Home All NURU IN’GARAYO

NURU IN’GARAYO

509
0
Accordion Content

Published By Said Al Habsy

NURU ING’AAYO KATIKA NJIA YA UADILIFU
FIKRA YA KIIBADHI KUHUSU ITIKADI

Baada ya babu kumaliza kusoma aya za Qur an tukufu alimtazama mjukuu wake akiwa mbali kwa fikra zake, amezama katika kuwaza, akamuwahi kwa swali :

BABU: Umefika wapi mjukuu wangu ?
MJUKUU: alizinduka na kujibu hali akitabasamu: Bado nipo karibu yako ewe babu yangu, ninasubiri umalize kusoma nikuulize jambo limeshughulisha fikra yangu tangu niachane na rafiki yangu
BABU: Itakuwa mlikuwa katika safari ya majadiliano kuhusu historia kama kawaida yenu, leta ulionayo ewe mwanangu
MJUKUU: Nimemtajia rafiki yangu kuwa kufarikiana kwa umma huu katika zama za ukhalifa wa Imaam Ally – Karramallahu wajhahu- na baada yake zinahesabiwa kuwa ni khilafu za kisiasa, Madhehebu zimetokana na khilafu hizo baadaye na zikatengenezeka itikadi zake na rai zake, wakati yeye anaona kuwa khilafu za kisiasa hazina mahusiano na madhehebu za kidini.
BABU: Alikaa vizuri na akasema: ‘’Jua ewe mwanangu kuwa kuna ufahamu uliokosewa wameueneza baadhi ya mustashriqiin ((Wakristo waliosomea masomo ya kiislamu)) na waandishi wa kiislamu wakawafuata, wamezusha kuwa ummah umegawanyika makundi makundi na kimadhehebu, nao ni ufahamu uliokosewa, kwa kuwa siasa katika uislamu inatengeneza sehemu ya hukmu za kisheria, na hakuna madhehebu ya kiislamu isiyokuwa na rai zake katika itikadi, siasa na fiqh, Amma mwanzo wa khilafu ni pale walipotoka Talha, Zubeir, na Muawiya dhidi ya Ally. Na ni kutokana na hawa ndio yametengenezeka madhehebu za kundi kubwa la waislam. Na kutokana na wafuasi wa Ally ndio yametengenezeka madhehebu za kishia. Na madhehebu yote mawili yana misingi yake katika siasa, itikadi na fiqh”
MJUKUU: Kwa hivyo Ibadhi wako wapi baina ya makundi haya mawili, Ewe babu yangu?
BABU:…

Njoo nasi katika makala ya pili kwa jawabu la babu

Khamis bin Yahya Alghammawi

khamis.alghamawi@ibadhi.com
_________________________________________________________________________________________________
Muamma, Ally Yahya: Al ibaadhiyya bainal firaqil Islaamiyyah inda kuttabil Maqaalat fil qadiim wal hadith jz2, wizarat turaathi qawmiyy wathaqaafah, Sultanat Oman, 1406h/1986m uk 185

Published By Said Al Habsy

NURU ING’AAYO KATIKA NJIA YA UONGOFU

IBADHI BAINA YA KUNDI LA ALLY BIN ABII TALIB NA MUAWIYA BIN ABI SUFIANI

MJUKUU: Kwa hivyo Ibadhi wako wapi baina ya makundi haya mawili, Ewe babu yangu?

BABU: Jua – Allah mtukufu akuhifadhi- kuwa “Pale mambo yalipovurugika katika ukhalifa wa kiislamu, na ikawa hukmu inaelekea katika ufalme wa kurithishana, wa kutumia nguvu, uliokamtwa na Banii Umayya, Misimamo ya watu iligawanyika katika makundi mengi… wapo waliojifungamanisha na dola na kujisalimisha, wakijitahidi kujikurubisha na dola ili iwe ni njia ya kufikia ubwana mkubwa.

Na wapo waliojaribu kuifunga haki ya Ubwana kwa watu wa nyumba ya Mtume – Sallallaahu alayhi wasallam- kwa njia ya kurithishana au kuzusha kuwa kuna wasiyya unaofuatana kwao wao pasina wengine, na wapo waliokataa hili na lile na wakatoka katika dola hiyo kwa nguvu, na wakaweka njia ya kufikia hukmu ni kumchagua kiongozi kwa uhuru, kisha hawakumpa udhuru Yule aliyekhalifu rai hiyo.
Na wakati wa mgongano huu mkubwa baina ya makundi haya matatu wakati wa mwanzo wa dola ya Banii Umayya, lilitokea kundi lingine lilopita njia ya kati na kati baina ya makundi haya yenye kupinzana, halikuchukua njia ya kujisalimisha kwa ile hali iliyopo vyovyote itakavyokuwa, lakini pia haikuchukua ya kuwa wao ndio mfano kamili kiasi iwe lazima kwa watu wote kuwafuata wao, kwa njia hii wakawa wamekhalifu njia ya kundi la mwanzo kwa kujuzisha kwao kutoka dhidi ya utawala ikiwa kutoka huko kutaleta maslaha kwa ummah, wala haitoleta madhara zaidi na makubwa zaidi ya maslaha. Pia kundi hili limekhalifu njia yakundi la pili hivyo halikukubali utaratibu wa kurithishana utawala. Na pia kundi hili limekhalifu njia ya kundi la tatu kwa kuwa halikuwajibisha kutoka dhidi ya viongozi waovu katika hali zote, wala hawakulazimisha msingi wao kwa watu wote,na wakampa udhuru aliyewakhalifu wao, na hawa ndio IBADHI”1″

