Home All MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA MWANAMKE.

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA MWANAMKE.

843
0

MTAZAMO WA UISLAMU JUU YA MWANAMKE:

Allah mtukufu ameumba ulimwengu mzima na akaumba ndani yake viumbe vyenye aina tofauti. Miongoni mwa viumbe hivyo alivyo viumba ni mwanaadamu, akamjaalia binaadamu huyo kua na moja kati ya jinsia mbili, ima mwanamume au mwanamke, tena akayafahamu vyema  maumbile ya kila jinsia, na kutokana kufahamu kwake maumbili hayo ndiyo akamjaalia mwanamume kua ni mwenye nguvu zaidi, anaeweza kuhimili mambo mazito, na kwaajili hiyo akamuwajibishia yeye kupigana jihadi katika njia ya Allah, na akamjaalia kua ni msimamizi wa mahitaji ya familia.

Lakini pia katika upande wa pili akamjaalia mwanamke kua ni dhaifu kuliko mwanamume, na akamkalifisha kwa yale mambo ambayo yanaendana na uwezo wake. Hivyo, akamjaalia mwanamke huyo kua ni mlinzi wa nyumba ya mumewe, mwenye kukidhi  haja za mumewe na kumsaidia katika kumtii Allah. Huku akamuwajibishia mwanamume kumuheshimu mwanamke, na kuithamini kazi nzito anayoifanya kwaajili yake; kwa kua yeye ni mshirika wake katika kuendesha pirika za maisha.

Miongoni mwa mambo ambayo Allah amemlazimisha mwanamke kuyafanya ni kujistiri kwa ujumla, ikiwemo kuvaa hijabu, wala kuvaa huko hijabu hakukua ni kwa lengo la kumyima uhuru na haki zake, bali ni kwaajili ya kumuhifadhia heshima na usafi wa nafsi yake, kama vile alivyokatazwa kufanya baadhi ya mambo ambayo yatamsababishia kero na maudhi kutoka kwa wanaume, ikiwemo kulainisha sauti yake wakati wa maongezi, na kudhihirisha mapambo yake; yote hayo ni kwaajili ya kumkirimu yeye na kumuepushia kila aina ya udhalilishaji. Anasema Allah mtukufu kuwaambi wake wa Mtume (ﷺ):

﴿یَـٰنِسَاۤءَ ٱلنَّبِیِّ لَسۡتُنَّ كَأَحَدمِّنَ ٱلنِّسَاۤءِ إِنِ ٱتَّقَیۡتُنَّۚ فَلَا تَخۡضَعۡنَ بِٱلۡقَوۡلِ فَیَطۡمَعَ ٱلَّذِی فِی قَلۡبِهِۦ مَرَضوَقُلۡنَ قَوۡلا مَّعۡرُوفا﴾ [سُورَةُ الأَحۡزَابِ: 32].

Enyi wake wa Nabii! Nyinyi si kama yeyote katika wanawake wengine. Kama mnamcha Mungu basi msiregeze sauti zenu, akaingia tamaa mwenye maradhi katika moyo wake. Na semeni maneno mema.﴿

Pia anasema:

﴿یَـٰۤأَیُّهَا ٱلنَّبِیُّ قُل لِّأَزۡوَ ٰجِكَوَبَنَاتِكَوَنِسَاۤءِ ٱلۡمُؤۡمِنِینَ یُدۡنِینَ عَلَیۡهِنَّ مِن جَلَـٰبِیبِهِنَّۚ ذَ ٰلِكَأَدۡنَىٰۤأَن یُعۡرَفۡنَ فَلَا یُؤۡذَیۡنَۗ وَكَانَ ٱللَّهُ غَفُورا رَّحِیما﴾ [سُورَةُ الأَحۡزَابِ: 59].

Ewe Nabii! Waambie wake zako, na binti zako, na wake za Waumini wajiteremshie nguo zao. Hivyo ni karibu zaidi kuweza kutambulikana wasiudhiwe. Na Mwenyezi Mungu ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu.﴿

Ikiwa maamrisho haya wameelekezwa hasa wake wa Mtume(ﷺ)pamoja na kua wao ni katika wanawake bora wanaosifika kwa uchamungu, basi bila ya shaka wasiokua wao wanatakiwa kuyatekeleza zaidi maamrisho hayo.

Ili tuweze kuthibitisha kua Uislamu haujamdhulumu mwanamke wala kumnyima haki zake, bali umemkirimu na kumnyanyua cheo, inatupasa tuvizingatie baadhi ya vipengele:

  • Mtume (ﷺ) amewafanya wanawake kua na cheo sawa na wanaume, akasema: «Kwa hakika si vyengine vyovyote vile bali wanawake ni kama wanaume».Pia akausia kuwatendea wema wanawake hao, na akaamrisha kuwashuhulikia na kuwatilia umuhimu pale aliposema katika hotuba yake ya mwisho siku ya hijja: «Usianeni kuwafanyia wema wanawake».
  • Uislamu umemkirimu mwanamke pindi anapokua mama; kwani Allah mtukufu ameusia kumfanyia wema mama katika sehemu zaidi ya moja ndani ya Qur-ani tukufu, akasema:

﴿وَوَصَّیۡنَا ٱلۡإِنسَـٰنَ بِوَ ٰلِدَیۡهِ حَمَلَتۡهُ أُمُّهُۥ وَهۡنًا عَلَىٰ وَهۡنوَفِصَـٰلُهُۥ فِی عَامَیۡنِ أَنِ ٱشۡكُرۡ لِی وَلِوَ ٰلِدَیۡكَ إِلَیَّ ٱلۡمَصِیرُ﴾ [سُورَةُ لُقۡمَانَ: 14].

