Home Introduction MLANGO WA KWANZA – 2.Hadithi ya yule mtu aliyekosea kusali, na imepokewa...

MLANGO WA KWANZA – 2.Hadithi ya yule mtu aliyekosea kusali, na imepokewa katika njia mbili

231
0

PILI

Hadithi ya yule mtu aliyekosea kusali, na imepokewa katika njia mbili:

1-Kwa njia ya Abi Hurayrah (r.a) ambayo imekuja kwa ujumla, na hii ndiyo naswi ya hadithi yenyewe ambayo ameipokea Imam Muslim:

 

عَنْ أَبِى هُرَيْرَةَ أَنَّ رَسُولَ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- دَخَلَ الْمَسْجِدَ فَدَخَلَ رَجُلٌ فَصَلَّى ثُمَّ جَاءَ فَسَلَّمَ عَلَى رَسُولِ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- فَرَدَّ رَسُولُ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- السَّلاَمَ قَالَ « ارْجِعْ فَصَلِّ فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ ». فَرَجَعَ الرَّجُلُ فَصَلَّى كَمَا كَانَ صَلَّى ثُمَّ جَاءَ إِلَى النَّبِىِّ -صلى الله عليه وسلم- فَسَلَّمَ عَلَيْهِ فَقَالَ رَسُولُ اللَّهِ -صلى الله عليه وسلم- « وَعَلَيْكَ السَّلاَمُ » . ثُمَّ قَالَ

« ارْجِعْ فَصَلِّ فَإِنَّكَ لَمْ تُصَلِّ ». حَتَّى فَعَلَ ذَلِكَ ثَلاَثَ مَرَّاتٍ ، فَقَالَ الرَّجُلُ وَالَّذِى بَعَثَكَ بِالْحَقِّ مَا أُحْسِنُ غَيْرَ هَذَا عَلِّمْنِى. قَالَ « إِذَا قُمْتَ إِلَى الصَّلاَةِ فَكَبِّرْ ثُمَّ اقْرَأْ مَا تَيَسَّرَ مَعَكَ مِنَ الْقُرْآنِ ثُمَّ ارْكَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ رَاكِعًا ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَعْتَدِلَ قَائِمًا ثُمَّ اسْجُدْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ سَاجِدًا ثُمَّ ارْفَعْ حَتَّى تَطْمَئِنَّ جَالِسًا ثُمَّ افْعَلْ ذَلِكَ فِى صَلاَتِكَ كُلِّهَا »2.

___________________________

2-صحيح مسلم شرح الإمام النووي ـ المجلد 2/ج4 /ص107 ـ 106 ـ دار الفكري للطباعة والنشر والتوزيع ـ 1401 هـ / 1981

_________________________

TAFSIRI:

Kutoka kwa Abi Hurayrah (r.a)

kuwa: “Hakika Mjumbe wa Allah (s.a.w) aliingia msikitini, na punde akaingia mtu akaja akasali kisha (alipomaliza) akaja kumsalimia Bwana Mtume (s.a.w), na Bwana Mtume akamrudishia salamu na akamwambia rudi ukasali kwa hakika wewe hukusali, yule mtu akarudia kusali kama alivyosali mwanzo, kisha akaja kwa Bwana Mtume (s.a.w) kumsalimia, Bwana Mtume akamjibu salam yake, na akamwambia rudi ukasali kwani wewe hujasali, mpaka akafanya hivyo mara tatu, yule mtu akasema kumwambia Bwana Mtume (s.a.w): “Naapa kwa yule ambaye amekutuma wewe kwa haki, hakika siwezi kusali vizuri zaidi ya hivi nilivyofanya, (basi) nielimishe”, akasema (s.a.w) “Utaposimama kwa ajili ya swala piga takbira, kisha soma chochote kidogo katika Qur-ani, kisha utarukuu hadi utulie katika rukuu, kisha utainuka hadi usimame sawa sawa, kisha utasujudu hadi utulie sawa sawa katika sijda, kisha utainuka hadi utulie katika kukaa kwako, utafanya hivyo katika swala yako yote”.

2-Kwa njia ya Rifaa bnu Raafi-i na katika hadithi hii imekuja kwa ufafanuzi zaidi na hii ndio hadithi yenyewe ameipokea Abu Daud:

“Kuna mtu aliingia msikitini akaelezea kama alivyoelezea Abu Hurayrah … akasema Mjumbe wa Allah (s.a.w): “Kwa hakika haitimii swala ya mtu yeyote mpaka atawadhe inavyotakikana, kisha alete takbira amshukuru Allah mtukufu na amsifu, kisha asome chochote anachokitaka katika Qur-ani, kisha aseme Allahu akbar, halafu arukuu hadi viungo vyake vitulie, kisha atasema samiallahu liman hamidah, mpaka asimame sawa sawa kisha atasema Allahu akbar, kisha atasujudu hadi viungo vyake vitulie, kisha atasema Allahu akbar, kisha atainuka na kukaa sawa sawa, kisha atasema Allahu akbar, kisha atasujudu mpaka viungo vyake vitulie, kisha atainua kichwa chake na kupiga takbira, basi ikiwa atafanya hivyo swala yake itatimia”.3

Na katika riwaya nyengine katika upokezi wa Abi Daud mwisho wake amesema: “Atakaa sawa sawa kwa kukalia makalio yake na kuweka sawa mgongo wake, -akaielezea swala namna hiyo katika rakaa zote nne hadi kumaliza-, na kusema: Haitimii swala ya mmoja wenu mpaka afanye kama hivyo”.4

Amesema mwanachuoni Assubkiy kwenye sherhe ya sunan Abi Daud: “Kauli yake akaielezea swala namna hiyo …hadi mwisho” yaani amesema Rifaa akaielezea Bwana Mtume (s.a.w) namna hiyo iliyotajwa, mpaka akaelezea rakaa zote nne hadi mwisho wa swala, na Bwana Mtume (s.a.w) baada ya kumaliza kuielezea hiyo swala akasema haitimii swala ya mmoja wenu mpaka afanye kama nilivyoelezea.

