Published By Said Al Habsy Ibadhi ni Madhehebu adilifu ya kiislamu yenye kusimama kwa mafundisho yafuatayo: 1. Kuitakidi kuwa Allah mtukufu ndiye muumba mkwasi (asiyesifika kwa kuhitaji) basi inalazimika kumsifu Allah kwa yanayokubaliana na utukufu wake na ukamilifu wake wa kidhati, na inalazimika kumtakasa Allah na yote yasiyokubaliana na utukufu wake na ukamilifu wake wa kidhati, basi Allah mtukufu hasifiki kwa lazimisho la kuhitaji, wala kwa sifa yoyote yenye lazimisho la kuhitaji, haiwezekani kuonekana Allah mtukufu, haiwezekani kusifika Allah mtukufu kwa sifa yoyote yenye mipaka ya kudhibitika kwa kuzingirwa na sehemu, ametakasika Allah mtukufu, hasifiki kwa sifa za viungo wala harakati; kwani Allah hayumo katika sehemu; kwa sababu sehemu ni kiumbe chake, yeye alikuwepo kabla yake. 2. Kuitakidi kuwa Allah mtukufu ndiye muumbaji, na kila kisichokuwa yeye hicho ni kiumbe na kiwe kitakavokuwa, basi Qur-ani ni maneno ya Allah, na Allah ni msemaji, sifa yake ni usemaji si maneno, basi Qur-ani bila shaka ni kiumbe chake; kwa sababu Qur-ani ni kitu kisichokuwa Allah mtukufu, na kila kisichokuwa Allah hicho ni kiumbe, na Qur-ani imabarikiwa na kujaaliwa na Allah mtukufu, na kila alichokibariki Allah na kukijaalia bila shaka kitakuwa ni kiumbe chake Allah mtukufu. 3. Kuitikadi ulazima wa kumsifu Allah kwa kuelezea ukamilifu wake wa kidhati, na sio kuelezea sifa zisizokuwa dhati; kwani Allah hasifiki kwa kutegemea sifa; kwa hiyo inalazimika kuwa yeye anasifika kwa kuelezea ukamilifu wake wa kidhati, basi Allah ni hai kwa dhati yake, mkwasi kwa dhati yake, yupo kwa dhati yake, muweza kwa dhati yake, msemaji kwa dhati yake, mjuzi kwa dhati yake, msikivu kwa dhati yake, muoni kwa dhati yake….. 4. Kuitakidi kuwa Imani inakabiliana na Ukafiri, na kuwa kila mkaidi wa kutubia katika asi alilomo ndani yake huyo atakuwa amechana na imani kisheria naye atasifika kwa ukafiri kisheria. 5. Ukafiri ndio uovu na ufasiki na udhalimu; kwa hiyo ukafiri haumaanishi ushirikina ingawa ushirkina ni ukafiri; kwa sababu ushirkina ni udhalimu na uovu na ufasiki pia, basi kila mshirikina ni kafiri, lakini sio kila kafiri ni mshirikina. 6. Maasi yako aina tatu:- 1.Makubwa ya Kishirikina. 2. Makubwa yasiyokua ya kishirkina. 3. Madogo. 7. Kuitakidi kuwa mwenye kujiepusha na maasi makubwa (ya kishirikina na yasiyokua ya kishirikina) ndiye mwenye kusamehewa maasi madogo, na ambaye hajiepushi na maasi makubwa huyo atazongwa na maasi yake yote makubwa na madogo. 8. Kuitakidi kuwa mwenye kufanya asi kubwa la kishirikina huyo ndiye kafiri mshirikina, hana haki yoyote katika haki za wana tauhidi (waislamu). 9. Kuitakidi kuwa mwenye kufanya asi kubwa lisilokuwa la kishirikina bila kuwemo katika asi la kishirikina huyo hatakuwa mshirikina, bali yeye ni kafiri wa neema (mnafiki), anapata haki zote za wana tauhidi (Waislamu) isipokua Walaayah tu (Mapenzi kwa ajili ya Allah). 10. Kuitakidi kuwa Imani inayozingatiwa kisheria ni kutokuwemo mja katika asi lolote kubwa, na Imani inaongezeka kwa matiifu na inaondoka kwa asi kubwa lolote. 11. Kuitakidi kuwa mja wa Peponi atabakia humo milele akineemeka bila ya kutoka wala kumalizika, na mja wa Motoni atabakia humo milele akiadhibika bila ya kutoka wala kumalizika. 12. Kuitakidi ubatili wa Itikadi ya kutoka motoni, na Itikadi ya mja mwema (muumini) kuadhibiwa siku ya kiama. 13. Kuitakidi kuwa uombezi (Shafaa) ni haki siku ya kiama, nayo ni kwa ajili ya waliotubia. 14. Kuitakidi kuwa mkaidi wa kutubia kwa asi kubwa lolote hatapata uombezi (Shafaa) wa yoyote siku ya Kiama. 15. Kuitakidi ulazima wa haki ya Walaayah nayo ni kupenda na kuridhia kwa ajili ya Allah tu, ni haki ya kila muumini mchamungu. 16. Kuitakidi ulazima wa haki ya Baraa-a nayo ni kuchukia maasi na wahusika wake na kujiepusha nayo na wahusika wake, basi haki ya Baraa-a inamkamata kila mwenye kuthibiti ukaidi wake wa kutubia kwa dhambi yoyote kubwa. 17. Katika Walaayah na Baraa-a hakizingatiwi isipokua uchamungu na ufasiki, basi yule ambaye umethibiti uchamungu wake atakuwa katika watu wa Walaayah, na yule ambaye umethibiti ufasiki wake atakuwa ni katika watu wa Baraa-a, na ambaye hali yake imefichika na kuingiwa na utata huyo atakuwa katika Wuquuf, hataingizwa katika Walaayah wala katika Baraa-a. 18. Baraa-a haivunji haki, basi haisababishi udhalimu kwa mwenye haki zake. 19. Ulazima wa kuamrisha mema na kukataza mabaya kwa kiwango ambacho mja ana uwezo nacho. 20. Muislamu wa kike au wa kiume ikiwa ameteleza kwa dhambi ya uzinifu haitakua halali kwake milele kufungana kindoa na yule aliyezini naye, basi Muislamu mwenye kukutana na mwengine kiuzinifu utafungika usahihi wa ndoa baina yao milele. Hayo ndiyo waliyopambika nayo Ibadhi kimafundisho, basi muislamu yoyote mwenye kuyakubali huyo atakua ni muibadhi, na ambaye hatayakubali huyo hatakua muibadhi |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo. TAREKHE FUPI YA IBADHIBaada ya kufa Mtume (s.a.w), waislamu walimchagua Khalifa Abu Bakar (r.a) awe kiongozi wao kwa mujibu wa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume (s.a.w). Abu Bakar (r.a) aliongoza kwa uadilifu mkubwa kwa makubaliano ya waislamu wote, na ilipokaribia kufa kwake alimpendekeza Omar bin Khattab (r.a) kwa Masahaba wenzake ili awe kiongozi baada yake, nao hawakupinga jambo hilo, bali waliliunga mkono; kwani sifa za uongozi bora zilipatikana kwa Omar bin Khattab (r.a) naye akawa ni kiongozi wa Waislamu baada ya Abu Bakar (r.a). Khalifa/Abu Bakar (r.a) aliongoza kwa muda wa miaka miwili (11-13H). Amiri wa Waumini Omar bin Khattab (r.a) aliongoza kwa uadilifu mkubwa sana kwa makubaliano ya waislamu wote, na ilipokaribia kufa kwake alipata shahada ya haki kwa upanga wa kunyemelea wa Mmajusi mmoja aliyejulikana kwa jina la Abu Lu-lua (l.a), na khatimaye Amiri Al-Muuminina Omar Al-Faaruuq (r.a) aliondoka duniani kutokana na jeraha hilo la upanga, hali ya kuwa Waumini wote wako radhi nae. Katika hali ya kujiuguza kwa jeraha zito la Mmajusi Abu Lu-lua, Maswahaba (r.a) walimtaka Amiri Al-Muuminina Omar (r.a) afanye kama alivyofanya Khalifa Abu Bakar (r.a) kwa kumpendekeza mmoja kati yao, lakini baada ya kuangalia ni nani anafaa zaidi katika suala la utawala, akaona heri aliweke kuwa ni Shuraa (Ushauriano wa pamoja) kama ilivyoongoza Qur-ani tukufu, basi akachagua Masahaba sita kwa suala hilo, nao ni:
Pia akamchaguwa mtoto wake Sahaba Abdullah bin Omar; ili awepo katika vikao kwa njia ya kushuhudia, kisha akawausia wasije wakatofautiana, na ikitokezea kuzozana na kutofautiana basi wawe pamoja na Abdu-Rahman bin Auf (r.a). Amiri wa Waumini Omar bin Khattab (r.a) alikufa, na uongozi baada ya mashauriano ukawa kwa Amiri wa Waumini Othman bin Affaan. Uongozi wa Omar bin Khattab (r.a) ulidumu kipindi cha miaka kumi (13-23H) iliyojaa uadilifu wa kupigiwa mfano. Amiri wa Waumini Othman bin Affaan aliongoza kwa uadilifu kwa muda wa miaka sita kwa makubaliano ya Waislamu wote, kisha baada ya hapo mambo yakaanza kubadilika kidogo kidogo; kwani tayari uzee ulikuwa umeingia kwake, pia mapenzi mengi ya jamaa zake, yote hayo yalipekea kuharibu uadilifu katika kipindi kilichobakia cha uongozi wake, hayo ni kwa sababu ya kuinamia zaidi kwa jamaa zake katika suala la utawala na ugawaji wa mali ya Dola, na mengine ambayo yameelezwa katika vitabu vya tahere, na tukirejea vyanzo vinatuambia kuwa miongoni mwa hayo ni:-
Ametuandikia Ibnu Qutaibah (Mwanachuoni msunni wa karne ya tatu hijiriya) katika kitabu chake Imamatu wa Siyaasah uk. 35-36 haya yafuatayo ((Na wametaja kuwa walikusanyika watu miongoni mwa Masahaba wa Nabii (s.a.w), basi wakaandika barua na kuyataja ndani yake yale ambayo Othaman amekwenda kinyume na Sunna ya Mtume wa Allah (s.a.w) na mwenendo wa Makhalifa wawili waliopita kabla yake, nayo ni yale yaliyokuwa kwake ya kumgawiya Marwan khumus 20% ya ngawira yote ya Afrika ndani yake kuna haki ya Allah na Mtume wake, ambazo ni haki za watu wa karibu wa Mtume (s.a.w) na mayatima na masikini, na yale yaliyokuwa katika kujitanulia majumba ya fakhari mpaka wakamuhesebia majumba saba ya kifakhari (Maqasri) aliyoyajenga Madina, nyumba ya Naila, na nyumba ya Aisha, na wengineo katika mabanati wa jamaa zake, na majumba ya Marwan ya kifakhari yaliyojengwa kwa mbao safi ambayo ujenzi wake ni kwa mali za khumus 20% ya ngawira, nayo ni haki ya Allah na Mtume wake, na katika yaliyokuwa katika ugawaji wake wa majukumu ya kazi na utawala wa miji (madaraka) kwa jamaa zake na watoto wa ami yake katika Bani Umayyah, nao walikuwa ni vijana chipukizi hawakuwa na usahaba wa Mtume (s.a.w) wala uzoefu katika mambo, na yale yaliyokuwa kwa Waliid bin Uqubah huko Kuufah wakati walipokuwa ni msimamizi wake wa utawala (Gavana); kwani yeye aliwasalisha watu sala ya Alfajiri hali ya kuwa yuko ndii amelewa rakaa nne, kisha akawageukia na kuwambia mukitaka nitawaongezea rakaa tatu nyengine. Na kuvunja kwake kumsimamishia haddi (Adabu ya ulevi) na kumcheleweshea hilo, na kuwaacha Muhajirina na Maansari akawa hawatumikishi kwa chochote wala hawashauri, na akatosheka na rai yake bila ya rai zao, na yaliyokuwa katika mipaka ambayo aliiweka pembezoni mwa Madina na katika ushughulikiaji wa ngamia na mapeo ya watu waliopo Madina, watu ambao hawana usahaba wa Nabii wala hawatoki kikazi wala hawatetei (hawamo katika safu za jihadi), na yaliyokuwa katika kuihama wake hizirani kwa kuitumia bakora ya gongo, na kuwa yeye ndiye mtu wa mwanzo kuipiga migongo ya watu kwa viboko, na yalivyo walikua Makhalifa wawili wa mwanzo wakipiga kwa durra na hizirani. Kisha wakapeana ahadi ya kuifikisha barua hiyo katika mkono wa Othman, na miongoni mwa waliohudhuria uandishi wa barua hiyo ni Ammaar bin Yasir na Miqdaad bin As-wad na jumla yaowalikuwa kumi, basi walipotoka hali ya kuwa barua imo mkononi mwa Ammaar wakawa wanachomoka kwa kumuacha Ammaar mpaka akabakia peke yake, basi aliendelea mpaka akaufika mlango wa nyumba ya Othman, na akamtaka ruhusa ya kumfika, naye akampa ruhusa katika siku ya baridi, basi aliingia huku Othman yuko pamoja na Marwan bin Hakam na jamaa zake wa Bani Umayyah, basi akampa ile barua naye akaisoma, kisha akamwambia: Wewe umeandika barua hii? Akasema: Ndio. Akauliza: Na nani alikuwa pamoja na wewe? Akasema: Walikuwa pamoja na mimi watu wametawanyika kwa kukuogopa wewe. Akasema: Ni nani hao? Akasema: Sikuambii kuhusu wao. Akasema: Basi kwa nini ukajipa ushujaa juu yangu baina yao? Akasema Marwan: Ewe Amiri wa Waumini hakika huyu mtumwa mweusi –anamkusudia Ammaar- amewachochea watu dhidi yako, na kwa hakika wewe ukimuua utawatia adabu -kwa sababu yake- walioko nyuma yake. Akasema Othman: Mpigeni. Basi wakampiga, na Othman pia akaingia katika kumpiga pamoja nao, mpaka wakamjeruhi tumbo lake na akazimia, kisha wakamkokota mpaka wakamuacha katika mlango wa nyumba, na akaamrisha Umu Salamah mke wa Mtume (s.a.w) aingizwe Ammaar (r.a) katika nyumba yake na akaingizwa, basi Bani Mughiirah wakakasirika sana kwa sababu ya Ammaar; kwani alikuwa upande wao. Alipotoka Othman kwa Sala ya Adhuhuri akampitia Hishaam bin Waliid na kumwambia: Naapa wallwaahi lau Ammaar angaalikufa kwa sababu ya kipigo alichopata, kwa hakika ningelimuua -kwa sababu yake- mtu mkuu katika Bani Umayyah. Basi Othman akasema: Huko huko…)) Anatuambia Sayyid Qutub Ibrahim Hussein Shaadhili (Mwanachuoni wa karne 14 Hijiria katika Misri) katika kitabu chake Adaalatu Ijtimaaiyah ukurasa wa 159: ((Na muweko huu wa uhakika wa hukumu adilifu ulibadilika bila ya shaka katika kipindi cha utawala wa Othman hata kama ulibakia katika mkondo wa Uislamu, kwa hakika utawala ulimkuta Othman hali ya kuwa ni mzee mkongwe na mbele yake yuko Marwan bin Hakam anapindisha amri ya uongozi kwa mapindisho mingi ya kuuweka mbali na Uislamu, na kama ilivyokuwa tabia ya Othman ya ukarimu na mapenzi yake mingi kwa jamaa zake, hayo mawili yalichangia kuchomoza mienendo walioikataa wengi katika Masahaba waliomzunguka, na mienendo hiyo ilipata ukosoaji mwingi, na ilipalilia fitina ambayo Uislamu umeteseka nayo sana. Othman alimgawia Harith bin Hakam ambaye ni mume wa Binti yake, alimgawia katika siku ya harusi dirham laki mbili, basi ilipopambazuka alifikiwa na Zaid bin Arqam Mshika hazina ya Baiti Mali ya waislamu (Benki kuu ya dola kwa nidhamu ya leo) huku ikionekana huzuni imetanda katika uso wake, kiasi cha macho yake kuogelea katika machozi, huku akimtaka amuondoshee majukumu ya kazi yake, basi alipoijua sababu na akatambuwa kuwa ni peo lake kwa mkwe wake akamuambia huku akishangaa: Hivi unalia ewe Ibnu Arqam kwa kuwa nimeunganisha ujamaa wangu?! Basi Mtu aliyekuwa na hisia za Uislamu alimjibu: Hapana ewe Amiri wa Waumini, lakini ninalia kwa sababu mimi nakudhania umechukuwa hii mali kwa kujilipiza uliyotoa katika njia ya Allah wakati wa uhai wa Mtume (s.a.w), wallahi lau ungelimpa dirham mia moja (100) basi zingelikuwa ni nyingi. Hapo Othman akamkasirikia yule mtu ambaye kifua chake hakikuweza kuvumilia ubadhirifu wa mali ya waislamu kwa jamaa wa kiongozi wa waislamu, huku akimwambia: Weka ewe Ibn Arqam, hakika sisi tutapata mwengine asiyekuwa wewe. Na mifano ni mingi katika mwendo wa Othman katika ubadhirifu huu, kwa hakika alimpa Zubeir siku moja laki tisa, na alimpa Twalha laki mbili, na alimgawia Marwan bin Hakam thuluthi ya pato la Afrika (33%), na kwa hakika walimlaumu katika hilo watu miongoni mwa Masahaba na mkuu wao alikuwa ni Aliy bin Abi Twalib, basi alijibu: Hakika mimi nina jamaa na udugu. Nao wakamkatalia hilo kwake na wakamuuliza: Hivi Abu Bakar na Omar hawakuwa na jamaa na udugu?! Akasema: Hakika Abu Bakar na Omar walijikaribisha kwa kuwazuilia jamaa zao, na mimi najikaribisha kwa kuwapa jamaa zangu. Basi walisimama na kumuacha huku wamekasirika wakisema: Uongofu wao wallahi unapendeza kwetu zaidi kuliko hili.)) Mwisho wa kunukuu. Baada ya hayo tuchukuwe riwaya za walizopokea Maulamaa wa Sunni kuhusu Othman bin Affaan:
