Kumsalia Mtume S.A.W. inakuwa katika ttahiyatu ya mwisho kabla ya kutoa salam kufuatana na kauli iliyo mashuhuri ya wanavyuoni. Ziko namna nyingi za kumsalia Mtume S.A.W. zilizothibiti kutoka kwake, inaruhusiwa kutumia yoyote ile miongoni mwake. Kasema Abi Masoud R.A.A., “Mtume (S.A.W.) alitujia katika seble (ukumbi) wa Sa`ad bin `Ubaadah, Bashiyr akamwambia (Mtume S.A.W.), “Mwenyezi Mungu ametuamuru tukusalie basi vipi tukusalie?” Akanyamaza kimya mpaka tukasahau kama kamwuliza “Akasema, Semeni,[1] “
اللَّهُمَّ صَلِّ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا صَلَّيْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ وَبَارِكْ عَلَى مُحَمَّدٍ وَعَلَى آلِ مُحَمَّدٍ كَمَا بَارَكْتَ عَلَى إِبْرَاهِيمَ وَعَلَى آلِ إِبْرَاهِيمَ فِي الْعَالَمِينَ إِنَّكَ حَمِيدٌ مَجِيدٌ.
ALLAHUMMA SSALI ALA MUHAMMAD WA ALAA ALI MUHAMMAD KAMA SALAYTA ALA IBRAHIM WA ALAA ALI IBRAHIM WA BARIK ALAA MUHAMMAD WA ALAA ALI MUHAMMAD KAMA BARAKATA ALAA IBRAHIM WA ALAA ALI IBRAHIM FIL ALAMIINA INNAKA HAMIDU MAJID.
Maana yake, “Ewe Mwenyezi Mungu mpe Rehema Muhammad na watu wake, kama ulivyompa rehema Ibrahim na watu wake. Na umbarikie Muhammad na watu wake, kama ulivyombarikia Ibrahim na watu wake. Wewe ndiye unastahiki kuhimidiwa[2] na kila kiumbe, na ndiye Mwenye Utukufu.”
[1] AAt-Ttirmidhiy 11/9 (3144).
[2] Kutukuzwa na kushukuriwa.