Assalaamu alaykum warahmatullahi taala wabarakaatuhu ndugu zangu, baada ya salamu rehma na amani zimfikie Bwana wetu mpenzi Nabii Muhammad na Swahaba zake watukufu na wote waliofuata nyayo zao hadi siku ya kiama.
Sina budi kumshukuru Allah mtukufu kwa kuniwafikisha katika moja ya mambo ya kheri nikaweza kukifanyia tarjuma kijitabu hiki.
Baada ya kukisoma kitabu hiki ambacho kimeandikwa na Sheikh Ahmad bin Soud Assiyaabiy na kuona kilichomo ndani yake na faida zilizomo, nikaonelea ipo haja ya kukifanyia tarjuma kwa lugha ya Kiswahili ili na wengine wasioelewa lugha ya kiarabu na wao wapate kufaidika, hasa Maibadhi wapate kujua kwa nini wao hawainui na hawafungi mikono na vile vile ndugu zetu wasio Maibadhi wajue angalau kwa ufupi sababu zilizowafanya ndugu zao Maibadhi wasiinue na wasifunge mikono wakati wa kusali.
Pamoja na kuwa kitabu chenyewe ni kidogo kwa kurasa kama alivyosema mwenyewe mtunzi wa kitabu hicho, lakini faida iliyomo ni kubwa sana, kwani uzuri wa kitabu hautizamwi wingi wa kurasa bali hutizamwa faida iliyomo ndani yake.
Kazi niliyoifanya ni :
1- kutarjumu kitabu chote (Teremsha Kitabu Kamili Kwa PDF)
2- kuhakikisha usahihi wa maneno aliyonukuu Sheikh kwa kurudia na kuangalia kwenye asli ya vitabu alivyovitaja
3- kuna baadhi ya maneno yamerukwa ima ameyawacha makusudi au yamesahauliwa wakati wa kuchapishwa kitabu, kutokana na umuhimu wake mimi nimeyaingiza ingawa ni machache mno na nimeyaweka ndani ya mabano [ … ] na kuelezea na atakaeangalia kitabu cha kiarabu na tarjuma hii anaweza kuona jambo hilo kwa hivyo namuomba radhi Sheikh wangu juu ya hilo na nataraji amenisamehe
4- kufanyia takhriji ya kauli hizo kwa kutaja kitabu, jina la Mtunzi Mujallad, juzuu na ukurasa
5- kufanya takhriji ya wapokezi wa hadithi aliowataja Sheikh ambao wamesababisha hadithi walizozipokea kuwa dhaifu au kuwa na illa kwa kutaja jina la kitabu, Mujallad au Juzuu na ukurasa
6- Takhriji nyingi nimetumia disc ya Almaktabatu-shshamilah na nyengine nimerudia katika vitabu vyenyewe na kutaja kimechapishwa na nani, mwaka kilochapishwa n.k.
Natarajia kuwa tarjuma yangu hii itaeleweka kirahisi kwa hivyo kama nimepatia basi hiyo ni tawfiki kutoka kwa Allah na kama nimekosea makosa hayo yatakuwa yametokea kwangu.
Tunamuomba Allah atuwafikishe katika kila jambo analoliridhia na analolipenda.