Maelezo haya na riwaya hizi ni kutoka kwa Maimamu wa Kisunni, sasa la ajabu ni kulivalia jambo hili nguo ya upendeleo, ama Waislamu wa wakati huo ambao ni Matabiina na Masahaba (r.a) wao walifanya kazi kubwa sana ya kumkumbusha Othman, na kila mara Othman alikubali makosa na kutubia mbele ya Waislamu, lakini baadae hakuna linalofanyika na mambo yalizidi kuwa magumu na mabaya zaidi, ndipo mwisho Waislamu Masahaba na Matabiina[1] walipoitana, na kufanya jihadi ya kusimamisha uadilifu kwa kuun`goa utawala uliotoka nje ya uadilifi wa Uislamu, kama alivyoamrisha Allah na Mtume wake (s.a.w), basi walimzunguka Othman katika nyumba ya utawala kwa muda usiopungua siku arubaini (40), wakimtaka Othman aachie uongozi kiusalama, lakini alikataa kata kata, na hapo ndipo walipomuua, na Maswahaba wapo na khabari wanazo, na lau kama hawakuridhia hayo wasingalithubutu kuyaacha namna hiyo, bali wangalipigana na kuunusuru utawala wa Kiislamu, wao waliushinda ulimwengu katika vita, vipi washindwe kumuhami kiongozi wao?[2] Lakini alifanya makosa yaliyopelekea kuitana wao kwa wao kwa ajili ya kuondosha utawala uliotoka katika njia sahihi aliyoiacha Mtume (s.a.w) na Abu Bakar na Omar bin Khattab (r.a). Othman bin Affaan aliuliwa, na utawala ukaja katika mikono ya Imamu Aliy bin Abi Twaalib (k.a.w) kwa makubaliano ya Masahaba (r.a), naye alipewa Baia (Ahadi ya Uongozi) hapo hapo Madina wakiwemo wanamapinduzi waliomuua Othmaan, naye aliridhia kuwemo katika safu zake na wengine kupata nafasi za uongozi katika utawala wake. Utawala wa Oth-man ulidumu kwa miaka 12 (23-37H). Amiri wa Waumini Aliy bin Abi Twalib alishikilia utawala kwa nguvu za uadilifu, naye alianza kubadilisha watawala wa miji (Magavana) ili kurejesha hali ya uadilifu kama ilivyokuwa, lakini mambo yalibadilika na yakawa ni magumu upande wake, kwani ilianzishwa siasa ya kudai Kisasi cha damu ya Othman bin Affaan, na walioongoza siasa hii kwa mara ya kwanza ni Twalha bin Ubaidillahi na Zubair bin L-Awwam na Mama wa Waumini Bibi Aisha bint Abi Bakar (r.a) Mke wa Mtume (s.a.w), Masahaba hawa waliwaita watu katika kuinusuru damu ya Othman kwa njia ya kulipiza kisasi, nao walikataa kumtii Imam Aliy na kuwa chini ya uongozi wake, lakini wamlitaka Imam Aliy awe pamoja na wao katika shauri lile ya kulipiza kisasi. Imam Aliy alipinga siasa yao hiyo batili, na kuwahukumu kuwa wapinzani hao kua ni kundi lilioasi, kwa hivyo ni kusimamishwa hoja za kuwataka watubie na warejee katika Amri ya Allah inayowataka kuwatii viongozi waadilifu, lakini jambo hilo lilishindikana, na hapo ikawa hakuna dawa nyengine isipokuwa ni kuwapiga vita kama alivyoamrisha Allah mtukufu kwenye Kitabu chake, basi walipigana katika vita vikali vinavyoitwa Vita vya Jamal. Twalha bin Ubaidillaahi na Zubair bin L-Awaam waliuliwa katika vita hivo, ama Bibi Aisha (r.a) yeye alichukuliwa mateka, na alikubali kua alikuwemo katika makosa, na alitubia. Ilikuwa Bibi Aisha (r.a) kila akikumbuka au kukumbushwa vita vile machozi yakimtoka kwa kulia na kutubia. Vita hivyo alishinda Imam Aliy, lakini haikupita muda mara Gavana wa Shaam Muawiyah bin Abi Sufiyaan akishirikiana na Amru bin L-assi walikuja na siasa ile ile ya kudai kisasi cha damu ya Othman, nao walikusanya jeshi kubwa sana na wakaaza kuja zao Iraq, Imam Aliy aliwahukumu kwa hukumu ya Allah[3] kama ilivyokuwa kwa waliopita kabla yao, basi walikutana katika sehemu inayoitwa Siffiin na kupigana hapo, vita vilikua ni vikali sana, na kundi la Muawiyah bin Abi Sufiyaan likaanza kushindwa, basi waliopoona kuwa hakuna njia nyengine isipokua ni kusimamisha vita na kuingia katika njia nyengine ya kumvunja adui yao au kusalimu amri, fikra ya kumvunja adui yao ilikuja, nayo ni fikra aliyoitoa Amru bin L-Assi, ilikua ni fikra ya kutaka suluhu kwa njia ya kuhukumisha watu wawili, basi walisimamisha misahafu ikiwa ni alama ya kusimamisha vita. Vita vilisimama na Imam Aliy alipeleka wajumbe wake wa kuwataka warejee katika haki, alikini wao wakaleta fikra ya usuluhishi kwa kuchaguwa kila upande mwakilishi awe msuluhishi, kisha hao wawili wakae pahala pamoja na wahukumu kwa makubaliano, na kuwa vyovyote vile watakavohukumu kila upande uridhie hukumu hiyo, fikra hii ilipofika katika safu za Imam Aliy ilipelekea kugawika safu zake makundi mawili:
Sulhu hiyo ililazimisha jina la uongozi wa dola ya Uislamu lifutwe kwa Imam Aliy[4]; kwa sababu upande wa Shaam ulikataa kuwa Aliy ni kiongozi wa Waislamu; kwani wao hawakutoa ahadi ya kumtii bado, na lau yeye ni kiongozi wa Waislamu wote basi wasingalimpiga vita, kwani wao ni Waislamu pia. Ilipofika hatua hiyo ya kufanywa sulhu, wale Quraa waliopinga jambo hilo, ambao ni sehemu muhimu sana ya jeshi la Imam Aliy kwani wao ndio wasomi wa Imam Aliy, wao hawa waliamua kujitenga na kusema kuwa “HAKUNA HUKUMU ISIPOKUWA YA ALLAH” na kumtia makosani Imam Aliy, makosa ya kuacha hukumu ya Allah iliyo wazi na kuivunja hukumu hiyo ya kulipiga vita kundi la waasi, nao ni uvunjaji uliofanyika kwa kufuata ulinganio wa kundi la waasi, basi Maquraa hao walichukua hatua ya kujitenga kwa kutoshiriki katika kosa hilo waliloliona kuwa ni kosa la wazi kabisa, na hapo waliamua kwenda katika sehemu iliyoitwa Haruraa, na khatima ya sulhu -ambayo Imam Aliy alitoa ahadi ya kukubali matokeo yake- ikawa ni kuachwa Umma bila Uongozi kwa kuondoshwa Imam Aliy madarakani hali ya kuwa Muawiyah bin Abi Sufiyaan ameshikilia uongozi wake wa Shaam. Hapo wale Quraa waliokimbilia Haruraa walichagua kiongozi mpya kwa njia ya Shuura kama alivyoamrisha Allah mtukufu katika Kitabu chake, uongozi huo ukawa kwa Imam Abdullahi bin Wahabi Raasibiy (r.a) ambae pia ni Sahaba wa Mtume (s.a.w). Baada ya uchaguzi huo wa Imam Adbullahi Raasibiy (r.a) waliamua kwenda sehemu inayoitwa Naharawani. Imam Aliy aliwataka watu wa Naharawani kurejea katika safu zake, na wao walikataa wito huo, bali walimtaka Imam Aliy aje katika utiifu wa Kiongozi mpya wa Waislamu Imam Abdullahi bin Wahab Al-Rasibii (r.a). Hapo alishindwa la kufanya isipokua kuchukua hatua ya kwenda kumpiga vita Muawiyah bin Abi Sufyaan, lakini washauri wake walimshauri kwanza aende kwa hawa wa Naharawani; kwani wao wamesimamisha uongozi katika misingi ya kisheria, kwa hiyo ni kuvunjwa kabla ya kujiimarisha na kuwa kubwa nguvu yao. Imam Aliy alikubali ushauri huo, basi alikwenda kuwapiga vita vikali sana, nao walipigana kwa kujitetea, walizidiwa kwa uchache wao na wingi wa jeshi la Imam Aliy, waliuliwa wengi wao akiwemo kiongozi wao Imam Abdullahi bin Wahab Ar-asibiy (r.a) katika vita hivo vya kidhalimu[5], na wengine waliookoka nao walitawanyika ndani ya miji ya Iraq, miongoni mwao alikua ni Imam Abu Bilali Mir-daas bin Hudair Tamimi (r.a). Baada ya kumalizika vita vya Naharawan Imam Aliy alijuta sana, amepokea Baihaqi katika Sunan Kubraa riwaya no 16722 kuwa Shaqiiq bin Salamah alisema: ((Alisema mtu mmoja: Ni nani anamjua nyumbu siku waliyouliwa Washirkina? Anamaanisha Watu wa Naharawani. Akasema Aliy bin Abi Twalib: Ushirikina wameukimbia. Akasema (yule mtu): Basi ni Wanafiki? Akasema (Aliy): Wanafiki hawamtaji Allah isipokuwa kidogo. Akasema (yule mtu): Basi ni nani wao?! Akasema (Aliy): Ni watu wametufanyia uadui tukanusuriwa dhidi yao)) basi ilibainika katika jeshi lake kuwa vita vile vilikua ni vya kidhalimu; kwa sababu aisyekuwa Mshirkina wala Mnafiki huyo bila ya shaka ni Muumini sahihi, hapo walimuasi baadhi yao na kukimbilia katika safu za Muawiyah bin Abi Sufyaan, kisha zilifanywa njama za kumuuwa Imam Aliy[6], na ndio kama yalivyopangwa Imam Aliy aliuliwa[7] kwa mkono wa Abdurahman bin Muljim Al-Muradi[8] na hapo akabakia Muawiyah bin Abi Sufiyaan peke yake katika safu ya uongozi wa kisiasa kiubabe, jambo ambalo ilikuwa tishio kubwa kwa wapenda haki na kumuingiza Hassan bin Aliy bin Abi Twalib kusalimu amri kwa kufanya sulhu na Muawiyah na kupelekea kusimama rasmi Dola ya Muawiyah bila ya kuwepo upinzani wowote wenye nguvu za kumuelekea, na hapo aliendeleza utawala wake katika siasa mbaya sana ya kutisha na kuuwa kila anayepinga siasa hiyo, hali ikawa ya kutisha sana, hapo wale waliookoka katika vile vita vya Naharawani walifanya wito wa haki kwa njia ya siri, nao waliongozwa na Abu Bilali Mir-daas bin Hudair Tamimi (r.a), hawa walipinga siasa ya Dola ya Muawiya bin Abi Sufyaan na waliotawala baada yake, nao walifanya kazi kubwa sana ya kuwafikishia watu haki na kuwabainishia njia ya haki kwa siri kabisa, na Dola ya Bani Umayyah iliwatungia wapenda haki hao kila jina baya lisilopedwa na watu ili kuharibu sura yao katika vichwa vya raia kwa ujumla, lakini waliendelea na katika jamaa hii alijiunga mwanachuoni mkubwa anayekubalika na wote naye ni Imam Jabir Bin Zaid Al-Azdy (r.a), na kutokana na Elimu yake kubwa iliyoshuhudiwa na Maswahaba, akawa yeye ndio marejeo yao wote, na akawa ndio kiongozi wa kielimu baina yao, na kila siku zilivyoendelea ndio siasa ilivyokuwa mbaya zaidi kwa wapenda haki hao, na dhulma iliongezeka vibaya sana na usalama wa wapenda haki ulipungua, na maisha yao kuwa hatarini, katika hali hiyo aliamua Mir-daas bin Hudair huihama Iraq na kwenda katika Ardhi isiyofika hukumu ya viongozi wale madhalimu, naye alifuatwa na baadhi ya wafuasi wake, kiasi wote walifikia idadi yao Arobaini, nao walitoka katika miji ya Iraq, lakini mara khabari za kuhama kwao zilifika kwa mtawala wa Iraq, naye aliamrisha jeshi la wapiganaji elfu mbili litoke mara moja liende kuwarudisha au kurudi na vichwa vyao, jeshi hili lilikutana na wale Arobaini, na ikabidi vifanyike vita vikali sana, nao Elfu mbili walishindwa na kuuliwa baadhi yao, na kukimbia wengine waliobaki, ilikuwa ni fedheha kubwa sana kwa utawala, na hamaki na ghadhabu zilipanda kwa mtawala wa Iraq, na hapo alitowa jeshi la watu elfu nne, na hawa elfu nne walipofika katika uwanja wa mapambano waliwadoelea wale waliobaki katika arubaini, wakati wamo katika sala ya Ijumaa baina ya kurukuu na kusujudu, hapo waliwavamia na kuwaua wote bila kutoka hata mmoja, bila ya mmoja wao kujua mavamizi yale kutokana na unyenyekevu waliokua nao katika Sala zao, ilikuwa ni mwaka 61H. Khabari hizo zilopofika katika miji ya Iraq ziliwakasirisha sana wale wafuasi wake waliobaki katika miji ya Iraq, na kupandisha hamasa zao, na kuazimia kulipiza kisasi, huku mwanachuoni wao Imam Jabir Bin Zaid (r.a) akiwatuliza na kuwarejesha katika njia ya uadilifu, na hayo yalipelekea kuleta mgawiko wa kujimegua baadhi yao katika mwaka wa 64H, kujimegua huko kulipelekea kujitokeza makundi matatu yaliyoongozwa na viongozi wao watatu, na kumuacha Imam Jabir Bin Zaid (r.a) na waliobakia, hayo makundi matatu ni:
Makundi haya matatu yakaamua kuingia katika vita vikali sana, kwani walikuja na itikadi mpya ilizuwa hukumu mpya wasiyoijua Waislamu, na hukumu hiyo ni kuwa: “Kila anayemuasi Allah mtukufu huyo ni Mshirikina, damu yake na mali yake ni ngawira halali” kwa hivyo ukikataa kwenda katika vita unakuwa ni Mshirikina; kwa sababu kwa mujibu wa Itikadi yao kuwapiga vita Washirikina hasa walioritadi ni lazima katika sheria ya Allah. Hawa kutokana na itikadi yao hiyo kali sana, ilikua vita vyao ni vibaya sana, nao walifanikiwa kukamata baadhi ya Miji, lakini watu wenye itikadi hii inaonekana wazi kuwa hawatoendelea, kwa sababu vita viliwamaliza hawakuvuuka miaka mingi isipokuwa hakuna aliyebakia katika wao, na hawa ndiwo Khawariji kwa mujibu wa mafundisho sahihi ya Mtume (s.a.w); kwa sababu katika mafundisho hayo inabainika kwa uwazi kuwa Khawariji watahukumu Waislamu kuwa ni Washirikina na kuingia katika wimbi la kuwaua na kuhodhi mali zao na hawa ndivyo walivyofanya[9]. Ama wale waliobakia na Imam Jabir Bin Zaid (r.a), wao waliendelea katika msimamo sahihi, ule ule wa Abu Bilal Mir-daas bin Hudair (r.a), nao ni msimamo wa kujiimarisha kwanza kisha ndio kusimamisha Dola ya Kiislamu katika Uadilifu wa Uislamu, na hawa kwa sababu ya mmeguko uliotokea katika safu zao ililazimika kutangaza upotevu wa yale wakundi matatu, na kuidhihirisha haki na kuufedhehesha upotevu walioufanya, lakini kutokana na siasa ilivyokuwa ililazimika kazi hii aifanye mtu anayeweza kupata himaya ya kabila kubwa ndani ya Iraq, basi hakuwa mwengine isipokua ni kijana aliyejulikana kwa jina la Abdullahi bin Ibadh Tamimi (r.a), na hapo ikapelekea kuitwa wale waliomo katika msimamo ule kuwa ni wafuasi wa Ibn Ibadhi, na ndio mwazo wa kuitwa Ibadhi, kwa hivyo hapa tunaweza kuwatambulisha maibadhi kwa kusema: ((Maibadhi ni wale waliobakia katika mafundisho sahihi ndani ya Uislamu baada ya kuzuka fitna mapaka hivi leo)).[1]: Mapendwa moyo yamefanya kazi kubwa, hata kutungwa kisa hichi kuwa ni mkasa ulioandaliwa na Abdullahi bin Sabai, na kuwa wao walikuwa ni wafuasi wa Ibn Sabai na ndio waliokuwa Makhawarij baadae; Jee!! unawajua hao? baadhi yao ni hawa:
وقيل لهم تعالوا قاتلوا في سبيل الله أو ادفعوا قالوا لو نعلم قتالا لاتبعناكم هم للكفر يومئذ أقرب منهم للإيمان ((Na huambiwa: Njooni mupigane katika njia ya Allah au muhami. Wanasema: Lau tunajua kupigana tungeliwafuata nyinyi. Wao katika ukafiri siku hiyo ni karibu zaidi kuliko katika Imani)) Kwa hakika Maswahaba (r.a) wanaijuwa Amri hii vizuri sana, na wao hawakumuhami kiongozi kwa sababu waliona kuwa uongozi wake ulitoka nje ya uadilifu wa Uislamu, na hakuna matarajio ya kurejea, kwa hivyo kumuhami kiongozi ni kuihami dhulma, kwa sababu inatendeka chini ya kivuli chake, na Allah amekataza kusaidiana katika uadui na makosa, kama ilivyo katika Suuratu Taubah (5:2); basi wao hawakufanya makosa Allah awape radhi zake. [3]: Anasema Allah: فإن بغت إحداهما على الأخرى فقاتلوا التى تبغي حتى تفيء إلى أمر الله ((Na kama moja wapo katika makundi mawili litaasi (kwa kufanya uadui) juu ya mwenginge, lipigeni vita hilo lililofanya uadui mpaka lirejee katika Amri ya Allah (ya kuacha uadui))). Hii ndiyo Amri ya Allah katika kulipiga kundi lililoasi (Fiatu Al-Baaghiyah), ili iwe ni sababu ya kuvunja uadui wao kwa mwenye haki. [4]: Na hapa tunaona baadhi ya waandishi wanaomnusuru Imam Aliy katika kosa hili wanamtetea kwa kukisia kukubali Mtume (s.a.w) kufuta jina la Utume katika Sulhu ya Hudaibiya, basi kukisia huko ni batili kwa sababu zifuatazo:
Anapiga mfano Sheikh Salimiy (r.a) katika hali mbili hizi kwa kusema: “Mfano wa Utume ni mfano wa Mama haiwezi kuondoka kuwa ni Mama wa mtoto wake ikiwa atakubali au atakataa, ni sawa kama atakataa mwengine au hakukataa, haki zake zimethibiti; na mfano wa uongozi ni mafano wa mke wa mtu amekuwa mke wake kwa fungo sahihi la ndoa na kuridhia mwanamke na kwa idhini ya walii wake, na itaondoka hukumu ya kuwa ni mke kwa talaka, au khulugh (kujivua mwanamke) na kwa njia zote za kuondosha hukumu hiyo” [5]: Hakuna shaka kuwa watu hawa walipigwa vita kidhalimu, kwa sababu Imam Aliy hakuwa tena kiongozi kwa kulivua jina hilo kabla ya sulhu, na kuondolewa katika uongozi na msuluhishi wake. [6] :Wengi wanasoma na kuambiwa kuwa waliomuuwa Imam Aliy ni miongoni mwa wale watu wa Nahrawani, na kinaletwa kisa kizuri cha kukutana watatu katika wao nao ni Abdulrahman bin Muljim na Buraak bin Abdillah na Amru bin Bakr, na kuwa Abdulrahman bin Muljim alikutana na mwanamke nzuri wa kupita kiasi anayeitwa Qatwaam, na mwisho wa kisa ndio Abdulrahman alimuuwa Imam Aliy. Tunasema kuwa kisa hichi ni batili; kwa sababu hakikuthibiti kwa mapokezi sahihi, kisa hiki amekipokea Twabariy na Twabaraniy na Ibn L-Athir na Al-Hakim na Baladhuriy; na katika mapokezi ya kisa hiki yumo Otham bin Abdlrahman Taraaifiy Al-Harraniy, naye anaitwa Abu Abdlrahman, amesema:
Na mpokezi huyu yumo katika mapokezi ya Twabariy na Twabaraniy, ama mapokezi ya Ibn L-Athir ni mapokezi yaliyokatika kwa sababu mpokezi wake ni Muhammed bin Saad aliyezaliwa mwaka 168H na Imam Aliy alikufa mwaka 40H basi ameyapata wapi? Na vile vile katika mapokezi hayo yumo Husain bin Fahm, na yeye sio wa kutegemewa ameyasema hayo Daar-qutniy. Ama mapokezi ya Haakim yumo ndani yake Ismaili bin Abdlramhan Saddiy ambaye ndie mpokezi, na huyu hakushuhudia mauaji ya Imam Aliy kwa sababu yeye ni wanaohisabiwa kuwa ni wa tabaka ya nne, na pamoja na kukatika kwa mapokezi haya bwana huyu hajasalimika na majeraha amesema:
Ama mapokezi ya Baladhuriy pia yamekatika; kwa sababu Shaabiy hakuhudhuria makutano ya Ibn Muljim na wenzake wakati walipopanga mpango huo. Basi kutokana na haya vipi mapokezi hayo yakubaliwe na jambo hilo liwe ni la uhakika lisilokubali kurejeshwa? Kwa hakika hayo ni katika ya ajabu. Juu ya yote haya Amesema Sheikh Saabii: :Hakika makubaliano yamepita kuwa Ibn Muljim ndie aliyemuua Imam Aliy”. Kwa hiyo hili halina shaka, ama kisa hakikubaliki. [7]: Anajiuliza Ustadh Ahmed Sulleiman Maaruf akisema: Jee!! Upanga uliomuua Aliy ulikuwa ni upanga wa Kikhawariji kweli? Au ulikuwa ni upanga wa kisasi cha kibinafsi cha baadhi ya waliouliwa wa Nah-rawan, wala hakuna mkono wa Khawariji wote ndani yake? Au ni ujumbe wa kimapenzi wa mwanamke wa kikhawarij jina lake Qutwaam? Au ni pigo la kunyemelea na mipango ya kisiasa lilipitishwa kwa jina la Khawarij na mkono kwa Mjanja wa Shaam na mshauri wake hodari Amru bin L-aas? Alisema Muhammad bin Mah-buub bin Ruhail Qurashiy (r.a) -ni katika wanavyuoni wakubwa wa Kiibadhi katika mwisho wa karne ya pili ya hijiriya- alipoulizwa kuhusu Ibn Muljim: Sijamsikia yeyote akimsifu wala akimlaumu, wala hakijanifikia chochote kuhusu yeye” Ikasemwa: Pengine hayo (mauaji) ni kwa mipango? akasema: Hapana” Anasema Ustadh Ahmed Siyabiy: Abdul-rahman bin Muljim ni mtu ameingizwa katika safu za Muhakkima au Ahalu Nahrawani uingizo, na akachanganywa na wao mchanganyo, pamoja na kuwa yeye hajulikani katika safu zao.. na neno la Imama huyu: Sijamsikia yeyote akimsifu” ni kwa sababu hayumo katika wao wala hana fungamano nao; na neno lake: Wala akimlaumu” kwa sababu ya kujitakasa kwao na kujiweka mbali na matusi na kulaani ovyo ovyo. [8]: Anasema Ustadh Ahmed Siyabiy: Mambo yalivyo hasa ni kuwa Ibn Muljim alitengenezwa kwa njia ya Ash-ath bin Qais, nalo ni jambo la kitabia kutimia hayo kwa msukumo wa Muawiyah au kujua kwake” Basi maneno haya yana mtazamo wake; kwa sababu tuangalie matokeo ya kitarekhe ya Bwana huyu anayeitwa Ash-ath bin Qais:
Basi ndio akasema Ibn Abi L-hadiid: “Kila Uharibifu katika Utawala wa Aliy – Alaihi Salaam- na kila mvurugiko uliotokeza asili yake ni Ash-ath” na Shaharistaani anamzungumzia Ash-ath kwa kusema: Ni katika waliotoka sana kwa kumpiga vita (yaani Imam Aliy) na waliotoka katika Dini” Na kwa hakika suala hili halihitaji utafiti mkubwa, kwa sababu uhakika ukulikuwa ni kuondosha upinzani katika uwanja wa siasa, na ukiangalia siasa ya Dola ya Bani Umayyah tokea mwanzo wake mpaka mwisho wake –isipokuwa kipindi cha Omar bin Abdulazizi (r.a)- utaliona jambo hili liko wazi kama jua:
Basi ni katika tabia tukaona katika watu wa Imam Aliy yuko anayemtuhumu Muawiyah anasema Abu L-aswad Dualiy: ألا أبلغ معاوية بن حرب * فلا قرت عيون الشامتين أفي شهر الصيام فجعتمونا * بخير الناس طرا أجمعين Ee mfikishie Muawiya bin Harb * Hayajatulizana Macho ya wanaotukana Jee!! katika mwezi wa Funga mumetuvamia * Kwa mbora wa Watu wote. Juu ya yote hayo tulioleza kuhusu khabari hizi, ifahamike kuwa hata kama ni kweli mashirikiano hayo yalitokezea na yalifanywa na Ibn Muljim na wenzake, na wao ni miongoni mwa watu wa Nahrawani, basi kitendo hicho kinawarejea wenyewe; kwa sababu hakikufanywa kwa makubaliano wala kwa hukumu iliyotoka kwao, na ndio akasema Mas-udiy: Na wengi katika Makhawarij wanajitenga na Ibn Muljim kwa kumuuwa Imam Aliy kificho” Basi hili lifahamike vizuri. 9: Hili ni Jambo linalobabaisha wengi, na mapendwa moyo katika sehemu hii yanafanya kazi, kwa sababu wengi waliopandikiziwa yasiyokuwa ya ukweli na kuwapelekea kuwakusanya Maibadhi na Khawarij katika hukumu moja ya Ukhawariji, na hili bila shaka ni kosa, tena ni kosa lisilokuwa na shaka, na kosa hili linapatikana hasa hasa kwa sababu mbili:
Ama sababu ya mwanzo inapatikana kwa kuwa hawa waliotoka katika utiifu wa Imam Aliy kwa sababu ya kubainika kwao makosa ya wazi upande wake, na baada ya kuwa wao ni sehemu ya jeshi lake, basi kwa vile walijitoa ndio wakaitwa Khawarij na sio kwa sababu nyengine yoyote, na hukumu hii kwa maana hii haiwakamati wao tu, kwa sababu hata Twalha bin Ubaidillahi na Zubeir bin Awwaam nao walifanya hivyo, bali sio hivyo tu wao hawa yaani Twalha na Zubair walikusanya jeshi hasa na kumpiga vita Imam Ali, kwa hivyo na wao watakuwa ni Makhawarij kwa zingatio hili, basi jina hilo likitumika kwa maana hii tu hakuna tatizo kwani wataingia katika hukumu ya Ukahwariji wengi wengine wasiokuwa Ibadhi kama vile Twalha na Zubair na Muawiyah na Amru na waliokuwa pamoja nao. Ama sababu ya pili ni kuwa yalitokezea makundi hayo matatu yaliyojimeguwa katika safu za waislamu waadilifu, na waislamu wote –Ibadhi na wasiokuwa Ibadhi- walikubaliana kuwajuwa hawa kwa jina la Khawarij, lakini mara hii jina hili lilibeba maana nyengine sio ile ya mwanzo, mara hii lilibeba sura ya kutoka katika Dini, kwani ulikuwa kwao uhakika wa kuitoka Dini alioubashiria Mtume (s.a.w) katika mafundisho yake, basi kutoka kwao hawa ni kwa sababu ya kuhukumu kwao hukumu ambazo zinakwenda kinyume na mafundisho sahihi ya Uislamu yanayojulikana kidharura na kwa makubaliano. Basi kutokana na kufanana majina haya mawili; wasiojua uhakika wakachanganya mambo, na hapo ikapatikana fursa kwa wale wenye kubeba sababu ya pili, basi wakaanza kuchanganya hukumu za hawa na kuwapa wale na kuzidi uchafuzi wa uhakika, na haya ndio yaliyomo katika maandiko ya wengi tokea kuanza kwa utunzi, lakini uhakika vyovyote utakavyofichwa hauwachi kujitokeza, hili lifahamike. Na kutokana na uhakika huu ndio akasema Sheikh Saalimiy (r.a): ((Na ujuwe kuwa jina la Khawarij lilikuwa katika wakati wa mwanzo ni sifa nzuri, kwa sababu ni mkusanyo wa waliotoka, nalo ni kundi lililotoka kwa kupigana katika njia ya Allah mtukufu, amesema Allah aliyetukuka: (Na wangalitaka kutoka wangalitayarisha siliha kwa ajili yake) kisha jina hili likawa ni sifa mbaya kwa wingi wa tafsiri za walioko kinyume na watu wa haki, tafsiri zao za kuzifasiri hadithi za sifa mbaya watakazosifika nazo watu waovu katika mwisho wa wakati, kisha likazidi jina hilo kuwa baya pale walipolitumia Azaariqah na Suf-riyah, basi jina hilo ni katika majina yaliyofichika sababu yake na kuharibika kwa makusudio ya majina mengine, kutokana na hayo utawaona As-habu wetu (Maibadhi) hawajiiti wao kwa jina hilo na wanajiita Ahlu Istiqaamah kutokana na Istiqaamah waliyonayo katika Dini)). Basi hii ndio sababu kubwa inayowafanya Maibadhi kulikataa jina hilo la Khawariji na kulizingatia kwa wengine kwa mujibu wa mafundisho, wamejiepusha nalo kutokana na ufahamu mbaya unaochukuliwa kwa sifa zake mbaya, kwa sababu jina sio muhimu lakini maana inayobebwa na lile jina ndio muhimu, basi Maibadhi kwa maana hizo za upotofu sio Khawarij, na wala hatuwezi kuwaita Khawarij kwa sababu ya kuenea maana hizo zilizoenezwa kwa waliobeba jina hilo. Kwa hivyo Ibadhi sio Khawarij. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliyejaalia kupambanuka vitu kwa mahusisho yake, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad pamoja Aali zake na Masahaba wake na kila mwenye kuongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya Malipo.
Allah mtukufu -kwa rehma zake na fadhila zake- ametuletea Mtume mwema kabisa naye ni Muhammad (s.a.w) ambaye aliuacha umma huu katika njia safi ya uongofu, usiku wake ni kama mchana wake, hapoteni ndani yake isipokuwa mpotevu wa wazi kabisa, lakini -kwa masikitiko makubwa kabisa- baada ya kupita miaka 28 tu ya kipindi cha mwanzo cha Makhalifa wanne waongofu -Allah awe radhi nao- umma huu ukakumbwa na mawimbi makali sana ya tofauti za kisiasa na kufikwa na mtihani mkubwa wa utawala wa kundi la waasi ilitawala kimaabavu kwa kipindi cha miaka 90, matokeo yake baada ya kumalizika karne ya mwanzo ukajikutia katika mawimbi mengine makali sana ya tofauti za kiitikadi na kifiqhi zilizosababisha mawimbi makali ya kupaikana firaqu na madhehebu na kufikia kutupiana tuhuma na hukumu kali kali zilizowaingiza waislamu katika uhasama wa wao kwa wao katika tarehe yao mpaka hivi leo.
Ni kweli kuwa Wanavyuoni katika kila wakati ndiwo wanaobeba jukumu kubwa zaidi la kuuhifadhia umma umoja huu wake na kushikamana kwake, lakini wakati huo huo siasa za serikali -mara nyengine- huchochea na huchangia katika kuzipa nguvu tofauti hizo kwa kuifanya madhehebu fulani kuwa hakimu wa kuhukumu madhehebu nyengine zilizobaki, na miongoni mwa walioteseka sana kwa tuhuma batili za kila namna na kupigwa vita vikali kwa kila njia ni Maibadhi na madhehebu yao, lakini juu ya yote yaliyotokezea, na ambayo mpaka leo hii yanaendelea kutokezea, madhehebu hii ya Ibadhi iliweza kujipatia nguvu zake wenyewe kwa wenyewe na kuweza kubakia mpaka hivi leo ikiwa ni kusudio la kila mtaka haki ulimwenguni ikitegemea nguvu za hoja na dalili za wazi mbele ya hoja za nguvu na upotoshaji zilizotumika dhidi yake.
Na sote tunafahamu kuwa madhehebu yenye nguvu zaidi katika jamii za Kiislamu ni madhehebu ya kisunni ambayo kimaarufu inajulikana kwa jina la Ahalu Sunna Wal-Jamaa, nayo ndiyo Madhehebu inayoishi zaidi na Ibadhi katika miji tofauti ulimwenguni, kutokana na hapo -bila shaka- wapo wengi wanaotaka kujua ni tofauti gani hasa za msingi zilizopo baina ya Ibadhi na Sunni?
Twabaan tafauti ndizo zilizojenga umadhehehebu; kwa sababu hakuna umadhehebu katika yenye makubaliano ndani yake, na bila shaka kuwepo tafauti ni jambo la msingi katika maisha ya Binadamu; kwa hiyo anayepinga kutafautiana huyo ni mwenye kuhangaika bila mafanikio yoyote, wala si hekima kupinga kutafautiana, lakini linalolazimika kwetu sote ni kushirikiana pamoja na kulinda mshikamano wetu katika yale tuliyokubaliana, na kila upande uheshimu mwengine katika yale yenye tafauti baina yetu.
Ibadhi kwa upande wetu hatuna hukumu zinazopelekea kuufanyia uadui upande wowote uliotafautiana na Ibadhi kimadhehebu, na hatujali katika hilo hukumu za wengine dhidi yetu; kwani mwisho kila upande unabeba majukumu yake kwa mujibu wa mafundisho yake.
Basi hapa tunatoa tofauti za msingi zilizopo baina ya madhehebu hizi mbili Ibadhi na Sunni, na baada ya kufuatilia kiundani tufahamu kuwa tofauti zilizopo baina ya Ibadhi na Sunni Kiitikadi zimejengeka katika msingi miwili mikubwa nayo ni:
1. Msingi wa kumsifu Allah mtukufu.
2. Msingi wa Imani na Ukafiri.
Pia ziko tofauti za Kifiqhi (Matendo), lakini hizi sio nyingi sana na hazina mivutano sana.
