Home HABARI ZA WAKATI HONGERA YA IDDI – 1438 HIJIRIA

HONGERA YA IDDI – 1438 HIJIRIA

147
0

Published By Said Al Habsy

4. HONGERA YA IDDI – 1438 HIJIRIA
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu aliyetuneemesha kwa nuru ya Imani na Uislamu na kutujaalia kutimiza funga ya mwezi mtukufu wa Ramadhani, na rehma na amani ziwe kwa kipenzi chetu aliyeteuliwa kuwa khitimisho la Manabii Mtume wetu Muhammad pamoja na Aali zake na Masahaba wake na kila aliyeongoka kwa uongofu wake mpaka siku ya malipo.

Assalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.
Tunachukua fursa hii adhimu ya kufanikisha utekelezaji wa Ibada ya funga ya Ramadhani ya mwaka huu 1438 Hijiria kwa kuwapongeza Waislamu wote Duniani kwa mnasaba wa Iddi Al-Fitri iliyobarikiwa, na kumuomba Allah mtukufu atukubalie funga yetu na ya kila muislamu na atujaalie taufiki yake katika anayoyaridhia hadi mwisho wa uhai.

Ndugu Waislamu:
Tunajua kuwa Ibada ya funga ya Ramadhani ni moja kati ya nguzo tano za Uislamu nayo ni nguzo ya nne aliyoijaalia Allah mtukufu kuwa ni kituo cha kuitekeleza kila mwaka mara moja, tusisahau kuwa lengo kuu ya ibada hii ni kuhakikisha uchamungu katika maisha ya Muislamu aliye Muumini wa kweli, na uchamungu huu ndio daraja inayohakikisha mafanikio ya kupata maridhio ya Allah mtukufu hapa Duniani na kesho Akhera, basi tusikubali kuharibu sifa hii baada ya kumaliza mfunguo wa Ramadhani, na tujue kuwa uchamungu unapatikana kwa kujiepusha na kila asiloliridhia Allah mtukufu kwa lengo la kupata maridhio yake Allah mtukufu, na kujiepusha huko hakupatikani isipokuwa kwa kutenda malazimisho ya Allah mtukufu na kuepuka makatazo yake Allah mtukufu, basi tusibatilishe malipo ya funga yetu katika siku za Iddi na zinazofuata kwa kujitosa katika maasi, kwani tukifanya hivo tutamfurahisha sana adui yetu Ibilisi mlaaniwa.
Tujue kuwa siku ya Iddi ni siku ya furaha na kula na kunywa vya halali na katika maridhio ya Allah mtukufu, wala si siku ya kujitosa katika makasiriko yake na michezo ya upuuzi na ubadhirifu wa mali na malaji na wakati, Allah atujiepushe nayo, basi imesemwa kuwa alama ya kukubaliwa funga ya mja ni kujishika kwake na uchamungu baada ya kumaliza Ibada hii tukufu.

Ndugu Waislamu:
Kwa hakika Mtume wetu Muhammad S.A.W. amesema:

((مَنْ صَامَ رَمَضَانَ ثُمَّ أَتْبَعَهُ بِسِتَّةِ أَيَّامٍ مِنْ شَوَّالٍ فَكَأَنَّمَا صَامَ الدَّهْرَ كُلَّهُ))

“Yule atakayefunga Ramadhani kisha akaifuatiliza kwa funga ya siku sita katika Shawwali (Mfunguo mosi) basi huyo ni kama aliyefunga mwaka nzima.”

[Rabii 312]

Basi tujihimu katika kufunga siku sita za mwezi huu wa Shawwali, nao ni mwezi unaofuata baada ya Ramadhani, na tukumbuke kuwa hakuna ulazima wa kuzifuatisha wala kuzifunga mara tu baada ya Iddi, bali mwenye kutaka thawabu yake anatakiwa atimize funga ya siku sita za mwezi huu kabla ya kumalizika kwake, ni sawa ikiwa atazifunga kwa mfululizo au kwa kuachanisha muhimu azimalize kabla ya mwezi kumaliza, pia tujue kuwa siku ya Iddi imeharamishwa kuifunga kwa hiyo haimo katika siku hizo sita.

