Home KUSAHAU NA HUKUMU ZAKE KUSAHAU NA HUKUMU ZAKE : 6

KUSAHAU NA HUKUMU ZAKE : 6

240
0

Mtu alisalisha jamaa katika sala ya magharibi akasahau kusoma baada ya alfaatiha akarukuu, walipomsabihia akarudi kwenye kusoma na akakamilisha sala yake. Alipomaliza mmoja wa maamuma alimwambia kwamba aliharibu sala yake kwasababu ya kurejea nguzo mara mbili, je unaona Mstahiwa Sheikh uharibifu wowote katika sala yake?Mwenye kuacha kusoma kilicho zaidi ya alfaatiha katika rakaa ya kijahara kwa kusahau akatanabahishwa au kutanabahi baada ya kuwa ameshashuka kurukuu, basi katika kurejea kwake kwenye kusoma kuna khilafu. Kauli sahihi ni kwamba kisomo hicho kinalipwa kwa sujudu ya sahau, kwasababu – ingawa haijuzu kwa hali yo yote kukiacha kwa makusudi – hakifikii daraja ya kuwa nguzo. Hivyo akikiacha akenda kwenye rukuu kwa sahau haruhusiwi kukirejelea –kama ilivo katika nguzo. Ama akitokezea kufanya hilo mtu ambaye hana uwezo wa kuipa uzito kauli moja kuliko nyengine na kwa hiyo akarejea kwenye kisomo basi huyo amefuata kauli mojawapo kati ya rai za maulama wa umma, na kwa hiyo haipasi kulazimishwa kurudia sala, isipokuwa tu ikiwa hilo ni kwa ajili ya kuchukua hadhari katika Dini na kufanya hima ya kutokana na jukumu la khilafu, na hiyo ni katika ziada ya hadhari ambayo mwenye ilmu anapaswa asiwalazimisha watu kuifanya kwa fatwa yake. Na Allah anajua zaidi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here