[1]) wanakula mali za Watu kwa (njia ya) batili, na wanazuia kunako njia ya Allah. Na wale wanaokusanya Dhahabu na Fedha na hawazitoi katika njia ya Allah, hao wabashirie Adhabu yenye kuumiza * Siku zitakapochomwa (Mali zao) katika moto wa Jahannamu, basi zitasuguliwa nazo mapaji yao na mbavu zao na migongo yao; (Wataambiwa) haya ndio muliokuwa mukiyakusanya kwa ajili ya nafsi zenu, basi onjeni yale muliokuwa mukiyakusanya﴿
[Tawba 09/34].
(Alikuja mwanamke kwa Mtume wa Allah (s.a.w) na akiwa na mtoto wake, naye amevaa katika mkono wake bangili mbili nzito za dhahabu, basi alisema Mtume wa Allah (s.a.w) kwa mwanamke huyo: ((Hivi unatoa zaka ya Mabangili haya?)) Akajibu: Hapana”. Hapo akasema (s.a.w): ((Hivi itakuwa ni furaha kwako ikiwa Allah atakuvisha kwa ajili yake siku ya kiama Mabangili mawili ya Moto?)). Basi yule mwanamke aliyavua na kuyatupa kwa Mjumbe wa Allah (s.a.w) na akasema: “Hayo hapo ni kwa ajili ya Allah na Mtume wake”). [Sunan Abi Daudi 1563, Nasaai Sunan Al-kubra 2270, Sunan Daraqutni 1982, Musnad Ahmed 6667]
KIWANGO CHA MALI INAYOTOLEWA ZAKA
Italazimika Ibada ya Zaka kila mwaka([2]) mara moja kwa yule atakaye miliki Nisaabu (kiwango chake), na baada ya kumiliki kiwango chake (Nisaabu) kikazungukiwa na Mwaka wa Kiislamu bila ya kupungua, na kiwango hicho (Nisaabu) ni kuanzia Gram themanini na tano (85g) za Dhahabu, na hapo kila zikiongezeka Gram kumi na saba (17g) zinaingizwa katika hisabu ya zaka ikiwa tu zimeongozeka kabla ya kutoa fungu la zaka, na nyongeza ikiwa chinia ya gramu 17 itaanguka kwa maana haiingizwi katika hesabu ya Zaka.
NAMNA YA KUKUSANYA MALI NAYOTOLEWA ZAKA
Utazingatia kuwa mali yako inayohisabiwa katika Zaka, ni lile limbikizo lako lote ulilonalo, na madeni yako ambayo yameshafika wakati wake wa kulipwa hali unayo matarajio ya kuyapata, na kila ambacho ni miliki yako nacho kimo katika mzunguko wa biashara kwa mujibu wa thamani yake ya soko, na hakuna Zaka katika vitu vinavyotumiwa ambavyo mwenye kuvimiliki haviuzi navyo sio madini ya Dhahabu wala Fedha, kwa mfano Gari ikiwa ameliingiza katika Soko la mauzo basi thamani yake itazingatiwa, na ikiwa bado mwenye nalo haliuzi analitumia kwa kazi zake basi haliingizwi katika makusanyo ya Zaka.
NAMNA YA KUFANYA HESABU YA KUTOA ZAKA
Utauliza thamani ya Gramu moja ya Dhahabu katika soko, kisha utaizidisha mara kumi na saba (17), na hicho utakachokipata ndio tegemeo lako katika hisabu mzima ya Zaka, basi tukiite Y, kwanza utakizidisha mara tano (Y x 5) utakachopata ndio kiwacho cha mwanzo cha Mali yenye kutolewa Zaka (Nisaabu); kwani ndio kiwango cha gramu 85 za dhahabu, na hiki tukiite Z ikiwa kitafikia hapo au kitaongezeka zaidi yake, basi mali ikiwa chini ya Z mali hiyo haina zaka; kwani bado haijafikia kiwango cha zaka (Nisaabu).
Sasa ikiwa mali imefikia Z au iko zaidi yake, mali hiyo utaigawa kwa Y namna hivi (Z ÷ Y) utakachokipata utachukuwa kile kizima tu, na kilichoongezeka utakiwacha, yaani kilicho mbele ya nukta, kisha hicho kizima utakizidisha tena kwa Y, na hapo utakuwa umeshapata Mali yako ambayo inalazimika kuitolea Zaka kisheria, na tuiite W, na mali hiyo utaigawa kwa arubaini (W ÷ 40) na hicho utakacho kipata ndio fungu la zaka linalopaswa kutolewa.
