ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR ALLAHU AKBAR WA LILLAAHIL-HAMDU
Shukurani zote ni kwa Allah mwingi wa kuneemesha mwingi wa kukirimu, na rehma na amani ziwe kwa Mtume wetu Muhammad na kila aliyeongoka kwa uongofu wake.
Kwa hakika ni neema kubwa sana kuweza kutimiza ibada ya funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, ibada ambayo lengo lake ni kuhakikisha uchamungu katika maisha ya Muislamu, basi kwa mnasaba huu www.ibadhi.com inatanguliza hogera za utimilivu wa Ibada hii kwetu na kwa Waislamu wote, pia inawatakia Iddi ya kheri na barka, pia tunachukua fursa ya kusema kuwa Allah mtukufu ametuambia:
وَلِتُكَبِّرُوا اللَّهَ عَلَىٰ مَا هَدَاكُمْ وَلَعَلَّكُمْ تَشْكُرُونَ
((Na ili mutimize hesabu kamili na mumtukuze Allah na muweze kumshukuru)) [Baqarah 185]
Basi tujue kuwa siku ya Iddi ni kwa ajili ya kumtukuza Allah na kumshukuru katika neema zake, inatulazimu kuzitumia neema zake katika anayoyaridhia kwani huko ndiko kumshukuru, na tujiepushe kuzitumia neema zake katika aliyokataza na kuharamisha kwani kufanya hivo ni kumkufuru katika neema zake.
Iddi si kuitika wito wa Shetani katika maasi ya kushibisha matamanio ya nafsi katika haramu, bali ni kuunganisha jamaa na ndugu na majirani na marafki, ni kupongezana, na kuunganisha yaliyokatika kwa uhasama, ni kusameheana, na kuzawadiana katika aliyoridhia Allah mtukufu.
Na risala yetu kwa Waislamu wote ni HAKIKISHA UCHAMUNGU WAKO KATIKA IDDI YAKO.
Tunamuomba Allah mtukufu azikubali Ibada na asamehe makosa.
KULLU AAMIN WA ANTUM BIKHAIRIN.
IDDI YA BARKA NA UPENDO.
