Home Mujtahiduna BARUA YA MTUME MOHAMMED (SAW) KWA WAFALME WA OMAN

BARUA YA MTUME MOHAMMED (SAW) KWA WAFALME WA OMAN

511
0

JAYFAR NA ABDI WANA WA JULANDA AL AZDY (R.A)

KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHEMA MWIGI WA KUREHEMU

KUTOKA KWA MUHAMMAD MTUME WA ALLAH KWENDA KWA JEYFAR NA ABDI WANA WA JULANDAA. NA AMANI KWA MWENYE KUFUATA UONGOFU.

AMA BAAD.

HAKIKA MIMI NINAKUITENI KATIKA WITO WA UISLAMU, SILIMUNI MUTASALIMIKA; KWANI HAKIKA MIMI NI MTUME WA ALLAH KWA WATU WOTE KWA KUMUONYA ALIYE HAI NA LISHIKE NENO LA ADHABU KWA MAKAFIRI. BASI MUKIUKUBALI UISLAMU NINAWATAWALISHA NA MUKIKATAA HAKIKA UFALME WENU UTAONDOKA NA FARASI WANGU WATAKUWA KATIKA SEHEMU ZENU NA UTADHIHIRI UNABII WANGU KATIKA UFALME WENU.

RASUULULLAHI MUHAMMAD.

Barua hii iliwafika Wafalme hao wawili wema kabla ya ufunguzi wa mji wa Makka, basi katika mwaka wa 8 A.H. – 630 – ndipo Mtume (s.a.w.) alipowapelekea Barua katika mkono wa Bwana Amru bin Al Aasi Assahami. Bwana huyu alimwendea Bwana Abdi kwanza; kwani ndiye aliyekuwa akisifiwa kwa upole na ubaridi. Baada ya kuamini yeye ndipo alipofuatana naye kwenda kwa mkubwa wake Bwana Jayfar. Bwana mkubwa huyu alimdadisi vyema Bwana Amru. Alimuuliza tarehe ya Mtume (s.a.w.) tangu kuzaliwa kwake mpaka siku hiyo na watu gani watukufu walioacha dini zao wakafuata dini hiyo mpya. Bwana Amru baada ya kumtajia watukufu hao, na baada ya kuyakinisha ukweli wa maneno ya Bwana Amru, alisilimu pale pale na watu wake wote waliokuwa katika mji wa Suhar – uliokua mji mkuu wa nchi ya Oman siku hizo –. Kisha watu wa miji mengine nao wakafuata.

Bwana Amru baada ya haya hakuondoka akaenda zake, bali alikaa kuwafundisha dini na kutazama namna gani mambo yake yalivyopitishwa. Katika muda huu wa kuwapo Bwana Amru katika Ardhi ya Oman akiwa pamoja na wale Wafalme wawili Abdi na Jayfar, yule mkubwa alifanya bidii kubwa ya kuwataka kila waliokuwa chini ya mamlaka yake wafuate dini ya Uislamu, aliwapelekea barua za kuwafahamisha Uislamu na kuwataka wasilimu – na wasilimishe kila Maliwali wake waliokuwa katika nchi za kusini – kama nchi za Wamahara na wengineo na waliokuwa kaskazini. Maliwali wote hawa walileta jawabu nzuri za kubainisha kuwa wao wamesilimu na kila aliopo nchi yao kwa kishindo kikubwa.

Baada ya siku nyingi kidogo kupita Bwana Amru alipata habari ya kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa. Akapatwa na majonzi makubwa, hata asiweze tena kukaa Oman, akaazimia kwenda zake Madina. Bwana Abdi – yule Mfalme mdogo katika ya ndugu wawili – na baadhi ya mabwana wakubwa wa Kioman walifuatana na Bwana huyu mpaka Madina wakiwa pamoja na mjumbe wa Mtume Muhammad (S.A.W) Bwana Amru Assahami. Na huko walimkuta Sayyidna Abu Bakr ndiye Khalifa. Khalifa huyu aliwatukuza sana watu wa Oman na akawashukuru mno kwa wema wao wa kuusihi Uislamu kwa hiyari zao na ukarimu wao waliomfanyia Bwana Amru tangu kufika kwake huko Oman mpaka kurejea kwake. Baada ya kukaa huko kidogo na kujuana na mabwana wakubwa wa Kisahaba, mabwana hawa wa Kiomani walirejea kwao nao wamejaa mambo mengi mazuri ya dini ya kawafunza watu wao. Na wajukuu wa Mfalme huyu Bwana Abdi – naye ni Bwana Suleyman bin Abdallah bin Abd, na ndugu yake Bwana Saad – wao na wenzao waliokuja pande za Afrika Mashariki kiasi cha mwaka 75 A.H (695) kwa sababu ya mavamizi yaliyofanywa na Utawala wa Kifalme wa Bani Umayyah dhidi ya Oman. Nao ndiwo waliolimbusha Uislamu ndani ya Afrika Mashariki mapema sana na kuendelea mpaka hivi leo.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here