MFANO:
Ninamiliki limbikizo la pesa 5,000,000. Fbu, na 1,000. $US na Biashara yangu ina thamani ya 4,000,000. Fbu, pia ninayo Bangili ya Dhahabu yenye uzito wa 100g. na Madeni ninayotarajiwa kuyapata na muda wake umeshafika ni 300,000. Fbu.
Gramu moja ya Dhahabu ina thamani ya 15000. Fbu.
Dolla moja ina thamani ya 1050 Fbu.
1. Kutimiza idadi inayolazimika kuitolea zaka, basi ikiwa idadi ya wanyama hao haijafikia kiwango cha kuitolewa zaka hapo itakuwa hakuna zaka ndani yake.
2. Kutimiza mwaka, kwa sababu zaka ya Wanyama inalazimika kila mwaka mara moja, na hesabu ya mwaka itazingatiwa kwa mujibu wa kalenda ya Kiislamu, na sio kalenda ya Kikiristo kama watu walivyozowea.
3. Wanyama wawe ni mifugo, kwa hivyo wakiwa ni wanyama wa biashara kwa kuwa mtu ananunua kisha anakwenda kuuza hao wanaingia katika zaka ya biashara kama ilivyotangulia, au wakiwa wanyama wa kutumikisha kwa kazi, na hasa wanaingia n`gombe waliohusishwa kwa kazi za ukulima, au kufungwa gari kwa ajili ya kubebea mizigo, wanyama hao hawaingii katika hesabu ya zaka.
4. Wawe ni milki ya mwenye kutowa zaka.
ZAKA YA N`GOMBE
Zaka ya n`gombe na ngamia ni sawa sawa haina tofauti katika kuifanyia kazi isipokuwa majina tu ya wale wanyama wanaotolewa kuwa ni zaka yake, basi inafaa kuyajuwa majina ya n`gombe wanaotolewa katika zaka, na sifa za majina hayo:
1. TABIIAH ni n`gombe jike mwenye umri wa mwaka mmoja.
2. JIDH-AH ni ngombe jike mwenye umri wa miaka miwili.
3. THANIYAH ni n`gombe jike mwenye umri wa miaka mitatu.
4. RUBAIYAH ni n`gombe jike mwenye umri wa miaka minne.
IDADI YA N`GOMBE NA KIWANGO CHA ZAKA YAKE.
IDADI YA N`GOMBE |
KIWANGO CHA ZAKA |
(5 – 9). |
Mbuzi mmoja jike. |
(10 – 14). |
Mbuzi wawili majike |
(15 – 19). |
Mbuzi watatu majike |
(20 – 24). |
Mbuzi wanne majike |
(25 – 35). |
Tabiiah mmoja. |
(36 – 45) |
Jidh-ah mmoja |
(46 – 60). |
Thaniyah mmoja |
(61 – 75). |
Rubaiyah mmoja |
(76 – 90). |
Jidh-ah wawili |
(91 – 120). |
Thaniyah wawili |
(121 – 129) |
Jidh-ah watatu |
Wakifika n`gombe mia na thelathini (130) na kuendelea. |
1. Kwa kila ngombe arubaini atatolewa Jidh-ah mmoja. 2. Na kwa kila n`gombe hamsini atatolewa Thaniyah mmoja. |
(130 – 139) |
Jidh-ah 2 + thaniyah 1. |
(140 – 149) |
Thaniyah 2 + Jidh-ah 1. |
(150 – 159) |
Thaniyah 3. |
(160 – 169) |
Jidh-ah 4. |
Na hesabu inaendelea namna hiyo. |
Zingatia: Anaingia katika hesabu ya zaka hata yule aliyezaliwa jana yake, ikiwa tu kabla ya kufanya hesabu ya zaka.
ZAKA YA MBUZI NA KONDOO
Kondoo na mbuzi zaka yao ni moja, hakuna tofauti kati yao, tena ni rahisi sana kueleweka, haina tabu kabisa, kwani hailazimiki zaka ndani yake mpaka wafikie arubaini (40) wakifika hapo inalazimika kutoa kila mwaka mbuzi mmoja jike au kondoo mmoja jike, na itaendelea kila mwaka kutoa namna hiyo mpaka wafikie mia moja na ishirini na moja (121) hapo ndio italazimika kutoa mbuzi wawili, na itaendelea hivyo hivyo mpaka wafikie mia mbili na mmoja (201) hapo italazimika kutoa mbuzi watatu (3). Hapo tena itaendelea mpaka wakifika mbuzi mia nne (400) inakuwa sasa katika kila mbuzi mia moja (100) anatolewa mbuzi mmoja, na namna hivyo kwa idadi itayokuwa, kila mbuzi mia moja (100) atatolewa mbuzi mmoja, na linalofuata ni jaduweli lake.