MJUKUU: Kweli, ufafanuzi wako ni wa kutosheleza na uko wazi ewe babu yangu…– Allah mtukufu akupe umri mrefu katika kumtii yeye – umetaja kuwa Ibadhi hawawajibishi kutoka dhidi ya viongozi waovu, Je hili linamaanisha kuwa wao wanawatii na kuzinyenyekea amri zao ?
BABU: Kuwa na hakika na amini kwa yaqini ewe mwanangu kuwa Ibadhi wanaona kuwa katika wajibu wa waislamu ni kusimamisha dola ya uadilifu, inayokwenda juu ya msingi wa sharia ya kiislamu, inatekeleza hukmu za Allah mtukufu, inasimamaisha huduud, inahifadhi haki, inarejesha dhulma, inahifadhi mipaka, na inapeleka daawa ya kiislamu katika miji ya kikafiri.
Amma ikiwa dola itakayosimama ni ovu, inajuzu kubaki chini ya hukmu yao, na inawajibika kuwatii katika yote yasiyokhalifu hukmu za uislamu, kama ambavyo inapaswa kwa waislamu wasilale tu, inatakiwa wajaribu kubadilisha hukmu zilizopo ikwa hilo halitoleta madhara makubwa kwa ummah na kusimamisha uadilifu, hii ni kwa kutazama vitendo, Amma kwa kutazama ukosoaji ((kuamrisha mema na kukataza mabaya)) basi haijuzu kwa muislamu mwenya pupa na uislamu wake kuacha au kukaa kimya kunako maovu.”2″

MJUKUU: Allah mtukufu anizidishie sehemu ya elimu yako ewe babu yangu na aninufaishe kwayo.. na ulikuwaje mwenendo wa Maibadhi katika kutekeleza sharia ya Allah mtukufu na kusimamia uadilifu katika ardhi wakati wa dola ya Amawiyya ? Njoo nasi katika makala ifuatayo…!

Khamis bin Yahya Alghammawi

khamis.alghamawi@ibadhi.com

__________________________________________________________________________________
1 – Muammar, Marejeo yaliyopita uk 185 – 187 (kwa mabadiliko kidogo)
2 – Marejeo yaliyopita uk 54-55 ((kwa mabadiliko kidogo))

Published By Said Al Habsy

NURU YENYE KUNG’AA KATKA NJIA YA UADILIFU


MWENDO WA MAIBADHI KATIKA KUSIMAMISHA UADILIFU


MJUKUU: Allah mtukufu anizidishie sehemu ya elimu yako ewe babu yangu na aninufaishe kwayo.. na ulikuwaje mwenendo wa Maibadhi katika kutekeleza sharia ya Allah mtukufu na kusimamaisa uadilifu katika ardhi wakati wa dola ya Amawiyya ?
BABU: Waislamu –wakiwemo Maibadhi-walijaribu kurejesha upindaji huu na kurudisha hukmu katika njia yake ya sawa, amma kwa kuwaambia wafalme na watawala warudi katika kushikamana na hukmu za kiislamu au kwa kuibadilisha dola yenyewe kwa kubadilisha nidhamu ya hukmu”
Na hivi ndivyo ilivyokuwa, Maibadhi walijitahidi na wakapambana kwa ajili ya kutekeleza Uimam adilifu, ambao wanaamini ni lazima kwa mujibu wa itikadi yao, kwa dalili za Qur-an na Sunnah na makubaliano ya Ummah.
MJUKUU: Ndio, ewe babu yangu, nimesoma kuwa Maibadhi wameweka Masharti zinazohusiana na uimamu, kama ambavyo wanalo neno la “Masaalikuddin”, Basi nakuomba unifafanulie yote hayo na unifafanulie ewe babu yangu
BABU: Ndio ewe Mwanangu,ili uwe katika ubainifu, na ili kuondosha uzito wowote uliopo nitakufafanulia kuhusu uimamu, na nitakuelezea njia wanazozichukua kufikia kusimamisha uimamu adilifu.
MJUKUU: Allah mtukufu akuzidishie elimu babu yangu, nami nina kiu sana ya kujua upambanuzi wa mambo haya
BABU: Jua ewe mwanangu… kuwa “Uimamu, Ukhalifa, Uamiri, na Uraisi, ni maneno tofauti yenye maana yenye kuwafiqiana kwa maana ya pamoja. Huo ni uraisi wa pamoja wa mambo ya dini na dunia kwa mtu aitwaye IMAMU, nao ni ukhalifa wa Mtume sallallahu alayh wasallam- katika kusimamisha dini, kuhifadhi mipaka ya dini kwa wenye kuhusika nayo, na kwa hivyo wanaamrishwa raia wote kumfuata na kumtii maadam hajaamrisha kumuasi muumba. Hivyo kazi ya msingi ya uimam ni kusimamisha dini na kutekeleza hukmu za dini na kuhifadhi umoja wa kiislamu na kuutetea ummah. Nazo ndizo kazi za Mtume –sallallaahu alayh wasallam- baada ya kupewa utume mpaka alipofariki, basi kila aliyekamata kazi hizi anazingatiwa kuwa ni khalifa wa Mtume –sallallahu alayh wasallam- katika kuchunga mambo ya ummah huu”
Jua ewe Mwanangu – Namuomba Allah mtukufu aangazie uoni wako kwa haki- kuwa “mpangilio wa kiibadhi umesimama kimsingi katika kuitazama jamii, maana yake ni kuipa uzito wa uhakika rai ya jamii katika kila jambo miongoni mwa mambo ya jamii. Na hili limechaguliwa na Maibadhi kutokana na kufahamu kwao vizuri sharia ya kiislamu ihimizayo Shura, kwa ajili hii Masheikh au wanachuoni wa kiibadhi ndio wenye kumiliki utawala wa mambo, nao ndio wenye haki ya kumkosoa Imam, kumchunga na kuhakikisha kufuata kwake sharia, nao ndio wenye haki ya kumuuzulu akijaribu kuchupa mipaka, kama ambavyo inawajibika juu ya Imam kuwaomba ushauri wanachuoni katika anayoyasimamia.
Na hivi ndivyo inavyokubainikia ewe mwenye kutafuta uongofu kuwa msingi wa shura na kushirikiana ni msingi wa fikra ya kisiasa ya kiibadhi, bali ni upambanuzi wa roho ya Madrasa ya kiibadhi, na katiba ya kiibadhi inasema kuwa Shura kwa Imam ni Lazima, akiipinga anakuwa kafiri – wa neema sio wa kutoka katika uislamu – sawa akiwa ni mwananchuoni au dhaifu” Itaendelea makala ijayo….


