((Na tumewafanya viongozi wanaoita katika Moto)) [Qasas 41] Na Allah ndiye anajua zaidi.” [Fatawa 1/158]

Kwa hiyo waliofanya hapo kabla walifanya kwa mujibu wa Sheria kwa mujibu wa ilivyodhihirika hukumu ya Suala hili kwa marejeo ya Wakati wao, na tunayofanya hivi sasa pia tunafanya kwa mujibu wa Sheria kwa mujibu wa ilivyodhihirika hukumu ya Suala hili kwa marejeo ya Wakati wetu, wala hakuna tatizo katika hili kwani wote hawana lengo isipokuwa la kuwemo katika maridhio ya Allah mtukufu na kwa misingi yenye kukubalika kisheria, kwa hili suala hili halina utata isipokuwa kwa wasiofahamu misingi sahihi ya Uislamu.

Wabillahi taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

10. WALIOAMINI NAO HAWAKUCHANGANYA IMANI YAO NA DHULMA
Kushurani zote ni kwa Allah mtukufu na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja na Masahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya Malipo.

TUHUMA:

Imetufikia tuhuma inayosema kuwa Allah mtukufu amesema kwenye Kitabu chake yoyote atakayeamini kisha hakuichanganya imani na dhulma basi huyo amefaulu naye ndiye aliyeongoka kama ilivyo katika Surati Al-An`am Aya ya 82. Na kuwa dhulma katika Aya hiyo ni ushirikina, na kwa tafsiri hiyo amefasiri Sh Abdallah Saleh Al-farisi katika Tarjuma yake ya Qur-ani takatifu, nayo ndiyo Tafsiri ya Mtume (s.a.w) naye ndiye mbainishaji wa Qur-ani. Sasa Allah anatuambia kuwa Muislamu ni mwenye mafanikio ikiwa tu hakufanya Shirki lakini Ibadhi wao wanatuambia hapana ataadhibiwa kila mwenye dhambi kubwa ni sawa ya ushirikina au si ya ushirkina.

JAWABU:

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ أُولَئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُمْ مُهْتَدُونَ

((Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao kwa dhulma hao watapata amani nao ndio walioongolewa))

[An-aam 82]

Anatuambia Sheikh Qutub/ Mohamed Youssuf Itfaish (r.a) katika tafsiri yake Taysiri Tafsiri.

{ الَّذِينَ آمَنُوا } بالله ورسوله وكل ما يجب الإِيمان به عليهم { وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ } ولم يخلطوا { بِظُلْمٍ } لأَنفسهم بكبيرة فيما بينهم وبين الله ، أَو فيما بينهم وبين الخلق ، والتنوين للتعظيم ، فإِن الكبيرة ذنب عظيم كاسمها { أُولئِكَ لَهُمُ الأَمْنُ } فى الآخرة من عذَابها { وَهُمْ مُهْتَدُونَ } إِلى ما ينفعهم دنيا وأُخرى ، وأَما من آمن ومات على كبيرة غير تائب فلا أَمن لهم وهم ضالون ، وهذا رد على المرجئة الخلص الذين لا يجزمون بالهلاك على من مات وهو مصر وعلى الأَشعرية الذين أَجازوا دخول المصر الجنة ، وقالوا بأَنه يقع لبعض والبعض الاخر يدخل النار ، ويخرج منها عندهم فكانوا فى طرف من المرجئة

(Wali walioamini) Allah na Mtume wake na kila lilikowa ni lazima kwao kuliamini (Na hawakuchanganya Imani yao) hawakuaichanganya (Kwa dhulma) ya nafsi zao kwa dhambi kubwa yoyote katika yaliyo baina yao na Allah, au baina yao na viumbe, na tanuwinu – yaani kasratani- ni kuwa uzito wake, kwani hakika dhambi kubwa ni dhambi nzito kama lilivyo jina lake (Hao ndio wenye amani) katika Akhera kutokana na adhabu yake (na wao wameongolewa) katika yenye kuwafaa duniani na akhera. Ama mwenye kuamini na akafa katika dhambi kubwa yoyote bila ya kutubia hao hawana amani nao wamepotea. Na hili ni kuwarudi Murajia waliotopea ambao hawaitaitakidi kuangamia mwenye kufa hali ya kuwa ni mkaidi wa kutubia kwa dhambi aliyomo ndani yake, na kwa Ash-ariyah ambao wanakubalisha kuingia peponi aliye mkaidi wa kutubia na wakasema kuwa baadhi yao watapata amani na baadhi nyengine wataingia motoni na kutolewa humo, basi wakawa na wao ni sehemu ya Murjia.

Tunawambia ndugu zetu hawa -Allah awaongoe- kuwa Aya imesema hivi:

الَّذِينَ آمَنُوا وَلَمْ يَلْبِسُوا إِيمَانَهُمْ بِظُلْمٍ أُولَئِكَ لَهُمُ الْأَمْنُ وَهُمْ مُهْتَدُونَ

((Wale walioamini na hawakuchanganya imani yao kwa dhulma hao watapata amani nao ndio walioongolewa))

[An-aam 82]

Hiyo ndiyo tafsiri yake, ikiwa Sh Abdallah Al-Farisi kaifasiri vyengine hilo litakuwa ni kosa lake, na wajibu wa kielimu ni kuifasiri Qur-ani kwa mujibu wa maneno yake na sio kwa mujibu wa itikadi ya Madhehebu fulani, ikiwa kuna maelezo ya neno basi yanawekwa pembeni. Kwa hiyo Allah katuambia (بظلم) kwa dhulma, wala hajatuambia (بشرك) kwa ushirikina kama wanavyosema wenye tuhumu hiyo batili.