JADUWELI LA ZAKA YA MBUZI NA KONDOO
IDADI YA MBUZI |
KIWANGO CHA ZAKA |
(40 – 120) |
1 |
(121 – 200) |
2 |
(201 – 399) |
3 |
(400 -) |
Kila idadi ya mia moja atatolewa mbuzi mmoja. |
Zingatia: Anaingia katika hesabu hata yule mbuzi au kondoo aliyezaliwa jana yake ikiwa tu kabla ya kufanya hesabu ya zaka.
ZAKA YA MAZAO YA SHAMBA
1. Mazao yenye kutolewa zaka:
Italazimika kutowa zaka ya mazao ya shamba kwa wakulima wa mazao ya nafaka tu, na hizo nafaka ni kila zao ambalo ninakaushwa baada ya mavuno nalo ni chakula kama vile mahindi, mpunga, ngano, maharage, kunde, mbaazi, choroko, zabibu, mtama, njugu, njugu mawe, tende na mengineo.
2. Mazao yasiyotolewa zaka:
Ama mazao mengine yasiyokuwa ni nafaka hayo hayana zaka ya mazao ya shamba, lakini zaka yake itaingia katika zaka ya biashara kama tulivyoeleza hapo mwanzo, kwa sababu sio mazao ya kubakia kwa bwana shamba, bali baada ya mavuno tu yanahitaji kutumiwa kwa ajili ya chakula kwa watu, na kwa hiyo atalazimika kwa mwenye mavuno hayo kuyatumia kwa haja zake au kuyagawa kwa masikini na jirani na watu wake wa karibu au kuyafanya kuwa ni mauzo, kwa hivyo mazao hayo yanaingizia pato la thamani, na hapo atakuwa mwenye nayo mfanya biashara, na atakuwa ni mwenye kumiliki kiwango chake basi ikaingizwa zaka yake katika zaka ya biashara. Na mazao hayo ni kama vile mboga mboga, tomato, viazi, nyanya, bilinganya, tikiti, maembe… na mfano wake.
KIWANGO CHA MAZAO YENYE ULAZIMA WA KUTOLEWA ZAKA
Mavuno ya mazao yatalazimika kutolewa zaka yake yatakapofikia kiwango cha pishi sitini (60) ambazo ni sawa na kilogramu mia sita na hamsini (650kg), hapo italazimika kutowa zaka ndani yake, ama ikiwa ni chini ya hapo itakuwa hamna zaka ndani yake, atakayetowa huyo ametowa sadaka tu.
Kwa hivyo inalazimika kutowa zaka kwa kutimiza uzito wa kilogramu mia sita na hamsini na kuendelea juu, na zaka hii itatolewa katika siku ya mavuno, kwa hivyo uzito huo utazingatiwa katika siku hiyo ya mavuno amesema Allah mtukufu:
﴿وَهُوَ ٱلَّذِى أَنشَأَ جَنَّـٰتٍ مَّعْرُوشَـٰتٍ وَغَيْرَ مَعْرُوشَـٰتٍ وَٱلنَّخْلَ وَٱلزَّرْعَ مُخْتَلِفًا أُكُلُهُ وَٱلزَّيْتُونَ وَٱلرُّمَّانَ مُتَشَـٰبِهاً وَغَيْرَ مُتَشَـٰبِهٍ كُلُواْ مِن ثَمَرِهِ إِذَا أَثْمَرَ وَءاتُواْ حَقَّهُ يَوْمَ حَصَادِهِ وَلاَ تُسْرِفُواْ إِنَّهُ لاَ يُحِبُّ ٱلْمُسْرِفِينَ﴾
﴾Yeye (Allah) ndie aliyeziumba bustani zenye kutambaa na zisizotambaa, na mitende, na mimea yenye malisho tofauti, na mizaituni, na mikomamanga inayofanana na isiyofanana, kuleni mazao yake inapozaa, na toweni haki yake siku ya mavuno yake, na musitumie kwa fujo, hakika yeye hapendi wenye kutumia kwa fujo﴿ [An-aam 141].