Khamis bin Yahya Alghammawi khamis.alghamawi@ibadhi.com

__________________________________________________

– Marejeo yaliyopita uk 56
-Alwuheibi, Musallam bin Salim: Alfikrul aqadiy indal ibadhiyyat hattaa nihaayatil qarni thaani l hijri, chapa ya kwanza, Maktab Dhaamiri, Seeb, 1427h/2006m uk 405 (( kwa uchambuzi))
– Marejeo yaliyopita, uk 405 ((kwa uchambuzi))

Published By Said Al Habsy

NURU ING’AAYO KATIKA NJIA YA UADILIFU

KUMCHAGUA NA KUMUUZULU IMAM KWA IBADHI

MJUKUU: Allah mtukufu akukirimu ewe babu yangu na anyanyue cheo chako.. umenibainishia yaliyokuwa magumu kwangu, kwa hakika yote haya sikuwa nayajua. Nimejua kutoka kwako kuwa msingi wa Shura ni katika misingi ya hukmu ya kiibadhi, naomba unisifie ewe babu yangu njia ya kumchagua na kumuuzulu Imamu.
BABU: Umegusia jambo muhimu ewe mwanangu…!, “Hakika njia ya kumchagua Imamu Muadilifu inatimia kwa wanachuoni kumchagua na waislamu kumpa ahadi ya utiifu, Amma mtu anayechaguliwa kuwa Kiongozi inawajibika awe ametimiza baadhi ya masharti; zilizokuwa muhimu: Awe ni katika wenye elimu na uchamungu katika dini, kwa kuwa kitakiwacho Imam awe ni kiongozi wa ummah katika kila Nyanja ya maisha yake, na hakuna lililo muhimu katika jamii ya kiislam kama dini, na katika jambo la msingi kulikumbushia hapa ni kuwa Ibadhi haiweki sharti la Uquraishi katika uimam, kwani Uislamu haukuweka mizani ispokuwa ya uchamungu ((Hakika mtukufu zaidi baina yenu kwa Allah mtukufu Yule mchaji zaidi, Hakika Allah mtukufu ni Mjuzi mwenye khabari)).
Jua -ewe mwanangu- kuwa Imam Muadilifu si haki kumuuzulu ispokuwa katika mambo manane, muhimu katika hayo: KUFANYA DHAMBI KUBWA INAYOWAJIBISHA KUSIMAMISHIWA HADDI, hapo atavuliwa na kuwekwa Imamu mwingine amsimmishie Haddi ya kisheria, au ikiwa atafanya dhambi isiyowajibisha haddi kisheria hapo atatakiwa atubie, akitubia ataendelea kama hakutubia atakuwa amejivua utawala”
MJUKUU: Allah mtukufu aninufaishe kwa elimu yako ewe babu yangu… basi vipi kuhusu njia za kuisimamisha dini ambazo wanazifuata Maibadhi kufikia Ukhalifa ?
BABU: Nakuona ni mfuatiliaji na mwenye hamasa, umetanabahi na kufahamu, umejua na kuhifadhi, Allah mtukufu akubariki na adumishe jitihada yako.
“Njia za kusimamisha dini ((Masaalikuddin)) kwa maibadhi ndizo njia za kufikia kwazo kutekeleza hukmu za kisheria; Kwa kutazama uwajibu wa kumchagua kiongozi muadilifu kwa Maibadhi, na kwa vile Maibadhi wanatofautiana na wengine katika fikra hii na madhehebu zingine, na kwa vile daawa ya kiibadhi inapitia katika udhaifu na nguvu, basi wamekubaliana wanachuoni wa kiibadhi kuwa kuna namna nne za uimamu, kila aina moja inafaa kwa wakati maalumu, na aina hiyo inakuwa na masharti na wajibu maalumu yenye kuendana na marhala ambayo daawa ya kiibadhi inapitia, basi sikiliza ewe mwanangu ubainifu wa kila marhala…
AINA YA KWANZA: UIMAM WA SIRI ((KITMAAN))
Aina hii huwa pale maibadhi wanapokuwa hawana nguvu ya kutangaza uimamu, katika hali hii hulingania katika madhehebu yao kwa siri, na wanamchagua mmoja wao awe kiongozi wao na kikawaida huwa mwanachuoni na mchamungu, ili awe ndio msimamizi wa daawa, mpangaji na kusimamia mambo ya wafuasi wake, kama ambavyo atachagua walinganiaji watakaotumwa miji tofauti kueneza madhehebu huko, na ataitwa ((IMAM WA KITMAN)), Maimam Mashuhuri wa marhala hii katika historia ya kiibadhi ni Imam Jabir bin Zaid Al uzdi Muomani na Imam Abu Ubaidah Muslim bin Abi Karimah Altamimi – Allah mtukufu awaridhie- na kwa hakika maimam hawa wawili wana kazi kubwa walioifanya kuendeleza ulinganio wa kiibadhi na kuutangaza, kupitia karne mbili za mwanzo na karne ya pili za hijra.