Neno dhulma katika Aya tukufu limekuja katika mfumo wa kukataliwa likiwa ni nakira (نكرة منفية) na mfumo huu wa maneno unamaanisha ukusanyaji kamili wa kila lenye kukubalika kwa neno husika, tena ukusanyaji huo huwa haukubali kuhusishwa chochote chenye kukubalika kwa neno husika isipokuwa uhusisho wa hapo hapo.

Kwa mfano anatuambia Allah mtukufu:

مَا اتَّخَذَ اللَّهُ مِنْ وَلَدٍ وَمَا كَانَ مَعَهُ مِنْ إِلَهٍ

((Hajajifanyia Allah mtoto wala hakuna pamoja naye mungu))

[Al Muuminuna 91]

Na kule ametuambia na hawakuchanganya imani yao kwa dhulma.

Basi kama ilivyokuwa katika Aya hii maana yake Hajajifanyia mtoto wowote na hakuna pamoja na yeye mungu yoyote na Aya ile vile vile maana yake hawakuchanganya imani yao na dhulma yoyote.

Qur-ani tukufu imetuekea wazi kabisa kuwa dhulma inazingatiwa kwa madhambi ya kishirkina na kwa madhambi yasiyokuwa ya kishirikina.

Anatuambia Allah mtukufu:

يَا أَيُّهَا النَّبِيُّ إِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَطَلِّقُوهُنَّ لِعِدَّتِهِنَّ وَأَحْصُوا الْعِدَّةَ وَاتَّقُوا اللَّهَ رَبَّكُمْ لَا تُخْرِجُوهُنَّ مِنْ بُيُوتِهِنَّ وَلَا يَخْرُجْنَ إِلَّا أَنْ يَأْتِينَ بِفَاحِشَةٍ مُبَيِّنَةٍ وَتِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ وَمَنْ يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّهِ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ لَا تَدْرِي لَعَلَّ اللَّهَ يُحْدِثُ بَعْدَ ذَلِكَ أَمْرًا

((Ewe Nabii! Mtakapo wapa talaka wanawake, basi wapeni talaka katika wakati wa eda zao. Na fanyeni hisabu ya eda. Na mcheni Allah, Mola wenu Mlezi. Msiwatoe katika nyumba zao, wala wasitoke wenyewe, ila wakifanya jambo la uchafu ulio wazi. Hiyo ndiyo mipaka ya Allah, msiikiuke. Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allah, basi amejidhulumu nafsi yake. Hujui; labda Allah ataleta jambo jengine baada ya haya.)) [Talaq 1]

Aya hii tukufu inatuambia wazi wazi kuwa mwenye kuzikiuka sheria za Allah katika suala la kumuacha Mke, tena kwa kumuacha nje ya eda yake na kumtoa mke aliachwa katika nyumba, kuwa atakayekiuka hayo huyo ameidhulumu nafsi yake, na sote tunafahamu kuwa makosa hayo sio ya Kishirkina.

Pia anatuambia Allah mtukufu katika mlango huo huo:

وَإِذَا طَلَّقْتُمُ النِّسَاءَ فَبَلَغْنَ أَجَلَهُنَّ فَأَمْسِكُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ أَوْ سَرِّحُوهُنَّ بِمَعْرُوفٍ وَلَا تُمْسِكُوهُنَّ ضِرَارًا لِتَعْتَدُوا وَمَنْ يَفْعَلْ ذَلِكَ فَقَدْ ظَلَمَ نَفْسَهُ

((Na mtakapo wapa wanawake t’alaka, nao wakafikia kumaliza eda yao, basi warejeeni kwa wema au waachilieni kwa wema. Wala msiwarejee kwa kuwadhuru mkafanya uadui. Na atakaye fanya hivyo, amejidhulumu nafsi yake.))

[Baqarah 231]

Allah anatuambia kuwa kuwarejea wake baada ya kuwapa talaka kwa njia ya kuwadhuru ni kuwafanyia uadui, na mwenye kulifanya hilo huyo amejidhulumu nafsi yake, na sote tunafahamu kuwa hilo sio kosa la Kishirkina.