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Baada ya kuona misingi yenye tofauti baina Ibadhi na Sunni tunaingia katika kufafanua msingi wa mwanzo ambao ni:- KUMSIFU ALLAH MTUKUFU. Ibadhi na Sunni wametofautiana katika suala la Sifa za Allah mtukufu, na kupelekea hilo kutofautiana katika mazalio yake, na ufunguo wa kuzifahamu tofauti za msingi huu ni suali hili: Jee! Sifa za Allah ni vitu vyengine visivyokuwa Allah mtukufu, au si vitu vyengine visivyokuwa Allah mtukufu? 1. SIFA ZA ALLAH MTUKUFU:
Kisha Sunni wakatafautiana baina yao tafauti ya kukufurishana wenyewe kwa wenyewe, na hilo limepelekea kuwaniana jina la Usunni (Ahlu Sunna Wal-Jamaa), kwani walipoyafika matamko ambayo kiudhahiri yanamaanisha maana za hisia zenye kujenga maana za kimwili kama vile mikono, uso, mguu, ubavu, kulia, kushoto, kukaa kitako, kushuka, kupanda, kuwa na sura n.k. hapo wakagawika makundi mawili:
لأن الحي القيوم يفعل ما يشاء، ويتحرك إذا شاء، ويهبط ويرتفع إذا شاء، ويقبض ويبسط إذا شاء، ويقوم ويجلس إذا شاء، لأن أمارة ما بين الحي والميت التحرك، كل حي متحرك لا محالة، وكل ميت غير متحرك لا محالة “Kwa sababu aliye hai msimamisi mkuu anafanya anachotaka, anatikisika akitaka, na anateremka na anapanda akitaka, na anakunja na anakunjua akitaka, na anasimama na anakaa kitako akitaka; kwa sababu alamaa inayo tafautisha baina ya aliye hai na maiti ni kufanya harakati, kila aliye hai anatikisika kwa hali yoyote, na kila maiti hatikisiki kwa hali yoyote.” [Rf. Othman Daarimi – Naqdhu uk. 71] Sunni hawa wanajulikana zaidi kuwa jina la Mawahabi, nao aghlabu ni wafuasi wa Madhehebu ya Hambali kifiqhi, na ubaya wa Sunni hawa ni kuwepo maandiko ya Maimamu wao wakuu yenye kuhimiza kuua na kufanya uadui dhidi ya kila muislamu asiyekubaliana na wao katika kumsifu Allah mtukufu kwa viungo na harakati kama wanavyomsifu wao, na katika hilo wamewatungia jina wasiokubali itikadi yao katika kumsifu Allah mtukufu kwa sifa hizo za viungo na harakati kwa kuwaita Muattwila. 2. KUONEKANA ALLAH MTUKUFU:
3. QUR-ANI NI KIUMBE AU SI KIUMBE:
ZINDUO NO 1. Fahamu kuwa Ibadhi hatuitakidi kuwa sifa za Allah ni vitu vyengine visivyokuwa Allah, kwa maana hiyo tunamsifu Allah kwa sifa ya usemaji na sio kwa sifa ya maneno kinyume na Sunni na Jahamia. ZINDUO NO 2. Fahamu kuwa Sunni Ash-ariya na Maturidiyah wamezingatia kuwa Qur-ani isiyokuwa kiumbe sio hii tunayoisoma, bali ni sifa ya maneno ya Allah isiyoachana na dhati yake Allah mtukufu wameiita (Maneno ya Kinafsi), ama hii Qur-ani tukufu tunayoisoma wanaitakidi kuwa ni kiumbe kama wanavyoitakidi Ibadhi sawa sawa, na wako baadhi ya Masheikh wa Ibadhi walisema neno kama lao sawa sawa. Amesema Imam wa Kisunni Al-Baijuri katika Tuhfatu Al-Muridi Alaa Jauharati Tauhidi Uk. 160: ((Na Madhehebu ya Ahalu Sunna ni kuwa Qur-ani kwa maana ya Maneno ya Kinafsi sio kiumbe, ama Qur-ani kwa maana ya tamko ambalo tunalisoma (Quraani) hiyo ni kiumbe)). |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi MSINGI WA IMANI NA UKAFIRI: Huu ni msingi wa pili, nao unakamatana na matawi mingi ya kiitikadi yenye tofauti ndani yake baina ya Ibadhi na Sunni, na ili tuweze kulifahamu hili vizuri inabidi kwanza tuwe waadilifu wa kukubali ufahamu walio nao Ibadhi na Sunni katika msingi huu. IBADHI NA SUNNI: wote wanaamini kuwa imani inakabiliana na ukafiri, hili halina tofauti ndani yake, na kwa maana hiyo mkalifishwa kisheria ikiwa sio muumini huyo atakuwa ni kafiri kwa makubaliano ya wote. IBADHI: wanaamini kuwa Imani ni usadikisho kamilifu, kwa maana usadikisho huo hauwezi kuwepo -kwa mujibu wa kisheria- isipokuwa kwa kupatikana uhakika wake kikamilifu kwa mja mkalifishwa ambae ni kila baleghe mwenye akili timamu aliyefikiwa na hoja ya kisheria. Usadikisho huu -kwa mujibu wa mafundisho ya Ibadhi- utapatikana uhakika wake katika kwa kuzingatia mambo matatu:
Basi yoyote atakaye kuwemo katika asi (dhambi) kubwa la kiitikadi au kimaneno au kivitendo huyo hatakuwa muumini wa kweli mpaka atubie kwa Allah mtukufu, kwa hakika Ibadhi haikubali kuacha nafasi yoyote ya kubakia mja katika kumuasi Allah mtukufu. Kwa maana hiyo, mja aliyejitosa katika dhambi kubwa yoyote huyo -kwa mujibu wa mafundisho ya Ibadhi- hatakuwa muumini, na kwa maana hiyo atakuwa ni kafiri, na kuwa kwake kafiri hakulazimishi kuwa ni mshirikina -hii ndiyo Itikadi ya Ibadhi kwa mtenda dhambi kubwa yoyote-, na iwapo atatubia basi atarejea katika safu za waumini wa kweli. SUNNI: wanaamini kuwa Imani ni usadikisho wa moyoni na ulimini tu, kwa maana hiyo -kwa mujibu wa mafundisho ya Kisunni- imani itaendelea kuwepo kwa mja mkalifishwa ikiwa tu atakua ni mwenye kusadikisha katika moyo wake na ulimi wake hata kama yumo katika madhambi makubwa. Kwa maana hiyo uhakika wa Imani -kwa mujibu wa mafundisho ya Kisunni- utapatikana kwa mja katika vitu viwili tu:
Ama matendo ya mja katika utiifu kwa kutenda amri au kuepuka katazo: hayo -kwa mujibu wa Itikadi ya Kisunni- hayaathiri kitu katika asili ya Imani, kwa maana hiyo, yule atakayekuwemo katika maasi yasiyokuwa ya kishirikina bila ya kuitakidi uhalali wa maasi hayo huyo atazingatiwa kuwa ni muumini wa kweli, anayo Imani kisheria, hata madhambi hayo yawe makubwa namna gani na mingi namna gani. Kutokana na hapo, yoyote atakaye kuwemo katika asi lolote kubwa lisilokuwa la kishirikina, ikiwa asi hilo ni la kiitikadi au kimaneno au kivitendo, huyo -kwa mujibu wa itikadi ya Sunna- atakuwa ni muumini wa kweli hata kama hatatubia kwa Allah mtukufu, kutokana na hapa tunagundua kuwa mafundisho ya Kisunni yanatoa mwanya mkubwa wa kuasiwa Allah mtukufu; kwani muislamu asi -hata ajitose katika madhambi namna gani- hatasifika kwa ukafiri ikiwa tu hajaasi kwa dhambi ya ushirkina, na kuwa mja huyo anakatiwa pepo kwa hali yoyote; kwa sababu ni muumini. MATOKEO: Mja mkalifishwa aliyejitosa katika dhambi kubwa yoyote isiyokuwa ya Kishirikina:
Mfano:
Hiyo ni mifano mitatu tu, lakini hayo tuliyofafanua yanaingia katika maamrisho yote na makatazo yote kwa madhambi yote yasiyokuwa ya kishirkina. ZINDUO 1. IBADHI: Wanaitakidi kuwa Imani inavunjika kwa dhambi kubwa yoyote ila akitubia muhusika wake, basi Ibadhi hawasemi kuwa Imani inapungua kwa kumuasi Allah kwa dhambi kubwa isiyokua ya kishirikina. Kutokana na hapa tunafahamu kuwa daraja ya chini ya Imani -kwa mujibu wa Ibadhi- ni kutokuwemo mja katika dhambi kubwa yoyote, tena baada ya hapo inaongezeka kila mja anapomtii Allah mtukufu kwa kufanya aliyoamrisha na kuepuka aliyokataza, na inaweza kudhoofika kwa uvivu wa ibada za nyongeza na kuimarika kwa ukakamavu wa ibada za nyongeza. SUNNI: Wanaitakidi kuwa Imani inapungua kwa kumuasi Allah mtukufu kwa madhambi makubwa, na kwa hiyo muislamu aliyejitosa katika madhambi makubwa huyo ni muumini wa kweli mpungufu wa imani, na imani yake itakamilika kwa kutubia kwa Allah mtukufu. ZINDUO 2. IBADHI: Wanaitakidi kuwa Ukafiri haumaanishi Ushirikina, bali Ukafiri na Ufasiki na Udhalimu yote hayo yanamaanisha kusudio moja, basi kila kafiri ni fasiki na dhalimu, kama ilivyokuwa kila dhalimu ni kafiri na fasiki, kama ilivyokuwa kila fasiki ni dhalimu na kafiri, hakuna tofauti baina yake, kutokana na hapo -kwa mujibu wa mafundisho ya Ibadhi- UKAFIRI una daraja mbili:
Basi fahamu kuwa -kwa mujibu wa Itikadi ya Kiibadhi- kila mshirkina ni kafiri lakini sio kila kafiri ni mshirkina, kama ilivyokua kila muumini wa kweli ni muislamu lakini sio kila muislamu ni muumini wa kweli. SUNNI: Wanaitakidi kuwa Ukafiri unamaanisha Ushirkina, kwa maana hiyo kila kafiri ni mshirkina na kila mshirikina ni kafiri; basi muislamu hatokuwa kafiri isipokuwa kwa kuritadi kwa kuacha uislamu au kufanya dhambi ya kishirkina au kuitakidi uhalali wa maasi anayoyafanya. ZINDUO 3. IBADHI INAONA KUWA:
ZINDUO 4: SUNNI: Kwa sababu wao wanaitakidi kuwa Ukafiri ni Ushirkina kama Makhawariji -ingawa wametofautiana na MAKHAWARIJI katika aina ya madhambi ya ukafiri- wakaingia katika kosa la kuwakusanya Ibadhi katika safu za MAKHAWARIJI bila kujali tofauti iliyopelekea kutofautina baina yao; kwani Sunni waliona kuwa ikiwa Ibadhi wanaitakidi kuwa kila mtenda dhambi kubwa ni kafiri basi hakuna tofauti baina yao na Makhawariji; kwani hiyo pia ndio Itikadi ya Makhawariji kuwa kila mtenda dhambi kubwa ni kafiri, na likapelekea hilo kuchukua maovu ya Makhawariji na kuwabandika nayo Ibadhi kidhulma. Kutokana na hapo haiwezekani kuujua Uibadhi kwa kupitia Sunni wala kwa kupitia Shia; kwani uhakika wa Ibadhi umeharibiwa na kuchafuliwa katika maandiko ya Masunni na Mashia. IBADHI: Kweli wamekubalina na Makhawariji katika itikadi ya kuwa kila kosa kubwa ni ukafiri, lakini Ibadhi wametofautiana na Makhawariji na Masunni katika Itikadi ya kuwa Ukafiri ni Ushirkina, itakadi ambayo:
|
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Ni jambo la fakhari na heshima kubwa, pia nafsi inatulizana ndani yake; tunapoona mapokezano ya dini kielimu kwa Maimamu na Wanavyuoni wa Kiibadhi, hayo yanapatikana tokea zama za Mtume (s.a.w) kizazi kwa kizazi mpaka hivi leo, bila ya kukhitalifiana ndani yake katika mambo muhimu ya dini kiitikadi na kimatendo, na huu hapa ni mtiririko wa wanavyuoni wakubwa tokea kwa Masahaba waliochukuwa dini kutoka kwa Mtume (s.a.w) mpaka hivi leo, na tunaanza na kwa Maswahaba (r.a) na Matabiina, karne kwa karne mpka zama zetu hizi (R.A). Karne ya kwanza: Imamu Sahaba Abdullahi bin Wahab Raasibiy, Sahaba Zaid bin Souhan Al Abadi, Sahaba Hurquus bin Zuhair Al Saadi, Sahaba Mazin bin Ghadhubah Saadiy, Sahaba Seif bin Hubairah Qurashiy, Sahaba Sohar bin Abaas Abadiy, Tabii Mirdas bin Hudair Tamimiy, Tabii Jabir bin Zaid Uzudiy, Tabii Abdullahi bin Ibadhi Tamimiy ambae madhehebu yamenasibishwa na yeye. Allah awawie Radhi. Karne ya pili: Imamu Abu Ubaidah Muslim bin Abi Karimah Tamimiy, Rabii bin Habib Farahidiy, Mahboub bin Ruhail bin Seif bin Hubairah Qurashiy, Munir bin Nayir Jaalaniy Riyamiy, Muhammad bin Mualaa Kindiy, Bashir bin Mundhir Nizwaniy, Mussa bin Abi Jabir Azkawiy, Julan-nda bin Masoud, Kahlan bin Atiyah. Allah awawie Radhi. Karne ya tatu: Mussa bin Aliy Azkawiy, Muhammad bin Mah-bub Qurashiy, Salti bin Khamis Kharusiy, Muhammad bin Jaafar, Bashir bin Muhammad bin Mahboub, Mualaa bin Munir (r.a). Karne ya nne: Muhammad bin Said Kudamiy, Abu Muhammad bin Barakah, Hawariy bin Oth-man, Muhammad bin Abdillah (r.a). Karne ya tano: Hasan bin Said bin Quraish, Salamah bin Muslim Sohariy, Abu Hasan Basyawiy, Muhammad bin Issa (r.a). Karne ya sita: Khadhar bin Sulaiman , Ahmed bin Abdillah bin Mussa, Muhammad bin Ibrahim bin Mussa, Abdullah bin Muhammad bin Ibrahim (r.a).
Karne ya saba: Ahmed bin Nadhir bin Sulaiman, Abu Omar Nakhaliy, Said bin Ahmed bin Mahmoud, Abu Mukyal Mussa bin Kahlan, Abu Othman bin Abi Abdillah Asam (r.a). Karne ya nane: Said bin Ahmed bin Muhammad, Abu Kasim bin Abi Shaaiq, Abdurahman bin Abi Shaaiq, Sulaiman bin Rashid bin Saqr Adawiy, Dahman bin Rashid bin Saqr Adawiy (r.a). Karne ya tisa: Aliy bin Abdilbaqi, Ahmed bin Mufarij, Abu Hasan bin Khamis bin Amir (r.a). Karne ya kumi: Muhammad bin Abdilhaqi, Abdullahi bin Omar bin Ziyad Shaqsiy, Muhammad bin Ahmed bin Ghasaan, Ahmed bin Maddad, Muhammad bin Abdillah bin Maddad (r.a). Karne ya kumi na moja: Khamis bin Said Shaqsiy, Massoud bin Ramadhan Nabhaniy, Khamis bin Ruweishid Majrafiy, Saleh bin Said Zamiliy, Abdullahi bin Muhammad bin Ghasaan Kindiy (r.a). Karne ya kumi na mbili: Said bin Bashir Subhiy, Jaaid bin Khamis Kharusiy, Said bin Ahmed Kindiy, Khalef bin Sinan Ghafiriy, Nasir bin Sulaiman, Muhammad bin Maddad (r.a). Karne ya kumi na tatu: Said bin Khalfan Khaliliy, Saleh bin Aliy Harithiy, Muhammad bin Sulaim Gharibiy, Nasir bin Jaaid Kharusiy, Sultan bin Muhammad Batashiy (r.a). Karne ya kumi na nne: Abdullahi bin Humaid Salimiy, Amir bin Khamis Kindiy, Muhammad bin Abdillahi Khaliliy, Nasir bin Salim bin Adiim Rawahiy, Majid bin Khamis Abriy, Abdullahi bin Muhammad Riyamiy (r.a). Karne yetu ya kumi na tano: Ahmed bin Hamed bin Sulaiman Khaliliy, Majid bin Khamis Abriy, Abdullahi bin Muhammad Riyamiy, Issa bin Saleh Harithy, Khalfan bin Jamil Siyabiy, Humoud bin Humaid Sawafiy, Said bin Mabrouk Qannubiy (r.a). Basi angalia mtiririko wa Maimamu na Mashekhe waaminifu katika dini, waliokua mbali na kila uongo na waongo, unaposoma mtiririko huu moyo unafarijika na utulivu unapatikana, na yamepokewa kua Mtume (s.a.w) amesema: “يَحْمِلُ هَذَا الدِّيْنَ مِنْ كُلِّ خَلَفٍ عُدُوْلُهُ يَنْفُوْنَ عَنْهُ تَحْرِيْفَ الْغَالِيْنَ وَانْتِحَالَ الْمُبْطِلِيْنَ وَتَأْوِيْلَ الْجَاهِلِيْنَ” “Wataichukua Dini hii katika kila watakaokuja Waadilifu, wataiwekea mbali uharibifu wa wenye kuchupa mipaka, na waliojifanyia Wabatilifu, na Tafsiri za Wajinga…” Basi waadilifu walioitwa Maibadhi wameichukua dini hii kielimu na kimatendo tokea kwa Mtume (s.a.w) mpaka hivi leo karne ya kumi na tano, na wao wamo katika kazi hiyo aliyoisema Mtume (s.a.w), hawadhuriki na wenye kwenda kinyume na wao, na hiyo ndio hali yao. Na la kuituliza nafsi ni kuwepo maandiko yaliyohifadhiwa tokea karne ya pili mpaka hivi leo, hata barua ya Mtume (s.a.w) mwenyewe kwa watu wa Oman ipo imehifadhiwa, zipo sera za Maimamu na vitabu tokea karne ya pili mpaka hivi leo, atayakubali haya mwenye kuyakubali na atayakataa mwenye kuyakataa, lakini uhakika utabakia pale pale. Na la jengine linaloifanya nafsi ya mwenye kuujua uhakika huu iwe na utulivu zaidi, ni kua Allah amejaalia kubakia uongozi wa Uislamu katika ardhi ya Oman kama ulivyofuatwa na Abubakar na Omar (r.a) katika uadilifu wa Uislamu tokea karne ya pili mpka karne ya kumi na nne (132A.H/750A.D→1374A.H/1956A.D). Basi tuwe na wasi wasi gani baada ya haya yasiyokua na shaka? Na ameshuhudia katika hili kila muadilifu mpaka yakasajiliwa na mkono wake Dr. Ghabaash -na yeye sio katika Maibadhi- maneno haya: “Kwa hakika ilipata Harakati ya Kiibadhi muweko wake wa Kiitikadi na Kifikra katika Wakati wa mapema. Na kutokana na kuhifadhi kwake Msingi wa Shuraa na Uchaguzi Huru wa Maimamu, Msingi wa Makubaliano na kufungana Ahadi, inawezekana ikahesabiwa au ikajiisabu wenyewe kuwa ndio warithi wa uhakika wa mfumo wa Makhalifa walioongoka, na hasa Kipindi cha Mwanzo wake, kipindi cha Abu Bakr na Omar.”([1]) [1]. Uman Dimuqratiyya Islamiyya. uk. 11 |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Amesema Sheikh Abu Al-Hassan Aliy bin Mohamed Al-Basiyawi (r.a): Nimechunguza itikadi nyingi tofauti ndani na nje basi sikupata itikadi iliyo safi kuliko itikadi yetu, na lau tunajua itikadi nyengine ni bora zaidi kuliko hiyo tusingali ikubalia Jahannamu kwa nafsi zetu, basi inatulazimu katika zama zetu na baada ya zama zetu tujishike vizuri na kamba ya Allah ambayo ni Qur-ani, na yale waliyotunukulia Maulamaa wetu Allah awarehemu, kwani wao ni wakweli, na sisi tumewasadiki na tumekubali kutoka kwao, na tumemtegemea Allah katika kusadikisha kwetu. Na amesema Mtume (s.a.w): ((Haukubaliani umati wangu katika kosa)) basi akahusisha kwa neno lake hili watu wa Sheria hii na wao ndio Mashahidi wa haki juu ya kila madhehebu; kwa sababu sisi tumeona kuwa mzinifu na mwizi na mnywapombe (mlevi) na dhalimu katika madhehebu zote hao wanaitwa Waumini, nami nimeona Madhehebu hii (Ibadhi) haifanyi matendo hayo machafu si kidogo wala kwa wingi, na nimeona madhehebu yetu (Ibadhi) imetakaswa na machafu, basi tukajua kuwa ndiyo Itikadi ambayo Allah haridhii isipokuwa kwa Itikadi hiyo, kwa sababu ni madhehebu iliyotakaswa iko wazi ni sahihi kwa njia ya sheria na sio kwa njia ya lugha)) Na Allah ndiye anajua zaidi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
بِسْمِ اللَّهِ ٱلرَّحْمَـٰنِ ٱلرَّحِيمِ
Rehema na Amani ziwe juu ya Bwana wetu Muhammad.
