Home kujenga uongofu katika nyoyo za vijana Wajibu wa mwanzo wa Muislamu

Wajibu wa mwanzo wa Muislamu

279
0
Wajibu wa mwanzo wa Muislamu
Jua (ewe Muislamu) Allah akuongoze wewe pamoja nasi katika kumtii Subhanahu Wataala kuwa kitu cha mwanzo kinachomuwajibikia Muislamu kukijua ni kumjua Mola wake aliyemuumba na kumpa riziki, naye ni “Allah”. Allah ambaye ameumba kila kitu na hakuna kitu kilicho kama Yeye, wala haonekani Duniani wala Akhera; kwani angekuwa aonekana basi angefanana na viumbe vyake. Hana mshirika wala msaidizi, wala waziri wala mshauri. Yuhai siku zote na ni mwenye uwezo na ujuzi wa kila kitu.
Kasema Allah katika sura Al-An’aam, aya 59:
وَعِنْدَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لاَ يَعْلَمُهَا إِلاَّ هُوَ وَيَعْلَمُ مَا فِي الْبَرِّ وَالْبَحْرِ وَمَا تَسْقُطُ مِنْ وَرَقَةٍ إِلاَّ يَعْلَمُهَا وَلاَ حَبَّةٍ فِي ظُلُمَاتِ الأَرْضِ وَلاَ رَطْبٍ وَلاَ يَابِسٍ إِلاَّ فِي كِتَابٍ مُبِينٍ (الأنعام: 59)
“Na ziko kwake funguo za siri; hakuna azijuaye ila yeye tu. Na anajua yaliyomo katika bara na bahari. Na halianguki jani ila anajua; wala (haianguki) punje katika giza la ardhi (ila anajua), wala (hakianguki) kilicho kibichi wala kikavu (ila anajua). (Hapana chochote) ila kimo katika kitabu kinachobainisha (kila kitu).”
Kasema Allah katika sura Fatir, aya 11:
وَاللَّهُ خَلَقَكُمْ مِنْ تُرَابٍ ثُمَّ مِنْ نُطْفَةٍ ثُمَّ جَعَلَكُمْ أَزْوَاجًا وَمَا تَحْمِلُ مِنْ أُنْثَى وَلاَ تَضَعُ إِلاَّ بِعِلْمِهِ وَمَا يُعَمَّرُ مِنْ مُعَمَّرٍ وَلاَ يُنْقَصُ مِنْ عُمُرِهِ إِلاَّ فِي كِتَابٍ إِنَّ ذَلِكَ عَلَى اللَّهِ يَسِيرٌ (فاطر: 11)
 “Na Allah Amekuumbeni kwa udongo, kisha kwa tone la manii, kisha akakufanyeni wanaume na wanawake. Na mwanamke ye yote hapati mimba wala hazai ila kwa kujua Yeye (Mola). Na mwenye kupewa umri hapewi umri (zaidi) wala hapunguziwi umri ila mambo hayo yamo katika kitabu (cha Mola). Bila shaka (kuyapitisha) haya ni sahali kwa Allah”
Hayo ndiyo mambo ya mwanzo ambayo ni lazima Muislamu ayajue. Kisha inampasa amjue Mtume wake Muhammad Salallahu Alayhi Wasalam kuwa ndiye aliyeletwa na Allah Subhanahu Wataala ili awaongoze watu katika njia ya Haki na yeye ni mkweli kwa ayasemayo, na ni wajibu wa kila Muislamu kufuata ayasemayo Salallahu Alayhi Wasalam na ayatendayo. Na kuwa yeye Salallahu Alayhi Wasalam amezaliwa Makka na akapewa Utume na Ujumbe huko huko Makka, kisha akahamia Madina na kuanzia huko ikatangaa Dini ya Kiislamu. Alifia huko Madina na kaburi lake liko huko mpaka Siku ya Kiyama.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here