Na katika mlango huu huu wa talaka Allah mtukufu anatuambia:

الطَّلَاقُ مَرَّتَانِ فَإِمْسَاكٌ بِمَعْرُوفٍ أَوْ تَسْرِيحٌ بِإِحْسَانٍ وَلَا يَحِلُّ لَكُمْ أَنْ تَأْخُذُوا مِمَّا آتَيْتُمُوهُنَّ شَيْئًا إِلَّا أَنْ يَخَافَا أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّهِ فَإِنْ خِفْتُمْ أَلَّا يُقِيمَا حُدُودَ اللَّهِ فَلَا جُنَاحَ عَلَيْهِمَا فِيمَا افْتَدَتْ بِهِ تِلْكَ حُدُودُ اللَّهِ فَلَا تَعْتَدُوهَا وَمَنْ يَتَعَدَّ حُدُودَ اللَّهِ فَأُولَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

((T’alaka ni mara mbili. Kisha ni kukaa kwa wema au kuachana kwa vizuri. Wala si halali kwenu kuchukua chochote mlicho wapa wake zenu, ila ikiwa wote wawili wakiogopa ya kwamba hawataweza kushikamana na mipaka ya Allah. Basi mkiogopa kuwa hawataweza kushikamana na mipaka ya Allah hapo itakuwa hapana lawama ikiwa mwanamke atajikomboa. Hii ndiyo mipaka ya Allah; basi msiikiuke. Na watakao ikiuka mipaka ya Allah, hao ndio madhaalimu.)) [Baqarah 229]

Na Aya hii iko wazi kabisa katika wasifu kwa dhulma wenye kuchupa mipaka aliyoiweka Allah mtukufu katika suala la Talaka, na makosa yake sio makosa ya Kishirkina bila ya shaka yoyote.

Pia Allah mtukufu ametuambia kuwa wasiotubia kwa makosa yao hao ndio Madhalimu.

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا لَا يَسْخَرْ قَوْمٌ مِنْ قَوْمٍ عَسَى أَنْ يَكُونُوا خَيْرًا مِنْهُمْ وَلَا نِسَاءٌ مِنْ نِسَاءٍ عَسَى أَنْ يَكُنَّ خَيْرًا مِنْهُنَّ وَلَا تَلْمِزُوا أَنْفُسَكُمْ وَلَا تَنَابَزُوا بِالْأَلْقَابِ بِئْسَ الِاسْمُ الْفُسُوقُ بَعْدَ الْإِيمَانِ وَمَنْ لَمْ يَتُبْ فَأُولَئِكَ هُمُ الظَّالِمُونَ

11. ((Enyi mlio amini! Wanaume wasiwadharau wanaume wenzao, wala wanawake wasiwadharau wanawake wenzao. Huenda hao wakawa bora kuliko wao. Wala msivunjiane hishima, wala msiitane kwa majina ya kejeli. Ni uovu kutumia jina baya baada ya kwisha amini. Na wasio tubu, hao ndio Madhalimu.)) [Hujurati 11]

Na Aya iko wazi kabisa, wala haisemwi kuwa makosa yaliyotajwa hapo ni makosa ya Kishirikina.

Na katika Aya za Qur-ani na Sunna ya Mtume wetu (s.a.w) kuna maandiko mengi sana yenye kujulisha wazi wazi kuwa madhambi makubwa yote ni dhulma, na bila shaka Aya tunayoizungumzia imekusanya dhulma zote.

Wao husema Ushirikina ndio dhulma kubwa yao, tunawambia ndio katika hilo hatutafautiani, basi Aya imekusanya dhumla zote kubwa yao na nyengine zilizobakia.

Wao katika sehemu hii wameweka hadithi kadha wa kadha kwa ajili ya kutetea Itikadi yao, lakini inafahamika kabisa kuwa hadithi hizo si sahihi kwa kupingana kwake na maelezo ya Qur-ani katika mfumo wa Aya na katika Aya nyengine nyingi tulizozieleza na ambazo hatujazieleza.

Kisha suali linakuja, ni nini athari ya neno lao katika kuifahamu Aya hii tukufu?

Bila shaka athari yake ni kupalilia utendaji wa madhambi yote yasiyokuwa ya kishirkina katika jamii, kwa sababu mwenye kubeba Itikadi yao hiyo -kwa mujibu wa Aya hii- atakuwa na itikadi kuwa yeye madamu hayumo katika kosa la Ushirikina tu basi ni mwenye amani tena ni muongofu hasa hata kama atakufa huku akiwa ni mlevi, mzinifu, mtenda matendo la kaumu luti, msengenyangi, mfitinishaji, mwizi, jambazi, muuaji n.k. kwani amejipa amani katika nafsi yake kutokana na adhabu ya Allah mtukufu, na Allah mtukufu anatuambia:

أَفَأَمِنُوا مَكْرَ اللَّهِ فَلَا يَأْمَنُ مَكْرَ اللَّهِ إِلَّا الْقَوْمُ الْخَاسِرُونَ

((Je, wamejiaminisha na mipango (adhabu) ya Allah? Kwani hawajiaminishi na mipango (adhabu) ya Allah ila watu waliokhasirika.))

[Aaraf 99]

Ndugu zangu hivi Uislamu umekuja na Itikadi ya kuchochea kumuasi Allah?!!! Haiwezekani, kwa hakika Imani ni ile iliyokita vizuri katika moyo na ikasadikishwa na matendo mema, na sio matendo maovu na maasi na mabaya.

Wasalamu alaykum warahmatullahi wabarakatuh.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

11. TUHUMA YA KUWA IBADHI WANAMRIDHIA IBN MULJIM AL-MURADI.
Imetufikia tuhuma ya kuwa Ibadhi wanamridhia Abdulrahman bin Muljim Al-Muradi muuaji wa Imam Aliy bin Abi Twalib. Ni ipi jawabu yetu?