MUONEKANO WA UENDELEZAJI UIMAM WA KITMAN KWA MAIBADHI.


Katika muonekano wa muendelezo uimam wa kitman ni kujuzu kutumia TAQIYYA ya kidini, ili waweze kuhifadhi itikadi yao, na kujiweka mbali mno na maadui na ujeuri wao, na Taqiyya ewe mwanangu kama anavyosema Imam wetu Alsalimi katika kitabu chake Bahjatul An-waar, na inaweza kuwa kwa Qauli au kwa vitendo: “Taqiyya ya vitendo haijuzu kwa Masahibu zetu ((Maibadhi)), nayo ni kama kuua nafsi au kuigharikisha, Amma Taqiyya ya Qauli inajuzu katika sehemu na inakataliwa sehemu nyingine, amma sehemu inapojuzu ni pale inapokuwa qauli hiyo haina madhara kwa yoyote katika viumbe na ikawa msemaji amelazimishwa kuisema qauli hiyo, hapo itamjuzia kuitetea nafsi yake kwa hiyo qauli hata kama ni neno la ushirikina kutokana na yale anayoyaogopea kama kuuwawa n.k., Kujuzu kwa hilo kumechukuliwa katika Quran na Sunnah, Amma Qur-an ni kwa Qauli yake Allah mtukufu {{ISPOKUWA ATAKAYELAZIMISHWA HALI MOYO WAKE UMETULIA KATIKA IMAN}} Alnahl:106 na kauli yake {{ Ispokuwa ikiwa kwa ajili ya kujilinda na shari zao.}} Al – Imran :21 na Amma sunnah, amesema Mtume sallallahu alayh wasallam- “Wamesamehewa ummah wangu kukosea kwa bahati mbaya, kusahahu, yanayoelezwa na nafsi zao, na yale waliyolazimishwa” na katika hayo ni yale yaliyomtokea Ammar bin Yasir pale washirikina walipomchukua… amma sehemu ambayo inakatazwa Taqiyya ya qauli ni pale itakapokuwa kauli hiyo italeta madhara kwa mwingine, kama kuiua nafsi nyingine, au kukatika kiungo chake, hapo haitajuzu kufanya hiyo taqiya kwa kuwa si halali kwa mtu kuiokoa nafsi yake kwa kumdhuru mwingine”
KUJUZU kubaki chini ya utawala wa madhalimu, na kujuzu kukaa pamoja na wenye kuwakhalifu.
Maibadhi katika wakati huu hawasimamishi baadhi ya hukmu na huduud; kwa kuwa Imam hana uwezo wa kutekeleza hayo, mfano ni kumpiga mawe mzinifu mwenye mke au mme”

Itaendelea wiki ijayo


Khamis bin Yahya bin Khamis Alghammawi
khamis.alghamawi@ibadhi.com

 

———————————————————————————————————————————————————————–

[2] – Alsaalimi, Abdullah bin Humeid: Bahjatul an-waar sharh an waarul uquul fii Tawhiid, chapa ya nne, Maktabat Imaam Nuruddiin Alssaalimi, Seeb, 2003m uk 165 – 166 kwa uchambuzi.

[3] – Alwuheibi, Musallam bin Salim: Alfikrul aqadiy indal ibadhiyyat hattaa nihaayatil qarni thaani l hijri, chapa ya kwanza, Maktab Dhaamiri, Seeb, 1427h/2006m uk 408 – 409 (( kwa uchambuzi))

Published By Said Al Habsy

UIMAM WA SHARAA (KUMUUZIA NAFSI ALLAH MTUKUFU)


MJUKUU: Ewe babu yangu hakika hii ni dalili ya usawa wa fikra ya kisiasa kwa Maibadhi; kwa kuwa wanazingatia hali inayowazunguka na hujiweka kwa namna itakavyowawezesha kueneza daawa yao na kuipa nguvu katika nafsi, ili waweze baada ya hayo kufikia marhala nyingine ya Dhuhuur.
BABU: Ahsante ewe mwanangu, mambo ni kama ulivyotaja, lakini ipo namna nyingine ya Uimam kabla ya kufikia marhala ya Dhuhuur nayo ni marhala ya “Uimam wa Sharaa”; uimam ambao kikawaida husimamishwa wakati wa kitmaan, pale ambapo baadhi ya wapiganaji, wanaume, waliobaleghe, wasiopungua arobaini huchagua kumuuzia Allah mtukufu  nafsi zao, basi wao hutoka dhidi ya hukmu za madhalimu, lakini wao huwa hawamlazimishi yoyote kujiunga nao, wajibu wao ni kutowatisha watu katika waislamu, wala wasiwapige vita mpaka wao wawapige vita. Hili ni jambo la kujitolea hakuna kulazimishwa na yoyote. Na wakichagua njia hii baadhi ya Maibadhi basi watachagua baina yao Imam, ataitwa “IMAAM SHURAA”, utawala wake utakuwa juu ya kundi hilo tu maadam wapo katika marhala hii, atawaongoza katika vita na kuyapanga mambo yao, watampa kiapo cha utiifu cha kupigana jihad na maadui kwa kutetea nafsi  na dini mpaka mauti au kupata ushindi. Na namna ya kuweka kiapo cha utiifu ni kama ifuatavyo:


Atatangulizwa mtu aliyechaguliwa kuwa Imam, hupewa mkono wa kulia kisha anaambiwa: “Hakika sisi tumekutanguliza uwe Imam juu ya nafsi zetu na waislamu, uhukumu kwa kitabu cha Allah mtukufu na Mtume wake –sallallahu alayh wasallam- utaamrisha mema, utakataza mabaya,  utaidhihirisha dini ya Allah mtukufu ambayo amewalazimisha waja wake kumuabudu, na utalingania katika dini na jihaad kwa kadri utakavyopata njia” Akisema: “Ndio” basi inakuwa kiapo chake kimewajibika, hapo atasimama mmoja mmoja katika kundi hilo nao watampa kiapo cha utiifu. Kisha Khatibu atatoa khutba baada ya hapo juu ya usahihi wa kiapo cha utiifu na kufungika kwake kisha atasema “ Hapana mola apasaye kuabudiwa kwa haki ispokuwa Allah mtukufu, hakuna hukmu ispokuwa ya Allah mtukufu, na hakuna hukmu kwa anayehukumu tofauti na alivyoteremsha Allaah mtukufu, na hakuna utiifu kwa mwenye kumuasi Allah mtukufu, Hakuna hukmu ispokuwa ya Allah mtukufu, kuuzuliwa na kufarikiana na maadui wa Allah mtukufu”


MJUKUU: kwa kuthibiti itikadi yao katika nafsi zao imekuwa rahisi kuzitoa muhanga nafsi zao katika njia ya Allah mtukufu kwa kuinusuru dini ya Allah mtukufu na kuisimamisha sharia yake.
BABU: Umesema kweli ewe mwanangu, Itikadi ikithibiti inakuwa rahisi kutoa muhanga kila kitu, kuzitoa nafsi katika njia ya Allah mtukufu ni moja ya muhanga mkubwa walioutoa maibadhi katika njia ya Allah mtukufu, na katika masharti ya Sharaa ni:
1.    “Haijuzu kwa Mashuraati – waliouza nafsi zao katika njia ya Allah mtukufu – kutumia Taqiyya ya kidini, vyovyote itakavyokuwa hali na matatizo, na kwa sababu yoyote itakayokuwa”
2.    “Haijuzu kwa atakayechagua njia hii kurudi nyumbani kwake ispokuwa kama kuna shida kubwa, na kukaa kwake kutabakia kwa muda, na katika hali hii yeye atazingatiwa ni mgeni pale na itamuwajibikia kusali kupunguza sala kama msafiri”
3.    “Haijuzu kwa watakaochagua njia hii kurudi nyuma na kuacha ispokuwa kama watakapofanikiwa kumshinda adui yao”
Je kuna masharti mengine, au kuna marhala nyingine…. Tukutane makala ijayo


By: Khamis Yahya Khamis Alghammawi (Abu Muslim)

Published By Said Al Habsy

UIMAMU WA KUJITETEA –DIFAAI


MJUKUU: Ajabu iliyoje!, Ajabu iliyoje!,  ((Na katika watu yupo ambaye huiuza nafsi yake kwa kutaka radhi za Allah mtukufu; na Allah mtukufu ni Mpole kwa waja wake.)) Baqarah:207, Zimebakia aina mbili za Uimam, nina hamu sana ya kuzijua, niambie yanayohusiana na aina hizo ewe babu yangu.
BABU: Kwa hivyo unafuatilia vizuri ewe mjukuu wangu, basi endelea kujitahidi… Allah mtukufu akubariki.
Aina ya tatu: Ni Uimam wa Difai – Kujiitetea-, “Kikawaida Uimam huu hutokea baina ya Uimam wa siri na dhahiri, wanapokuwa maibadhi wapo katika uimam wa siri na wakakvamiwa na maadui hapo hutangaza hali ya kujitetea, na kujitetea ni katika mambo ya lazima kwa Maibadhi unapokosekana Uimam wa Dhahiri, watamchagua mmoja katika masheikh wao, mjuzi wa mambo ya vita, maarufu kwa ushujaa, ili awaongoze katika mapigano dhidi ya maadui, watamwita Imam wa Difai, mapigano yakimalizika na uimam wake utakuwa umemalizika”
MJUKUU: Hakika mimi nashangazwa na hikma iliyojaa katika fikra ya kisiasa ya Maibadhi, njia yao hii iliwezesha kubaki kwao karne nyingi.
BABU: Usifanye haraka ewe mjukuu wangu, imebakia aina ya mwisho ya uimamu nayo ndiyo aina muhimu zaidi, bali hilo ndio lengo wanaloliendea maibadhi zama zote za historia yao, nao ni UIMAM WA DHUHUR – Dhahiri – “ Maibadhi wanapofikia idadi yao nusu ya maadui kinguvu, mali na elimu, au muda wowote watakaoweza kumshinda adui yao  na kuwa juu yao, itakuwa imewawajibikia kusimamisha Uimamu wa dhahiri na kumchagua Imamu muadilifu, na kama hawakufanya watakuwa kama walioua dini ya Allah mtukufu, na wao Maibadhi  bila shaka wako mbali  na kuiua Itikadi ya kiislamu, ambayo wamepambana muda mrefu, na wamepigana katika njia ya kuihifadhi ibaki safi na iliyosalimika, kwa mujibu wa mafundisho ya Qur-an tukufu na Sunnah sahihi ya Mtume –Sallallahu alayhi wasallam-.
MJUKUU: Nizidishie ewe babu yangu, bado nina hamu ya kusikia mengi kuhusu fikra ya kisiasa kwa Maibadhi.
BABU: Haya yanakutosha ewe mwanangu, leo mazungumzo yamerefuka, kama unataka ziyada rejea katika maktaba ya kiibadhi, usome vitabu vifuatavyo:
1.    Alwuheibi, Musallam bin Salim: Alfikr al-aqadiyy indal ibadhiyyah hattaa nihaayatil qarni thanil hijry, chapa ya mwanzo, Maktabat Dhaamiri, Siib, 1427h/2006.
2.    Taalib, Mahdiyyu Haashim: Alharakatul Ibaadhiyyah fil Mashriqil Arabiyyi, chapa ya pili, Daarul hikmat, London 2003m.
3.    Muammar, Ally bin Yahya: Al-ibadhiyyah bainal firaqil Islaamiyyah inda kuttaabil maqaalaat fil qadiimi walhadiithi, jz 2, wizaaratu turaathil qawmiy wathaqaafah, Usultan wa Oman, 1406h/1986m.