Kutoka kwa Abdullahi bin Ibadhi kwenda kwa Abdulmaliki bin Marwani. ………
Salamu alayka,,,,
Hakika mimi namshukuru Allah, hakuna mungu isipokua yeye, nami nakuusia kwa uchamungu, kwa hakika mwisho mwema ni kwa uchamungu na marejeo ni kwa Allah.
Na elewa kuwa hakika Allah anawakubalia Wachamungu.
Ama baada ya hayo;
Imenifikia barua yako pamoja na Sinani bin Aasim, nawe ulinitaka nikuandikie barua, basi nilikuandikia, yamo humo uliyoyakubali na yamo uliyoyakataa.
Umezua kuwa uliyoyakubali ni yale niliyotaja kutoka katika Kitabu cha Allah (Quran), na niliyoyatilia mkazo katika kumtii Allah na kufuata Amri yake na Sunna na Nabii wake, na ambayo umeyakataa hayo kwa Allah mtukufu siyo mabaya.
Ama niliyoyataja kuhusu Othman, na niliyoyaweka wazi katika suala la viongozi, kwa hakika hakuna yoyote anayekataa ushahidi wa Allah katika Kitabu chake kwa alioteremsha kwa Mtume wake, kuwa [asiyehukumu kwa alioteremsha Allah, hao ndio Madhalimu], na [Makafiri] na [Mafasiki] 5/44-47.
Kisha mimi sikua nikutajie kitu chochote katika mambo ya Othman na viongozi isipokua Allah anajua kuwa hiyo ni haki, nami nakutajia katika hayo ubainisho katika Kitabu cha Allah alichokiteremsha kwa Mtume wake, na nitakuandikia katika niliyokutajia, na nitakupa habari za Othman na yale tuliyomtia makosani kwayo, ili nibainishe kwako jambo lake.
Kwa hakika alikuwa (Othman) -katika niliyokutajia- ni katika waliotangulia katika Uislamu na kuufanyia kazi vizuri, lakini Allah hakuwaondoshea waja mtihani.
Kwa hakika Allah alimpeleka Muhammad (S.A.W.) na akateremsha juu yake Kitabu ambacho ndani yake kuna ubainisho wa kila kitu, kinahukumu baina ya waja katika yale waliohitilafiana ndani yake, basi akahalalisha Allah katika kitabu chake yaliyo ya halali, na akaharamisha yaliyo ya haramu, na akalazimisha ndani yake yaliyo ya lazima, na akapambanua baina ya hukumu zake, na akabainisha mipaka yake na kusema: [Hiyo ni mipaka ya Allah musije ikaribia] 2/187 na akasema: [Na mwenye kuikiuka mipaka ya Allah; hao ndio madhalimu] 2/230.
Na akagawa Mola wetu vigao, na hakuna kwa waja wake mwenye hiari katika vigao vyake, basi akamwamrisha Mtume wake kufuata Kitabu chake kwa kumwambia: [Fuata yale yaliyofunuliwa kwako kutoka kwa Mola wako] 33/2 na akasema: [Utakapo somewa fuata kisomo chake * kisha ni juu yetu ubainisho wake] 75/18-19. Na hapo akawa Mtume Muhammad (S.A.W.) anafanya kwa mujibu wa amri ya Mola wake akiwa pamoja naye Othman na aliyemtaka Allah katika Masahaba wake, nao hawamwoni Mtume wa Allah (S.A.W.) kuchupa mpaka, wala kubadilisha faridha wala hukumu, wala kuhalalisha kitu alichokiharamisha Allah, wala kuharamisha alichokihalalisha Allah, wala hahukumu baina ya waja isipokuwa kwa alioteremsha Allah, na alikua akisema: [Hakika mimi naogopa ikiwa nitamwasi Mola wangu adhabu ya siku nzito] 6/15.
Alifanya (S.A.W.) aliyotaka Allah huku akiwa ni mwenye kufuata alioamrisha Allah, akifikisha yaliyomfikia kutoka kwa Allah, hali ya kuwa Waumini wako pamoja naye akiwafundisha huku wakiangalia mwenendo wake mpaka akamwondosha Allah -juu yake ziwe rehema na amani- nao wote wako radhi naye, tunamwomba Allah atupe taufiki ya kufuata njia yake, na kufanyia kazi sunna yake.
Kisha Allah akawarithisha waja wake Kitabu (Quran) alichokuja nacho Muhammad (S.A.W.), na akamuongoza kwa hicho, wala haongoki mwenye kuwaelekea watu kwa kukiacha Kitabu hicho.
Basi akasimama baada yake Abubakar kwa kuongoza watu, akashika njia ya kufanyia kazi Kitabu cha Allah na Sunna ya Nabii wake, na hakuna yoyote katika Waislamu aliyejitenga naye, wala hakuna yoyote aliyetia kosa katika hukumu aliyohukumu, wala katika kigao alichogawa, basi aliendelea katika njia hiyo mpaka akaondoka duniani hali ya kuwa Waislamu wako radhi naye, na kwake wamekusanyika.
Kisha akasimama baada yake Omar, naye alikua ni shupavu katika uongozi, ni mzito kwa Wanafiki, naye aliongoka kwa njia ya waumini waliopita kabla yake, anahukumu kwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Nabii wake, na Allah alimpa mtihani wa kuifungua dunia, mtihani ambao haukuwapata waliopita kabla yake, basi aliihama dunia ikiwa dini imedhihiri na neno la Waislamu ndilo linalokusanya, na ushahidi wao umesimama, na Waumini ni mashahidi katika Ardhi, amesema Allah mtukufu: [Na namna hiyo tumekufanyeni umma wa kati; ili muwe mashahidi juu ya watu, na mtume awe ni shahidi juu yenu] 2/143.
Basi baada ya kifo chake (Omar), Waumini walishauriana, nao wakamkabidhi Othman uongozi, naye akafanya aliyotaka Allah ayafanye katika wanayoyajua Waislamu, akaendelea katika hilo mpaka ikakunjuliwa kwake dunia, na zikafunguliwa kwake hazina za ardhi kwa yale aliyotaka Allah mtukufu.
Kisha akaleta mambo mapya, mambo ambayo hayakufanywa na wenzake waliopita kabla yake, hali ya kuwa yale waliyoyazoea watu kwa Mtume wao bado ni mapya.
Basi Waumini walipoyaona aliyoyazua walimwendea na wakamsemeza, nao wakamkumbusha kwa Kitabu cha Allah na Sunna za waliopita kabla yake katika Waumini, basi ikawa ni mazito juu yake kukumbushwa kwa Aya za Kitabu cha Allah, na hapo aliwachukua kwa maguvu (ubabe), na akampiga miongoni mwao aliyemtaka, na kuwafunga, na kuwahamisha.
Na umeniandikia -ewe Abdulmaliki- ukitaka nikuandikie jawabu ya barua yako na nijitahidi katika nasaha, kwa hakika mimi nilibainisha kwako ikiwa unajua cheo cha niliyokuandikia.
Na umenikumbusha Allah nikubainishie, kwa hakika nimekubainishia kwa jitihada kuu, na nimekupa habari za umma, na imekua ni haki juu yangu kukunasihi kwa niliyoyajua kuwa Allah anasema: [Hakika wale wanaoficha yale tulioteremsha katika mabainisho na uongofu baada ya kuyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao amewalaani Allah, nao wanalaaniwa na wenye kulaani; isipokua watakaotubia na wakafanya mazuri na wakabainisha; hao nitawasamehe, na mimi ni mwingi wa kusamehe mwingi wa kurehemu] 2/159.
Kwa hakika Allah hakunifanya niwe mja wa kumkufuru yeye, wala niwe mwenye kuhadaa watu kwa chochote kisicholazimika juu ya nafsi yangu, wala siwezi kwenda kinyume kwa ninayokataza.
Ninakuiteni katika Kitabu cha Allah na Sunna ya Nabii wake (S.A.W.), mhalalishe halali yake na mharamishe haramu yake, na mridhie hukumu yake, na mutubie kwa Mola wenu, na mukirejee Kitabu cha Allah.
Ninakuiteni kwenye Kitabu cha Allah, kihukumu baina yangu na nyinyi katika yale tuliyotafautiana ndani yake, yahalalishwe aliohalalisha Allah, na tugawe kwa vigao vya Allah, na tuhukumu kwa aliyohukumu Allah, na tujitenge na aliyejitenga naye Allah na Mtume wake, na tumuasi aliyeamrisha Allah kumuasi.
Haya ndio tuliyomdiriki nayo Nabii wetu -juu yake iko amani-.
Na -kwa hakika- umma huu haukumwaga damu isipokua pale ulipoacha Kitabu cha Mola wake, Kitabu ambacho ameamrisha kujishika nacho, na hakika wao wataendelea kugawika wenye kutafautiana mpaka wakirejee Kitabu cha Allah na Sunna ya Nabii wake, na wakihukumishe katika waliyotafautiana ndani yake, hakika Allah anasema: [Na chochote ambacho mtakua na tafauti ndani yake; basi hukumu yake hicho iko kwa Allah; huyo Allah ndiye Mola wangu, kwake ninategemea, na kwake ninanyenyekea] 42/10.
Na kuwa hii ndio njia iliyo wazi, nayo ndio aliowaongoza Allah kwayo waliokua kabla yetu nao ni Muhammad (S.A.W.) na Makhalifa wawili walio wema baada yake.
Basi hatopotea atakaye ifuata, wala hataongoka atakaye iacha: [Na hakika hii njia yangu iko sawa; ifuateni na wala msifuate njia nyingi zitakuekeni mbali na njia yake, hayo anakuusieni kwayo ili muwe Wachamungu] 6/153.
Basi tahadhari zisije zikakupoteza njia nyingi ukawa mbali na njia yake, na ukakupambia upotevu kwa kufuata mapendwamoyo yako katika uliojikusanyia wanaume (majeshi), hakika hao hawatakufaa chochote mbele ya Allah mtukufu, hakika hayo ni mapendwamoyo tu.
Na hakika watu wanafuata viongozi wawili, kiongozi mwongofu, na kiongozi mpotevu.
Ama Kiongozi mwongofu, huyo ni yule anayehukumu kwa alioteremsha Allah, na anagawa kwa kigao chake, na anafuata Kitabu cha Allah; na hao ndio wale aliowataja Allah: [Na tumejaalia katika wao viongozi wanaongoka kwa Amri yetu kwa vile walivyosubiri, na wakawa kwa Aya zetu ni wenye yakini] 32/24 na hawa ndio mawalii (vipenzi) wa Waumini ambao Allah ameamrisha kuwatii, na amekataza kuwaasi.
Ama Kiongozi mpotevu, huyo ni yule anayehukumu kinyume na alioteremsha Allah, anagawa kinyume na alivyogawa Allah, anafuata mapendwamoyo yake kinyume na Sunna itokayo kwa Allah, huyo amekufuru kama alivyomwita Allah, naye amekataza kuwatii viongozi hao, na ameamrisha kuwapiga vita kama alivyosema: [Basi usiwatii Makafiri, na uwapige kwa hilo vita vikubwa] 25/52.
Hakika hiyo ndio haki ameiteremsha Allah kwa haki, na hakuna baada ya haki isipokua upotevu.
Wala usiupige kumbo ukumbusho, ukawa mbali nao, na wala usiwe na shaka katika Kitabu cha Allah, na hakuna uwezo wala nguvu isipokua kutoka kwa Allah, kwa hakika yule asiyefaliwa na Kitabu cha Allah huyo hatafaliwa na chengine chochote.
Umeniandikia nikuandikie marejeo ya barua yako, hakika mimi nimekuandikia, na mimi ninakukumbusha kwa Allah aliye mkuu, usome barua yangu kwa mazingatio, nawe uko peke yako, kisha uniandikie -ikiwa utaweza- jawabu ya barua yangu, na utoe ubainisho juu yake katika Kitabu cha Allah, ili nisadikishe kwa ubainisho huo maneno yako.
Wala usinifungulie Dunia; hakika mimi sina hamu ndani yake, na wala sina haja nayo, lakini ziwe nasaha zako kwangu katika Dini, na kwa yaliyo baada ya kifo, hakika hayo ndiyo bora ya nasaha, na Allah ndiye muweza wa kutukusanya katika utiifu wake, kwa hakika hakuna kheri kwa asiyekua katika utiifu wa Allah, na kwa Allah ndio taufiki, na kutoka kwake maridhio.
Wasalamu alaika.
Na shukurani zote ni kwa Allah, na rehema na amani ziwe juu ya bwana wetu Muhammad na Aali wake(1)
[1]. Baaruniy: Mukh-tasar Taarikh L-ibadhiyah uk. 22-26
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
Baada ya kumshukuru Allah mtukufu na kumtakia rehma na amani kipenzi chetu Mtume wetu Muhammad pamoja na Aali zake na kila mwenye kuongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.
Jee! Ibadhi ni katika makundi ya Kikhawariji?
Ni suali linalowafika wengi, na pengine kuwachanganya, basi ili tuweze kufikia katika uhakika wa suali hili, inabidi kwanza kufahamu:
1. Ni nini maana ya Khawariji?
2. Ni nani Makhawariji?
Khawariji ni neno la kiarabu na maana yake ni WALIOTOKA, kutokana na hapo neno hili linaweza kutumika kwa sifa nzuri, pia linaweza kutumika kwa sifa mbaya.
SIFA MBAYA: Ikiwa litatumika kwa kumaanisha wale waliotoka nje ya haki au nje ya dini ya Allah mtukufu.
SIFA NZURI: Ikiwa Litatumika kwa kumaanisha wale waliotoka katika njia ya Allah mtukufu kwa kuipigania dini yake, pia wale waliotoka nje ya batili kwa kukimbia fitna na maasi.
Watangulizi wa mwanzo wa Maibadhi ni wale waliojitoa katika safu za Aliy bin Abi Twalib baada ya kukubali kwake Sulhu na Muawiyah; kwani wao waliona Suluhu hiyo ni kosa la kuvunja hukumu ya Allah mtukufu, tokeo hilo lilikua katika mwaka wa 38 Hijiria yaani baada ya kufa Mtume (S.A.W) kwa miaka 27, basi wao walijulikana kwa majina haya:
- AHALU NAHARAWANI: kwa unasibisho wa pale walipopigwa vita na kuuliwa wengi wao katika sehemu hiyo, napo ni NAHARAWANI huko Iraqi
- MUHAKKIMAH: kwa kaulimbinu yao (LAA HUKMA ILLA LILLAAHI) yaani (HAKUNA HUKUMU ISIPOKUA YA ALLAH TU), wakimaanisha sababu ya kujitoa kwao katika safu za Aliy bin Abi Twalib.
- KHAWARIJI: Jina hili waliitwa na mahasimu wao, kwa sababu ya kujitoa katika safu za Aliy bin Abi Twalib kwa sababu ya kukubali kwake kufanya sulhu na Muawiyah bin Abi Sufiyan.
Jee! Watangulizi hawa ((AHALU NAHARAWANI R.A)) waliipatia haki kwa kujitoa kwao katika safu za Aliy bin Abi Twalib au waliikosea haki? Kwani ikiwa waliipatia haki hakutakuwa na aibu kwao, na kama waliikosa haki hapo ndio kutakuwa na aibu kwao.
Kwa hakika sisi Ibadhi kuwakubali AHALU NAHARAWANI R.A kuwa ni Salafu wetu wema, ni kwa sababu ya kuipatia kwao haki, na hilo halina shaka yoyote kidalili, basi hiyo ndiyo sababu yetu, na sio kwa sababu nyengine yoyote, wengine husema kuwa hakuna sahaba yoyote katika safu yao, lakini uhakika wao unakadhibisha neno lao hao, kwa hakika hawakuwemo katika safu yao isipokua Masahaba na Matabiina wakuu R.A, nao walijulikana kwa elimu na uchamungu, wao ndio Maquraa yaani Maulamaa wa wakati ule, Allah awaridhie. Ingawa huo ndio uhakika, lakini sisi tunasema: Kuwemo Masahaba katika safu yao siyo sababu wala kigezo chetu cha kuwakubali wana haki hao; kwani sahaba akikosea na tabiina akipatia bila shaka usahaba wa aliyekosea hauwezi kulifanya kosa lake kuwa ni haki na haki ya tabiina aliyepatia kuwa ni batili, Mtume (S.A.W) ametuhadharisha kufanya upendeleo kama huo kwa kusema: ((Hakika waliangamia waliopita kabla yenu kwani wao walikuwa anapoiba mwenye cheo wanamuacha na akiiba aliye dhaifu wanamtia adabu)) [Bukhari 3475 Muslim 1688] na Allah kwenye kitabu chake anatuambia: ((ENYI MULIOAMINI KUWENI WASIMAMIZI KWA UADILIFU MASHAHIDI KWA AJILI YA ALLAH TU, HATA KAMA NI DHIDI YA NAFSI ZENU AU WAZAZI WAWILI AU JAMAA WA KARIBU, AKIWA NI TAJIRI AU FAKIRI HAKIKA ALLAH ANA HAKI ZAIDI KULIKO WAO, BASI MUSIFUATE MAPENDWA MOYO MUKAEPUKA KUFANYA UADILIFU…)) [4-Nisaa 135], kwa hiyo sisi kuwakubali AHALU NAHARAWANI R.A si kwa sababu ya cheo ya usahaba bali ni kwa sababu ya cheo ya kuipatia kwao haki.
VIPI AHALU NAHARAWANI R.A WALIIPATIA HAKI?