Kwa hakika hadithi hii imeweka wazi lililo wajib na sunna na imekusanya namna ya kuisali swala yenyewe, na wala hamkutajwa ndani yake kuinua mikono wala kuifunga, kutokana na hayo ndiyo washereheshaji wa hadithi hii wamesema: “Yaliyotajwa katika hadithi hii ndiyo yaliyo ya wajibu na yasiyotajwa si wajibu”, na hivi ndivyo alivyosema mtunzi wa kitabu cha Subulu ssalaam:

” وَاعْلَمْ ” أَنَّ هَذَا حَدِيثٌ جَلِيلٌ تَكَرَّرَ مِنَ العُلَمَاءِ الاِسْتِدْلاَل بِهِ عَلَى وُجُوبِ كُلِّ مَا ذُكِرَ فِيهِ وَعَدَمِ وُجُوبِ كُلِّ مَا لَمْ يُذْكَرْ فِيهِ أَمَّا الاِسْتِدْلاَلُ عَلَى أَنَّ كُلَّ مَا ذُكِرَ فِيهِ وَاجِبٌ ]فَلأَنَّهُ سَاقَهُ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ بِلَفْظِ الأَمْرِ بَعْدَ قَوْلِهِ : ” لَنْ تَتِمَّ الصَّلاَةُ إِلاَّ بِمَا ذُكِرَ فِيهِ ” وَأَمَّا الاِسْتِدْلاَلُ بِأَنَّ كُلَّ مَا لَمْ يُذْكَرْ فِيهِ لاَ يَجِبُ[[5 فَلأَنَّ الْمَقَامَ مَقَامُ تَعْلِيمِ الْوَاجِبَاتِ فِي الصَّلاَةِ فَلَوْ تُرِكَ ذِكْرُ بَعْضِ مَا يَجِبُ لَكَانَ فِيهِ تَأْخِيرُ الْبَيَانِ عَنْ وَقْتِ الْحَاجَةِ وَهُوَ لاَ يَجُوزُ بِالإِجْمَاعِ “.
_____________________________________________________

[3] -Abu Daud Hadithi nambari:857 – juzuu 1/ 288 المكتبة الشاملة ط 3 –

[4]-Abu Daud Hadithi nambari: – 858 juzuu 1/ 288 المكتبة الشاملة ط 3 –

[5] – Maneno niliyoyatia katika mabano [… ] Shekh ameyasahau kuyanukuu.

_____________________________________

TAFSIRI:

“Na elewa ya kuwa hadithi hii ni tukufu sana wameirudiarudia sana wanavyuoni katika kuitolea dalili juu ya kuwajibika kila kilichotajwa, na kutowajibika kila kisichotajwa ndani yake.

Ama udalili wa kuwajibika kila kilichotajwa ni kwa sababu Bwana Mtume (s.a.w) ameielezea kwa lafdhi ya kuamrisha baada ya kauli yake ” لَنْ تَتِمَّ الصَّلاَةُ إلاَّ بِمَا ذُكِرَ فِيهِ “. Ama udalili wa kuwa kila kisichotajwa ndani yake si wajibu kwa sababu pahala hapo ni pakufundisha mambo ya wajibu katika swala, na lau kama ingaliwachwa kuelezewa baadhi ya mambo yaliyo ya wajibu ingalipatikana kucheleweshwa kubainisha mambo wakati unaohitajika, na kufanya hivyo haijuzu kwa kauli ya ijmaa”.6

Na wewe unaona ya kuwa hadithi hii tukufu haijagusia lolote juu ya suala la kuinua na kufunga mikono, na akitokea msemaji akasema: “Kwa hakika kuinua na kufunga mikono ni vitendo viwili maarufu katika swala wala havihitajii kuelezewa katika hadithi hiyo”.

Jawabu juu hilo ni:

Wale wanaokubalisha kuinua na kufunga mikono wamepokea kutoka kwa Ibni Masoud (r.a) kuwa aliweka mkono wake wa kushoto juu ya kulia (katika swala), Bwana Mtume (s.a.w) alipomuona akauchukua mkono wake wa kulia na kuuweka juu ya kushoto, basi ikiwa Ibnu Masoud (r.a) naye ni miongoni mwa maswahaba wakubwa na mwanachuoni wao ambaye Mjumbe wa Allah amemsifu kwa kusema (amejaa elimu tokea juu ya utosi wake hadi chini ya nyayo zake) naye amekosea kuweka mikono yake kwa mujibu ya walivyopokea, basi vipi kwa huyu bedui ambaye hakuweza kuisali swala kwa usahihi kwa mara nyingi, jee? Hahitajii kuwekewa wazi suala la kufunga na kuinua mikono katika swala kama ingalikuwa jambo hili lina usahihi ?.

 

Previous articleMLANGO WA KWANZA – 3.Na simamisheni swala
Next articleMLANGO WA KWANZA – 1.RAI YA MAIBADHI KATIKA KUNYANYUA NA KUFUNGA MIKONO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here