Home kuwapelekea barua wafalme waliokuwa karibu na bara arabu 12. KUWAPELEKEA BARUA WAFALME WALIOKUWA KARIBU NA BARA ARABU

12. KUWAPELEKEA BARUA WAFALME WALIOKUWA KARIBU NA BARA ARABU

252
0

Alipokwisha kutulia na watu wake wakapumua roho zao kwa ile sulhu ya Hudaybiya iliyoahidi kuzuilia vita kwa miaka 10 – Mtume (s.a.w.) aliona ni shauri nzuri sana kuwaandikia barua Wafalme wa zama hizo na kuwataka kuingia katika dini ya Kiislamu. Kwa hivyo akafua mhuri wake wa kupigia chapa kila barua atakayowapelekea hao na wengine, kwani alipewa habari kuwa Wafalme hawakubali kupokea barua za mtu asiye kuwa na mhuri wake makhsusi. Chapa ya mhuri huo ulikuwa “Muhammad Rasulu Llah.”

 

Baada ya kutengeza mhuri huo Mtume (s.a.w.) alichagua Masahaba mahodari waliokuwa wakizijua vyema nchi za hao alioazimia kuwapelekea barua.  Wafalme wenyewe wanaojulikana kwa hakika kuwa wamepelekewa barua hizo ni kumi:

 

1. HIRAK (HERACLIUS) MFALME WA DOLA YA KIRUMI

 

Alipelekewa barua hii wakati alipokuja Palestine kuzuru mji wa Baitil Maqdis (Jerusalem) kwa ajili ya kumshukuru Mwenyezi Mungu aliyewapa nguvu wakawashinda Maajemi (Persians), na wakawaondoa katika nchi ya Asia Minor baada ya kuwa hawa Maajemi wamezihozi nchi hizo kwa Warume kwa muda wa miaka 10. Barua hii ilipelekwa katika mwaka 7 A.H. (628) aliyeipeleka ni Bwana Dihya bin Khalifa. Mfalme huyu aliipokea barua hii kwa uzuri, akaisomesha na akaifahamu madhumuni yake, lakini hakusilimu, bali katika mwaka wa pili 8 A.H. (629) alizatiti jeshi kubwa kuja kuwapiga Waislamu. Jeshi hili lilikutana na Waislamu katika mahali palipokuwa pakiitwa Muuta, na Waislamu wengi walikufa na Majamadari wao 3 aliowachagua Mtume (s.a.w.) waliuawa pia.

 

Baada ya kuuawa Majamadari hawa, wapiganaji wakamchagua Bwana Khalida bin Al Walid awe Amirijeshi. Bwana huyu alipiganisha kwa uhodari mkubwa hata akajipatia jina hili analotajikana nalo mpaka sasa. Tangu siku hiyo ndipo alipoanza kupewa Ujamadari wa vita na Mtume (s.a.w.) na kupewa jina la “Simba wa Mungu.”

 

2. KISRA IBARWIZ (CHOSROES EPARWIZ)

 

Mfalme wa Dola ya Kiajemi siku hizo, alipelekewa barua hii na Bwana Abdalla bin Hudhafa. Kupewa tu barua hii, huyo Kisra aliichana bila ya kuisomesha, na akaamrisha afukuziliwe mbali huyo aliyeileta. Mtume (s.a.w.) kupata habari hii, alikasirika sana akasema: “Na yeye Ufalme wake utachanikachanika kama alivyoichana barua yangu.”

 

Maneno haya ya Mtume (s.a.w.) hayakuanguka chini, kwani haikupita miaka 3 tangu kufa Mtume (s.a.w.) ila Ufalme wa Kiajemi ulianza kurithiwa na Waislamu, mpaka leo haukurejea tena, ingawa waliweza kuurejesha Ufalme wa nchi yao yote (Persia) tangu muda wa zaidi ya mika 1000 mpaka sasa.