 

Na tumemuusia mtu kwa wazazi wake wawili. Mama yake ameichukua mimba yake kwa udhaifu juu ya udhaifu, na kumwachisha ziwa baada ya miaka miwili. (Tumemuusia): Nishukuru Mimi na wazazi wako. Kwangu Mimi ndiyo marudio﴿.

Pia mtu mmoja alikuja kwa Mtume (ﷺ)kumuomba ruhusa ya kwenda jihadi pamoja na yeye, akamjibu Mtume (ﷺ)kwa kumwambia: «Mama yako yupo hai?». Akasema: “Ndio”. Akasema Mtume(ﷺ):«Ushikilie vizuri mguu wake; kwani huko ndiko iliko pepo». Pia alikuja mtu mwengine kumuuliza Mtume (ﷺ)kuhusiana na mtu anaestahiki zaidi kukaa nae kwa wema na hisani, akasema Mtume (ﷺ)kumwambia yeye: «Mama yako». Akauliza tena yule mtu: “Ikisha nani?”. Akasema: «Ikisha mama yako». Akauliza tena: “Halafu nani?”. Akasema: «Halafu mama yako». Akauliza tena yule mtu: “Ikisha nani?”. Akasema Mtume (ﷺ): «Ikisha baba yako».

  • Uislamu umemkirimu mwanamke hali akiwa ni mtoto, na ukamuhifadhia haki zake, na ukaharamisha kitendo kiovu cha kuwazika watoto wa kike wakiwa hai ambacho kilikua kikifanyika kabla ya Uislamu. Anasema Allah mtukufu:

﴿وَإِذَا ٱلۡمَوۡءُۥدَةُ سُىِٕلَتۡ ۝بِأَیِّ ذَنۢبقُتِلَتۡ﴾ [سُورَةُ التَّكۡوِيرِ: 8-9].

 

Na msichana aliye zikwa hai atapo ulizwa ۝ Kwa kosa gani aliuliwa?﴿.

  • Pia ulikisifu vibaya kitendo cha mtu kuchukiwa na kuuficha uso wake pale anaporuzukiwa mtoto wa kike, akasema Allah kusimulia hali hayo:

﴿وَإِذَا بُشِّرَ أَحَدُهُم بِٱلۡأُنثَىٰ ظَلَّ وَجۡهُهُۥ مُسۡوَدّا وَهُوَ كَظِیم۝یَتَوَ ٰرَىٰمِنَٱلۡقَوۡمِ مِن سُوۤءِ مَا بُشِّرَ بِهِۦۤۚ أَیُمۡسِكُهُۥ عَلَىٰ هُونٍ أَمۡ یَدُسُّهُۥ فِیٱلتُّرَابِۗ أَلَا سَاۤءَ مَا یَحۡكُمُونَ﴾ [سُورَةُ النَّحۡلِ: 58-59].

Na mmoja wao akibashiriwa kwa msichana, uso wake unasawijika, naye kajaa chuki ۝Anajificha asionekane na watu kwa ubaya wa aliyo bashiriwa! Je, akae naye juu ya fedheha hiyo au amfukie udongoni? Tazama uovu wa wanavyo hukumu!﴿.

  • Uislamu umemuondoshea mwanamke uwajibu wa kupigana jihadi kutokana na udhaifu wake.
  • Uislamu umeharamisha kumuacha mwanamke hali akiwa katika kipindi cha hedhi; kutokana na dhiki na shida anayoipata katika kipindi hicho.
  • Uislamu umeweka adhabu kali mmno kwa atakae mtuhumu mwanamke katika heshima yake bila ya kua na uthibitisho wowote, adhabu hiyo ni kupigwa mijeledi thamanini, pamoja na mtu huyo aliyezusha kupokonywa haki ya kutoa ushahidi katika kadhia yeyote ile milele.
  • Miongo mwa yanayoonyesha thamani ya mwanamke katika Uislamu ni kua hata anapofariki basi imewekwasheria ya kuoshwa na mumewe au na wanawake wenziwe, ili kuihifadhi heshima yake.
  • Uislamu umemuekea mwanamke haki ya kupokea mahari atakapo tokezea anaetaka kufunga nae ndoa, na ukaharamisha kuchukua hata chembe ndogo ya mahari hayo bila ya ridhaa yake.
  • Uislamu umemuekea mwanamke haki ya kurithi, badala ya kunyimwa haki hiyo kabla ya Uislamu, bali na kufanywa yeye ni kama vitu vyengine vinavyo milikiwa na kurithiwa na sio kurithi.

Hivi ni baadhi tu ya vipengele ambavyo vinaonyesha utukufu na thamani ya mwanamke katika dini ya Kiislamu, na kiuhalisia ni kwamba yapo mambo mengi sana zaidi ya hayo, ambayo yanabainisha wazi cheo cha mwanamke katika Uisalamu, na kwamba yeye hakudhulumiwa hata kidogo, bali kila sheria aliyolazimishwa nayo miongoni mwa mambo ambayo dhahiri yake yanaonyesha kubanwa na kuto pewa uhuru, sheria hizo zote ni kwaajili ya maslahi yake mwenyewe kama ilivyo tangulia hapo kabla.

Muandishi wa asili:

Sanaa Aduwakaat

Imetafsiriwa na kuongezewa na:

Yahya suleiman Ally Al Tiwany.

 

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here