JAWABU
KWANZA: Tujue kuwa muuaji aliyemuua Imam Ali bin Abi Twalib bila ya kutafautiana anaitwa Abdurahman bin Muljim Al-Muradi, na jina kama linavoonesha ni Muislamu katika Matabiina, imeelezwa kuwa ni katika wanafunzi wa Sahaba Muaadh bin Jabal R.A.

Tunalokusudia hapa ni kuwa sisi Ibadhi tunawashangaa sana hawa wenye kuituhumu Ibadhi katika suala hili, vipi wao wanamlaani Ibnu Muljim Al-Muradi hali ya kuwa Itikadi yao inalazimisha kuwa Ibnu Mulijm huyu ni mtu wa Peponi, kwa sababu kuua nafsi si kosa la Kishirkina, kwa hiyo kwa mujibu wa Itikadi yao ima Ibnu Muljim huko Akhera atasamehewa au ataadhibiwa kwa muda tu katika moto kisha atakwenda Peponi, tena sio hivo tu bali ataombewa na Mtume S.A.W hayo ni kwa mujibu wa Itikadi yao, au waseme kuwa uuaji ni kosa la kishirikina na hilo si neno lao, au waseme kuwa uuaji ni kosa la kuadhibiwa motoni milele pia hawathubutu kwani wakisema hivo watakua ni Maibadhi hapo hapo ikiwa ni wakweli au itawakana Itikadi yao ya kutoka motoni ndani ya nafsi zao, basi sisi tunawashangaa kwa hili mshangao mkubwa kabisa, na tunawambia kuweni Ibadhi ili muwe katika kauli sahihi katika hili.

PILI: Baada ya kufuatilia kwetu suala la Ibnu Muljim imetubainikia wazi wazi kuwa yeye si katika safu za Salafu wetu wema Ahalu Naharawani R.A, na uhakika ni kuwa Ibu Muljim Al-Muradi alipewa jukumu la kumuua Ali kutoka kwa Muawiyah bin Abi Sufiyan ili iwe ni njia ya kujiondoshea mpinzani wake wa Kisiasa kwa njia ya uuaji wa kudoea, na hilo ni mashuhuri wa Muawiyah kuwafanyia wapinzani wake, na kuwa Ali ni mpinzani mkubwa wa Muawiyah ni suala sililokua na shaka ndani yake, tumeyasema haya kwa dalili zifuatazo:

Anatuambia Abul-Asawad Aduali ambaye ni moja ya nguzo za Imam Aliy naye likua ni Kadhi (Jaji) wake katika mji wa Basra katika kipindi cha Uongozi wa Imam Aliy, na imesemwa kuwa Abul-Aswad alisilimu wakati wa Mtume S.A.W, pia alishiriki katika vita vya Jamal na Siffain akiwa katika safu za Imam Aliy, amesema Ibnu A-Jauzi katika Kitabu chake Al-Muntadhim:

قد روى أبو الأسود عن عمر وعلي والزبير وأبي ذر وعمران بن حصين واستخلفه عبدالله بن العباس لما خرج من البصرة ، فأقـــرّه علي بن أبي طالب رضي الله عنه ، وكان يحب علياً رضي الله عنه الحب الشديـــد ..

“Abul-Aswad Aduali amepokea kutoka kwa Omar na Aliy na Zubeir na Imraan bin Hussein, na Abdullah Ibnu Abbas wakati alipotoka Basra alimuweka nafasi yake (ya Ukadhi) na akalikubali hilo Aliy bin Abi Twalib R.A, naye alikua akimpenda Aliy mapenzi makubwa sana”. Mtu yuko katika cheo hicho cha amana na elimu ndiye aliyesema maneno haya kuyaeleza mauaji ya Imam Aliy:

ألا أبلــــغ معاوية بن حـــــرب *** فلا قرت عيون الشامتينا
قتلتم خير من ركب المطايــــا***وأكرمهم ومن ركب السفينا

Ee!! Mfikishie Muawiyah bin Harbi *** hayajafurahika bado macho ya wapondaji.

Mumemuua mbora wa aliyepanda vipando *** na mkarimu wao, na aliyepanda Jahazi..

Kwa hakika lau kuwa si mokono wa Muawiyah, bali ni mkono wa Ahalu Naharawani R.A walioitwa Makhawariji basi Abul-Asawad asingelifanya kosa hilo hata kidogo, lakini uhakika ni kuwa Muawiyah na wapambe wake ndio waliowabambikiza Ahalu Naharawani R.A mauaji hayo kwa kujiondoshea majukumu na kuwavika wapinzani wengine wa Kisiasa wakati huo.