Ndio nini “Azzaaba” ….. Njoo pamoja name makala ifuatayo:


By: Khamis Yahya Khamis Alghammawi Abu Muslim

Published By Said Al Habsy

07. NIDHAMU YA AZZAABA

07. NURU ING’AAYO-AZZAABA

Kila sifa njema ni za Allah mtukufu, mola wa walimwengu wote, Sala bora na salam tukufu ziwe juu ya mbora wa viumbe, Amma baad…Kwa hakika kuna pande tofauti zenye kuvutana na kugongana katika ulimwengu, ikiwemo kheri na shari, tangu kuumbwa kwa viumbe mpaka leo, basi inapoenea shari, ikawa kubwa hatari yake, Kheri hutokeza kutoka katika maficho yake, ili anga ijae nuru yenye kung’aa, na kama utafuatilia historia utaona kuwa kheri na shari daima zimo katika kuvutana, baada ya zama za Mtume –Sallallahu alayhi wasallam- na makhalifa wake waongofu fitna ilianza kudhihiri katika umma wa kiislamu hata ilikaribia nguzo zake kuporomoka kutokana na kuliwa sana na fitna hiyo, Lakini Allah mtukufu hakubali ispokuwa kuitimiza nuru yake, basi huwaleta waja wake waumini ili wahifadhi usalama wa jamii hiyo.

Ukiwaona wanachuoni wa dunia na matamanio wanaegemea katika safu za viongozi madhalimu na wakiwanyenyekea, jua huo ndio mwanzo wa kutoka katika njia sahihi, hapo wanachuoni wachamungu, wenye ikhlasi, husimama kushindana na fikra hizi zilizopotoka,  zinazowajia kwa sura tofauti. Hutetea uislamu kwa azma na kuendelea ili ubakie katika usafi wake katika hukmu zake za kisiasa na kidini, na huendelea kufundisha tabia na kuzilea nafsi zisiambukizwe maradhi mengine.Hivyo Natarajia kutoka kwako ndugu yangu – msomaji mpenzi- usome mistari hii kwa akili iliyofunguka, isiyo na ubishi au ususuavu wa namna yoyote, ili haki ipenye katika moyo wako bila kuzuiliwa na Kufuli  za matamanio.

Jua –ewe mwenye kutaka matukufu- kuwa tangu dola dhalimu ya kishia ya Faatimiyya iimalize dola adilifu ya kiibadhi ya Rustumiyya, basi njia ilibadilika vibaya sana kuelekea dhulma, matumizi ya nguvu, na uovu. Na Maibadhi walikuwa wanaona kuwa dola hii haisimamishi sharia ya Allah mtukufu wala haiifanyii kazi..baada ya kuzima moto wao wa jitihada ya kusimamisha dola adilifu, wanachuoni wa kiibadhi walifikiri njia ya kuweka nidhamu watakayopitia ili kuhifadhi hukmu za Allah mtukufu katika maeneo yao, na wapate kuupeleka ummah katika mwenendo sahihi pasina kutaka kusimamisha dola mpya au kushikana na dola dhalimu isiyotaka shura.

Waliweka nidhamu inayoendana na marhala ya SIRI ((kitman)), Nidhamu ya kimalezi inayohifadhi umoja wao, inayohifadhi madhehebu yao isije kumalizika, na ili ibaki madhehebu yao imesimama imara dhidi ya majaribio ya kuifanyia uadui.

Kwa ajili hiyo Maibadhi waliacha kufikiria mambo ya dola na wakaanza kuifikiria jamii mpaka alipokuja Mwanachuoni hodari Mvumbuzi Abu Abdillahi bin Bakri Alfurstai ambaye aliweka pembeni kufikiria mambo ya dola na kuanzisha nidhamu nyingine badala ya dola adilifu, ikakua fikra hiyo na kuwa NIDHAMU YA AZZAABA, akaiwekea nidhamu hiyo misingi na kanuni, na akawaita watu  katika nidhamu hiyo.

Ninavyodhani… utakuwa una maswali mengi unajiuliza . Ngoja nishirikiane nawe katika baadhi ya maswali hayo ili tufikie majibu yanayotakiwa: Ni nini nidhamu ya Azzaaba ? Ni zipi sharti zake?

Je ina cheo gani katika dola yenye kuhukumu? Ni ipi kazi yake ?Je ni kweli ilikuwa ni badala ya dola adilifu ?

Njoo nami katika njia hii kwa roho ya uchangamfu ili tupambanue mwenendo huu.