 

3. NAJASH AS-HAM

 

Mfalme wa Dola yote ya Kihabushia ya siku hizo ambayo ilikuwa kubwa zaidi kuliko hii ya zama za Haile Selassie huyu, kwani nchi ya Somalia na baadhi ya Nubia zilikuwa ndani ya Dola hiyo. Mfalme huyu ndiye yule yule ambaye Mtume (s.a.w.) alimpelekea baadhi ya Masahaba zake wakakae katika nchi yake wakati Mtume (s.a.w.) alipokuwako Makka bado. Mpaka wakati huu wa kupelekwa barua hii wengi katika Masahaba hao walikuwa bado wapo kuko huko Uhabushia. Barua hii ilifikishwa kwenye mji wa Aksum, ambao ndiyo uliokuwa mji mkubwa wa Dola ya Kihabushia siku hizo. Aliyepewa kuifikisha barua hii ni Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Amr bin Umayya. Mfalme huyu kuipata barua hii aliifanyia hishma kubwa, na akafurahi nayo sana, akaitafutia mahali pazuri kabisa akaitia. Baadaye akamwandikia barua Mtume (s.a.w.) ya kumjibu, alimjibisha akamwambia: “Mimi na mwanangu na baadhi ya watu wa nyumbani kwangu tumekubali kuifuata dini hiyo, lakini siwezi kuwalazimisha raia zangu walio makasisi wa dini yangu ya zamani. Siku watakapoitakidi ukweli wa dini hii – kama tulivyoitakidi – wataifuata mara moja.” Baada ya kwisha kuandika alimpa yule mjumbe aipeleke, na akampa mjumbe huyu zawadi nzuri – zake yeye na za kumpelekea Mtume (s.a.w.) – .

 

Baadhi ya Masahaba waliokuweko huko walimfuata bwana huyu aliyeleta barua wakarejea Madina. Miongoni mwa waliomfuata siku hiyo ni Bibi Ramla bint Abi Sufyan – ndugu yake Bwana Muawiya bin Abi Sufyan – Bibi huyu aliposwa na Mtume (s.a.w.) na yeye yupo katika nchi ya Uhabushia kwa kufuatana na mumewe – Ubeydila bin Jahsh – kwa ajili ya kukimbia mateso ya Makureshi. Baada ya kukaa siku nyingi huko na kuingiana na makasisi wa Kimasihi bwana huyo alipenda kuacha dini hii ya Kiislamu na kuifuata hiyo dini ya Kimasihi. Basi akafanya alivyopenda bila ya kupingwa na yoyote katika jamaa zake, ama yule mkewe alikataa katakata kutoka katika dini yake ya Kiislamu bali alingangania kutukutu, ingawa mumewe alijitahidi kumchochea ili aiache hiyo dini ya Kiislamu. Mtume (s.a.w.) alipopata habari hii alifurahikiwa mno na bibi huyu ambae jamaa zake wote walikuwa katika dini ya Kikureshi ila yeye na mumewe, na sasa ijapokuwa mumewe amekwisha mwacha mkono katika dini hii – yeye ameikakamia vilivyo – Kwa ajili ya kumlipa kitendo chake hiki kizuri na kumwondoshea majonzi na upweke Mtume (s.a.w.) alimposa akamwoa, na hali ya kuwa yeye yupo katika nchi ya Mahabushia na Mtume (s.a.w.) yupo Madina. Bibi huyu hakupata wasaa kuja Madina ila alipokuja Bwana huyu na barua ya Mtume (s.a.w.).

 

Mtume (s.a.w.) alikuwa na furaha tatu siku aliporejea Bwana Amr bin Umayya. Alikuwa na furaha yake ya kuwashinda Mayahudi katika vita vya Khaybar; akapata furaha ya pili kwa kufikiwa na Masahaba zake waliokuwa Uhabushia, na akapata furaha ya tatu kwa kuwa Mfalme wa nchi hiyo amekubali kufuata dini ya Kiislam na kuacha dini yake ya asili.

 

Ulipatikana urafiki mkubwa baina ya Mtume (s.a.w.) na Mfalme huyu. Hata siku moja katika mwaka 9 A. H. (630) Mtume (s.a.w.) aliletewa habari na Jibril ya kuwa mchana huo Najash As-ham amekufa. Mtume (s.a.w.) alihuzunika sana, na akawaita watu wake waje msikitini wamsalie rafiki yao mkubwa tangu zamani – wamsalie Salatul Maytil Ghaib.