Na Mashairi haya ya Abul-Aswad hayakutajwa katika chanzo kimoja tu, bali yametajwa katika vitabu vifuatavyo:

Ansaabul-Asharaafi cha Albalaadhuri 3/365 chapa ya Darul-Fikri.
Diwan Abil-Aswad Aduali uk. 174-175.
Alkhulafaau Raashiduna cha Abdulwahaab Najaar uk. 459 chapa ya Daaru Turaathi.
Aalamu Nisaa cha Omar Ridhaa Kahaalah 3/261 Chapa ya Muasasatu Risaalah.
Al-Kaamil fi Taarikh cha Ibnu Kathiir 2/75 Chapa ya Darul-Kitaabi Al-Arabi.
Taarikhi Tabari cha Ibnu Jariri Tabari 4/116.
Ameeleza Ibnu Hibah Mshafii katika kitabu Tarehe Damashqi yafuatayo:

“Na Ibnu Muljim alikuatana na Shabiib bin Bujrah naye akampasha anayoyataka na kumtaka awe pamoja naye basi alimkubalia katika hilo, na alibakia Abdurahman -yaani Ibnu Muljim- usiku ule aliazimia ndani yake kumuua Aliy asubuhi yake akinon`gonezana na Ash-ath bin Qais Al-Kindi ndani ya msikiti wake mpaka ikapambazuka Alfajiri, basi Ash-ath akamuambia: Inakujulisha asubihi (anamuharakisha kwa kutoka kabla ya mwanga wa alfajiri kutanda vizuri asije akachelewa) basi walisimama Abdulrahman bin Muljim na Shabib bin Bujrah na kuchukua panga zao kisha wakaja mpaka wakakaa mbele ya kizingiti anachotokea Aliy” mwisho wa kunukuu.

Na kisa hiki cha kunon`gona kando Ash-ath bin Qais na Ibnu Muljim kimetajwa pia katika vitabu vifuatavyo:

Taarikhu Madiinatu Damashq 42/559 Chapa ya Daru Al-fikri.
Siyar Aalami Nubalaa cha Dhahabi uk. 285 chapa ya Muasasatu Risaalah.
Usudu Al-Ghaabah cha Ibnu Al-Athiir 4/113 chapa ya daru Al-kutubi Al-Ilmiyah.
Ansaabu Al-Ashraafi cha Al-Balaadhuri 3/180 chapa ya Daru Al-Fikri.
Tarikhu Tabari 5/144.
Muruuju Dhahab 2/424.
Msomaji na ahukumu mwenyewe katika uhusiano wa Ibnu Muljim na Ash-ath kama inavojulikana kuwa Ash-ath anatamani kifo cha Aliy pia anayo mabaya yaliyotangulia hususan na Imam Aliy bin Abi Twalib hata imefikia kwa Dhahabi katika kitabu chake Siyar Aalaami Nubalaa kusema:

” وعن قيس بن أبي حازم ، قال : دخل الأشعث على علي في شيء ، فتهدده بالموت ، فقال علي : بالموت تهددني ! ما أباليه ، هاتوا لي جامعة وقيدا ! ثم أومأ إلى أصحابه . قال : فطلبوا إليه فيه ، فتركه “

“Na kutoka kwa Qais bin Abii Haazim amesema: Aliingia Ash-ath kwa Aliy kuzungumzia kitu basi alimtishia kwa mauti, hapo Aliy alisema: Kwa kifo unanitishia! sikijali, nileteeni kikusanyaji na pingu (zana za kuulia ili ampe Ash-ath apitishe tishio lake kwake) kisha akaashiria kwa watu wake. Akasema: Basi walimletea yeye naye alimuacha”

Na haya ndiyo ualiyomkaa kifuani Abu Bakar Siddiqi R.A kuhusu Ash-ath pale aliposema:

” أما اللاتي تركتهن فوددت أني يوم أتيت بالأشعث بن قيس أسيرا كنت ضربت عنقه ؛ فإنه تخيل إلي أنه لا يرى شرا إلا أعان عليه” (7).

“Ama ambayo niliyaacha nilitamani siku niliyoletewa Ash-ath bin Qais akiwa ni mateka niwe nilipiga shingo yake, kwani hakika inanijia mimi kuwa haoni shari yoyote isipokua anasaidia ndani yake”.

Anatuambia Shaharistani katika Kitabu chake Milal wa Nihal haya yafuatayo:

” اعلم أن أول من خرج على أمير المؤمنين علي رضي الله عنه جماعة ممن كان معه في حرب صفين وأشدهم خروجاً عليه ومروقــاً من الدين : الأشعث بن قيس الكندي ومسعر بن فدكي التميمي وزيد بن حصين الطائي حين قالوا القوم يدعوننا إلى كتاب الله وأنت تدعونا إلى السيف ..” أ.هـ(8)

“Na ujue kuwa wa mwanzo aliyetoka kumpiga vita Amiri Al-muuminina Aliy R.A ni kundi miongoni mwa aliokua pamoja nae katika vita vya Siffain, na waliokua na ukhawariji zaidi kwake na kujimegua zaidi katika Dini ni Ash-ath bin Qais Al-Kindi na Mis-ar bin Fadaki Atamimi na Zaid bin Husain Ataai (Huyu hi Sahaba) pale waliposema: Watu wanatuita katika Kitabu cha Allah na wewe (yaani Aliy) unatuita katika upanga!!!”