KIWANGO CHA ZAKA YA MAZAO
Kiwango kinachotakiwa kutolewa kinazingatiwa kwa mujibu wa kilimo kilichotumika:
1. Ikiwa shamba halikuhitaji kumwagiliwa maji kwa sababu ya kujitosheleza ardhi yake kwa mvua, au maji yake wenyewe yaliyomo katika ardhi au ya kupita hapo hapo, basi zaka yake itakuwa ni asilimia kumi ya mavuno (10%) yaani kila kumi utatowa moja ikiwa ni kwa kilo au pishi au chochote utakachokitumia katika vipimo hata ukitumia cha ndoo.
2. Ikiwa shamba limehitaji kumwagilia maji basi kiwango cha zaka ya mazao yake ni asilimia tano (5%) yaani katika kila ishirini utatowa moja ikiwa ni kwa kilo au pishi au chochote utakachokitumia katika vipimo hata ukitumia kipimo cha ndoo.
WALIOKUWA NA HAKI YA
KUPEWA ZAKA
Allah mtukufu kwa hekima zake amebainisha wale ambao wana haki ya kupewa zaka katika jamii, basi amesema katika kitabu chake kitukufu:
﴿إِنَّمَا ٱلصَّدَقَـٰتُ لِلْفُقَرَاء وَٱلْمَسَـٰكِينِ وَٱلْعَـٰمِلِينَ عَلَيْهَا وَٱلْمُؤَلَّفَةِ قُلُوبُهُمْ وَفِى ٱلرّقَابِ وَٱلْغَـٰرِمِينَ وَفِى سَبِيلِ ٱللَّهِ وَٱبْنِ ٱلسَّبِيلِ فَرِيضَةً مّنَ ٱللَّهِ وَٱللَّهُ عَلِيمٌ حَكِيمٌ﴾
﴾Hakika ya Sadaka (ya zaka) ni kwa ajili ya mafakiri, na masikini, na wenye kuzifanyia kazi, na wenye kuchombezwa nyoyo zao, na katika kuwacha huru, na wenye kugharimia, na katika njia ya Allah, na mtoto wa njia. Ni ulazimisho utokao kwa Allah, na Allah ni mjuzi mwingi wa hekima﴿
[Tawbah 09/60]
Tunaona katika aya hii tukufu wamebainishwa wale wenye haki ya kupata mafungu ya zaka nao ni wanane:
1. Mafakiri:
Mafakiri ni wale ambao hali zao ndio za chini kabisa hawa wanahangaika kwa ajili ya kupata cha kutia tumboni katika siku yao, hawana sehemu ya kupata cha kusimamisha maisha yao, wao wanasubiria tu bila ya matarajio, hali zao ni taabani sana, hata pa kukaa kwao ni shida.
2. Masikini:
Masikini ni wale ambao hali zao ni taabani lakini wao wanajeweza weza kidogo, pengine wanapata cha siku yao lakini cha kesho yake ni tabu juu yao, na pengine wanamiliki lakini hali zao bado ni duni za chini, wakifikwa na ladharura hawana pa kufikia.
3. Wenye kuzifanyia kazi:
Hawa ni wale ambao wanasimamia ibada ya zaka kwa kuikusanya na kuifikisha kwa waliona haki nayo, wao wanapewa kwa kadiri ya kazi yao tu, ni kama wafanya kazi katika hilo, kwa hivyo wao wanapata sehemu tu ya zaka kwa kutimiza ibada hiyo katika jamii, ikiwepo dola ya Kiislamu zaka inafikishwa kwao ikiwa ni waadilifu katika hukumu zao, na kama haipo kama ilivyo katika wakati huu, basi ikiwa waislamu watachagua wa kuweza kuisimamia ibada hii wataingia katika fungu hili, na haifai kuwapa zaka isipokuwa wawe ni waadilifu wenye kuaminika, kama unaona hawana uaminifu katika mali kwa kuifikisha kwa wenyewe, basi itakulazimikia wewe mwenyewe kuifikisha kwa wanaostahiki.
4. Wenye kuchombezwa nyoyo zao:
Hawa ni wale wanaovutwa katika uislamu na masilahi ya uislamu, na wale wapya hatika uislamu na madhaifu wa imani, na mfano wa hao.