 

4. MAKAUKIS (PKAUCHIOS)

 

Liwali aliyewekwa na Warumi kuitawala nchi yote ya Misr. Lakini yeye mwenyewe hakuwa Mrumi, bali alikuwa mzalendo anayetokana na Maqipti – wakazi wa asili wa Misr –. Alikuwa mtu mkubwa sana na mwerevu kabisa ndipo akapata cheo hiki kikubwa mno. Hawa Maliwali wa kiwanamji walikuwa wakikaa karibu na mahali ambapo umejengwa huu mji wa Cairo baadae. Ama bwana mkubwa kabisa wa Kirumi yeye alikuwa akikaa katika mji wa Alexandria, na amri zilizokhusu uaskari zilikuwa chini ya mkono wake.

 

Aliyepewa utumwa wa kumpelekea barua hii ni Bwana Hatib bin Abi Baltaa. Baada ya kwisha kuisomesha barua hii na kuifahamu madhumuni yake Liwali huyu alimdadisi barabara huyu Bwana Hatib kwa kila habari za Mtume (s.a.w.). Miongoni mwa maneno aliyomwambia ni haya : “Ee Hatib! Kitu gani kilichomzuilia Mtume wenu – kama kweli yeye ni Mtume – kumwomba Mungu wake ampe nguvu za kuwashinda watu waliokuwa wakimtaabisha na kumtesa, hata ikampasa kutoka katika nchi ya wazee wake tangu asili yao? Kwa nini asimwombe Mungu wake akawapa maadui hao cha kuwapa? Hii ni alama ya kuwa yeye hana hadhi yoyote kwa Mungu.” Bwana Hatib alimjibu akamwambia: “Ee Bwana Liwali Hukiri kuwa Nabii Isa Mtume wa Mungu? Mbona yeye naye hakutaka kwa Mwenyezi Mungu awashushie balaa pale pale wale waliomhusuru na wakataka kumwua?” Liwali alicheka akasema: “Ahsante bingwa uliyeletwa na bingwa.” Bali alimwita karani na akamwamrisha aiweke ile barua katika mkakasi mzuri wa pembe kama alivyofanya yule Mfalme wa Mahabushia.

 

Baada ya kwisha kuiweka barua hii, Liwali alimwambia Bwana Hatib: “Mimi siwezi kufuata Mtume huyu, kwani raia zangu hawatakubali kunifuata, na mimi sitaki kukosa ukubwa wangu! Lakini chukua zawadi hizi umpelekee Mtume wenu na mwambie udhuru wangu huu. Nawe fanya upesi wende zako kabla haijatangaa habari yako kwa watu wangu, wasije wakenda kinyume na mimi” Zawadi zenyewe alizompa kumpelekea Mtume (s.a.w.)  ni hizi :

 

Baadhi ya vitambaa vya nguo.
Nyumbu mkubwa mwenye nguvu.
Punda mzuri mweupe sana.
Farasi “aliyeitwa akaitika”.
Baadhi ya chupa za asali ya mtaa wa Binha, mtaa maarufu mpaka leo kwa asali yake nzuri.
Shanuo la kani la kuchania nywele.
Kitana kizuri cha kupunia ndevu na kulazia nywele.
Mkasi mdogo wa kukatia kucha.
Marwedi ndefu ya kupakia wanja machoni.
Kioo kidogo cha kujitazamia.
-13.Wajakazi 3 ambao 1 akiitwa Maria, 2 akiitwa Sirin na 3 akiitwa Kisar na vinginevyo.
Huyu Maria Mtume (s.a.w.) alimweka usuria. Akamzalia mtoto mwanamume ambaye alimpa jina la Ibrahim. Ama huyu Sirin Mtume (s.a.w.) alimpa Shair wake mkubwa, Bwana Hassan bin Thabit. Mjakazi huyu alimzalia bwana wake mtoto ambaye alikuwa Shair kama baba yake. Yule mjakazi watatu Kisar, Mtume (s.a.w.) alimpelekea Sahaba mmoja aliyekuwa akiitwa Bwana Abu Jahm. Baada ya kumweka usuria naye alimzaa Bwana Zakariyya aliyekuwa Naib wa Liwali wa Misr.

 

5. HAWDHA BIN ALI AL HANAFY

 

Mfalme wa nchi ya Najd – nchi iliyoko Mashariki ya Hijaz –. Mfalme huyu alikuwa katika mji wa Al Yamama – mji mkubwa wa nchi ya Najd –. Sahaba aliyepewa barua yake kuipeleka ni Bwana Salit bin Amr. Baada ya kwisha kumpa zawadi kidogo mjumbe huyu, Mfalme huyu aliandika barua akamjibisha Mtume (s.a.w.) ya kuwa yeye hawezi kusilimu mpaka Mtume (s.a.w.) ampe ahadi kwanza ya kuwa atakuwa mshirika wake katika Ufalme atakao upata. Mtume (s.a.w.) asimjibishe lolote kwani Mtume (s.a.w.) alikuja kutangaza dini, si kutafuta Ufalme.