La ajabu katika haya ni kuwa Maibadhi tunashambuliwa sana na kutuhumiwa kuhusu baadhi ya waliyoyasema baadhi ya wanaelimu wetu kuhusu baadhi ya Masahaba, hali ya kuwa Ash-ath bin Qais Al-Kindi huyu amehisabiwa kuwa katika Masahaba unaweza kuyaona hayo katika:

Saharhu Adabi Al-Qaadhi Al-Khasaafi cha Omar bin Abdulazizi Al-Bukhari.
Al-Isaabah cha Ibnu Hajar Al-Asaqalani uk. 70 Tarjama no. 315.
Masailu Al-Imami Ahmad wa Is-haaq bin Raahawaih 1/1508.
Sisi tunawataka wenye kuwashambulia baadhi ya Masheikh wetu waliosema hukusu baadhi ya Masahaba kiuadilifu, pia wawe waadilifu pia wawashambulie akina Shaharistani bali na Ash-aath bin Qais na Abu Al-Ghaadiyah na Muawiyah bin Abi Sufiani bali na Amaar bin Yaassir Allah amridhie.

Wabillahi Taufiqi.

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

12. HUKUMU YA OTHMAN NA ALI R.A.
Aslamu alaykum wa rahmatullahi.

SUALI:
Ibadhi ina msimamo gani kuhusu Sayyidina Othman bin Affaan na Ali bin Abi Talib Allah awaridhie?

Tunafahamu sote kuwa hao walikua katika Makhalifa waongofu, pia walibashiriwa Pepo.

Tumesikia kuwa Ibadhi inawatusi Masahaba hawa na kuwalaani na kuwa wanawapiga vita.

Jee! Kuna uhakika wa hayo?

Jee! Ibadhi ina msimamo gani kuhusu wale wenye kufanya hivo?

Asanteni.

JAWABU:
Kiasili Masahaba wote wapo katika Maridhio na Mapenzi (Al-Walaayah); kwa hakika Allah mtukufu amenyanyua daraja yao na kuifanya bora, amesema Allah mtukufu:

((لَا يَسْتَوِي مِنْكُمْ مَنْ أَنْفَقَ مِنْ قَبْلِ الْفَتْحِ وَقَاتَلَ أُولَئِكَ أَعْظَمُ دَرَجَةً مِنَ الَّذِينَ أَنْفَقُوا مِنْ بَعْدُ وَقَاتَلُوا وَكُلًّا وَعَدَ اللَّهُ الْحُسْنَى وَاللَّهُ بِمَا تَعْمَلُونَ خَبِيرٌ))

((Hawi sawa miongoni mwenu yule aliyetoa kabla ya ufunguzi na kupigania, hao wana daraja kuu zaidi kuliko wale waliotoa baadaye na wakapigania, na wote amewaahidi Allah malipo mazuri, na Allah kwa munayoyafanya ni mwenye kuyajua vizuri)) [Al Hadidi 10].

Amesema Imamu Al-Mufassir Muhammad bin Youssuf At-Fayyish R.A:

وذلك خطاب للصحابة وتفضيل لبعض على بعض وزجر للمتأَخر عنهم أن يحقر المتقدم

“Na maelezo hayo ni ya Masahaba na kufadhilishwa baadhi yao juu ya wengine na kutahadharisha aliyefuatia baada yao asiye akadharau aliyetangulia” [Taysiru Tafsiiri 11/75]

Na Mtume wetu S.A.W amesema: ((Niachieni Masahaba wangu, naapa kwa yule ambae nafsi yangu imo mikononi mwake, lau mmoja wenu atatoa ujazo wa dunia nzima wa dhahabu hatafikia konzi ya mmoja wao wala nusu yake))

Na fadhila za Masahaba R.A ni nyingi, itosheleze kuwa kupitia kwao Allah mtukufu ameinusuru Dini yake, na bila shaka miongoni mwa Masahaba hao Allah awaridhie ni Othmana bin Affaan na Ali bin Abi Talib, hili hakuna kutafautiana ndani yake, kwa hiyo kwa mujibu wa Mafundisho ya Madhehebu ya Ibadhi tunasema kuwa kiasili Masahaba hao wawili wapo katika Maridhio (Al Walaayah) na Daraja ya juu kabisa, na wao ni miongoni mwa Makhalifa waliochukua Baia ya kuhukumu kisheria (Kiapo cha kushika Madaraka) kwa Masahaba wenzao, Othman bin Affan ni Khalifa wa tatu, na Ali bin Abi Talib ni Khalifa wa nne.

Ama kuhusu kusikia kwenu kuwa Ibadhi inawatusi Masahaba hao na kuwalaani na kuwapiga vita.

Sisi hilo hatujaliona mpaka muda huu, hatujaona andiko lolote la Mwanachuoni wetu la kuhimiza kumtukana Sahaba yoyote, au kumlaani, au kumpiga vita, hayo kwetu hakuna.

Ama kuwepo katika safu za Ibadhi baadhi ya Wanavyuoni wetu ambao waliwazungumza Othman bin Affaan na Ali bin Abi Talib kwa sifa mbaya kisheria, Wanavyuoni hao walifanya hivo kiuadilifu kwa kuzingatia kuwa Masahaba hao wawili -kwa mujibu wa ilivodhihiri kwa Wanavyuoni hao- waliingia katika makosa makubwa ambayo hawakutubia kwayo mpaka kufariki kwao, kwa hiyo wakatoa hukumu kwa mujibu wa ilivodhihiri kwao bila upendeleo, kwa sababu hakuna aliye juu ya Sheria ya Allah katika Masahaba si Othman wala Ali wala mwengine yoyote.

