Home HABARI ZA WAKATI UJUMBE WA IDDI AL-ADH-HAA 1438

UJUMBE WA IDDI AL-ADH-HAA 1438

307
0

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

5.UJUMBE WA IDDI AL-ADH-HAA 1438
Bismillahi wal-hamdu lillahi wa salaatu wa salaamu ala rasulillahi Muhammad wa alaa aalihi wa sahabihi wa sallama.

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Tukiwa katika siku tukufu ya Arafa nayo ni siku ya tisa ya mwezi wa mwisho wa mwaka ambao ni mwezi 12 kwa mujibu wa kalenda ya kiislamu, siku hii ambayo ni sunna kutekeleza ibada ya funga ndani yake kwa asiyekuwemo katika ibada ya Hijja, ibada ambayo Mtume wetu Muhammad S.A.W. ametueleza kuwa ni kafara ya mwaka unaomaliza na mwaka unaofuata, Allah atukubalie funga yake na atukubalie ibada zetu zote na atusamehe tuliyoteleza. Kwa kumaliza siku hii inafuata siku ya Iddi kubwa nayo ni Iddi Al-Adh-haa.

Inatupasa tujue kuwa furaha ya Iddi sio mlango wa kuvamia aliyo haramisha Allah mtukufu na Mtume wake, wala sio siku ya kuvutia katika maasi ya Allah mtukufu, bali siku hii ni siku ya kufurahia katika aliyohalalisha Allah mtukufu pia ni siku ya kuunganisha udugu na kuwaliwaza wagonjwa na manyonge na masikini, ni siku za kula na kunywa na kutoa sadaka.

Mtume wetu Muhammad S.A.W. ametuagiza katika Ibada tukufu ya siku ya Iddi nayo ni Ibada ya kuchinja kwa kusema: “Kuleni na wekeni na mutoe sadaka” kwa hakika hiyo ni ishara kubwa kwa waislamu katika yale yaliyokua muhimu zaidi katika siku hizi ya Iddi, basi ewe Muislamu usikubali kumfurahisha Ibilisi maluuni kwa kuitika vichochezi vyake vya maasi ya Allah mtukufu.

Tukumbuke kuwa Iddi hii ime katika mwezi wa mwisho wa mwaka kwa mujibu wa kalenda yetu ya Kiislamu, basi inatupasa tuienzi kalenda hii kwa kuijua na kuwafundisha watoto wetu miezi yake, kwani kalenda hii ndiyo aliyoiridhia Mola wetu mtukufu katika Dunia yetu na Dini yetu, ni aibu kubwa leo kumkuta mtoto wa Kiislamu anajua miezi yote 12 ya kalenda ya Kizungu lakini ukimwambia akutajie miezi ya kalenda la Kiislamu inakua ni mtihani mkubwa kwake, turejee katika kalenda ya Dini yetu tuwafundishe watoto wake, tufanye jitihada kuiweka katika maisha yetu ya kila siku.

Kumalizika kwa mwaka kutukumbushe kumalizika umri wetu na umri wa Dunia, kwani kama ilivokua tunakaribia katika kifo pia tunakaribia katika Kiama siku ya Malipo. Basi ni wakati wa kujihesabu na kuzirejea nafsi zetu kwa ajili ya kuhakikisha yaliyo bora zaidi ambayo Mola wetu Allah mtukufu anayaridhia kwetu kwa siku zetu zote.

Tunachukua fursa hii kuwapongeza Waislamu wote duniani kwa kuadhimisha siku ya Iddi tukufu ya Al-Adh-haa, na kuwatakia mwisho wa mwaka huu ulio mwema na mwanzo wa mwaka unaofuata wenye kila mafanikio.

Tunawapongeza Mahujaji kwa kufanikiwa kutekeleza Ibada ya Hijja ambayo ni nguzo ya tano ya Uislamu na tunamuomba Allah awakubalie amali zao.

Tunawaombea dua ya mafanikio wale wote walioma katika mitihani ya kujaribiwa kwa dhulma ikiwa kwa kuwemo vizuizini bila ya haki au vita vilivoripuka katika miji yao na kuteketeza mali na roho na nchi, au mateso ya kudhulumiwa bila ya haki. Allah awalipe hao wote malipo ya yao bila ya hesabu, na awaondoshee madhila na awafariji kwa amani upendo na huruma.

Amina.

Asanteni sana.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here