By Khamis Yahya Khamis Alghammawi

Published By Said Al Habsy

NIDHAMU YA AZZABA

Nidhamu ya Azzaba ni badala ya nidhamu ya uimamu wa kiibadhi ambao husimamia uadilifu, Nidhamu ya Azzaba ndio huwakilisha dola hiyo ikisimamiwa na viongozi mahodari katika jamii husika kwa elimu na wema, na neon Azzaba katika lugha ya kiarabu limetokana na neon “Aazib” ambalo linatumika kwa aliyejiweka mbali na kitu, kama ambavyo linatumika kwa maana ya kutokuwepo.
Anasema mwanachuoni Aldarjeini: (( Azzaaba ni wingi, akiwa mmoja anaitwa Azzaabiy, neno hili linatumika kama alama ya kila aliyejilazimisha njia ya wema, kutafuta elimu, na kufuata njia ya watu wa kheri, akazihifadhi na kuzifanyia kazi, mambo yote hayo yakipatikana ndio huitwa mwenye kuwa nayo ataitwa Azzabiyy”
Hapana shaka umejua – ewe mwanafunzi wa ilmu – kuwa nidhamu ya uimam kwa maibadhi imesimama kwa mashauriano (Shura) sawa ikiwa wakati wa Difai au Dhuhuur, na Azzaba inasimama kwa Mashauriano (Shura) wakati wa Kitman na Sharai ( Kujitoa Muhanga).
Ametaja Sheikh Muhammed Atfeish kuwa : “Kuwepo kwa Azzaba ni la Lazima, kwa sababu kuamrisha mema na kukataza mabaya kunalazimika kwa kuwepo kwake” na wamekubaliana kuwa itakuwa ni lazima kama wanaliweza, na hilo limetolewa katika Qur an na Sunnah.
Jua ewe ndugu yangu – Allah mtukufu akuzidishie fahamu- kuwa kila nidhamu ya utawala ina namna yake ya kutawala, kwa hivyo hapana budi kuwepo misingi na mipango, kwa ajili hii Azzaba inatengenezeka baina ya wajumbe kumi (10) mpaka kumi na sita (16) kwa mujibu ukubwa wa mji huo, na hao wajumbe ni katika wachamungu, wema, mwenye elimu, na muaminfu. Watachagua baina yao Sheikh wa Azzaba ambaye ni mjuzi wao, na mwenye uwezo zaidi wa kusimamia, atahesabiwa kuwa ndiyo marejeo yao, msemaji wao, na amri yake inatekelezwa. Makao makuu ya Azzaba yatakuwa katika pembe miongoni mwa pembe za Msikiti, na haiwajuzii kujadili jambo lolote nje ya makao makuu yake rasmi.


Kwa kuwa Nidhamu hii ndiyo yenye jukumu la kusimamia mambo ya mji ule, kwa hivyo watakuwa na majukumu yatakayogawanywa kwa wajumbe wake, kama ifuatavyo:
1. SHEIKH WA AZZAABA: Mjuzi zaidi wa mji ule, anasifika kuwa na Shakhsiya kubwa, atasimamia Kutoa mawaidha, kufikisha matangazo ya Azzaaba kwa watu wote, naye ana amri kama ya mtawala muadilifu, na atabakia katika cheo chake maisha yake yote.
2. WASHAURI: Idadi yao ni wanne, watakuwa na Sheikh Daima katika vikao vyake, hatoamua jambo ispokuwa kwa kukubali kwao.
3. IMAMU: Mtu mmoja, amekalifishwa kuwasalisha watu kwa Jamaa, na Inajuzu kuwa ni mmoja wa washauri.
4. MSOMA ADHANA: mtu muaminifu, mchamungu, mwenye kujua nyakati.
5. WASIMAMIZI WA WAKFU: watachaguliwa wajumbe wawili, wenye hali ya katikati, sio matajiri wala mafaqiri, ili wasimamie na kuendeleza waqfu, wadhibiti vyenye kuingia na vyenye kutoka, na Bajeti ya Azzaba.
6. WALIMU: watachaguliwa wajumbe watatu au zaidi ya watatu kwa mujibu wa mahitaji ili wasimamie kuweka mpango wa Malezi na mafunzo na kuwasimamia wanafunzi.
7. HALI ZA MAITI: watachaguliwa wajumbe wanne au watano kwa ajili ya kusimamia haki za maiti na yote yahusuyo kuzika, kutekeleza wasiya na kugawa urithi.


 Khamis Yahya Khamis Alghammaw

Published By Sh. Hafidh Al-Sawafi

09. FUNGA YA ARAFA BAINA YA MUANDAMO NA KISIMAMO
بِسْمِ اللَّهِ الرَّحْمَٰنِ الرَّحِيمِ

Shukurani zote ni kwa Allah mtukufu, na rehma na amani ziwe kwa kipenzi chetu Mtume wa Allah Muhammad pamoja na wafuasi wake na masahaba wake mpaka siku ya malipo.

Asalamu alaykum wa rahmatullahi wa barakatuh.

Kwa hakika mvutano baina na haki na batili ndio hali inayowafikia waja katika ulimwengu huu, na katika kila zama na mitihani yake, na katika hayo ndio linapatikana lengo la uwepo wetu katika ulimwengu huu, amesema Allah mtukufu:

كُلُّ نَفْسٍ ذَائِقَةُ الْمَوْتِ ۗ وَنَبْلُوكُم بِالشَّرِّ وَالْخَيْرِ فِتْنَةً ۖ وَإِلَيْنَا تُرْجَعُونَ

((Kila nafsi itaonja mauti, na tunakujaribuni kwa shari na kheri kuwatahini, na kwetu sisi munarejeshwa.)) [Al-Anbiyaa 35].

Dini ya Uislamu imetimia tokea miaka 1429 iliyopita kama ilivoeleza Qurani tukufu, miaka yote hiyo Waislamu walifanyia kazi mafundisho yake, yako ambayo walikubaliana ndani yake na yako waliyotafautiana ndani yake, yaliyoingiwa na tafauti yalisababisha kupatikana madhehebu tafauti ili kudhibiti misimamo ya kila upande na wahusika wake katika kila zama, ni sawa katika Itikadi au Fiqhi au Siasa, na mapote yalizuka, ni hali isiyoweza kupingika wala kukatalika, na kila wahusika wa madhehebu walitokeza ndani yake wanavyuoni na watetezi, kwa mwenye kusoma kitabu cha Allah mtukufu anajua kuwa hiyo si hali ngeni; kwani imeelezwa kuwafikia waliopita kabla yetu.