Na hayo ya kuwasema vibaya baadhi ya Masahaba pia yapo katika vitabu tegemewa vya Masunni, kwa mfano Ibnu Taimia Al-harrani ambae Masalafi wanamlakibu Sheikh Al-Islami anasema katika kitabu chake Minhaaj Sunna:

” ولم يكن كذلك علي ، فإن كثيرا من الصحابة والتابعين كانوا يبغضونه ويسبونه ويقاتلونه”

“Na Ali hakuwa hivo -yaani hakupata mapenzi wanayostahiki kuyapata wenye kuamini na kutenda mema- kwani hakika wengi katika Masahaba na Matabiina walikua wakimchukia na kumtukana na kumpiga vita.” [Minhaaju Sunnati Nabawiyyah 7/137-138]

Bila shaka Ibnu Taimia ilimdhihirikia kwa upande wa Ali bin Abi Talib hayo aliyoyasema hapo, basi kuna ubaya gani ikiwa baadhi ya Wanachuoni wetu yamedhihirikia kwao hayo au mfano wake kwa Ali au Othmani au Sahaba mwengine yoyote na wakamuweka muhusika wake katika hukumu ya Baraa-atu Dhaahiri ambayo inamstahiki kila aliyemo katika dhambi kubwa hali ni mkaidi wa kutubia?!!!

Na Wanavyuoni wetu hao baadhi ambao walisema kuhusu Masahaba hao wawili, wamesema kwa mujibu wa ilivodhihiri kwao kuwa waliingia katika dhambi kubwa ambayo walikufuru kwayo ukafiri wa neema na sio ukafiri wa Kishirikina, na neno lao hilo:

Kwanza: Linazingatia kuwa Masahaba hao ni Waislamu si Washirikina.

Pili: Linazingatiwa katika Madhehebu kuwa ni rai yao binafsi kwa yaliyothibiti kwao, si halali kwa mwengine kuchukua neno lao ila kama atajua kama walivojua wao, na sisi hatujalazimishwa kwa waliyoyajua wao, bali kwa tunayoyajua sisi, na Baraa-atu Dhaahiri ni kwa sababu yake, si kwa kufuata neno la Mwanachuoni.

Ama kuhusu msimamo wa Ibadhi kwa wenye kumtusi yoyote katika Masahaba hao au kumlaani au kumpiga vita.

Ikiwa amefanya hivo kiuadui bila ya haki huyo atakua katika Baraa-atu Dhaahiri ameangamia mpaka atubie.

Ama ikiwa amefanya kwa haki imethibiti kwake bila kuvuka mipaka na akabainisha yaliyomdhihirikia kidalili huyo hatutakua na haki ya kumuweka katika Baraa-a wala hatuondoshi Walaayah kwake, lakini pia hatulazimiki na neno lake isipokua kwa yule atayejua uhaki wa aliyosema, huyo itamlazimu haki katika nafsi yake, kwa sababu Masahaba mmoja mmoja hawakuhifadhika na kukosea makosa ya ufasiki, kwa hiyo uwezekano wa kufa katika ufasiki upo kwa baadhi yao, na madai kuwa Sahaba fulani kabashiriwa Pepo ni madai ya dhana hayajengi uhakika wa Itikadi.

Na haya ya uwezekano wa kupatikana hukumu ya ufasiki kwa baadhi ya Masahaba pia wameyasema Masunni, amesema Sheikh Mohammed Saleh Al-Uthaimin:

وقوله: “وَالصَّحَابَةُ عُدُولٌ، وَالمُرَادُ: مَنْ لَمْ يُعْرَفْ بِقَدْحٍ”؛ يعني: المراد من قوله: إنَّ الصحابة عدول مَن لم يُعرَف بقَدْح، فأمَّا مَن عُرِفَ بقدْح فإنَّه ليس بعَدْل حسَب القدح الذي فيه. ويدلُّ لذلك أنَّ الله تعالى قال: (والذين يرمونَ المُحصناتِ ثمَّ لم يأتوا بأربعة شهداءَ فاجلدوهم ثمانين جلدةً ولا تقبلوا لهم شهادةً أبداً وأولئكَ هُمُ الفاسقون * إلا الذين تابوا من بعد ذلك وأصلحوا) [النور:4-5]، فدلَّ ذلك على أنَّ فيهم الفَسَقة”

Na neno lake ((Na Masahaba wote ni waadilifu, na makusudio: Yule ambaye hajulikani kwa kasoro)) Yaani: Makusudio ya neno lake: Hakika Masahaba ni waadilifu ni yule asiyejulikana kwa kasoro, ama yule atakae julikana kwa kasoro kwa hakika huyo hatakua muadilifu kwa mujibu wa kasoro itakayokua kwake, na linajulisha hilo kuwa Allah mtukufu amesema: ((Na ambao wanawalengea (kosa la uzinifu) wanawake waliohifadhiwa kisha hawakuleta mashahidi wanne wapigeni mijeledi thamanini na musikubali kwao ushadihi milele na hao ndio Mafasiki * Isipokua wale waliotubia baada ya hayo na wakaboresha..) [Nuur 4-5], basi likajulisha hilo kuwa hakika ndani yao wako Mafasiki”. [Sharhu Mukhtasr Tahriir 669-670]

Kwa hiyo utafahamu kuwa kinachotafautisha baina ya Wanavyuoni waliozungumzia Masahaba kwa mujibu wa matokeo yalivojiri baina yao katika zama zao ni kuwa Wanavyuoni wa Kiibadhi walizingatia uadilifu bila upendeleo na Wanavyuoni wa Kisunni wao waliingiwa na upendeleo.