Ndugu Waislamu:
Tunafahamu sote machafuko yaliyotokezea katika miji mingi ya Waislamu kama vile Syria, Yemen, Somalia, Afgahanistani, Libya, Burma, Palestina n.k, pia tunadiriki vizuri tokeo la kukatika kwa mahusiano ya kimataifa baina ya Qatar na Nchi jirani za Kiarabu (Saudia, U.A.E., Baharain, Misri) hatuna budi kumuomba Allah mtukufu kuzirejesha nyoyo za Waislamu katika fungamano la Uislamu na Imani, pia aondoshe yenye kupelekea machafuko na uhasama katika jamii, basi Allah alete amani baina ya Waislamu na mapenzi na kuhurumiana na kuheshimiana katika waliyotafautiana, na kusaidiana katika wema na uchamungu, kwa hakika tafauti ni maumbile ya Binadamu, basi kuelewana na kuheshimiana ndio dawa yake, na sio uhasama na kugombana.
Allah aondoshe madhila ya vita na maradhi na hasadi na chuki baina ya Waislamu wote. Amin.

RISALA YETU YA IDDI:
Risala yetu kwa Umma wa Kiislamu ni ile aliyoisema Mstahiwa Sheikh Ahmed bin Hamed Al-Khalili Allah amuhifadhi:

“Hakika mimi -kwa jina la Uislamu ambao unakusanya wala hautawanyi, unaunganisha wala haukimbizi, unapoza wala haushongalishi- ninaliita kila kundi ambalo limo katika wimbi la kupigana vita na kuvutana lisimame kwa kujihesabu nafsi yake mwenyewe katika yale ambayo linayafanya, na lichunguze na kuzingatia ndani yake na lijiulize, kuna maslaha ya nani? Na kwa aajili ya nani linajiingiza katika mvitano na kujiangamiza na kudhoofisha Umma?!! Roho ngapi zimetolewa? Nguvu kiasi gani zinapotea? na Mali nyingi kiasi gani zinateketea?.

Kwa hakika linalolazimika kwa wote ni kujiondosha katika marithisho ya thakafa zao za mifarakano, basi waondoshe katika marejeo yao kila lenye uchochezi wa kasumba za kijahilia au kujigamba kibaguzi, na wote wawe ni ndugu kwa ajili ya Allah mtukufu, na wenye kusaidiana katika yenye kheri, na warekebishe kila pengo linalotenganisha baina yao kwa kuwatenga na nuru ya Uislamu inayokusanya, basi wawe tayari kuzima kila fitna inayokokea ukiritimba ili kuzizima kwa maji ya mamiminiko ya mapenzi kwa ajili ya Allah mtukufu ambaye nyoyo za waja wake inalazimika kuimarishwa kwa mapenzi yake.
Ama ikiwa mivutano ni kwa sababu za tafauti za kimadhehebu; kwa hakika sababu hiyo ima itakuwa chimbuko lake ni fahamu pofu ya kupatikana madhehebu tafauti katika safu za Waislamu, au itakuwa imesababishwa na kasumba za kimadhehebu, basi inawalazimu wajue kuwa hizi Madhehebu -iwapo wafuasi wake watakuwa na Ikhlasi kwa ajili ya Allah mtukufu- zinakua ni sababu ya kuimarika na si kidamirika, na kufahamiana sio kufarikiana, kwa sababu kutafautiana katika matawi ni neema na rehma na hazina ya umma isiyokadiriwa kwa thamani, kwani mara ngapi Muislamu anapata katika jitihada za ndugu zake Waislamu katika Madhehebu tafauti yale yenye kutuliza moyo wake na kutatua utata wake na kumfungulia tatizo lake, na hakuna jitihada yoyote iliyopo katika asili ya kisheria isipokua jitihada hiyo inayo kiwango fulani cha haki na kufikisha katika kuijua haki.”

Ndugu Waislamu:

Mpaka hapa tunawatakia Waislamu wote kheri za Iddi na fadhila za funga na taufiqi ya Allah katika kila lenye maridhio yake Allah mtukufu.
Wakullu Aaamin Wantum Bikhairin

Ndugu yenu: Abu Hamed Hafidh Al-Sawafi.

Kwa niaba ya www.ibadhi.com.

HAKI KWA DALILI.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here