Si tatizo kutafautiana, bali tatizo sugu ni kufanyiana uadui kwa sababu ya tafauti, kwa hiyo ni wajibu wa kila Muislamu kuheshimu tafauti iliyotokeza na inayotokeza na itayotokeza, kama ilivokua ni wajibu wa kila Muislamu kujiepusha na njia ya ubabe na uadui dhidi ya waliotafautiana naye kimadhehebu, na iwapo atajikuta kuwemo katika safu za fikra za kufanyia ubabe na uadui wengine kwa sababu ya kutafautiana kimadhehebu basi ajijue kuwa amekumbwa na maradhi mabaya yaliyoelezwa katika Quraani kuwapata waliopita kabla yetu, haraka sana airejee nafsi yake na ajue kuwa hapo alipo sipo; kwani yupo katika batili, kwa haya upendo utaenea, na jamii itaimarika, na umoja utapatikana, kwani mshikamano katika yenye makubaliano utaweza kuimarika, na heshima katika yaliyoingiwa na tafauti itaweza kupatikana, na kila wenye msimamo wataweza kueleza dalili zao katika jamii. Umoja kwamwe hauji kwa kulazimishana na kutetea wingi, kwani hakuna haki ya kuificha haki, na haki ni kwa dalili si kwa wingi.

Ibadhi kwa upande wetu ni tunda ya kujishika na haki kwa dalili katika kila lenye tafauti ndani yake, tunasema kwa wote: “Leteni dalili zenu ikiwa nyinyi ni wakweli mumepatia haki” tunajiongoza kwa Kitabu cha Allah na Sunna ya Mtume S.A.W. na yenye makubaliano ndani yake, hii ndiyo hali yetu tokea hapo mwanzo mpaka hivi leo.

Leo hii limekuja suala la funga ya siku ya arafa.

Jee! Kufunga siku ya arafa ni kwa kisimamo cha Mahujaji katika sehemu ya Arafa, au kwa Muandamo wa mwezi wa Dhul-Hijja (Mfunguo tatu)?

Kwa kweli inafahamika vizuri sana kuwa karne zote zilizopita Waislamu hawakua wakiijua siku ya arafa isipokua kwa kupitia muandamo wa mwezi wa Hija, na kuwa watu wa miji yote, kila mji waliijua siku hiyo ya arafa kupitia muandamo wa majira yao, na wanavyuoni wote waliijua siku ya kufunga arafah kuwa ni siku ya tisa ya mwezi wa Hijja (mfunguo tatu), kwa ufupi makubaliano ya wote ni kuwa siku ya arafa ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-Hijja (mfunguo tatu), na kuwa siku hii ina ibada zinayoihusu, nazo ni mbili:

1. Ibada iliyofungamana na sehemu maalumu.

2. Ibada isiyofungamana na sehemu maalumu.

Zote ni ibada za siku ya arafa ambayo ni siku ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja.

Ama ibada iliyofungamana na sehemu maalumu hiyo ni ibada ya kusimama katika sehemu inayoitwa arafa iliyoko katika mji mtakatifu wa Makka, na ibada hii inawahusu Mahujaji peke yao nayo ni nguzo mama ya ibada ya Hijja.

Ama ibada isiyojifunga na sehemu maalumu hiyo ibada ni kufunga siku hii ya tisa ya mwezi wa Dhul-hijja nayo ndiyo inayojulikana kuwa ndiyo siku ya afara.

Kwa hiyo ni haki kuwa kila muislamu ajishike na majira ya mji wake katika kutekeleza ibada hii ya funga ya arafa kama vile anavyoanza mchana wake kwa aljfajiri ya mji wake na kumaliza kwa kuchwa jua katika magharibi ya mji wake basi vile vile afunge siku ya tisa kwa mujibu wa muandamo wa mji wake; kwa sababu hayo ndiyo majira aliyofungwa nayo katika ibada zake zote za wakati, kwa hakika sehemu iitwayo arafa ina majira yake nayo haindoki mpaka dunia itamalizika, kwa hiyo uhakika ni kuwa ibada ya siku ya arafa ni ya wakati wa majira ya sehemu ya mji husika na si kwa ibada ya Mahujaji mbayo pia imefungwa kwa majira ya mji wanaotekeleza ibada hiyo ndani yake, vipi Muislamu anakubali kuondoshwa katika asili na sababu ya ibada na kufungwa na jambo jengine?

Leo hii wamezuka watu na jambo jipya na geni, kwa hakika halikuwepo kwa miaka zaidi ya elfu moja iliyopita, watu hao hao utawasikia wakisema: Jichungeni sana na mambo mapya mapya, kwani kila jipya ni bidaa, na kila bidaa ni upotevu, na kila upotevu ni motoni”.

Tunawambia: Ni yakini isiyokua na shaka yoyote kuwa Dini ya Uislamu imetimia tokea zama za Mtume S.A.W. na kuwa waislamu kwa miaka zaidi ya 1400 hawajui chengine katika ibada hizi isipokua kujifunga na tarehe ya muandamo kwa mujibu wa nyakati za majira yao tu, kama ilivokua hawasali wala hawafungi kwa mjira ya mji mtakatifu wa makka, basi vipi watafunga kwa ibada ya watu wa mji huo? Hakika ibada za walioko Makka zote zimefungwa kwa mujibu wa majira ya mji huo, kama ilivokua ibada zetu zote zimefungwa kwa majira ya miji yetu.

Mumepata wapi nyinyi sababu hiyo munayoidai hivi leo?

Vipi nyinyi leo munafanya kila pupa la kuwaondosha watu katika njia ya wema waliopita katika kila madhehebu na kuzua jambo jipya?

Ewe Allah hakika sisi tumeshabainisha.

Tunawatakia Waislamu wote siku kuu njema ya kheri na barka.

Amin.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here