Mtume S.A.W alitutahadharisha na upendeleo katika hukumu na kusema: “Hakika kuliwaangamiza waliopita kabla yenu kule kuwa kwao anapoiba mkuu humuachia na anapoiba mnyonge wanamuadhibu, naapa Wallahi lau Faatima binti Muhammad ameiba basi ningaliukata mkono wake.”

Na kwa hali zote hizo tunasema kuwa unabakia uoni kuhusu Sahaba fulani ni fasiki si msingi wa Madhehebu ya Ibadhi, bali ni rai ya Mwanachuoni anaeona hivo kwa mujibu wa ilivodhihiri kwake.

Kutokana na hapa huwezi kuona mwanadaawa wetu anahimiza watu kumfanyia Baraa-a Othman au Ali au mwengine yoyote.

Na lau kuwa si kushambuliwa Ibadhi kupitia kauli za baadhi ya Wanavyuoni wetu ambazo walizisema kiuadilifu basi tusingelisema neno lolote katika maudhui hii.

Wallahu Aaalamu wabihi Taufiiqi.

OPEN ARTICLE

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

13. HADITHI YA ALIYEKO MBINGUNI
TUHUMA:
Imetufikia tuhuma batili kutoka kwa Masalafi wanasema Ibadhi wanapingana na Mtume S.A.W kwa sababu Mtume S.A.W amesema: ((Hivi wamuniamini hali ya kuwa mimi ni muaminiwa wa aliyeko mbinguni)) [Kapokea Bukhari na Muslim)) sasa kwa nini Ibadhi wanapingana na Mtume S.A.W kiitikadi? Kwa sababu Mtume S.A.W amesema wazi wazi kuwa yeye ni muaminiwa wa aliyeko mbinguni na bila shaka huyo ni Allah mtukufu, kwa hiyo Allah yuko mbinguni.

JAWABU:
Hadithi kama ilivokuja na maana yake kwa mujibu wa maneno yake:

((ألا تأمنوني وأنا أمين من في السماء ياتيني خبر السماء صباحا ومساء))

((Hivi hamuniamini hali ya kuwa mimi ni muaminiwa wa ambae katika mbingu, inanijia khabari ya mbinguni asubuhi na jioni))

[Bukhari 4351 Muslim 1064]

Hadithi hii wanaitumia kuwa ni dalili ya kuthibitisha itikadi yao ya mungu aliyedhibitika kimwelekeo na eneo kwa mujibu wa makadirio yao yaliyopambwa katika nafsi zao kupitia Itikadi ya Mungu viungo na harakati.

Tunawambia: Lau kuwa tukubali kimjadala tu basi lafdhi ya hadithi hii haina dalili ya kuthibitisha madai yenu enyi Masalafi; kwa sababu kila muislamu anajua na kuitakidi kuwa Allah mtukufu si mwili wala umbo, ametakasika na sifa za viungo na harakati; kwa sababu yeye ni Mkwasi aliyetangulia kila kitu, uwepo wake hauhitaji sehemu wala wakati; kwa sababu hivo na vyenye kudhibitiwa kwavo vyote ni viumbe Allah ameviumba.

Kutokana na hapo tunawambia ni

((من في السماء أمره وليس من في السماء وجوده))

((Yule ambae ni katika mbingu Amri yake na sio yule ambaye ni katika mbingu uwepo wake)).

Haya ikiwa tutakadiria tu kuwa hii lafdhi ya hadithi ni sahihi, lakini kiuhakika hii lafdhi imepitiwa na ubadilishaji wa wapokezi kwa hiyo ni لفظ شاذ tamko geni lililotafautiana na lafdhi nyengine ya riwaya husika.

Ubainisho wa hayo ni kuwa tamko walilokuja nalo na kulitolea hoja limo katika riwaya iliyopita kwa Umaarah bin Al-Qaaqaa, nayo ni riwaya iliyopinzana na riwaya ya Saiid bin Masrouuq Athauri Baba wa Sufiyan Thauri, na riwaya yake imo katika Bukhari na Muslim pia, wala haina ndani yake ((من في السماء)) ((Yule ambae ni katika mbingu)) ambalo Masalafi wamelifurahia sana kwa sababu ya upofu wa itikadi yao.

Riwaya inasema:

((أيأمنني الله على أهل الأرض ولا تأمنوني))

((Hivi Allah ameniamini kwa wahusika wa Ardhi na nyinyi hamuniamini?!!))

[Bukhari 3344 Muslim 1064]

Na bila shaka lafdhi ya riwaya hii liko wazi na karibu zaidi na halina khilafu ndani yake kuliko lile la mwanzo na tokeo ni moja kwa mujibu wa riwaya, na kwa maana hilo lafdhi walilotegemea ni Shaadh (iliyopwekeka) si hoja ya kutegemewa.

Wabillahi Taufiiqi.