 

6. MUNDHIR BIN SAWA  AT TAMIMY

 

Liwali wa visiwa vya Bahreyn. Aliyepewa kumpelekea barua hiyo ni Bwana Al Alaa bin Al Hadhramy. Liwali huyu alisilimu pale pale, akaacha dini yake ya asili – dini ya Dola ya Kiajemi ya siku hizo – , na yeye alikuwa kama Liwali chini ya utawala wa Dola hiyo. Sehemu kubwa ya watu wake pia walimfuata katika dini hii. Wengine katika hawa walikuwa na dini ya Kiyahudi, wengine walikuwa na dini yao ya Kiarabu ya masanamu.

 

7. HARITH BIN ABI SHAMI AL GHASSANY

 

Liwali wa Sham, aliyekuwa chini ya amri ya Kirumi. Aliyepewa barua kumpelekea katika mji wa Damascus ni Bwana Shujaa bin Wahb. Baada ya kuisoma tu aliichana vipande vipande, akavirusha hewani. Kisha akamwambia Bwana Shujaa: “Kamhubiri rafiki yako kwa haya niliyoyafanya, na umwambie akae tayari kungojea jeshi nitakalomletea ambalo hakupata kuona mfano wake. Barua yake na ya yule mfalme wa Warumi zilipelekwa wakati mmoja. Na wakawa shauri moja kumpiga Mtume (s.a.w.).

 

8. HARITH BIN ABDI KULAL AL HIMYARY

 

Mfalme wa baadhi ya pande za Yaman, aliyempelekea barua hiyo ni Bwana Muhajir bin Umayya. Mfalme huyu alimjibu vizuri Mtume (s.a.w.), na akambainishia ya kuwa yeye amesilimu na anatumai kuwa wengi katika watu wake watasilimu kwa zama za karibu. Na akawapelekea Wafalme wengine wa Yaman, na wakati huo Hadhramaut ikihisabika ni sehemu ya Yaman.

 

9 – 10. JAYFAR BIN JULANDA NA ABDI BIN JULANDA AL AZDY

 

Ndugu wawili Wafalme waliokuwa wakitawala Oman zama za Mtume (s.a.w.). Wafalme hawa walikuwa wa kabila ya Bani Azd. Nchi ya Oman ilivyokuwa ipo mbali na nchi ya Hijaz. Wafalme wake walikawia sana kupelekewa barua hizi za Mtume (s.a.w.), mpaka katika mwisho wa mwaka wa 8 A.H. – 630 – ndipo Mtume (s.a.w.) alipowapelekea Barua katika mkono wa Bwana Amr bin Al As. Bwana huyu alimwendea Bwana Abdi kwanza kwani ndiye aliyekuwa akisifiwa kwa upole na ubaridi. Baada ya kuamini yeye ndipo alipofuatana naye kwenda kwa mkubwa wake Bwana Jayfar. Bwana mkubwa huyu alimdadisi vyema Bwana Amr. Alimuuliza tarehe[1] ya Mtume (s.a.w.) tangu kuzaliwa kwake mpaka siku hiyo na watu gani watukufu walioacha dini zao wakafuata dini hiyo mpya. Bwana Amr baada ya kumtajia watukufu hao na baada ya kuyakinisha bwana huyu ukweli wa maneno ya Bwana Amr, alisilimu pale pale na watu wake wote waliokuwa katika mji wa Suhar – mji mkubwa wa nchi ya Oman siku hizo –. Kisha watu wa miji mengine nao wakafuata.