Tunafahamu sote kuwa baada ya kifo cha Khalifa wa Tatu Othman bin Affaan (34 HJ) Waislamu walimchagua Aliy bin Abi Twalib kuwa kiongozi wao na Khalifa wao wa nne baada ya kufa Mtume wetu (S.A.W), na baada ya Khalifa wa nne kukamata hatamu za serikali kukatokea uasi uliofanywa na Gavana wa mji ya Shaam (Syria, Jordan na Palestina), Gavana huyo ni Muawiyah bin Abi Sufiyan, yeye aliasi na kutayarisha jeshi dhidi ya Serikali ya Khalifa wa nne Aliy bin Abi Twalib. Basi Khalifa alipitisha hukumu ya kuvunjwa Uasi wa Muawiyah na walioko pamoja naye (Pote la waasi); kwani Allah mtukufu amepitisha hukumu ya pote la waasi katika Kitabu chake kwa kusema: ((Iwapo kundi moja litafanya uadui kwa jengine, basi lipigeni vita kundi ambalo limefanya uadui mpaka lirejee katika amri ya Allah..)) [49-Hujuraati 9] na kuiasi serikali adilifu ni kuifanyia uadui, basi vita vya kuvunja uasi wa Muawiyah vikaanza huko Siffain-Iraq mpaka Muawiyah alipoona anashindwa akasema: “tufanye suluhu” hali ya kuwa bado yumo katika uasi wake, na huku pote lake limeshamuua Sahaba Ammaar bin Yaasir R.A ambaye Mtume (S.A.W) alimbashiria pepo na kumwambia: ((Ajabu ilioje kwa Ammaar atauliwa na pote la waasi akiliita kaatika Pepo nalo linamuita katika Moto)) [Bukhari 337], nayo ni dalili yakinifu kuwa Muawiyah ni kiongozi wa pote la waasi linaloita katika moto kwa mujibu wa ulimi wa Mtume (S.A.W). Kwa kutaka Muawiyah suluhu hiyo ndipo hao wasomi waliojitoa wakasema kuwa hukumu ni ile aliyokwisha hukumu Allah mtukufu basi HAKUNA HUKUMU ISIPOKUA YA ALLAH, yaani ni kulipiga vita pote hilo la waasi mpaka lirejee katika amri ya Allah ya utiifu wa Kiongozi wa Waumini ambae wakati huo ni Aliy bin Abi Twalib. Basi Imam Aliy aliposhikilia kufanya suluhu na Muasi Muawiyah hapo wale Wasomi waliojitoa wakasema: “Kwa hakika tumekupa ahadi ya kukutii kwa kumtii Allah na Mtume wake, na hili unalolifanya ni kosa la kumuasi Allah kwa kuivunja hukumu yake na kumtii muasi katika uasi wake, na hakuna kumtii kiumbe kwa kumuasi Muumba wala hakuna kusaidiana katika kosa na uadui”. Basi Aliy bin Abi Twalib aliposhikilia kufanya suluhu na Muasi Muawiyah ndio hao Wasomi wakajitoa katika safu zake; kwani walikataa kushiriki na kusaidia katika kosa hilo la kuvunja kuhumu ya Allah kwa kufanya suluhu na waasi ambao bado wamo katika uasi wao. Basi Wasomi hao wakajitoa na matokeo ya Suluhu yakawa ni kumuezua Aliy bin Abi Twalib katika Uongozi, matokeo ambayo Imam Aliy aliyakataa, sasa ikiwa Suluhu ni haki mbona unakataa matokeo yake? na ikiwa ni batili wana makosa gani walioipinga na kujitoa kwa kukataa kushiriki katika batili? Na hapo Aliy aliwataka wale waliojitenga warejee katika safu zake, lakini wapi, walikuwa tayari wameshachagua Kiongozi mpya Imam Abdullahi bin Wahbi Arraasibi (R.A), basi walimjibu kuwa Waislamu hawarejeshi toba, basi anakaribshwa kuwa chini ya bendra ya Amiri Al-Muuminina Abdullahi bin Wahbi Arraasibi, ndipo alipomtuma Ibnu Abbaas R.A kwa kujadiliana nao lakini alishindwa kihoja na dalili, ndipo alipokwenda na jeshi lake na kuwapiga vita kiuadui kabla ya kupata nguvu Uongozi huo mpya uliosimama kwa misingi sahihi ya kisheria, nao walipigana lakini walishindwa na kuuliwa wengi wao, kwa vita hivo zikadhoofika safu za Aliy na kushindwa kumuelekea Muasi Muawiyah na kupelekea Muasi Muawiyah kuhodhi Madaraka kiubabe na kuanzisha Ufalme wa Bani Umayyah, nao ulihukumu kwa miaka 92, hakupatikana kiongozi muadilifu katika miaka yote hiyo isipokua Omar bin Abdilazizi Allah amridhie, naye alihukumu kwa miaka 2 tu, na akauliwa kwa sumu R.A.
Kwa hiyo inabainika wazi kuwa AHALU NAHARAWANI R.A ndio salafu wema na ruwaza njema kwa kila mwenye kushikamana na Kitabu cha Allah Quraani tukufu wakati wengine wanapofuata rai za Wakuu wao kwa kuvunja au kupotosha mafundisho ya Allah mtukufu.
IKIWA KUJITOA KATIKA SAFU ZA IMAMU ALIY NI UKHAWARIJI, BASI ZUBEIR BIN AWWAAM NA TWALHA BIN UBAIDILLAHI NI MAKHAWARIJI; KWANI WALIJITOA KABLA YAO NA WAKAPIGANA NAYE KATIKA VITA MAARUFU VYA JAMAL NA KUULIWA HUMO.
NA IKIWA KUTOKUWEMO KATIKA SAFU ZA ALIY NI UKHAWARIJI, BASI MUAWIYAH NA AMRU BIN AL-AASI NAO NI MAKHAWARIJI; KWANI WALIKATAA KUINGIA KATIKA SAFU ZAKE NA WALIMPIGA VITA.
NA IKIWA KUPIGANA NA ALIY NI UKHAWARIJI, BASI ZUBEIR BIN AWWAAM NA TWALHA BIN UBAIDILLAHI NA MUAWIYAH NA AMRU BIN AL-AASI NAO NI MAKHAWARIJI; KWANI WOTE WALIPIGANA NAYE VITA.
Kutokana na hapa utagundua kuwa kuitwa AHALU NAHARAWANI R.A kwa jina la Ukhawariji ni propaganda batili za kuwapiga vita zilizopitishwa na wapinzani wao kwa masimulizi ya uongo.
MAKHAWARIJI WAOVU:
Mtume S.A.W amebainisha sifa za Makhawariji waovu nao ndio MAARIQAH, nazo ni hizi zifuatazo:
- Wingi wa Ibada na matendo mema kiasi cha kudharau wengine ibada zao mbale ya Ibada za Makhawariji (Hii si aibu, kwani kila muislamu anatakiwa ajipambe kwa wingi wa Ibada, lakini kutajwa kwake ni kwa kuhadharishwa tusije tukahadaika na udhahiri wao wenye kuvutia).
- Wasomaji wazuri wa Quraani.
- Quraani haivuuki koromeo zao (Hii ndiyo aibu yao ambayo ni chimbuko la aibu zao zote, basi mafundisho yao yatapingana na Quraani tukufu, hata ukiwaita katika Quraani wao hawakubali bali watakulazimisha na vyengine kwa mfano (Fahamu Salafu Saalih) basi utawakuta wametopea katika Itikadi zilizopondwa na Quraani kwa mfano:
- Mara wanafahamu kwa fahamu ya Firauni L.A. kuwa Allah yuko mbinguni.
- Mara wanafahamu kwa fahamu ya waovu wa kiyahudi kuwa Allah anaonekana kwa macho, hali ya kuwa amesema kumwambia Mtume Mussa A.S.W ((Hutaniona)) na amesema akijisifu ((Havimdiriki yeye nyenye kuona)).
- Mara wanasema hata tufanye maovu vipi tutasamehewa tu sisi, hali ya kuwa Quraani inasema kuhusu waovu waliopita wa Kiyahudi kuwa walisema (Tutasamehewa tu sisi).
- Mara wanasema hata tukiadhibiwa motoni basi ni kwa muda tu, hali ya kuwa Quraani inasema kuhusu waovu wa Ahalu Al-Kitaabi kuwa wamesema: (Hautatugusa moto isipokua siku chache tu na yakawadanganya katika dini yao waliyokuwa waliyazua) basi na hawa pia yamewadanganya waliyoyazua kama yalivyowadanganya waliopita kabla yao. MARADHI NI HAYO HAYO HATA WAGONJWA WAKIWA TAFAUTI.
- Mara wanasema: Tutaombewa ikiwa hakutubia, hali ya kuwa Quraani inasema: ((Hawana Madhalimu kipenzi yoyote wala muombezi yoyote wa kutiiwa)).
- Mara wanasema: Tutapita katika Daraja lililoko juu ya Jahannamu wakati Quraani inasema kuwa Jahannamu ina milango saba na waovu watapelekwa na kuingizwa kupitia milango hiyo ya Jahannamu na kuambiwa iingieni. Hakika wao wanasoma Quraani lakini haivuuki koromeo zao. Allah awaongoe.
- Wanaua Waislamu na kuwaacha Washirikina. Na hii ndio balaa ya Makhawariji waovu wa kila wakati, wao huwa wanaitakidi kila muislamu aliyetafautiana na wao kuwa ni Murtaddi Mshirikina, na hiyo ndiyo sifa ya Makhawariji wote, wa mwanzo (AL-AZAARIQAH, ANAJIDIYAH, NA SUFRIYAH), na Makhawariji wa zama hizi (WAHAABIYAH SALAFIYAH) wanaomuitakidi Allah kuwa anasifika kwa sifa za viungo na harakati, wanasema Allah ana mikono miwili na macho mawili na miguu, vidole, anatoa sauti…., naye yuko mbinguni amekaa kitako juu ya kiti cha enzi (Arshi) anatikisika na kuteremka pia anajigeuza…. Kisha wakasema kuwa asiyekubali sifa hizo za viungo na harakati kumsifu nazo Muumba Allah mtukufu huyo ni Mjahamia na Muattila ni mbaya kuliko Mshirkina wa Kiyahudi na Kinasara, ameritadi auliwe.
- Mbwa wa Moto wa Jahannamu na Mbwa wa watu wa Motoni, na huu ni mfano unaomaanisha kuwa Moto wa Jahannamu na Wahusika wake ambao ni Washirikina na Mafasiki wote (WANAFIKI) ndio mabwana wa Makhawariji, kwa maana watatumiliwa na Washirikina kwa kuudhuru uislamu na waislamu, na wataita katika Moto kwa kuwapendezeshea watu maasi, hata watasema Imani haidhuriki kwa maasi yote yasiyokua ya kishirikina, wengine watasema Allah katoa offer ya kumuasi, basi watawaambia watu: Nyinyi hata mufanye maasi yote yasiyokua ya kishirikina na musitubie pepo ni yenu tu.
Tujihadhari na Makhawariji waovu na Ukhawariji wao, na tuwahadharidhe watoto wetu na vizazi vyetu.
Kwa kuteremsha darsa muhimu ya maudhui hii fuata kiunganishi hapa
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Asalamu alaykum wa rahatullahu wa barakatuh. Yametufikia masula muhimu kuhusu Ibadhi nayo ni kama yafuatavyo:
JAWABU:Jina au neno Ibadhi limetoka katika nasabu ya A-Imam Abdullahi bin Ibadhi Al-Tamimi R.A, naye aliishi katika zama za Masahaba R.A. Umaarufu wa Imamu huyu ulienea sana katika zama za Utawala wa Bani Umayyah hususan kwa barua zake alizokua akimjibu Mtawala wa wakati huo Mfalme Abdulmalik bin Marwan Al-Umawi aliyefariki mwaka 86 Hijiria, naye alikua Mfalme aliyedhulumu raia na kukithiri uuaji wana haki katika miji ya Iraqi kupitia Liwali wake Hajjaj bin Youssuf A-Thaqafi muuaji wa Abdullahi bin Zubeir bin Awwaam na Saidi bin Jubeir na wengineo “Walidhibitiwa alowauwa (Hajjaaj) kwa kukata vichwa -mbali ya alowauwa katika kambi za vita na wakati wa vita- wakapatikana kua idadi yao ni laki moja na elfu ishirini (120,000) na walikufa katika jela zake wanaume 50,000. na wanawake 30,000, miongoni mwa wanawake hao 16,000 waliuliwa uchi, na alikua akiwafunga wanawake na wanaume katika sehehmu moja, na ilikua Jela yake haina sitara inayowazuilia watu Jua la wakati wa Kiangazi, wala Mvua na Baridi wakati wa baridi.” Mas-udiy – Muruju dhahab. Ch. 1. Dar ehia al-tourath al-arabi 1422H-2002M. Beirut – Lebanon. J3.Uk.118. Basi katika mji aliohukumu Liwali huyo chinjachinja wa Mfalme Abdulmalik Al Umawi aliishi Imam Ibnu Ibadhi Al-Tamimi R.A, naye alikua Mashuhuri kwa ushujaa wake wa kutangaza haki na kumjibu Mfalme Abdulmalik na kumtaka atubie kwa Mola wake na ajifunge na mafundisho ya Quraani na Sunna bila upendeleo, Imam Ibnu Ibadhi hakuwa marejeo ya kielimu kwa watunza haki katika zama hizo lakini alikua ni mwanaharakati shujaa wa kusema na kupeana hoja na wengine na kuamrisha nema na kukataza mabaya, wakati marejeo ya Kielimu alikua ni Imam Jabir bin Zaid Al-Uzdi Al-Omani R.A aliyakufa mwaka 93 Hijiria. Omani ni taifa lililokubali Uislamu kwa hiyari kabla ya kufa Mtume S.A.W. basi Waomani kuanzia Wafalme wa zama hizo Abdu na Jaifar wana wa Julandaa R.A na raia wao, wote waliusihi Uislamu kabla ya ufunguzi wa Makka. Omani ilihifadhi mafundisho ya Uislamu na kuwa pamoja na Makhalifa waongofu mpaka pale ulipozuka mtafaruku baina ya Masahaba, hapo Waomani hawakuingia katika yote yaliyojiri baina ya Masahaba na walijepusha nayo, ila yalipowafikia walikua wakiyahukumu kwa mujibu wa mafundisho ya Uislamu bila ya upendeleo. Waislamu hawa walibakia katika hali hiyo mpaka kilipofika kipindi cha Uliwali wa Chinjachinja Hajjaj bin Youssuf Al-Thaqafi ndipo Dola ya Ufalme wa Bani Umayyah ilipotaka kuichukua Oman kimabavu, na adui mkubwa wa Dola hiyo wakati huo walikua ni Makhawariji wafuasi wa Naafii bin AL-Zraq (Azaariqah) na Najdatu bin Aaamir na waliofuata Itikadi yao inayosema kuwa kila muasi ni kafiri mshirikina inalazimika kutubia au auliwe na kuhodhi mali yake na kua ngawira kwao, basi Dola hiyo dhalimu wakainasibisha Omani na Ukhawariji na kuisema kuwa ni Dola ya Kikhawariji ili kupata sababu ya kisiasa ya kuhalalisha uvamizi wao batili ambao haukudumu ndani ya Omani, kwani Waomani walibakia katika asili ya Uislamu basi fatwa yao katika yaliyotokezea iliona usahihi wa yale waliyonayo Jamaa ya Imam Jabir bin Zaid Al-Uzdi Al-Omani ambayo Imamu Abdullahi bin Ibadhi Al-Tamimi alikuwamo katika safu yake, basi Mabani Ummayah wakawanasibisha na Ibn Ibadhi Al-Tamimi R.A na kuwahukumu kuwa ni Makhawariji, ilikua tuhuma ya Ukhawariji wakati huo ni zaidi ya tuhuma ya Ugaidi katika zama zetu za leo, na ndio sababu ya kukithirisha Chinjachinja ovyo ya Hajjaj bin Youssuf kama tulivoona, anatuambia Imam Nassir bin Jaaid Al-Kharousi R.A: “Na watu wa Omani katika wakati huo (wa fitina) walikua mbali na fitna hizo, wanamuabudu Allah mtukufu kwa yale waliyoyachukua katika Elimu kutoka kwa Nabii (s.a.w) katika zama zake, na kutoka kwa Masahaba baada yake katika zama za Abu bakari Siddiiq na Omar bin Khatab, na wao hawajui Khawarij, wala Abdullahi bin Ibadhi, wala wengineo na hawakuchukua kutoka kwa Abdullahi bin Ibadhi hata mas-ala moja, basi zilipowafikia khabari hizo, na khabari za Abdullahi bin Ibadhi waliyaweka yote hayo yaliyotokeza katika yale waliyokuwa nayo katika Elimu iliyotangulia kuwa kwao, basi wakakuta kuwa Haki inayokubaliana na hayo waliyokuwa nayo katika elimu ni yale aliyoyasema Abdullahi bin Ibadhi, basi walinasibishwa wao kwake yeye huyo, na sio kwa kuchukua Sheria kwake yeye huyo.” [Jamil bin Khamis Saadiy – Qaamus Sharii-a. Jz 7 uk.311]. Waislamu hawa wakati huo hawakujiita Ibadhi, wala hawakukubali unasibisho wowote isipokua unasibisho wa Uislamu au Daawa au Istiqamah, lakini kwa sababu ya kugawika uma huu na kupatikana mapote tafauti katika Itikadi na madhehebu tafauti katika Fiqhi na wao wanajulikana na wengine kwa jina la kubandikwa ambalo ni Ibadhi, wakakubali jina hilo kuwa ni anuani (Title) ya kudhibiti yenye tafauti baina yao na wengine, ili kila upande uhusike na majukumu yake katika athari za mafaundisho, na mwanachuoni wa mwanzo katika safu yetu aliyekubali jina la Ibadhi ni Shahidi Imam Amruus bin Fat-hi Al-Musakini A-Nafousi R.A aliyefariki mwaka 283 Hijiria, hayo yamo katika kitabu chake maarufu Usuulu Daidunati Saafiyah na huyu ni kwa upande wa Magharibi leo ni Misri, Libya, Tunis, Al-Jeria, Mali, Ghana na Morroco, ama kwa upande wa Mashariki (Yemen, Oman, Afika Mashariki) jina la Ibadhi lilianza kukubalika katika karne ya sita Hijria, yote hayo ni kwa sababu ya kuheshimu na kudhibiti tafauti wakati jamii zao zilipoingiwa na waislamu waliotafutina na wao, walifanya hivo kuwambia wenzao kuwa Uislamu unatukusanya hata kama tumetafautina, na wajibu wetu kila upande uhusike na mafundisho yake katika yenye tafauti, ama yenye makubaliano tushirikiane ndani yake, na katika yenye tafauti njia iwe ni kuhakikisha kielimu kisha haki ikubalike, na kama ikidharurika kukubali haki kwa dalili basi heshima itukusanye bila kuifanya tafauti kuwa ni sababu ya kugombana na kushutumiana, hiyo ndio njia yetu ingawa wengine wanatuelekea kwa uadui na uhasama hali ya kuwa sisi hatukutii katika mafundisho yetu himizo lolote la kufanya uadui na uhasama kwa misingi ya tafauti zilizotokea, na hii ndio siri ya kuona jamii za Maibadhi zimejawa na mapenzi kwa wengine waliotafautiana na wao na zinajiondosha katika kugombana na wengine hata kama watadhulumiwa na kutuhumiwa bila ya haki. Tukilifahamu hili tutajua kuwa Ibadhi mafundisho yao ni kutoka katika Kitabu cha Allah Quraani tukufu na Sunna ya Mtume Muhammad S.A.W na Makubaliano ya Umma katika yenye makubaliano, na ambayo yamekosa andiko safi hubakia kuwa ni rai ya msemaji wake katika Wanavyuoni na yule aliekubalina na yeye katika rai husika. Ibadhi imejiweka katika misingi madhubuti ya kuihifadhi dini nayo ni:
Ama kuhusu mwanzilishi, tufahamu kuwa kupatikana Ibadhi si kwa njia ya kueka vikao vya kuianzisha wala kujifunga na mtu maalumu, lakini kupatikana Ibadhi ni matokeo ya kulazimika na haki kidalili katika yaliyoingiwa na tafauti, basi Ibadhi ni HAKI KWA DALILI katika kila zama, na kila zama ina wanavyuoni wake wahakikishaji, amesema Sheikh wa Abu Ghaanim Al-Khurasani kumwambia mwanafunzi wake huyo: “إن قومك يقولون حقا كثيرا، وإنما خالفهم المسملون فيما خالفوا فيه الحق” ((Fahamu kuwa Kaumu yako (Waislamu wasiokua Ibadhi wakati huo) wanasema haki nyingi, na Waislamu hawajatafautina nao katika walimoipatia haki ndani yake, lakini wametafautiana na wao katika walimoikosea haki ndani yake)). Wabillahi Taufiqi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh. Baada ya kumshukuru Allah muumba wa kila kitu na kumtakia wingi wa Rehma na Amani Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo. Tumeona dharura ya kuweka tafauti baina ya Ibadhi na Khawawariji ili kueneza faida ya kuitambulisha Madhehebu ya Ibadhi. Tufahamu kuwa ubaya wa Khawariji umesimama juu ya misingi miwili mikuu:-
Katika msingi wa pili ndipo Ukhawariji unapopatikana, basi Madhehebu yoyote yenye mafundisho ya kukandamiza na kuwafanyia ubabe wafuasi wa Madhehebu nyengine na kuwahukumu kuwa wameritadi wako nje ya Uislamu ujue kuwa hao ni Makhawariji hata wakijiita kwa jina lolote lile, jihadhari nao ndugu yangu Muislamu, kwani usipofanya hivo unaweza kujikutia umeingizwa katika kutekeleza mahimizo yao ya kuwadhuru Wanatauhidi (Waislamu) na kusababisha fitna katika jamii kwa sababu za tafauti za Kimadhehebu tu. Makhawariji wa Mwanzo walipatikana rasmi kati ya mwaka 61 hadi 64 Hijiria, na Imamu wao wa mwanzo ni Naafii bin Al-Azraq, na kutokea kwake huyo zikazuka tafauti zao zilizowagawa katika makundi mengine mengi. Nafii bin Az-raq alikhutubia wafuasi wake akasema: “Jee!! Hukumu yenu kwa kipenzi chenu si hukumu ya Mtume (s.a.w) kwa kipenzi chake? Na hukumu yenu kwa adui yenu si hukumu ya Mtume (s.a.w) kwa adui yake? Na adui yenu leo ndie adui wa Allah na adui wa Mtume (s.a.w), kama ilivyokuwa adui wa Mtume (s.a.w) siku hizo ndie adui wa Allah na Adui yenu leo?” Wakasema: “Ndio” Akaendelea kwa kusema: “Kwa hakika ameteremsha Allah mtukufu: Kujiweka mbali kutokako kwa Allah na Mtume wake kwa wale muliopeana Ahadi nao katika Washirikina” na (Allah) akasema: “Wala musiwaoe Washirikina mpaka waamini” Basi ameharamisha Allah mapenzi kwao, na kubakia pamoja nao, na kukubali ushahidi wao, na kula vichinjwa vyao, na kukubali elimu ya Dini kutoka kwao, na kuoana nao, na kurithiana nao…” Na khotuba hiyo kama tunavoiona inawaelekea wote wasiokua katika safu yao na kuwahukumu kuwa hao ni Washirikina. Anatumabia Mwanachuoni Muhammad bin Ibrahim Al-Kindi R.A: Amesema Abu Abdillahi Allah amrehemu: “Miongoni mwa hoja za Makhawariji walizozitoa kwa As-haabu wetu (Ibadhi) katika Waislamu, ni yale waliyoyasema: Iwapo mja atakua ni mnafiki au asi, au mshirikina basi huyo ni Mshirikina tu; kwa sababu waja ni wawili: Muumini na Mushriki, na Allah amesema: ((أَلَمْ أَعْهَدْ إِلَيْكُمْ يَا بَنِي آدَمَ أَن لَّا تَعْبُدُوا الشَّيْطَانَ ۖ إِنَّهُ لَكُمْ عَدُوٌّ مُّبِينٌ)) ((Hivi sikuweka ahadi kwenu enyi Wana wa Adamu ya kuwa musimuabudu Shetani hakika yeye kwenu ni adui aliye wazi)) [Yasiin 60]. Basi Makhawariji wamesema: “Kila mwenye kukubali Uislamu kisha akawa ni mwenye kumuasi Allah huyo ni mwenye kuabudia Shetani ni Mshirikina”. Wamesema Waislamu (Ibadhi): “Mwenye kukubali Uislamu huyo yumo ndani ya Uislamu, na hawi Mshirkina kwa kufanya maasi, lakini huyo anakua ni Mnafiki Kafiri wa neema.” Amesema Abu Sufiani: “Na Nafii bin Al-Azraq aliitakidi kuwa Wanakibla (Waislamu) ni Washirikina, na vita na wao ni sawa na vita vya Mtume S.A.W na Washirikina, basi akaitakidi uhalali wa kuwaua na kuteka vizazi na kuchukua ngawira, na akalazimisha Hijra (Kuhamia katika mamlaka yao), nae pia amejitenga na yoyote mwenye kuona uoni wake ikiwa hakuwemo katika jeshi lake, na hakumkubalia yoyote kuitikia daawa yake ila kwa kuhamia pale walipo wao na penye mamlaka yao, na akawaita Wanakibla (Waislamu) wenye kutafautiana na yeye kwa jina la Washirikina, na akahalalisha kuteka wanawake na watoto wao na kuingiza mali zao katika ngawira na kumwaga damu zao bila ya kuwalingania, na hakuona kuwepo dharura yoyote ya kuzuia kutoka kivita kwa yoyote yule, ikiwa ni mwanamme au mwanamke, huru au mtumwa, na aliwalingania wale wenye kukubaliana na yeye ikiwa watajiweka nyuma, pia aliweka mtihani wa mapenzi yake, na hapo yoyote anayekosea mapenzi yake humuua, naye ameishuhudia nafsi yake na walio katika itikadi yake kuwa wao watakua ni Washirikina iwapo hawataingia katika kupigana vita na wapinzani wao, na wakitoka wanaua kila anayekaa mbele yao na kuhodhi vizazi na mali, na wakimkutia yoyote aliyeko katika Itikadi yao lakini anaishi katika miji ya wapinzani wao huhalalisha kwake yale wanayohalalisha kwa wengine, na wamejishika katika hilo na neno la Allah mtukufu: ((إِنَّ الَّذِينَ يَكْتُمُونَ مَا أَنزَلْنَا مِنَ الْبَيِّنَاتِ وَالْهُدَىٰ مِن بَعْدِ مَا بَيَّنَّاهُ لِلنَّاسِ فِي الْكِتَابِ ۙ أُولَٰئِكَ يَلْعَنُهُمُ اللَّهُ وَيَلْعَنُهُمُ اللَّاعِنُونَ)) ((Hakika wale wanaoficha tuliyoyateremsha katika mabainisho na uongofu baada ya kuyabainisha kwa watu katika Kitabu, hao Allah amewalani na wamelaaniwa na wenye kulani)) [Baqarah 159].” Kwa dondoo hizi muhimu zinazohusiana na Madhehebu ya Makhawariji wa mwanzo tunafahamu sote kuwa ubaya wa Makhawariji hao ni kule kupindukia mipaka katika Itikadi yao yenye kusema: “Kila mtenda dhambi kubwa ni Kafiri Mshirikina”. Na kuitakidi kwao ulazima wa kumuua aliyetafautiana na wao kwa kumuhukumu kuwa ni Murtaddi (Mshirikina wa kuritadi) na kuhodhi mali zake na kizazi chake. Khawariji hao wa mwanzo -kabla ya kujimegua kwao kwa kuzusha Itikadi yao hiyo batili ya kuitakidi ushirikina kwa kila mtenda dhambi kubwa- walikua katika safu moja na Ibadhi, wote wako katika itikadi moja ya kuwa mtenda dhambi kubwa mkaidi wa kutubia ni kafiri, bila ya kuainisha kama ni Mshirikina au si Mshirikina (Mnafiki), na hiyo ndio Itikadi ya Kiislamu tokea zama za Mtume S.A.W. na kwa Itikadi hiyo walijishika Ahalu Naharawani R.A tokea kupatikana mgawiko mkubwa mwaka 38 Hijiria. Waislamu hao waliendelea wakiwa safu moja pamoja na Imam Abu Bilali Mirdaas bin Hudair Al-Tamimi R.A mpaka ilipofikia mwaka 61 Hijiria na Imamu huyo -Allah amridhie- kupata shahada ya haki, ndipo Naafii bin Al-Azraq alipoanza kuleta fikra zake za kuwa ukafiri ni ushirkina tu, na kwa kuwa mtenda dhambi ni kafiri basi ni mshirkina tu, na ilipofika mwaka 64 Hijiria ndipo Naafii alipotangaza rasmi Itikadi yake, na kulazimisha Waislamu hufanya Hijra kwa kuhamia pale alipo yeye na kuanzisha Mamlaka ya kujitawala iliyojengeka juu ya msingi wa kuwapiga vita wote waliotafautiana na yeye Kiitikadi. Naafii bin Al-Azraq aliandika barua yake kwa wanaharakati wa Ahalu Naharawani R.A, basi alipoisoma Imam Abullahi bin Ibadhi Al-Tamimi R.A alisema: “Amesema kweli Naafii lau kuwa hawa watu ni Makafiri Washirikina, kwa hakika hapo hukumu yake ingalikua kama hukumu ya Mtume S.A.W, lakini watu hawa ni Makafiri wa neema nao wako mbali na Ushirkina”. Kutokana na hapo ikatokezea tafauti ya wazi kabisa baina ya neno la Abdullahi bin Ibadhi Al-Tamimi -Allah amridhie- na neno la Naafii bin Al-Azraq, na kupelekea hilo kupambanuka tafauti kubwa na iliyo wazi kuwa mtenda dhambi kubwa mkaidi wa kutubia kwa mujibu wa Ibadhi ni Muislamu mnafiki kafiri wa neema, ama kwa upande wa Makhawariji wa mwanzo anakua ni Kafiri Mshirikina Murtaddi. Na kwa kadiri ya kutafautina sifa ya mtenda dhambi kubwa baina ya miono hiyo miwili ndivo hukumu zilivotafautiana. Na hapa tunaweza kusema kuwa Maulamaa wa Kisunni walipoona kuwa Ibadhi wanaitakidi kuwa mtenda dhambi kubwa yoyote ni kafiri, na kuwa kafiri kwa mujibu wa mafundisho ya Kisunni ni mshirkina -sawa na mafundisho ya Khawariji- basi wakawakusanya Ibadhi katika mjumuiko wa makundi ya Kikhawariji na kuwabandika makosa yaliyofanywa na Makhawariji, na hii ndiyo sababu kubwa ya kuchafuliwa uhakika wa Ibadhi katika maandiko ya Wanavyuoni hao. Basi tufahamu kuwa mtenda dhambi kubwa isiyokua ya Kishirikina kwa mujibu wa tafauti za Madhehebu hizi tatu: IBADHI wanaitakidi kuwa: Mtenda dhambi mkaidi wa kutubia ni Muislamu Mnafiki Kafiri wa neema hana sifa ya imani ya kustahiki maridhio ya Allah mpaka atubie kwa Allah mtukufu, si halali damu yake wala mali yake ila kwa haki ya Uislamu. KHAWARIJI: Mtenda dhambi huyo ni Kafiri Mshirikina Murtaddi ima atubie au atauliwa na kuhodhiwa mali yake na kizazi chake. SUNNI: Mtenda dhambi huyo ni Muislamu Muumini, hata aasi namna gani, ikiwa tu hajafanya dhambi ya Ushirkina basi yeye atabakia kuwa ni Muislamu Muumini yuko mbali na Ukafiri na Ushirkina, na akifa katika hali hiyo Pepo ni yake, nao wamemuita Muumini mpungufu wa Imani. ULIZO:Huenda mtu akasema kwa nini tumetumia neno Khawariji wa mwanzo? JAWABU:Tumetumia neno hilo ili kutafutisha baina yao na Makhawariji wa zama za mwisho ambao ni Mawahabi; kwani kuna tafauti kubwa baina yao hata kama sifa ya ukahwariji ipo kwao wote. Kwani sifa ya Ukhawariji ni kuitakidi kwao hukumu ya kuritadi kila aliyetafautiana na wao katika masuala ya kidini na ulazima wa kumfanyia uadui na kumuua na kuhodhi mali ya murtaddi huyo katika hali ya uwezekano, na hili linapatikana kwa Mawahabi pia; kwani wao wanamuitakidi kila Muislamu mwenye kumtakasa Allah mtukufu na uwezekano wa kusifika kwa sifa za viungo na harakati kuwa ni murtaddi, nao wamemtungia jina la Muattwilah wakamuita kwa jina hilo, na kupitia hilo wakaitakidi ulazima wa kumtenga na kumuua Muattwilah na kuhodhi mali yake na kizazi chake pindi likiwezekana kufanywa hilo, bali wamefikia kuona kuwa ubaya wa Muattwilah ni zaidi ya ubaya wa Wayahudi na Wansara na Waabudia masanamu. Ama tafauti yao, ni kuwa wale Makhwariji wa mwanzo (Al-Azaariqah, Najidiyah, Sufriyah) walibeba vifuani mwao Itikadi ya ulazima wa kujiepusha na kila dhambi; kwani waliitakidi kwao kuwa dhambi zote ni Ushirkina, ama hawa Makhawariji wa Kiwahabi wao wanaona Madhambi yaliyo chini ya Ushirkina kama vile uzinifu, ulawiti, ubakaji, wizi, uuaji bila ya haki, kudhulumu waja, kula mali ya yatima, kula riba, uongo, n.k hayo hayadhuru kitu katika Imani iwapo utajiepusha na Ushirikina tu, wao wanaitakidi kuwa Allah anasamehe yote hayo hata kama mjendaji wake hakutubia, na kama ataadhibiwa basi ni kwa kuoshwa tu katika moto kisha kutolewa humo kwa Shafaa ya Mtume S.A.W. na kwenda Peponi. Allah atuepushe na shari za Makhwariji wote. Wabillahi taufiqi. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
“Na sisi hatuna madhehebu isipokuwa uislamu, basi tunaikubali haki kutoka kwa yoyote atakaye kuja nayo hata kama hapendwi, na tunaikataa batili kwa yoyote atakaye kuja nayo hata kama ni kipenzi, tunawajuwa watu kwa haki, basi mkuu kwetu ni yule atakaye ikubali haki, na mdogo kwetu ni yule atakaye ikataa haki.
Na sisi hatujapangiwa Madhehebu na Mwana wa Ibadhi, na unasibisho wetu kwake huyo ni kwa dharura ya kuainisha wakati kila kundi lilipochukuwa njia yake”.
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Masahaba -Allah mtukufu awaridhie- ni wale waliomuwahi Mtume wetu Muhammad S.A.W. katika uhai wake, wakakutana naye hali ya kuwa ni wenye kumuamini, na wakaendelea katika hali ya uislamu wao hadi kufa bila ya kuritadi. Aliulizwa Msatahiwa Sheikh Ahmad bin Hamed Al-Khalili -Allah amuhifadhi-: Ni upi msimamo wa Muislamu kuhusu Masahaba wa Mtume wa Allah S.A.W.? Jee! inafaa katika yaliyotokezea zama zao katika fitna na tafauti kutegemea neno lake Allah mtukufu: ((تِلْكَ أُمَّةٌ قَدْ خَلَتْ ۖ لَهَا مَا كَسَبَتْ وَلَكُم مَّا كَسَبْتُمْ ۖ وَلَا تُسْأَلُونَ عَمَّا كَانُوا يَعْمَلُونَ)) ((Huo ni umma umeshapita, una yake uliyochuma na nyinyi muna yenu muliyochuma na wala hamutaulizwa kuhusu waliyokuwa wakifayafanya)) [Baqarah 134]? Akasema Sheikh Mstahiwa: Hatulazimishwa kupekua yaliyopita, hakika kinachotulazimu ni kuboresha yaliyopo na tuanze na nafsi zetu, na mwendo wa uhai haurudi nyuma, basi haiwezekani kuyadiriki yaliyo kwisha pita na kuyatengeza yaliyoharibika, basi tuna nini sisi hata iwe kazi yetu ni kujishughulisha na yaliyopita tukapitwa na yaliyopo mbele yetu. فما مضى قبلك لو بساعة * فدعه ليس البحث عنه طاعة Kilichopita kabla yake hata kwa saa kiachie kwani kukitafuta si utiifu. Na Allah anajua zaidi. Kutokana na hapo Ibadhi hatuna katika Vitabu vyetu vilivohusishwa kwa elimu ya Itikadi mlango wa kuchambua fitna zilizotokezea kwa Masahaba, wala himizo lolote kwa waumini katika kuwachambua wao, hilo haliko kwetu, na lau kuwa si hujuma na tuhuma tunazozipata kutoka kwa wengine katika suala la Masahaba basi lisingalitoka kwetu wala neno moja kuelezea baadhi ya yaliyoandikwa na Wanaelimu wetu wa kabla ambayo hayakutoka nje ya duara la uadilifu wa Kiislamu bila ya kuingiwa na upendeleo wowote. Basi sisi hatuna himizo lolote la kumuitakidi vibaya Sahaba yoyote. Allah awaridhie Masahaba wa Mtume wetu Muhammad S.A.W. |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi Katika jawabu za Imam Abu Saidi Al-Kudami Allah amrehemu. Na nilisema kuhusu mwenye kukutia katika sera za Waislamu zilizonasibishwa na zilizomashuhuri na zinazojulikana kuwa wao wanamfanyia Baraa-a fulani kwa hadathi yake (dhambi yake kubwa), na wanamfanyia Walaayah fulani kwa kukubaliana kwake na Waislamu katika waliyoyaitakidi kuwa ndio haki. Jee!! Itamlazimu na yeye kufanya Walaayah au Baraa-a? JAWABU:Ama kuhusu Baraa-a, sisi hatujui kuwa yeye atawafanyia Baraa-a wahusika hao (waliotajwa) wenyewe isipokua kwa ushahidi wa ahadaathi zao (madhambi yake makubwa) au kwa umashuhuri wa hayo ulio pamoja naye, au awafanyie Baraa-a kwa sharti ya (kuthibiti) yale aliyoyakuta katika sifa zao. Ama Walaayah kwa waliowafanyia Walaayah imesemwa: Atawafaanyia Walaayah wale atakaokuta utajo wao mwema katika sera za Waislamu ambazo zimewasifu. Na wako waliosema kuwa hatafanya Walaayah isipokua kwa kutegemea sifa, na hilo ndilo linalopendeza zaidi kwangu; kwa sababu mimi sioni kuondoka uwezekano wa kukosea unaoweza kupatikana kwa wachukuzi wa muandiko (waandishi) na kuongeza katika Walaayah mambo ambayo hayakuwepo kwa Faqiihi ambaye Walaayah unalazimika kwa kupitia neno lake. Basi ikiwa ni sahihi (imethibiti) kuwa Faqiihi alikua akimuweka katika Walaayah hapo itamfalia kwake Walaayah wake kwa kutegemea hili. [Mohamed Al-Kindi: Bayaanu Shar-ii 3/158] |
Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi
UFUNGUO:
Baada ya kufa Mtume S.A.W. ulikuja Uongozi wa Makhalifa wanne maarufu nao ni Abu Bakar, na Omar, na Othman, na Ali, -Allah awaridhie-.