5. Katika kuwacha huru:
Hawa ni watumwa wanaotaka uhuru wao, basi mali ya zaka inatumika kwa kuwanunua na kuwapa uhuru wao, na vile vile wale walioandikiana na mabwana wao kwa kuwa ni deni juu yao la kugomboa nafsi zao kunako utumwa, hawa wanakuwa huru kwa kuandikiana kwao huko na mabwana wao kisha wanapata mali ya zaka ili iwagomboe kwa deni lao.
6. Wenye kugharimia:
Hawa ni wenye madeni yaliyowashinda kuyalipa, na madeni hayo wameyachukuwa kwa njia isiyokuwa ya haramu wala sio kwa njia ya fujo, wala sio kwa kutumia kwa haramu, basi hawa kwa kushindwa kwao huko kulipa wanapata sehemu ya zaka kwa kuwaondoshea mzigo huo wa madeni.
7. Katika njia ya Allah:
Hii ni njia ya kunyanyua juu Dini ya Allah mtukufu nayo ni Dini ya Uislamu, Dini ya Mitume wote (a.s.w) kwani Mitume wote Dini yao ni moja na sheria zao ndio tafauti, na kila Mtume aliyekuja mbele huikalia sheria ya aliyekua kabla yake, na kulazimika waja kuifuata sheria ya huyo aliyekuja mwisho, basi Muhammad bin Abdillahi (s.a.w) ndie Mtume wa mwisho hakuna Mtume wala Nabii baada yake na Sheria yake imezikalia sheria za wote waliopita kabla yake, basi zaka inatumika kwa kuinyanyua Dini hii, na asili ya fungu hili ni kutumika katika Jihadi ya kupigana na Maadui wa Uislamu na Waislamu.
8. Mtoto wa njia:
Huyu ni msafiri amekwama katika njia kwa kumalizikiwa na anayoyahitaji katika safari yake, basi zaka inatumika kwa kumrejesha katika mji wake tu hata kama huku kwao ni Tajiri.
MAZINGATIO
1. Makundi yote yalifaa kupewa zaka yanapewa kwa mujibu wa mahitaji yake tu isipokuwa makundi matatu, hayo matatu yanaweza kupewa zaka yote, nayo ni Mafakiri, Masikini, na Katika njia ya Allah.
2. Zaka ni haki ya Waislamu tu basi haifai kupewa asiyekuwa Muislamu, isipokuwa kwa yule inayekhofiwa fitina yake katika kuwadhalilisha waislamu huyo ataingia katika fungu la wenye kuchombezwa nyoyo zao.
3. Unapompa mtu mali ya zaka unatakiwa umwambie kuwa hii ni sadaka ya Zaka, kwa sababu wewe umempa kwa mujibu wa vile ulivyomuona wewe na pengine yeye hayumo katika wenye haki ya kupewa zaka, basi ukimuambia tayari umesimamisha hoja juu yake kama hayumo katika hao atakuwa hana haki ya kuichukuwa na akiichukua utakuwa mzigo ni juu yake.
4. Asili ya zaka inatolewa hapo ilipopatikana haivuuki mji huo, isipokuwa ikipatikana dharura maalumu, kama vile kukosekana wa kupewa zaka katika mji huo, au kuwa mwenye kutowa zaka ana mtu wake wa karibu kiukoo na hali yake ni mbaya sana na yeye yuko nje ya mji huo, na juu ya hivyo katika hali hii haitakiwi kuimaliza zaka kwa huyo wa karibu, basi hapana budi na walio mafakiri na masikini wa mji wapate na wao japo kidogo.
Kwa haya machache natarajia kuwa yamefahamika, na kuwa yataleta faida katika jamii ya kiislamu.
Wassalamu alaykum
Masjidu L-istiqamah – Bujumbura
25/09/1426H – 29/09/2005M
[1]. Ah-baar ni Wataalamu wa dini wa Kiyahudi, na Ruh-baani ni Wataalamu wa dini wa Kinasara, na kutajwa jambo hili hapa ni kuhadharishwa Wataalamu wa dini katika Umma huu (Mashekhe) wasije wakafuata nyayo zao, kwa sababu mazingatio ni sababu ya kuingizwa katika makosa na sio Majina, na katika hili kuna tahadhari kwa wanaotoa zaka ya kuwa waangalie katika Wanavyuoni wenye kuaminika na sio kila anayepiga kelele za kuwa anakusanya zaka akubaliwe tu.
[2]. Mazingatio ni kalenda ya Kiislamu sio hii iliyozoeleka.