 

Bwana Amr baada ya haya hakuondoka akaenda zake, bali alikaa kuwafundisha dini na kutazama namna gani mambo yake yalivyopitishwa. Katika muda huu wa kuwapo Bwana Amr huko Oman pamoja na wale Wafalme wawili, yule mkubwa alifanya bidii kubwa kuwataka kila waliokuwa chini ya mamlaka yake wafuate dini hii mpya, aliwapelekea barua za kuwafahamisha Uislamu na kuwataka wasilimu – na wasilimishe kila Maliwali wake waliokuwa katika nchi za kusini – kama nchi za Wamahara na wengineo na waliokuwa kaskazini. Maliwali wote hawa walileta jawabu nzuri za kubainisha kuwa wao wamesilimu na kila aliopo nchi yao kwa kishindo kikubwa[2].

 

Baada ya siku nyingi kidogo kupita Bwana Amr alipata habari ya kuwa Mtume (s.a.w.) amekufa. Akapatwa na majonzi makubwa, hata asiweze tena kukaa Oman, akaazimia kwenda zake Madina. Bwana Abdi – yule Mfalme mdogo – na baadhi ya mabwana wakubwa wa Kioman walifuatana na Bwana huyu mpaka Madina.[3] Huko walimkuta Sayyidna Abu Bakr ndiye Khalifa. Khalifa huyu aliwatukuza sana watu wa Oman na akawashukuru mno kwa wema wao waliomfanyia Bwana Amr tangu kufika kwake huko Oman[4], mpaka kurejea kwake. Baada ya kukaa huko kidogo na kujuana na mabwana wakubwa wa Kisahaba, mabwana hawa wa Kiomani walirejea kwao nao wamejaa mambo mengi mazuri ya dini ya kawafunza watu wao. Na wajukuu wa Mfalme huyu Bwana Abd – Bwana Suleyman bin Abdallah bin Abd, na ndugu yake , Bwana Saad – wao na wenzao waliokuja pande hizi kiasi cha mwaka 75 A.H (695). Ndiyo waliolimbusha Uislamu huku, hata mwisho ukatapakaa hivi.

 

[1] – Historia.

 

[2] – Maneno “kishindo kikubwa” hapa hayakukusudii kwamba walitumia nguvu, bali anakusudia kusema kuwa walisilimu kwa shangwe kubwa.

[3] – Miongoni mwa waliofatana naye ni Ja’afar bin Khutham Al-‘Itki, Abu Sufra Sarif bin Dhalim na kundi la Azdi. Al-Salimi Tuhfatu Al-A’ayaan j. 1, uk. 12.

[4] – Kumkirimu mgeni ni sifa ambayo ndugu zetu wa Omani wamepambika nayo zaidi kuliko watu wengi, na kwa ajili hiyo Waomani wakasifiwa sana na Sayyidna Abu Bakr kwa ukarimu wao. Kapokea Al-Imam Ahmad bin Hanbal na Al-Imamu Muslim kuwa Mtume (s.a.w) alimwambia Sahaba wake baada ya kumtuma kwenda kulingania kwa watu na wakamkadhibisha na wakampiga, basi alimwambia:”لَوْ أَهْلَ عُمَانَ أتَيْتَ، مَا ضَرَبُوْكَ وَمَا سَبُّوْكَ”  (Lau ungaliwaendea watu wa Omani, basi wasingalikupiga wala wasingalikutukana). Na haya yote ni kuonesha ukarimu wao na upole wao. Bali Waomani walipokwenda kwa Abu Bakr na kumpelekea Zaka baada ya kufa Mtume (s.a.w.), walimwambia: “Ewe Khalifa wa Mtume (s.a.w.), na Enyi Makuraish! Hii amana iliokuwa mikononi mwetu na katika dhimma yetu: amana ya Mtume (s.a.w.)”. Abu Bakr akawasifu sana, na siku ya pili akahutubia na kuendelea kuwasifu na kuwaombea dua na akawambia: “Enyi watu wa Oman! Mumesilimu kwa khiari yenu, Mtume (s.a.w.) hakuigusa ardhi yenu kwa kwato (za jeshi la ngamia) wala kwato (za jeshi la farasi). Wala hamukumpa tabu kama walivyompa tabu Warabu wengine…kisha akamtuma kwenu Amru bin Al-‘Aas bila jeshi nanyi mukamkubali..na kumtii..basi kuna fadhila gani ilio bora kuliko hii na kuna kitendo gani kilichokitukufu kuliko kitendo chenu?! Inakutosheni kauli ya Mtume (s.a.w.) kuwa utukufu kwenu hadi siku ya kiama”. Al-Salimi Tuhfatu Al-A’ayaan j. 1, uk. 12-13.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here