Katika mwisho wa kipindi cha uongozi wa Othman jamii ya Waislamu ilikuja juu na kumtaka aachie madaraka ili achaguliwe Kiongozi mwengine watakaemridhia aongoze serikali. Walifanya hivo kwa sababu ya makosa yaliyovunja uadilifu ambayo yamethibiti kwao, na kwa sababu hiyo Othman alizingirwa katika Ikulu kwa muda wa siku 40 na kupelekea kuuliwa, anasema Muawiyah bin Abi Sufiani: ((Na watu wa Madina wamemuua Othman, basi Ukhalifa hautarudi tena kwao)) [Rf. Alhaafidhu Haithami Majmau Zawaaidi 8949]. Anasema Ibnu Abdilbarri katika Istiiabu: (1437): “Abdurahman bin Udais Albalawi ni mmisri, yeye alishuhudia vita vya Hudaibiyah.” Ameeleza Asad bin Mussa kutoka kwa Ibnu Lahiiaa kutoka kwa Yazid bin Abi Habiib amesema: “Abdulrahman bin Udais Albalawi ni katika waliompa baia Mtume S.A.W. chini ya mti (Baiatu Ridhwaan).” Amesema Abu Amru (Ibnu Abdilbarri): “Huyu alikua ndiye kiongozi wa jeshi lililokuja Madina kutoka Misri, ambao walimzingira Othman na kumuua.” [Rf. Istiiaabu fi maarifati Al-Ashaabi 2/840].
Baada ya kuuliwa Othman alipewa Ali bin Abi Talib baia ya Uongozi, lakini uongozi wake ulikumbwa na mawimbi ya uasi uliosimamishwa na Masahaba wenzake kwa madai ya kutaka kulipiza kisasi cha damu ya Othman. Anasema Ibnu Taimia Al-Harrani: “Hakika Allah ameeleza kuwa yeye amejaalia kupata mapenzi walioamini na kufanya mazuri, na hii ni ahadi ya kweli kutoka kwake, na inajulikana kuwa Allah amejaalia kwa Masahaba kupata mapenzi katika moyo wa kila muislamu, hasa hasa Makhalifa kati yao -Allah awaridhie-, hasa hasa Abu Bakar na Omar; kwa hakika Masahaba wote na Matabiina walikua wakiwapenda wawili hao, nao walikua ndio karne bora yao, ama Ali (bin Abi Talib) yeye hakua hivyo; kwani kwa hakika wengi katika Masahaba na Matabiina walikua wakimchukia na wakimtukana na wakimpiga vita.” [Minhaaj Sunnati Nabawiyah 7/138].
Zubeir bin Awwaam na Talha bin Ubaidillahi na Bibi Aisha Mama wa Waumini Mke wa Mtume S.A.W. walihamasisha waislamu dhidi ya Imam Ali na kituo chao kilikua Basra ndani ya Iraq, amepokea Bukhari katika sahihi yake kuwa: ((Wakati Ali alipowapeleka Ammar na Hassan katika mji wa Kuufa kwa ajili ya kuwahimiza kuwa pamoja na yeye, Ammaar alikhutubia na akasema: Hakika mimi najua vizuri sana kuwa yeye (Aisha) ni mke wake (Mtume S.A.W.) katika Dunia na Akhera, lakini Allah amekufanyieni mtihani nyinyi , jee! mutamfuata yeye (Ali katika haki) au huyo (Aisha katika batili)?.” [Bukhari 3772]
Basi vita vya kwanza baina ya Waislamu wenyewe kwa wenyewe vikapiganwa katika mwaka 36 baada ya kufa Mtume S.A.W. kwa miaka 25, vita hivi alishinda Imam Ali, na katika waliouliwa ni Zubeir na Talha, ama Bibi Aisha yeye alitubia Allah amridhie.
Baada ya kumaliza vita hivo ikabidi Imam Ali apambane na uasi wa Mkuu wa Wilaya ya Shaam Muawiyah bin Abi Sufiyan aliyekataa kuutambua Uongozi wa Imam Ali, vita vikali vilipiganwa baina ya Ali na Muawiyah katika sehemu inayoitwa Siffain huko huko Iraqi, imesemwa kuwa Waislamu zaidi ya elfu sabiini walikufa katika vita hivi.
Muawiyah alipoona vita vinammaliza na kumzidi akavumbua ujanja wa kisiasa, basi alitoa wito wa kufanyika sulhu kwa kutoa kila upande msuluhishi wake, na watakavyoamua wasuluhishi hao wawili iwe ndio maamuzi na suluhisho la mwisho, kwa upande wa Imam Ali msuluhishi alikua Abu Mussa Al-Ashari, ama kwa upande wa Muawiyah alikua ni Amru bin Alaasi.
Wito huo wa Muawiyah ulizigawa safu za Imam Ali katika makundi mawili, moja liliukubali na jengine liliupinga na kuupiga vita vikali sana.
Ingawa Imam Ali mwenyewe alianza kwa kuupiga vita wito huo, lakini mwishoni akaukubali na kuushikilia vizuri.
Hapo wale walioona kuwa kukubali wito huo wa Muawiyah ni kosa na kuvunja hukumu ya Allah mtukufu na kuzikhini damu za Mashahidi waliozitoa nafsi zao kwa ajili ya haki na kuulinda uongozi waliamua kujitoa katika safu za Imam Ali huku wakitoa wito wao wa kujishika vizuri na Kitabu cha Allah (Laa hukma illa lillahi) hakuna hukumu isipokua ya Allah tu, nao walielekea katika mji unaoitwa Haaruraa, hapo walishauriana na kuchagua kiongozi wao Imam Abdullahi bin Wahbi Alrraasibii R.A., na baadae wakaamua kwenda katika mji wa Nahrawani. Hawa ndio Muhakkima, nao ndio Ahalu Naharawani, ama wapinzani wao waliwatungia jina la kuwapiga vita wakawaita Makhawariji, na wakazua dhidi yao hadithi nyingi za uongo walizomsemea Mtume S.A.W. kwa lengo la kuhimiza kuwapiga vita.
Matokeo ya Sulhu ya Abu Mussa Al-Ashari na Amru bin Alaasi yalimtoa madarakani Imam Ali, na yeye aliyapinga vikali sana na kupinga sulhu hiyo, lakini wapi, yakishamwagika hayazoleki, akajikuta yuko mbele ya Uongozi mpya wa wale waliojitoa katika safu zake, alijaribu kuwaita upande wake nao walimuita upande wao chini ya bendera ya Imam Abdullahi bin Wahbi Alrraasibii R.A.
Hapo akaamua kuwapelekea Mwanchuoni maarufu sana katika safu za Masahaba pia ni mtoto wa Ami yake nae ni Abdullahi bin Abbaas R.A. ili akajadiliane nao kwa lengo la kuwarejesha.
Endelea kusoma mjadala huo kwa makini ili uzijue hoja zao.
MJADALA
Albarraadi ambae ni Mwanachuoni Mwanatarehe anatueleza kama ilivyo katika kitabu chake Jawaahiri yake uk. 136 kuwa “Ali alimpeleka Abdullahi bin Abbaas kwa Muhakkima, basi alipofika kwao.
Walimwambia: Tunakukaribisha ewe Ibnu Abbaas, na tusingalifurahi lau angetujia mwengine pahala pako.
Akawambia: Ni kitu gani mulichokitia doa kwa Amiri wa Waumini (Ali bin Abi Talib) enyi Waislamu?
Wakamwambia: Tunakushuhudisha Allah ewe Ibnu Abbaas, hebu tuambie kuhusu jambo ambalo sisi na Ali tulikua tumo ndani yake. Jee! Lilikua ni uongofu au upotevu?
Akasema: Ewe Allah, kwa hakika lilikua ni uongofu.
Wakamwambia: Tunakushudisha Allah, jee! Kumuua Othman hakukua kwa mujibu wa aliyozusha na kukataa kwake hukumu ya Kitabu cha Allah?
Akasema: Ewe Allah, ndio (kulikua kwa sababu hiyo).
Wakasema: Allahu Akbar.
Wakamwambia: Hakika sisi tunakushuhudisha Allah, hivi hujui ya kuwa tulimuua Talha na Zubeir na waliokua pamoja nao siku ya vita vya Jamal kwa sababu ya uasi wao kwa mujibu wa Kitabu cha Allah na Sunna ya Nabii wake?
Akasema: Ewe Allah, ndio.
Wakamwambia: Ewe Ibnu Abbaas, jee! Kuna amri yoyote imemteremkia jamaa yako (Ali) kutoka mbinguni, na ambayo imeharamisha amri ambayo tulikua sisi na yeye tumejishika nayo?
Akasema: Hakuna.
Wakamwambia: Limemlazimikia jamaa yako (Ali) hili jambo.
Ibnu Abbaas akasema: Hakika nyinyi munajua vuzuri kuwa Allah ameamrisha kuhukumishwa mahakimu wawili katika mwanamme na mwanamke iwapo watagombana, na katika ndege aliyeuliwa na (Muhrim) aliyehirimia, basi vipi hilo lisifae kwa Umma wa Muhammad?
Wakasema: Ama hakika ilivyo hasa ni kuwa, kila jambo ambalo ndani yake umekuja upambanuzi (wa hukumu) kutoka kwa Allah basi hakutakua na nafasi kwa watu ya kuhukumisha wasuluhishi ndani yake, na kila jambo ambalo Allah ameliegemeza kwa watu basi hilo litakua kwao wao.
Unaonaje Ewe Ibnu Abbaas, lau kuwa mwizi ameiba na mzinifu amezini na mshutumu uzinifu ameshutumu, kisha Imamu wa Waislamu akataka kupitisha hukumu ya Allah kwao hao, nao wakakataa hilo na wakasema: Tutoe wasuluhishi wawili, mmoja kutoka kwetu na mmoja kutoka kwenu ili waliangalie jambo letu hili, na watakalo pitisha tuliridhie sote.. jee! Watu hapo watapata nafasi ya kumuhukumisha yoyote katika jambo hili?
Aasema: Ewe Allah, hapana.
Wakasema: Ewe Ibnu Abbaas, ni ipi hukumu ya Allah katika kundi la waasi? Jee! Allah siye aliyesema: ((Na lipigeni vita kundi linaloasi mpaka lirejee katika amri ya Allah))?
Akasema: Ewe Allah, ndio.
Wakasema: Hivi wewe hujui kuwa Muawiyah na Amru na walio pamoja nao, wote ni kundi la waasi? Hivi humuoni jamaa yako (Ali) anataka kupeleka wasuluhishi wawili kwa yule ambae Allah ameshabainisha hakumu ndani yake?
Wakasema: Ewe Ibnu Abbaas, hukumu ya ndege aliyeuliwa na muhrimu, na hukumu ya mwanamke na mumewe si kama hukumu katika vita na damu za waislamu na dini yao; kwa sababu hakuna katika chochote cha hukumu ya vita alichofanya Allah hukumu yake iwe kwa watu kama alivyofanya hukumu kwao katika ugomvi wa mwanamke na mumewe au ndege aliyeuliwa na muhrimu, na hayo ni kwa sababu Allah ameshapitisha hukumu yake katika Kitabu chake na kuibainisha kwa watu, kwa sababu Allah ameshasema katika Kitabu chake: ((Na wapigeni vita mpaka isiwepo fitna na hukumu yote iwe ya Allah tu)) na amesema: ((Lipigeni vita kundi linaloasi mpaka lirejee katika amri ya Allah)).
Basi tunakushuhudisha Allah ewe Ibnu Abbaas, jee! Unajua kuwa Muawiyah amerudi katika hukumu ya Allah?
Akasema: Ewe Allah, hapana.
Wakasema: Hebu tuambie kuhusu hii Aya ambayo umeileta baina yetu na baina yako. Vipi wanakua wasuluhishi wawili ndani yake, wanatakiwa wawe waadilifu au sio waadilifu?
Akasema: Bali wawe waadilifu.
Wakasema: Vipi Amru awe muadilifu na yeye jana alikua anatupiga vita na anamwaga damu yetu?! Ikiwa yeye ni muadilifu basi sisi hatutakua waadilifu hali ya kuwa ni wenye kumpiga vita, bisi vipi nyinyi mumemuhukumisha katika amri ya Allah, na kwa hakika Allah ameshapitisha hukumu yake kwa Muawiyah na kundi lake ya kuwa wapigwe vita mpaka warejee na warudi katika amri ya Allah na akasema: ((Na wapigeni vita mpaka isiwepo fitna na dini yote iwe kwa ajili ya Allah tu)) kwa hakika mumemuhukumisha Amru bin Alaasi naye ndiye aliyekua akimtia doa Mtume wa Allah S.A.W. imeteremka kuhusu yeye ((Hakika mtia doa wako ndiye aliye katikiwa na baraka)) pia alimshambulia Mtume wa Allah S.A.W. kwa beti sabiini za ushairi, basi S.A.W. akaema: “Ewe Allah hakika mimi sijui mashairi basi mlaani kwa kila beti laana moja.” Basi sisi hatuna utata kuhusu jambo lao na wewe unajua ya kuwa sisi tuliwaita kabla ya hapo katika Kitabu cha Allah wakati bado tuko pamoja na wabora wetu na wema wetu: Ammar bin Yaasir, na Khuzaimah bin Thaabit muhusishwa kwa shahada mbili, na wana wawili wa Budail Al-Khuzaai, na Haashim bin Uyainah, na Zaid bin Warqaa, basi walikikataa Kitabu cha Allah na kwa hili Waislamu walipigana mpaka wakapita, hivi unatuamrisha ewe Ibnu Abbaas tumuhukumishe Abu Mussa na Amru bin Alaasi na tuingine katika hukumu ya Muawiyah na tushuhudie kuwa yeye yuko katika uongofu baada ya kuwa sisi tunashuhudia kuwa yuko katika upotovu?!! Hivi unaridhia kwa hilo, tujisalimishe kwa hukumu yao na tushuhudie kuwa mashahidi wetu waliotangulia Ammaar na wenzake kuwa waliuliwa wakiwa katika batili?! Na kuwa wao wako Motoni, na kuwa wao ni watu wa upotevu hali ya kuwa waliuliwa wakiwa katika haki? Na tushuhudie kuwa wauliwa wao (yaani jeshi la Muawiyah) ya kuwa wameuliwa wakiwa katika haki baada kubainika kwetu na kujua ya kuwa waliuliwa wakiwa katika batili na udhalimu na uadui? Na nyinyi mumeshaandika baina yenu na baina yao maandiko mumeweka ndani yake kuahidiana na kuweka sila chini baina yenu, hali ya kuwa Allah amevunja kuahidiana baina ya Waislamu na wenye kupigana nao vita, na kwa hakika Suuratu Baraa-a haikuteremka isipokua kwa mwenye kukubali jizya tu, na haikusimamisha vita wala silaha wala hukumu kwa wenye kupigana vita mpaka warejee katika amri ya Allah.
Amenihadithia Abdullahi bin Yazid Al-Fuzari ya kuwa baadhi yao walisema: Ewe Ibnu Abbaas, ni ipi hukumu ya muhrimu aliyeua panzi?
Akasema: Ni kuhukumishwa waadilifu wawili.
Wakasema: Ewe Ibnu Abbaas, Jee Muislamu ana haki ya kuenziwa zaidi au panzi?
Akasema: Muislamu.
Akasema: Jee! Amru bin Alaasi amekua muadilifu nanyi mumempa jukumu ya kuhukumu katika damu za Waislamu?!!!
Tunakushuhudisha Allah ewe Ibnu Abbaas ya kuwa utakaporejea kwa jamaa yako (Ali) muambie hayo, na asije akatuwekea sisi vita kama vita vya Muawiyah hali ya kuwa hoja imeshamlazimu, na kwa hakika sisi tunachukia kumfanyia haraka mpaka hoja ya Kitabu imlazimu; kwani hapo tutakua tumeshatoa udhuru wetu baina yetu na Mola wetu.
Basi Ibnu Abbaas akaondoka hali ya kuwa ameshindwa hoja na ameshajua dalili zao na hakuweza kufanya chochote, na aliporejea kwa Ali alimuuliza: Umefanya nini?
Akasema: Kwa hakika hawa watu wamekushinda hoja ewe Ali, kwa hakika wamekutana na mimi kwa hoja ambazo nilikua nikiwashinda kwazo watu, nao wamenishinda hoja.